Friday, January 17, 2014

MWANAKONDOO WA MUNGU NA MWANA MBUZI WA WATU


 

                                                JUMAPILI YA 2 YA MWAKA                              

Tazameni, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu” (Yohane 1: 29)

1. Isa 49: 3. 5-6
2.  1 Kor 1: 1-3
3.  Yn 1: 29-34

 
Siku moja kondoo, mbuzi na mbwa wakiwa wanatoka kwenye sherehe walikodi daladala. Kondoo alipokaribia kufika nyumbani kwake alilipa nauli na kutelemka kituoni karibu na alipokuwa anaishi. Mbwa alilipa nauli lakini hakurudishiwa chenji. Mbuzi yeye aliruka na kukimbia bila kulipa nauli. Ndiyo maana hata sasa kondoo akiona gari hatoki haraka barabarani. Hadaiwi. Alilipa deni. Mbwa akiona gari anakimbia kulikamata anadai chenji. Mbuzi akiona gari anakimbia. Hakulipa deni. Yesu msalabani alilipa deni la upendo hadaiwi. Ni mwanakondo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu.

SIFA YA KONDOO NI UPOLE NA UNYENYEKEVU

Kuna watu ambao wanaweza kupinga kuwa Yesu hasiitwe Mwana Kondoo kwa vile katika kitabu cha Ufunuo 5:5 anaitwa Simba wa Yuda, “Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, ‘Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, chipukizi wa Daudi, ameshinda.” Katika maneno ya nabii Yeremia tunamwona Yesu Mwanakondoo mnyenyekevu, “Nami nilikuwa kama kondoo mpole anayepelekwa machinjoni; sikujua kuwa njama walizozifanya zilikuwa dhidi yangu.” (Yeremia 11: 19)

SIFA YA KONDOO NI KUTOKUWA NA HILA, UBAYA NA KOSA

Yesu ni mwanakondoo hasiyekuwa na hila, ubaya, wala kosa, kama tunavyosoma katika biblia. “Lakini hamkukombolewa kwa vitu vyenye kuharibika: kwa fedha na dhahabu; bali kwa damu tukufu ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwanakondoo asiye na dosari wala doa.” (1 Petro 1:19) “Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake.” (1 Petro 2:22) Kabla ya Kukomunika maneno “Mwana Kondoo wa Mungu,” yanatajwa mara nne katika Ibada ya Misa. Kwanza yanatajwa mara tatu katika sala ya Mwana Kondoo. “Mwana Kondoo wa Mungu huondoaye dhambi za dunia, utuhurumie. Mwana Kondoo wa Mungu huondoaye dhambi za dunia, utuhurumie. Mwana Kondoo wa Mungu huondoaye dhambi za dunia, utujalie amani. Kabla ya kumuomba Mungu atujalie amani tunaomba atuhurumie. Kwa sababu gani? Amani ni tunda la moyo usio na hila, usio na udanganyifu, usio na doa, usio na kasoro. Hatuwezi tukawa na amani kama kuna dhambi mioyoni mwetu. Minyoo inaingiaje kwenye tunda. Unakuta tunda lina tundu na katikati kuna munyoo mkubwa. Umetoka nje ama ndani. Umetoka ndani. Ua linapochanua ndipo hapo mayai yanatagwa. Mdudu anakua wakati tunda linakua. Shida inatokea wakati watoto wakiwa wadogo wanasikia mazungumzo ya watu wakubwa. Wanasikia kuwa watu wa kabila hili ni wabaya. Uovu unakua na mtoto. Matokeo yake ni ukosefu wa amani. Je tunapanda mbegu ipi?

 

 

Jina hili la heshima linadokeza  mateso ya Yesu na kifo chake msalabani (Isa 19: 36; 53:7). Jina hili Mwanakondoo limerudiwa na Yohane mara 29.

SIFA YA KONDOO NI KUVUMILIA 

Kufa kikondoo maana yake kuvumilia shida bila malalamiko. Mwokozi Yesu alikufa kikondoo. “Alidhulumiwa na kuteswa, lakini alivumilia kwa unyenyekevu, bila kutoa sauti hata kidogo. Alikuwa kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni, kama kondoo akaavyo kimya anapokatwa manyoya. Hakutoa sauti hata kidogo.” (Isaya 53: 7) Ni yeye aliyesema ukipigwa shavu moja   la kulia geuza la kushoto. Yeye hakugeuza la kushoto tu aligeuza mwili mzima. Lakini bado alikuwa na kadi nyingine kadi ya kumtumia Roho Mtakatifu. Maadui zake walifikiri ameshindwa. Matumaini yake aliyaweka kwa Mungu, hakimu mwenye haki. “Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake. Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki.” (1 Petro 2: 22) Ili kuimarisha umoja wa wakristu tunahitaji kuvumiliana na kupendana. MUNGU NI HAKIMU MWENYE HAKI.

SIFA YA MWANAKONDOO NI KUWA SADAKA YA UPATANISHO

Katika jamii nyingi za kiafrika kondoo hutumiwa katika kupatanisha watu. Nabii Isaya 11: 1-9 alitabiri ufalme wa amani utakaoletwa na Yesu ambaye ni mwanakondoo wa Mungu. “Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwanakondoo, chui watapumzika pamoja na mwanambuzi. Ndama na wanasimba watakuja pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.” (Isaya 11:6) Ili kupatana lazima tuangalie yale yanayotuunganisha. Mwanamke mmoja na Bwana wake walifarakana. Waliamua kutengana. Wakawa wanaishi sehemu zilizokuwa mbali. Siku moja mwanaume alirudi kwenye hilo jiji akiwa katika shughuli zake. Akaamua kwenda kwenye makaburi kutembelea kaburi la mtoto wake. Akiwa amesimama kwenye kaburi hilo alisikia hatua za mtu anayetembea au mtitimo wa miguu ya mtembeaji. Aliogeuka alimuona mke wake waliyetengana. Wote walikuwa na hamu ya kutembelea kaburi. Badala ya kupeana migongo waligeuka na kukumbatiana. Walipatana. Walipatanishwa na kifo cha mtoto wao. Tuangalie yale yanayotupatanisha na sio yanayotutenga. Tusisitize yanayotupatanisha na sio yanayotutenga.

Naomba umtazame mwenzako machoni. Huyo uliyemtazama Yesu alimfia. Mwanakondoo wa Mungu alichinjwa kwa ajili yake. Huyo anayemtazama Mungu anamfahamu kwa jina. Mwanakondoo wa Mungu yupo tayari kuondoa dhambi zake. Huyo anayemtazama ni mtu. Huyu anayemtazama ana thamani kubwa kiasi cha Yesu kumfia. Huyo unayemtazama sio takataka. Mungu haumbi takataka Yesu amemwaga damu kwa ajili yake. Huyu unayemtazama sio mtumba. Mungu haumbi mtumba. Yesu Mwanakondoo hakuchinjwa kwa ajili ya mtumba. Huyu unayemtazama sio kivuli au photocopy. Mungu haumbi vivuli au photocopy Mungu anaumba watu. Huyo unayemtazama ni Yesu. Huyo ni binadamu. Huyo ni zaidi ya Mkenya ni binadamu. Ni mwana Adamu. Ni mwana wa Mungu. Mkatoliki ni zaidi ya Mkatoliki ni mwana wa Mungu. Mwanglikani ni zaidi ya Mwanglikani ni mwana wa Mungu. Huyo uliyemtazama na huyo ambaye nabii anamzungumzia katika kitabu cha Isaya, “Mwenyezi-Mungu, ambaye aliniita tangu tumboni mwa mama ili nipate kuwa mtumishi wake.” (Isaya 49:5)

SIFA YA MWANAMBUZI WA WATU NI KUBEBESHWA LAWAMA

Wayahudi walikuwa na desturi ya kufanya toba kwa Mungu. Siku ya kufanya toba walimutwisha mbuzi mmoja makosa yao yote na dhambi zao zote na kumfukuzia mbali na kumnyoshea mbuzi huyo kidole kuwa makosa sasa yote ni yako. Tabia ya kuwalaumu wengine inalinganishwa na kumnyoshea mbuzi kidole (scapegoat complex). Huko India watu walijaza mtumbwi makosa ya watu kiishara na kuweka mtumbwi huo katika mto Ganges . Namna hiyo watu walitumaini kutakaswa dhambi zao.

 

“Akiishamaliza kufanya malipizi ya patakatifu, ya hema ya kukutania, na ya altare, atamleta yule beberu aliye mzima. Haruni atamwekea mikono yote miwili juu ya kichwa chake, na kuungama juu yake makosa yote ya wana wa Israeli, maovu yao yote, na dhambi zao zote. Akiisha kuyaweka hivyo  juu ya kichwa cha huyo beberu, atampeleka jangwani kwa mkono wa mtu mmoja aliye hapo tayari, na huyo beberu atajichukulia makosa yao yote mpaka huko mahali palipo jangwa. Atamwachia mbuzi jangwani” (Mambo ya Walawi 16: 20 -22).

Tabia ya namna hiyo inajitokeza katika familia. Unakuta kuna mtu katika familia ambaye anatwishwa makosa ambayo hakuyatenda. Glasi ikivunjika, ndugu wakigombana, fedha ikiota mbawa kama ndege na kuruka na kupotea, pakiwepo na mafuriko ya madeni yeye anasingiziwa kuwa ndiye chanzo cha matatizo. Katika hali mbaya ya uchumi dunia nzima kuna watu ambao wanaweza kuwalaumu wengine kuwa wanawaroga ndio maana biashara yao imekwama. Katika sehemu zenye ukame kijiografia ndiko kuna hadithi za wachawi wa mvua. Watu wanadiriki kuwalaumu wengine kuwa wanaroga mvua isinyeshe. Mtu msafi anapochafua hewa watu humlalamikia mtu mchafu kati yao . Ni methali ya Yoruba. Ni mchezo ule ule wa Adamu na Eva wa kulalamikia nyoka na mazingira.

 

Ukweli ungawa unauma lazima kukubali ukweli ulivyo na kurekebisha palipo na kasoro zilizo ndani ya uwezo wetu kurekebisha. Ukweli unatutaka tuwajibike kwa makosa yetu, tuwajibike kwa maamuzi yetu na tubebe misalaba yetu badala ya kuwatwisha wengine misalaba yetu. Badala ya kuwalaumu wengine tuwakomboe wengine. Hakuna ambaye anapika nyama iliyooza na kuitia kwenye mdomo wa rafiki yake na kusema mdomo wako unanuka.

Watu wakishatenda dhambi na kufanya makosa wanatafuta “mwanambuzi” wa kubebesha lawama badala ya kuungama. Wanatafuta mchawi ni nani? “Utafutaji wa mbuzi anayebebeshwa dhambi ni safari rahisi kati ya safari zote za uwindaji,” alisema  Dwight D. Eisenhower.

Lazima tumlaumu mwizi kwanza kabla ya kumwambia mwenye mali kuwa mali yake aliitunza vibaya. Ni methali ya Nigeria . Samaki wengi hula watu lakini ni nyangumi tu anayelaumiwa. Ni methali ya Jamaica . Methali hizo zinahusu lawama na kuwanyoshea wengine kidole. Nyani haoni kundu lake. Ni methali ya Kiswahili. Nyani haoni makalio yake. Methali hii inamaanisha kuwa mtu yuko tayari  kuona makosa yaw engine na hata kuwalaumu lakini haoni makosa yake. Yuko tayari kuona kipande kidogo cha mchanga kwenye jicho la mwenzake lakini haoni jiwe kubwa katika jicho lake. Mwafunzi ambaye alikuwa anakuwa wa kwanza miaka mingi darasani alipokuwa wa pili kwenye mtihani wa kufunga mwaka aliulizwa na mwalimu wake kwa nini amekuwa wa pili alisema kuwa hata watu mashuhuri wamekuwa wa pili. Mwalimu alitaka mwanafunzi atoe mfano. Mwanafunzi alisema, "George Washington alikuwa Rais wa kwanza wa Amerika, alikuwa wa kwanza katika vita, wa kwanza katika kuleta amani, wa kwanza kuchukua nafasi kubwa katika mioyo ya Waamerika lakini alioa mjane, katika hilo alikuwa wa pili." Mwanafunzi hakutoa sababu zake zinazomhusu ambazo zilimfanya arudi nyuma.

 

 

 

SIFA YA MWANAMBUZI WA WATU NI KUSINGIZIWA

Mtu mmoja alikua karamuni na wakwezake pamoja na mkewe na rafikize wakati wa chakula yulemtu akaweka pilipili nyingi kwenye chakula chake kwaajili ya tamaa alipo kula ghafla akaaza kuwashwa akatulia kimya akisikilizia maumivu mara machozi yakaanza  kumtiririka machonig,baba mkwe akamuliza unalia nini akamjibu natafakari wema wa mungu namatendo yake yaajabu ,mkewe na wote walio kuako karamuni walimsifu sana kuaameguswa  ,laki kwakua yule bwana na mkewe walikua wana kula katika saani moja mkewe naye akanaza kutokwa machozi mama yake akamsifia binti yake kua nayeamjua mungu lakini binti akasema chakula kina pilipili nyingi,sasa watu wote walitambua kilichokua kina mliza yule bwana kua nipilipili  akapatwa naaibukubwa sana.Fundisho tukubali matokeo ya makosa yetu wala tusimsingizie  mtu wala mungu.mungu haonekani bali yeye anatuona sisi.  

  Katika masuala ya maadili kuna ambao wanasingizia wazazi hao kwa kushindwa wao kuishi ipasavyo. Mlevi anaweza kumsingizia mjomba wake na kusema nimemfanana na mjomba wangu yeye alikuwa akilewa chakali kila siku.  

 HITIMISHO

 ILI MWANAKONDOO WA MUNGU ATUJALIE AMANI TUFANYE NINI?

Gari likigongana na gari lingine gari linapelekwa kwenye gereji au karakana. Mkristu akigongana na Shetani anaenda kwa Yesu. Tufanye nini?  Kwanza: Usilipe uovu kwa uovu: uwe mkweli kwa nafsi yako.Usipokuwa mkweli kwa nafsi yako hauwezi kujua. Mara unasikia mtu analalamika. Wananionea. Hasemi yeye amewatendea kosa lipi. Amenipiga. Hasemi kwa nini amepigwa.Tuwe wakweli kwa nafsi zetu.  Pili: Tutakieni amani. “Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi” (1 Wakorintho 1: 3). Tatu: Kuwa na shukrani katika kila hali

 

 

Counter

You are visitor since April'08