Saturday, February 22, 2014

KISASI KILICHO BORA NI MSAMAHA


 
                                                           JUMAPILI YA 7 YA MWAKA A
1. Law 19: 1-2. 17-18
2. 1 Kor 3: 16-23
3. Mt. 5: 38-48
 
Mmesikia ya kuwa imenenwa, ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’ Mimi lakini nawaambieni, msibishane na mtu mbaya” (Mt 5: 38).

Mzee Joe alikuwa kufani kwenye kitanda cha mahuti. Kwa muda wa miaka mingi alikuwa hapatani na Bill, ambaye zamani alikuwa mmoja wa marafiki zake. Akitaka kunyosha mambo yake kabla ya kuaga dunia alimtuma Bill waongee na kumaliza mambo. Bill alipofika, Joe alimwambia kuwa anaogopa kwenda mbinguni akiwa na kinyongo naye. Kwa kusita na kwa kujikaza Joe aliomba msamaha kwa mambo aliyoyasema na kuyatenda. Alimwaakikishia Bill kuwa amemsamehe kwa makosa yote aliyomtendea. Mambo yote yalionekana kwenda vizuri mpaka hapo Bill alipojiandaa kuondoka. Alipokuwa anatoka chumbani, Joe alimuita, “Lakini kumbuka, nikipona, haya yote niliyosema hayana maana wala uzito.”

“Jicho kwa jicho” mtazamo huo  utawaacha watu wengi wakiwa vipofu. “Jino kwa jino” mtazamo huo utawaacha watu wengi wakiwa vibogoyo. Kisasi kilicho bora ni kusahau. Ndivyo isemavyo methali ya Kiswahili. Lakini kisasi kilicho bora zaidi ni kusamehe.  Na pia kisasi kilichobora zaidi ni kutokuwa kama yule aliyekufanyia jambo baya ili pasiwepo watu wabaya wawili, yeye aliyekufanyia ubaya na wewe unayeshindwa kujibu ubaya kwa wema. Nelson Mandela alikuwa na haya ya kusema juu ya kusamehe waliomtendea vibaya: “Nilivyotembea kutoka mlangoni nakuelekea lango ambalo likuwa natokea na kwenda kwenye uhuru wangu, nilijua kuwa kama nisingeacha ukali wangu na chuki nyuma yangu, ningeendelea kuwa gerezani.” Kusamehe ni kumfungua mfungwa utagundua mfungwa ni wewe. Kabla ya kusamehe unakuwa kwenye gereza la chuki na kulipiza kisasi. Kumbuka chuki umchoma anayeitunza. “Msamaha ni manukato ambayo ua huacha kwenye kisigino kilicholikanyaga,” alisema Mark Twain. Kutosamehe ni kurudi nyuma. Nakubaliana na Libba Bray aliyesema: “Hatuwezi kurudi nyuma. Tunaweza tu kwenda mbele.”

 

Msamaha ni Dawa Kutosamehe ni Sumu

“Kutosamehe ni kama kunywa dawa ya panya na kungoja ili panya afe,” alisema Anne Lamott. Naye Nelson Mandela alikuwa na mawazo hay ohayo aliposema: “Chuki ni kama kunywa sumu ukitumaini kuwa itawaua adui zako.” Kuomba msamaha na kukubali kupokea msamaha ni tiba. Karl Menninger, daktari bingwa wa magonjwa ya akili kama kichaa alisema kuwa kama angeweza kuwafanya wagonjwa kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili kuamini kuwa dhambi zao zimesamehewa, asilimia 75 ya wao wangetoka wamepona siku inayofuata.

Zawadi nzuri ya kumpa adui yako ni msamaha

Kabla hatujasamehe hatutulii. Kumsamehe mtu hakubadili yaliyopita bali kunabadili yajayo. Kunabadili mahusiano mabaya yanakuwa mazuri, kunabadili fikra hasi zinakuwa chanya. Kunatibu vidonda vya chuki. Kwa mtazamo huo, zawadi nzuri ya kumpa adui yako ni msamaha.  Mshangaze adui yako kwa kumpa zawadi ya msamaha. Zawadi hiyo itakumbukwa na kuzunguziwa vizazi hata vizazi. Ni zawadi ambayo Yesu aliwapa waliomtesa na kumtundika msalabani. Ni zawadi ambayo Stefano katika kitabu cha matendo ya mitume, aliwapa waliomua. Ni zawadi ambayo Papa Yohane Paulo II alimpa Ali Agca ambaye alimpiga risasi. Ni zawadi ambayo Josephina Bakhita wa Sudani aliwapa waliomuuza utumwani. Kuna umuhimu wa kusamehe, lakini kuna umuhimu wa kuwa tayari kupokea msamaha. Ishara ya kuwa mtu amepokea msamaha ni kutokurudia kosa. Zipo hatua nyingi katika za kupokea msamaha na kusamehe.

Kwanza anayepaswa kusamehewa lazima atambue kosa lake. Na kosa kubwa ni kutokutambua kosa. Pili kutubu na kuungama ni muhimu katika hatua za kupokea msamaha. Mtume Paulo anatuasa, “Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele na matusi. Acheni kila uovu! Mwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe nyinyi kwa njia ya Kristo” (Waefeso 4: 31-31).  Kuwa na hasira na uhasama, chuki, kelele na matusi ni kuamua kujiweka kwenye gereza la kujitakia. Kama kusamehe ni muujiza basi tuna uwezo wa kufanya huo muujiza. Msamaha si jambo la mzaha. Mwalimu aliwauliza wanafunzi wa darasa la kwanza, “Kabla ya kumpa mtu msamaha mtu anatakiwa kufanya nini?” Mwanafunzi akajibu, “Kwanza mtu afanye kosa.” Mwalimu alitegemea mwanafunzi ajibu, “Kwanza lazima atambue kosa lake.” Tunazungumzia msamaha katika mazingira ambapo kosa limetendeka.

Kwa kawaida ni vizuri kupasha moto chakula lakini si vizuri kupasha moto wa kumbukumbu ya mabaya uliyotendewa. Kama Nelson Madiba Mandeka angepasha moto kumbukumbu ya mabaya aliyotendewa hasingezungumzia kusameheana baada ya kukaa gerezani kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini na tano. Kusamehe ni tendo la kibinadamu, mbwa hawezi kutafakari juu ya kumsamehe mbwa mwenzake. Tendo la kusamehe ambalo ni la kibinadamu linainuliwa na kuwa la kimungu. Zipo faida nyingi za kusamehe. Kusamehe kunaleta amani ya moyoni. Kusamehe kunaleta mwanga katika maisha yetu.

Mungu sio Adui wa Adui Zako

Martin  Niemoller alitoka katika gereza la Hitler akisema, “Ilininchukua muda mrefu kujifunza kuwa Mungu sio adui wa adui zangu. Na sio adui  wa maadui zake.” Kama unapenda watu wakupende nawe uwapende. Injili ya leo inatutaka tuwapende adui zetu: “Mmesikia kwamba imenenwa, ‘umpende jirani yako, na umchukie adui yako.’ Mimi lakini nawaambieni, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowadhulumu…” (Mathayo 5:43-44).  Adui mpende. Ni methali ya Kiswahili. Usimchukie hasidi au adui yako. Adui zetu yafaa kuwachukulia makosa yao watutendeavyo. Huenda wakatubu na kuacha uovu wao. Tunaaswa na methali ya Kiswahili, Adui aangukapo mnyanyue. Ni methali nyingine ya Kiswahili kuhusu kumpenda adui na kumtendea mema. Ni ubinadamu kumsaidia adui yako akiwa na shida. “Tunapowachukia maadui wetu tunawapa uwezo juu yetu: uwezo juu ya usingizi wetu, hamu yetu ya chakula, shinikizo letu la damu, afya yetu na furaha yetu.” (Dale Carnegie) “Jinsi miti yote inavyojulikana kwa vivuli vyake, ndivyo hivyo watu wazuri wanajulikana kwa maadui wao.” (Methali ya Kichina).

Masharti ya msamaha

“Usiposamehe uhalifu unatenda uhalifu.” “Anayesamehe anapata ushindi.” “Anayesamehe anamaliza ugomvi.” “Hasiyejua kusamehe hasitegemee msamaha.” Hizo ni baadhi ya methali toka makabila mbalimbali katika Afrika. Msamaha una nafasi katika tamaduni za kiafrika. Kusamehe makosa ni tendo la huruma. Yesu alisisitiza sana hitaji la kuwasamehe wengine kama tunavyosoma katika Biblia “Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, ‘Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?’ Yesu akamjibu, ‘Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba.’” (Mathayo 18:21” Kusamehe mara sabini na saba kunamaanisha kusamehe kila mtu kila mara. Kunamaanisha kusamehe bila kikomo. Lakini kutoa msamaha na kusamehe kuna masharti yake.

Sharti la kusamehewa ni kusamehe. Katika sala ya Baba yetu (Mathayo 6: 9-13) ambayo ina maombi saba ni ombi moja lililo na masharti. “Utasamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukusea.” (Mathayo 6: 12) Maombi mengine kama “Utupe leo mkate wetu wa kila siku,” “Usitutie vishawishini,”  hayana masharti. Ukitaka Mungu akusamehe samehe wale waliokukosea. Samehe mtu mbaya aliyekukosea ili pasiwepo watu wabaya wawili: yule aliyekukosea na wewe ambaye hukutoa msamaha.

Sharti lingine la msamaha ni kuweka makosa katika kaburi la sahau. Samehe na sahau. Kuna baadhi ya watu ambao hupamba methali ifuatayo katika nyumba zao. “Kwangu uingie lakini kumbuka mabaya uliyonitendea.” Methali kama hiyo haionyeshi msamaha. Kila mmoja anabidi awe na “kaburi dogo,” la kuzika makosa ya wale waliomkusea. Kuna Mzee mmoja alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa kufani akichungulia kaburi. Alimuita mchungaji ampatanishe na jirani yake kusudi akifa Mungu awe tayari kumsamehe kwa vile naye anasamehe. Basi Mchungaji aliwapatanisha. Wakasameheana. Lakini jirani yake alipojiandaa kurudi nyumbani mgonjwa huyo katika kitanda cha mauti alisema, “Mapatano haya yana maana iwapo nitakufa, kama sitakufa usikanyage kwangu.” Mgonjwa huyu alikuwa hajasamehe. Alikuwa anatunza kinyongo.

Sharti lingine la msamaha ni kutokujiingiza katika kutenda maovu. Hakuna mahali popote katika ujumbe wa Biblia ambapo msamaha au huruma kama kiini chake humaanisha kujiigiiza katika kutenda maovu, kujiigiza katika kashfa, kutia wengine hasara au kutukana wengine. Katika hali yoyote ile kufanya malipizi kwa ajili ya maovu na kashfa, kufidia hasara na kufanya malipizi ya matukano ni masharti ya msamaha. 

Lakini katika maisha tunakuta vizuizi na vikwazo vya kutoa na kupokea msamaha. Kutokuwa tayari kutubu makosa na kubadilika ni kikwazo katika kupokea msamaha. Mtu anafanya kosa na hayuko tayari kubadili nia na kumgeukia Mungu. Kumsamehe mtu ambaye hayuko tayari kutubu ni kama kuchora picha kwenye maji. Kikwazo kingine ni moyo mgumu. Moyo mgumu ni moyo unaotunza chuki. Lakini chuki humchoma anayeitunza. Zaidi ya hayo, kukata tamaa, kukataa ukweli ulio wazi, visingizio, kuficha ukweli wa mambo, ni vikwazo na vizuizi katika kutoa na kupokea msamaha.  Lakini hatuna budi kutambua ukweli huu, kisasi kilicho bora ni kusamehe.  

Samehe na Sahau

“Naweza kusamehe, lakini siwezi kusahau” ni namna nyingine ya kusema “Siwezi kusamahe”, alisema Henry Ward Beecher. Bwana wetu Yesu Kristu alisamehe na kusahau. Jambo ambalo linamtofautisha shahidi wa kweli na shahidi bandia (wa uongo) ni moyo wa kusamehe. Sifa kubwa ya wafiadini na mashahidi ni moyo wa kusamehe. Mtakatifu Stefano alilia kwa sauti kubwa: “Bwana usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii” (Matendo 7:60). Katika kila msamaha kuna upendo. Kusamahe ni kuchagua kupenda. Kusamehe ni chaguo bora. Neno la kwanza la Yesu msalabani ni neno la msamaha: Baba uwasamehe kwa vile hawajui watendalo.

 

Yesu hakulipa kisasi cha jicho kwa jicho au jino kwa jino. “Sheria ya zamani “jicho kwa jicho – inaacha kila mtu akiwa kipofu,” Martin Luther King anatukumbusha. Mtu akikosa na mwingine aliyetendewa vibaya akakataa kata kata kutoa msamaha panakuwepo na watu wabaya wawili. Kama mtu mbaya akikukosea msamehe, pasije pakawepo watu wawili wabaya. Methali ya kichina inaweka bayana ukweli huu, “Yeye anayetaka kulipa kisasi itambidi kuchimba kaburi mbili.” Kulipa kisasi ni kumkomoa mtu, lakini ni zaidi ya hapo ni kujikomoa, kwa sababu “Yule ambaye hawezi kuwasamehe wengine anaharibu daraja ambalo lazima avuke yeye mwenyewe; kwa sababu kila mtu anahitaji kusamehewa,” jambo hili aliliweka vizuri Thomas Fuller. Tendo la Yesu kusamehe waliomkosea ni changamoto kwetu.

Wasamehe Wanafamilia

Baba fulani alikuwa anamwambia siri mtoto wake. “Kila mara mama yako na mimi tunapokuwa na mabishano huwa nina neno la mwisho.” “Huwa unafanya nini?” aliuliza mtoto kwa mshangao, “Ni rahisi”, alitabasamu mzee, “Naomba msamaha”. Msamehe mama yako ambaye hataki uwe mtu mzima. Msamehe baba yako ambaye ni mlevi. Msamehe dada yako ambaye hakuheshimu. Msamehe mama mkwe mwenye wivu. Msamehe mke wako kwa usumbufu wake. Msamehe mzazi wako kwa kukusahau.

Wasamehe Marafiki Zako

“Ni rahisi kumsamehe adui kuliko kumsamehe rafiki yako,” alisema Austin Malley. Msamehe rafiki yako licha ya kasoro zake. Msamehe rafiki yako ambaye alikuacha ukiwa na upweke wakati wa shida. Msamehe rafiki yako ambaye hatimizi ahadi. Msamehe rafiki yako ambaye anajifanya kuwa hamjuani mbele ya watu.  Msamehe rafiki yako ambaye hakukutendea haki. “Kila mtu anapaswa kutunza kaburi la usawa wa kadiri, ambalo ndani ndimo atazika makosa ya rafiki zake,” alituasa Henry Ward Beecher.

 Ujisamehe Wewe Mwenyewe

Kama ambavyo hauwezi kuwapenda wengine kama hujipendi, hauwezi kuwasamehe wengine kama wewe mwenyewe hujisamehe. Ujisamehe kwa kutopokea ushauri na kwa kukosa la jiwe. Ujisamehe kwa kukosa ujasiri, ujisamehe kwa hofu isiyo na msingi. Ujisamehe kwa kukerwa na yale yasiyokuhusu. Ujisamehe kwa ya kwako kuyaweka chumbani na ya wengine sebuleni. Jisamehe kwa kutoona lako. Jisamehe kwa kubaki na labda. Jisamehe kwa kusherekea vita na kulilia amani.

Kwa Nini Yesu Aliomba Baba Awasamehe Wakati Yeye Angesamehe?

Mtakatifu Bernard analo jibu: “Alimwomba Baba, siyo kwa sababu yeye asingeweza kuwasamehe, bali ili atufundishe kuwaombea wanatukosea”. Mtawa huyo alizidi kusema: “Ee jambo la ajabu! Anapaza sauti, samehe; wanapaza sauti, msulubishe”. Hii ni changamoto kwetu. “Mtazame Mungu wako msalabani; ona anavyowaombea walimsulubisha; na halafu ukatae kumsamehe ndugu yako aliyekukosea! “Alitoa changamoto Mtakatifu Augustino.

 

 

 

Counter

You are visitor since April'08