Saturday, August 23, 2014

WATU WANASEMA NINI JUU YAKO?



                              

                                             JUMAPILI YA 21 YA MWAKA A
1.      Isaya 22: 19 – 23
2.      Warumi 11: 33 – 36
3.      Mathayo 16: 13 – 20



Aliwauliza wanafunzi wake, ‘Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?’ “Kristu aliwauliza swali hili wafuasi wake ili katika majibu yao tujifunze kuwa wakati huo kati ya wayahudi yalikuwepo maoni mbalimbali juu ya Kristo; na mwishowe tufanye utafiti watu wana maoni gani juu yetu; wakitusema vibaya tupuzie; wakitusema vizuri tujiongezee fursa hizo,” alisema Origen Baba wa Kanisa.


Uwezi kuwazuia ndege wa mateso wasiruke juu ya kichwa chako, lakini unaweza kuwazuia wasijenge viota kwenye nywele zako. Ni methali ya Kichina. Watu watakusema. Si rahisi kuzuia hilo. Kama unafanya mambo mazuri usiyumbishwe na wanayosema juu yako. Usikubali ndege wajenge viota kichwani mwako. Nakubaliana na Askofu Mkuu Desmond Tutu wa Afrika ya Kusini aliyesema: “Mungu amekuita akijua wewe ni nani. Anakutaka ulivyo wewe na upekee wako. Usikubali wengine wakubadili.”  Kuna aliyekuwa kwenye tamasha anasikiliza wimbo alikuwa na bwana mmoja wanazungumza. Akamwambia bwana huyo: “Mwanamama anayeimba hana sauti nzuri sijui ni mke wa nani?” Akajibiwa. Ni mke wangu. Bwana huyo akasema: “Nlitaka kusema aliyetunga wimbo huo alitunga wimbo mbaya sijui ni nani?” Bwana huyo alijibu: “Ni mimi.” Mfano huu unaonesha huwezi kuwazuia watu kusema.

Wakikusema vibaya tumia maneno wanayosema kama mawe ya kuvukia. “Mtu aliyefanikiwa ni yule ambaye anaweza kujenga msingi imara akitumia matofari waliomrushia,” alisema David Brinkley (1920 – 2003) mtangazaji wa habari wa Amerika.  Yatumie maneno wanayokusema kama mawe ya kuvukia. Stephen Arnold Douglas (1813 – 1861) mwanasiasa wa Amerika katika kampeini za kuwania urais wa Amerika mwaka 1858 katika mchuano mkali na Abraham Lincoln (1809 – 1865) aliwaambia wapiga kura kuwa wasimchague Abraham Lincoln kwa vile alikuwa na kilabu ya kuuza pombe kali. Naye Abraham Lincoln aliwaambia wapiga kura kuwa ni kweli na mteja wake mkubwa alikuwa Douglas, yeye aliacha shughuli ya kuuza pombe kali lakini Douglas hakuacha shughuli ya kuwa mteja. Abraham Lincoln aliyatumia maneno aliyorushiwa kama matofari ya kujengea msingi wa kukubalika kwa wapiga kura.

Katika maisha utasemwa. “Ili kukwepa kusemwa usiseme lolote, usifanye lolote, usiwe yeyote,” alisema Aristotle. Yesu alijua kuwa watu walimsema. Kuna siku alitaka kujua maoni ya watu juu yake: “Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, ‘Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?’ Wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.’ Yesu akawauliza, ‘Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?’ Simoni Petro akajibu, ‘Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.’ (Mathayo 16:13-16). Yesu hakuuliza mafarisayo na wanasheria wanasema mimi ni nani? Hakuuliza makuhani na walawi wanasemaje? Alitaka kujua watu wa kawaida wanasemaje. Mafarisayo na wanasheria walisema ni mlafi kwa vile anakula na kunywa na watoza ushuru. Mafarisayo na wanasheria walisema anatumtumia Beelzebub mkuu wa pepo wabaya.

Licha ya kusemwa hivyo Yesu alizidi kuimarika.  “Watu wanaotusema vibaya wanatuimarisha. Hofu zetu zinatufanya tuwe jasiri. Wanaotuchukia wanatufanya tuwe na busara. Adui wetu wanatufanya tusibweteke. Vikwazo vyetu vinatufanya tuwe na shauku. Tulivyovipoteza vinatutajirisha. Maudhi yetu yanatufanya tupandishwe hadhi. Hazina zetu zisizoonekana zinatupa amani inayojulikana. Lolote lililopangwa dhidi yetu litafanya kazi kwa ajili yetu,” alisema Israelmore Ayivor

Watu wanasema wewe ni mkristu wa aina gani. Kuna aina mbali mbali za wakristu. Kuna wakristu wanaoitwa: “Nguzo.” Hawa wanakuja Kanisani kila siku, nakutoa sadaka. Kuna wakristu wanaoitwa “Wachangiaji.” Hawa wanatoa pesa kama wanampenda mchungaji na mtunza pesa. Kuna wakristu wanaoitwa: “Waegemeaji.”  Hawa wanafanya kazi lakini hawatoi chochote. Kuna wakristu wanaoitwa: “Watu wa Kila mwaka.” Hawa wanakuja Krismasi na Pasaka. Kuna Wakristu wanaoitwa: “Watu wa pekee.” Hawa wanasaidia na kutoa kila mara. Kuna wakristu wanaoitwa: “Sponji.” Hawa wanachukua baraka zote na huduma lakini hawasaidii. Kuna wakristu wanaoitwa: “Watembezi.”  Hawa wanatoka Kanisa hili na kwenda Kanisa lingine na hawasaidii. Kuna wakristu wanaoitwa: “Wambea.”  Hawa wanawesengenya watu wote isipokuwa Yesu Kristu. Kuna wakristu wanaoitwa “Yatima.” Watoto wanatumwa Kanisa kuja kusali lakini wazazi hawaji kusali. Kuna wakristu wanaoitwa: “Wanafiki.” Hawa ni watu ambao wanasema hawaendi kanisani kwa sababu kanisani kuna wanafiki. Je, watu wanasema wewe ni nani?  

UTASEMWA TU
Huwezi kuwakataza ndege wasiruke juu ya kichwa chako. Wataruka tu. Ila wasijenge viota kichwani. Hauwezi kuwakataza watu wasiseme juu yako. Yesu alitetwa, alinung’unikiwa, alikataliwa, alinenwa. Kama alivoagua Nabii Simeoni “Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.” Yesu ni
ishara iliyopingwa na watu”. Mbele ya Kristu hakuna “Kutofungamana na upande wowote”. Kati ya mawili ni chaguo lako ama uko upande wake au kinyume chake. Yesu alipingwa, alibishiwa, alikuwa na wapinzani. Ukiwa wake kabisa siyo kusema umekingiwa kunung’unikiwa, au kutetwa. Yesu aliambiwa maneno ya matusi chungu nzima.
Mjinga: “Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema, ‘Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?” (Yn 7:15). Yesu hakuwa mjinga. Akiwa na umri wa miaka kumi na miwili aliketi katikati ya waalimu huko Yelusalemu. “Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake” (Lk 2:47).
MWENDAWAZIMU: Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?” (Yn 10:20). MLAFI NA MLEVI: “Akaja mwana wa mtu; yeye anakula na kunywa, mkasema “Mwangalieni huyu mlafi na mlevi, rafiki ya watoza ushuru na wenye
dhambi!” (Lk 7:34).
MCHAWI: Lakini Wafarisayo wakawa wanasema, “Anawatoa pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo wabaya” (Mt 9:34).
MWOVU: Pilato aliwaendea nje, akasema, “Mna mashtaka gani juu ya mtu huyu?” Wakamjibu, “Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako”. (Yn 18:29-30).
NABII WA UWONGO: Walimfunga kitambaa usoni, wakawa wanamwuliza, “Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!” (Lk 22:64).

Yesu alikutana na watu wenye majungu, uzushi na fitina. Tukumbuke hawajawahi kujenga mnara katika historia ya dunia ya kuwaenzi wazushi, na waongo. Watu walimsema Kristu sembuse wewe. Mtu akiwa mkarimu, wanasema anajitangaza. Asipokuwa mkarimu wanasema ana gundi kwenye vidole, ni mnyimi, ni bahili. Mtu akitoa hotuba fupi sana wanasema hakujiandaa. Akitoa hotuba ndefu wanasema hatunzi muda. Akiwa mtoto mchanga wanasema ni malaika. Akiwa mtu mzima wanasema achana na yule shetani. Akiwa mcha Mungu wanasema ni mkatoliki zaidi ya Papa. Asipokuwa mcha Mungu wanasema shetani amemweka mfukoni. Akiaga dunia katika uri wa ujana wanasema angefanya mengi mazuri. Akifariki umri wa uzeeni wanasema miaka yake aliiharibu tu bila kufanya chochote. Watu watakusema tu. Miaka mitatu ya utume wa Yesu kwa Bikira Maria ilikuwa ni miaka ya majonzi, miaka ya masikitiko. Alishuhudia kutanda kwa wingu la wivu dhidi ya mwanawe, mlima wa matusi kwa mwanawe, mafuriko ya chuki dhidi ya mwanawe. Yote yaliutonesha moyo wake, yote yaliuchoma moyo wake. Binadamu si pesa ambayo hupendwa na kila mtu. Yesu Kristu hakupendwa na kila mtu. Naye hakuwa bendera ya kufuata upepo wa maneno ya watu. Alikuwa na msimamo. Huwezi ukampendeza na kumridhisha kila mtu. Baba mmoja na mtoto wake wa kiume walimpeleka punda Sokoni. Baba huyo alikaa juu ya mnyama na mtoto alitembea. Watu waliokutana nao njiani walilalamika, “Ni jambo baya sana: Pande la mtu, limekaa mgongoni mwa punda wakati mtoto mdogo anatembea”. Kusikia hivyo baba huyo alitelemka toka mgongo wa punda mtoto alichua nafasi yake. Watazamaji walitoa maoni yao. “Ni jambo baya sana: mzee anatembea, na mtoto amekaa”. Kusikia hivyo wote
wakawa wamempanda punda - wakawasikia wengine wakisema, “Ni ukatili ulioje: watu wawili wamekaa juu ya punda”. Kusikia hivyo wote walitelemka. Lakini watazamaji wengine waliotoa maoni, “Ni ujinga ulioje: punda hana kitu chochote mgongoni na watu wawili wanatembea”. Mwishowe, wote wawili walimbeba punda na hawakufika sokoni.
Yesu hakuyumbishwa na maneno ya watu kama mzee huyo na mtoto wake.

Watu hawapigi teke mbwa aliyekufa bali aliye hai. Watu hawautupii mawe mwembe usio na matunda. Ukiwa na “matunda” watu watakutupia mawe ya maneno ya kukukatisha tamaa.
Vumilia. Mvumilivu hula mbivu. Mama hupenda mtoto wake acheze ashangiliwe badala ya kuzomewa. Yesu alitukanwa. Matusi hayo ni Upanga uliochoma moyo wa Maria. Lakini alivumilia. Usiogope upinzani, kumbuka tiara huruka angani dhidi ya upepo na
si pamoja na upepo.


MABABA WAKANISA WASEMAVYO
Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi: “Anaongeza ‘Filipi’ ili kutofautisha na pande nyingine za Kaisarea kama Strato na anauliza swali hili akiwa Filipi. Hapa palikuwa mbali na wayahudi ili kuwaondoa wafuasi wake hofu zozote ili waongee kwa uhuru lilikokuwa kwenye akili zao. Filipi alikuwa ndugu wa Herod…ambaye alilipa jina mji la Kaiseria kwa heshima ya Kaiseria Tiberias,” alisema Mtakatifu Yohane Krisostomu. Watu wataongea mengi juu yako wakiwa huru, wakiwa mbali.

aliwauliza wanafunzi wake, ‘Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?’ “Kristu aliwauliza swali hili wafuasi wake ili katika majibu yao tujifunze kuwa wakati huo kati ya wayahudi yalikuwepo maoni mbalimbali juu ya Kristo; na mwishowe tufanye utafiti watu wana maoni gani juu yetu; wakitusema vibaya tupuzie; wakitusema vizuri tujiongezee fursa hizo,” alisema Origen.

Wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.’ “Ilikuwa rahisi kwa umati kukosea kwa kumfikiri a Yesu kuwa ni Eliya na Yeremia kama Herod alivyomfikiria kuwa ni Yohane Mbatizaji; nashangaa baadhi ya wahakiki wangejaribu kutafuta sababu ya makosa haya,” alisema Jerome.   

Yesu akawauliza, ‘Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?’ “Wafuasi baada ya kutoa maoni ya watu wa kawaida Yesu anawakaribisha wafikiria mawazo ya juu zaidi kumhusu yeye na hivyo linafuata swali ‘Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?’ Nyinyi ambao mmekuwa pamoja name kila mara na mmeona miujiza mikubwa zaidi ya watu wengi, hampaswi kukubaliana na maoni hayo. Kwa sababu hiyo hakuwauliza swali hilo alipoanza kuhubiri lakini baada ya kufanya miujiza mingi,” alisema Mtakatifu Yohane Krisostomu.

Simoni Petro akajibu, ‘Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.’ (Mathayo 16:13-16). “Anamuita ‘Mungu aliye hai,’ ukilinganisha na miungu wale wanaoheshimiwa lakini wamekufa; kama Saturn, Jupiter, Venus, Hercules na miungu wengine,” alisema Jerome. Yesu ni Mungu aliye hai.

Saturday, August 9, 2014

MAWIMBI KATIKA BAHARI YA MAISHA



                           
                                       Jumapili ya 19 ya Mwaka A
  1. 1 Wafalme 19:9, 11-13
  1. Warumi  9:1-5
  1. Mathayo 14:22-33

Kumbuka kuwa bahari shwari haitoi wanamaji stadi. Matatizo kama mawimbi yanaweza kukuimarisha. Hivyo usipoteze wakati wako kupambana na ukuta ukifikiri utageuka kuwa mlango! Kuwa na mtazamo hasi dhidi ya matatizo ni kama kupambana na ukuta. “Wavuvi wanajua kuwa bahari ni hatari na ina dhoruba ya kuogopesha, lakini hawajawahi kuona hatari hizi kama sababu tosha za kubaki kandokando ya bahari au ufukweni,” alisema Vincent van Goth. Wavuvi hujitosa kwenye maji marefu. Wavuvi ni mfano wa kuigwa tunapokumbana na mawimbi ya matatizo katika bahari ya maisha. Kuna mtu aliyemwambia mvuvi hivi: wewe hauogopi kwenda baharini kuvua samaki. Mjomba wako, kaka yako, babu yako wote walikufa maji kwa nini hauogopi? Mvuvi alijibu hivi: watu wengi hufa wakiwa vitandani lakini watu hawaachi kulala vitandani. “Kuna mambo ambayo unajifunza vizuri sana wakati kuna utulivu na mengine wakati kuna dhoruba,” alisema Willa Cather
Kwa Yesu kila mara mawingu hayakuwa bluu. Kuna wakati wingu lilikuwa jeusi likiashiria dhoruba ya matatizo. Alikataliwa na wasamaria katika kijiji cha Wasamaria. Kwa Ayubu mawingu hayakuwa kila mara ya bluu. Kuna wakati alifikiria kuwa kama hasingezaliwa. Katikati ya mawimbi ya matatizo Ayubu alizidi kuimarika. Ni kama jani la chai linapata nguvu ya kugeuza rangi ya maji likiwa kwenye maji moto. Ukiwa kwenye mawimbi ya matatizo kumbuka ukweli huu: Kwanza tuko salama kwenye mawimbi ya matatizo tukiwa na Mungu kuliko tukiwa pasipokuwa na mawimbi ya matatizo bila Mungu. Mungu anaweza kutuliza mawimbi au akayaacha mawimbi akamtuliza binadamu. Pili, maisha bila mawimbi ya matatizo na magumu yatafanya uwezekano wa mazuri kuwa ni ziro. Tatu, joto likizidi kutanuka kunazidi. Matatizo makubwa yanaweza kukufanya uwe mkubwa. Kuna methali isemayo: anayesema sijawahi kuliona jambo hili huwa si mkubwa kiumri. Nne ukiomba mvua inyeshe kuwa tayari kukanyaga matope. Tano jua kuwa mawimbi ya matatizo yanakujia ili kukuimarisha na wala sio kukudhoofisha.
                                                IMANI HABA
“Ewe mwenye imani haba mbona uliona shaka” (Mathayo 14:31)
Maisha ni kigeugeu. Mambo yalimgeuka mtume Petro. Petro alikuwa ni mtu aliyefanya maamuzi ya ghafla na ya haraka. Hakufikiri sana kabla ya kutenda. Jambo hili pengine ni busara ulikilinganisha na mtu ambaye anafikiri sana mwishowe hatendi lolote. Katika nafsi ya Petro kuna mchanganyiko wa mambo. Anatamani kuwa na Yesu. Pia anatamani kuonesha kuwa anaweza kutenda analolitenda Yesu: kutembea juu ya maji. Kuna upendo na majivuno kama ilivyo kwa kila mmoja wetu. Petro ana ujasiri na woga. Anaanza vizuri, anaona dhoruba na kuogopa. Anakosa imani.

Sababu kubwa ya kupotea kwa imani ya Petro ni kuwa macho yake, mawazo yake, moyo wake alivielekeza kwenye dhoruba badala ya Kristu. Alipomtazama Yesu Kristu imani ilipatikana akalia kwa sauti, “ Bwana, niokoe !” ( Mt 14; 30). Licha ya Petro kuwa na imani haba Yesu alimuokoa. “ Hapo, Yesu akanyosha mkono wake, akamshika … wakapanda mashuani, na upepo ukakoma”. ( Mt 14: 31-32). Nasi tunapambana na matatizo. Matatizo ya siku hizi ni kama: umasikini, makazi yasiyofaa, ukosefu wa kazi, magonjwa yasiyo na tiba, ukosefu wa riziki, uzinifu, uzazi kwa namna isiyo halali, ukatili na vita, ukabila- damu inakuwa nzito kuliko maji ya ubatizo. Wakati tunazama kwenye lindi la maji ya matatizo tumuombe Yesu atuokoe.

Katika kilele cha dhoruba Yesu alijitokeza. Katika kilele cha hatari, katika upeo wa wasiwasi Yesu alijitokeza. Anakuja wakati ambapo hategemewi kabisa. Mitume walifikiri ni mzuka wakauotea mbali. Yesu ni Mkombozi wakubariki. Ni Mkombozi tunayeweza kumkimbilia. Alifanya kile ambacho binadamu hawezi kufanya. Alitembea juu ya maji. Vile ambavyo hatuwezi kufanya tumuachie yeye. Wakati tunapozama kwenye bahari ya matatizo tulie kwa sauti: “Bwana utuokoe !”
Shibisha imani yako na mashaka yako utayakondesha. Imani ikiongezeka mashaka yanapungua na kinyume chake ni kweli. “Imani si kujaribu kuamini jambo bila ya kuzingatia ushahidi: imani ni kujaribu kufanya jambo bila kuzingatia matokeo,” alisema Sherwood Eddy.
“Wanashinda wale wanaoamini wanaweza,” alisema Virgil. Ni katika mtazamo huo Erasmus alisema, “Amini kuwa unacho na unakuwa nacho.” Swali kubwa hapa si kuwa una imani au hauna imani. Jambo la msingi ni imani katika nini na imani katika nani. Ili kufanikiwa na kushinda unahitaji kuwa na imani katika Mungu na kujiamini hata ikiwa imani ndogo au haba inatosha kukuondolea vikwazo, vihunzi na vizingiti. Tunasoma hivi katika biblia, mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii” (Luka 17: 5-6).
Kifungu cha Biblia hicho kinabainisha ukweli huu, imani kidogo yaweza kufanya mambo makubwa. Ni ukweli unaoendana na ujumbe wa methali ya Kiswahili, Kidogo kidogo kamba ukatika. Nguvu ya mbegu haitegemei ukubwa au udogo wake inategemea uhai uliofichwa katika mbegu hiyo. Kuna nguvu ambayo imefichwa ndani mwako. Kama ni hivyo unahitaji kujiamini kuwa utaweza kufanikiwa katika maisha. Kwa imani na kujiamini ndege imevumbuliwa. Kwa imani na kujiamini simu za mkononi zimegunduliwa. Kwa imani na kujiamini utalaamu wa kutengeneza runinga umefunuliwa.
Mitume walipoomba kuongezewa imani, Yesu hakusema nimewaongezea imani. Hakuahidi kuwaongezea imani. Ni kama aliwaambia anza na mlicho nacho, kidogo huvuta kikubwa, kidogo huzaa kikubwa, laini huzaa ngumu. Walikuwa kama mfanyabiashara asemaye nina pesa kidogo sana ngoja iwe nyingi ndipo nianze kufanya biashara. Je, itaongezekaje bila kuzalisha, kuuza na kununua? Walikuwa kama mkulima asemaye nina mbegu lakini hazitoshi nitalima nikiwa na mbegu za kutosha. Anza na ulicho nacho. Hawezi kusema sina pesa yote ya kujenga na kumalizia nyumba. Anza kujenga na pesa uliyo nayo. Ili kuwa na zaidi anza na ulicho nacho. Aliyenacho ataongezewa ndivyo  Bwana Yesu alivyofundisha.
Imani ni ufunguo wa mafanikio. Na sifa ya mtu anayefanikiwa ni kuwa ana imani. Imani kamili ndiyo kumtegemea Mungu na kumtumaini na kumtii. Tukiwa na imani kwa Mungu twaweza kusema, “Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa” (Waebrania 13:6). Hatuna budi kuwa na imani na uwezo Mungu aliotujalia yaani kujiamini. Kuna hadithi juu ya wakristu ambao walimuomba mchungaji wakati wa ibada wa Jumapili iliyokuwa inafuata waombe kupata mvua baada ya mvua kutonyesha kwa kipindi cha muda mrefu. Walishangaa siku hiyo ya maombi ya Jumapili mchungaji aliposema hayuko tayari kuomba kupata mvua maana watu hawaonyeshi imani kwa vile hawakwenda na miavuli ya kujikinga mvua. Imani lazima ionekane katika matendo. Ni Mungu nisaidie na wewe unaweka juhudi na maarifa. Henry Ford alisema, “Kama unaamini unaweza kufanya jambo fulani au hauamini kama unaweza kufanya jambo fulani, uko sawa.” Usipoamini kwamba jambo fulani linaweza kufanyika halitafanyika. Ukiamini litafanyika. Imani inafukuza mashaka kama mwanga hufukuzavyo giza. Mashaka yakibisha hodi mlangoni mwako itume imani ijibu mashaka. Sala yetu iwe kama ya kijana mmoja kwenye Biblia, “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu” (Marko 9: 24).
Yesu anaweza kunyamazisha mawimbi ya matatizo. Tunasoma hivi katika Biblia: “Ikatokea dhoruba kubwa na mawimbi yakapiga chombo, hata kikaanza kujaa maji. Naye Yesu alilala usingizi shetrini juu ya matandiko. Wakamwamsha na wakamwambia, “Mwalimu, huhangaiki tukiangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiamuru bahari, “Nyamaza! Tulia!” Upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa (Marko 4: 37-39). Tuwe pamoja na Yesu  alale kwetu tunaposafiri katika bahari ya maisha. Bahari, kama yalivyo maisha yote si lazima ituchachafye. Mambo yanaweza kuelea na kwenda kwa raha; ikiwa yanatugeukia basi Yesu hatakosa kutusaidia kwani tunaye karibu. “Yesu alinyamazisha bahari si kwa kutumia fimbo kama Musa, si kwa kutumia sala kama Elisha alipokuwa Jordan, na wala si kwa sanduku la agano kama Joshua, mwana wa Nun kwa sababu hizi wafuasi wake walifikiri kuwa Yesu ni Mungu kweli, lakini wakati alikuwa amelala walifikiri yeye ni binadamu tu,” alisema Theophil.
Dunia ni bahari yenye mawimbi inahitaji wanamaji stadi. Duniani kuna mengi sawasawa na bahari. Kuna papa na nyangumi tena wale wa hatari. Lakini ukweli unabaki: Bahari shwari haitoi wana maji stadi. Bahari iliyotulia haiwezi kuwatoa wanamaji hodari. Kuna methali ya Kiswahili isemayo: Bahari haishi zinge. Zinge ni machafuko ya mara kwa mara (mabadiliko ya ghafla). Bahari daima imo katika mabadiliko wala haitabiriki. Maisha kama vile bahari yamejawa na mema na maovu na yanapotujia sharti tuwe tayari kuyakabili. Huko Mkoa wa Kagera nchini Tanzania kuna mashindano ya kupatia mwaka mpya jina. Mshindi huwa anapewa zawadi. Kuna mwaka ulioitwa kwa lugha ya Ruhaya “Galaziwa enzii” maana yake: “Ataogelea mwanamaji stadi”. Nchi ilikuwa katika matatizo makubwa ya kiuchumi baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda miaka ya 1978 na 1979. Matatizo hayo ni kama mawimbi kwenye bahari. Kuvuka mwaka huo kulilinganishwa na kuvuka bahari na ni mwanamaji stadi alitegemewa kuvuka. Mfano huo unaipa nguvu falsafa hii: DUNIA NI BAHARI inahitaji wanamaji stadi.
Watoto wasipopata malezi mazuri familia inakuwa ni mtumbwi unaoyumbishwa na mawimbi. Watoto wanahitaji kueleweshwa. Mfano kuna mtoto aliyefungua chumba cha wazazi wake bila kubisha hodi. Baba akupenda jambo hilo. Akamwambia. “Kila unapotaka kufungua mlango wowote ule, lazima ubishe mlango kwa kusema, hodi hapa!” Siku moja baba huyo alimtuma mtoto akalete soda toka friji au jokufu . Baada ya kumgonja dakika kumi mtoto bila kurudi. Baba alienda kutazama kulikoni. Akamkuta mtoto anabisha kwenye mlango wa friji akisema. “Hodi hapa! Hodi hapa!” Biblia inasema, “NAYE YESU AKAENDELEA KUKUA KATIKA HEKIMA NA KIMO; AKAZIDI KUPENDWA NA MUNGU NA WATU” (LUKA 2: 52). Muombee mtoto wako azidi kukua katika hekima, azidi kupendwa na Mungu na watu.
Tunapozungumzia bahari kuwa na picha ya vurugu, machafuko, ghasia, fujo. Ni picha hiyo tunasoma kitabu cha Mwanzo: “Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia. Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji” (Mwanzo 1:1-2). Tunapozungumzia bahari kuwa na picha ya maharamia wa kisomalia wanaoteka meli baharini. Kuwa na picha ya meli ya maharamia. Tunapozungumza mambo ya maji kuwa na picha ya Kisiwa cha Migingo na vita vya maneno vinazunguka kisiwa hicho. Kuwa na picha ya kuzama kwa meli ya RMS Titanic. Usiku wa tarehe 14 Aprili 1912 meli hiyo ilikuwa ikitokea Uingereza na kuelekea jiji la New York ilipogonga mwamba wa barafu ilizama baadaye baada ya masaa 2 na dakika arobaini na tano usiku wa kuamkia tarehe 15 Aprili 1912. Watu walioaga dunia ni 1, 517. Waliokoka ni watu 706. Jumla ya watu walikuwa ni 2,223. Huko Tanzania mwaka 1996 meli ya MV BUKOBA ilizama katika ziwa Victoria watu zaidi ya 700 waliaga dunia.
 TUFANYE NINI ILI KUKABILIANA NA MAWIMBI YA MATATIZO KATIKA BAHARI
Yesu alikuwa na sehemu tatu za kutafuta usalama, sehemu tatu za kupumzika: kwenye mtumbwi, mlimani na jangwani. Alipokuwa amezungukwa na watu wengi sana na alipohitaji kupumzika alienda sehemu mojawapo. Tunahitaji kupumzika na Yesu. Lakini zaidi ya hayo tunahitaji yafuatayo:
1. KABILI MAWIMBI KWA UTULIVU BILA HOFU
Tukiona mawimbi tunakuwa na hofu, pengine hofu kubwa inatuingia ghafla. Hakuna kufikiri sawa sawa. Tunahangaika, tunakuwa na wasiwasi kama wafuasi wa Yesu kwenye mtumbwi. Watu wana namna mbalimbali za kujiliwaza. Siku moja baba mmoja kijana alikuwa anamsukuma mtoto wake ambaye alikuwa akilia kwenye kigari cha watoto. Aliendelea kusema, “Tulia Donald. Nyamaza sasa, Donald. Mambo yatakuwa shwari, Donald.” Mwanamke aliyekuwa akipita alimwambia baba huyo, “Unajua namna ya kumbembeleza mtoto ambaye analia kwa utulivu na pole pole.” Mwanamke huyo aliinama kwenye kigari na kuanza kusema “Unasumbuliwa na nini Donald.” Baba yake aliingilia kati haraka, “Hapana, hapana yeye ni Henry! Mimi ni Donald.!” Mama huyo akauliza, “Mbona ulikuwa ukimbembeleza aache kulia ukimwita Donald!” “ Nilikuwa ninajibembeleza mimi mwenye moyoni ninalia kama mtoto huyu!”
KABILI MAWIMBI YA MAWAZO MABAYA
KABILI MAWIMBI YA MAHUSIANO MABAYA
KABILI MAWIMBI YA KUSHINDWA
KABILI MAWIMBI YA MATARAJIO KUVUNJIKA
2. YESU NI JIBU: MWAMBIE AKUSHIKE MKONO
“Yesu alinyamazisha bahari si kwa kutumia fimbo kama Musa, si kwa kutumia sala kama Elisha alipokuwa Jordan, na wala si kwa sanduku la agano kama Joshua, mwana wa Nun kwa sababu hizi wafuasi wake walifikiri kuwa Yesu ni Mungu kweli, lakini wakati alikuwa amelala walifikiri yeye ni binadamu tu,” alisema Theophil.
3. MATATIZO MAKUBWA YANAHITAJI IMANI KUBWA
Nyakati za kujaribiwa imani ni nykati za kuimarisha imani. “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto” (1 Pet 1: 6-7).
4. JUA KUWA YANA MWISHO
Mateso, shida, matatizo yana mwisho. Mateso hayana kauli ya mwisho. Furaha ina kauli ya mwisho. Katika kitabu cha Ufunuo tunasoma hivi: “Kisha, nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuwako tena” (Ufunuo 21: 1). Bahari haikuwako tena. Mawimbi ya matatizo hayakuwako tena.
5. JIANDALIE SIKU MBAYA
“Umkumbuke Muumba wako siku za ujana wako kabla hazijaja siku mbaya wala haijakaribia miaka utakaposema: ‘Sina furaha katika vitu hivyo” (Mhubiri 12:1). Sasa ndio wakati wa kujenga msingi katika Mungu. Sasa ndio wakati wa kuanza ukurasa mpya na sura mpya. Sasa ndio wakati wa kujiwekea bonga pointi mbinguni. “Kwa hiyo, kila mtu anayesikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba” (Mathayo 7: 24-25).
6. KWEPA PICHA HASI FIKIRIA PICHA KUBWA NA PICHA CHANYA
Kwepa picha hasi ya mambo: kwa nini mimi tu nataabika, Mungu ananiadhibu. “ Maisha yangu yamekwisha kwa machozi; naam, miaka yangu kwa kulalamika. Nguvu zangu zimeniishia kwa kutaabika; hata mifupa yangu imekauka” (Zaburi 31: 10).
  






Saturday, August 2, 2014

SHUKRANI INATANGULIA MUUJIZA



                                     
                                             JUMAPILI YA 18 YA MWAKA A
1. Isaya 55: 1-3    
2.  Warumi 8: 35, 37 -39
3. Mathayo 14: 13-21

“…alitazama juu mbinguni (Mathayo 14:19)” . “ Alimshukuru Mungu (Yohane 6:11).”

Toa shukrani kwa jambo dogo na utapata makubwa,” ni methali ya kabila la Hausa Nigeria.  Asiyeshukuru hupewa mara moja.” Ni methali ya wahaya. Kusema kweli tukishukuru katika kila jambo Mungu atatufanyia miujiza. Shukuru kabla ya kula. Shukuru kabla ya kusafiri. Shukuru kabla ya kufanya mtihani. Shukuru kabla ya kutafuta mchumba. Shukuru kabla ya kutafuta kazi. Shukuru kabla ya kuanza kazi. Shukuru kabla ya kwenda Hospitalini. Na baadaye shukuru, yaani baada ya kula, baada ya kutoka Hospitalini kutaja machache. “shukrani kila mara hutangulia muujiza,” alisema Ann Voskamp. Kukumbuka kusema “asante” kunaongeza miujiza katika maisha yetu. Maneno mawili haya “asante sana,” ni maneno ya kimiujiza. “Shukrani ni utajiri. Malalamishi ni umaskini,” alisema Doris Day. Anton Dvorak, mwanamuziki mashuhuri wa Czeche alizoea kuandika kwenye ukurasa wa mwisho wa kila mswaada wake maneno haya: “Namshukuru Mungu! Nimeridhika na kazi hii!
Bwana wetu Yesu Kristu alipofanya muujiza wa kulisha watu zaidi ya elfu tano alipopewa samaki wawili na mikate mitano alitazama juu mbinguni (Mathayo 14:19). Alimshukuru Mungu (Yohane 6:11). Muujiza huu aliufanyia jangwani. Shukrani ilitangulia muujiza. Mtakatifu Yohane Chyrisostom alikuwa na haya ya kusema: “Wayahudi katika kuelezea muujiza walikuwa na msemo: ‘Je, aweza kutupa chakula jangwani’ (Zaburi 78: 19). Kwa sababu hii aliwaongoza kwenda jangwani, ili muujiza usiwe na chembe yoyote ya kudhaniwa vibaya na mtu asifikiri kuwa chakula kimeletwa toka mji wa karibu. Lakini hata kama mahali ni jangwa ni yeye anayelisha dunia; ingawa saa ilikuwa imepita yeye hayuko chini ya masaa. Ingawa Bwana mbele ya mitume aliponya wagonjwa, mitume hawakuwa wakamilifu kiasi cha kuweza kutambua ambacho angeweza kufanya kuhusu chakula. Wao walisema, ‘uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula” (Mathayo 14: 15).
Kuna hadithi ya Wayahudi juu ya nani wa kushukuru. Omba omba wawili walizoea kuomba misaada kwa mfalme kando kando ya barabara kwenye jiji kubwa. Walizoea kwenda kwenye ikulu ya mfalme, ambaye alihakikisha wanapewa msaada. Mojawapo wa omba omba alimshukuru mfalme kwa ukarimu wake, lakini mwingine alimshukuru Mungu kwa kumpa mfalme nguvu na njia za kusaidia watu wake. Hilo lilimhuhumiza mfalme alimwambia omba omba huyo: “Kwa nini ninapokuonesha ukarimu unamshukuru Mungu na sio mimi.” Maskini alimjibu: “Kama Mungu hasingekuwa mkarimu kwako, usingekuwa na chochote cha kunipa.” Mfalme aliamua kumpa omba omba huyu fundisho. Alimwamuru mpishi wake kutengeneza mikate miwili na kuficha kwenye mkate mmoja madini yenye thamani sana na kuhakikisha maskini aliyekuwa anamshukuru mfalme na sio Mungu anapata mkate huo wenye madini. Mpishi alifanya hivyo.
Walipotoka kwa mfalme, njiani maskini aliyekuwa anamshukuru mfalme badala ya Mungu aligundua kuwa mkate wake ni mzito isivyo kawaida; kwake ilimaanisha uliokwa vibaya. Hivyo alimwomba mwenzake wabadilishane mikate. Walifanya hivyo na baada ya hapo kila mmoja akashika njia yake. Yule maskini ambaye kila mara alimshukuru Mungu alipoanza kula mkate alikuta madini yenye thamani sana kwenye mkate na alimshukuru Mungu kuwa sasa hataenda tena ikulu na kuomba msaada toka kwa mfalme.
Baada ya muda mfalme aligundua kuwa mmoja wa omba omba haji tena ikulu kuomba. Alimuuliza mpishi wake kama hakukosea katika kuwapa mikate ile na kuchanganya. Alikuwa na uhakika kuwa hakuchanganya hiyo mikate. Mfalme alimuuliza maskini ambaye aliendelea kuja kwake: “Ule mkate wangu usio wa kawaida uliopewa kipindi fulani uliuweka wapi?” Maskini alikiri kwa kusema kiukweli: “Mkate wangu ulikuwa mzito, hivyo nilifikiri uliokwa vibaya. Hivyo nilibadilishana na mwenzangu.” Mfalme alielewa kwa nini ombaomba mwingine alimshukuru Mungu. Tukumbuke kuwa utajiri wote na mali zote hutoka kwa Mungu. Mungu pekee anaweza kumfanya mtu maskini awe tajiri na tajiri awe maskini – bila kujali watu hata wafalme wanafikiria nini.”
Kumshukuru Mungu ni utangulizi wa muujiza. Muujiza katika hadithi ya wayahudi ni somo tosha juu ya kumshukuru Mungu. “Unapoamka asubuhi toa shukrani kwa ajili ya mwanga wa asubuhi, kwa ajili ya uhai wako na nguvu. Toa shukrani kwa ajili ya chakula chako na furaha ya kuishi. Kama hauoni sababu ya kushukuru, kosa liko kwako,” alisema Tecumseh (1768-1813). Wamebarikiwa wale ambao wanaweza kutoa bila kukumbuka na wale ambao wanaweza kupokea bila kusahau. Kutosahau kunamaanisha kuwa na shukrani.
Pale ulipoweka nukta Mungu anaweka alama ya mkato mambo mazuri yanakuja. Yeye akiamua kuweka nukta usiweke alama ya kushangaa.  Filipo aliweka nukta kwenye masuala ya kulisha wanaume elfu tano. Filipo mfuasi wa Yesu aliona kuna tatizo raslimali kidogo zisioweza kutosha kulisha wanaume elfu tano wanaojua kula chakula. “Filipo akamjibu, “Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, ili kila mmoja apate kidogo tu.” (Yohane 6: 7). Yesu anatwaa utajiri kutoka kwenye ufukara wa mtoto mwenye samaki wawili na mikate mitano . Anabadili  kidogo kinakuwa kikubwa. “Kuongezwa kwa mikate kunasimuliwa kikamilifu katika Injili zote nne. Muujiza huo una uhusiano wa moja kwa moja na Ekaristi.” Mfululizo wa vitenzi: Akaitwaa…akaibariki, akaimega, akawapa unadokeza Ekaristi. Kidogo unachoweka mikononi mwa Yesu atakibariki kiwe kingi. Neno kula katika Biblia limetumika mara elfu. Katika masimulizi ya Injili mara nyingi tunamuona Yesu anaenda kula au anatoka kula. Tunajifunza kuwa njaa ni tatizo. Ni tatizo la kiuchumi. Ni tatizo la kijamii. Ni tatizo la kidini pia. Linahitaji pia suluhisho la kidini. Lisilowezekana linawezekana.
MAMBO YA KUKATISHA TAMAA
Mazingira: Nyika Tupu
“Palikuwa na nyasi nyingi mahali  pale”  (Yohane 6: 10). Katika Injili ya Marko tunapata maelezo haya: “Mahali hapa ni pa ukiwa (Nyika tupu)” (Marko 6:35). Mahali pa ukiwa kuna njaa. Penye nyika tupu kuna njaa. Palipo na njaa ya upendo ni nyika tupu. Ofisini ukiwa na njaa ya upendo ni nyika tupu. Kwenye familia ukiwa na njaa ya upendo ni nyika tupu. Lakini katika maisha kuna ambao wanaona nyika tupu bila kuona raslimali zilizopo. Kuna Kampuni ya kutengeneza viatu iliyotuma watu wawili kwenda visiwani kuona uwezekano wa kuanzisha biashara ya kuuza vitua huko. Mmoja alipoona watu hawana viatu wanatembea peku peku, akatuma ujumbe kuwa ziandaliwe konteina tano huku watu wanahitaji viatu. Mwingine akatuma ujumbe kwenye makao makuu ya kampuni ya viatu kuwa visiwani watu wana utamaduni wa kutovaa viatu kwa hiyo wasiandae mzigo wowote wa kutuma visiwani.
Kupita kwa Wakati
“Mahali hapa ni ukiwa na saa imepita” (Mathayo 14: 15). Wakati ulikuwa umekwenda. Labda kuna jambo ulitegemea kupata muda unaona umepita. Ulitegemea kupata mme lakini saa imepita. Ulitegemea kupata kipato kizuri lakini saa imepita. Ulitegemea kwenda chuoni  lakini saa imepita. Kumbuka maneno haya: “Mawazo yangu si mawazo yenu” (Isaya  55: 8). Wakati wa Zechariah na  Elizabeth kuzaa ulikuwa umepita lakini Mungu akawafanyia muujiza wakampata mtoto Yohane Mbatizaji. Kupita kwa muda pengine ni suala la mtazamo. Kijana anapokalia stovu yenye moto dakika moja ni kama saa moja. Lakini msichana mrembo anapokaa karibu naye saa moja ni kama dakika.
Ukubwa wa Tatizo
“Yesu alipoinua macho na kuona umati mkubwa wa watu wanamjia, alimwambia Filipo, tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula?” (Yohane 6: 5). Watu walikuwa wengi wanaume wapata elfu tano bila kuhesabu watoto na wanawake. Watu walikuwa wengi. Tatizo lilikuwa kubwa. Mungu wetu ni mkubwa kuliko matatizo yetu. Ukiwa na tatizo usimwambie Mungu nina tatizo kubwa bali liambie tatizo Mungu wangu ni mkubwa. Unapopata tatizo kubwa kama Goliathi, unajibu vipi? Ni kubwa si rahisi kushambuliwa. Jibu kama Daudi. Ni mnene sana, siwezi nikalenga nikakosa. “Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya samba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa mfilisti huyu” ( 1 Sam 17:37).
Uchache wa Raslimali
“Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, “Yupo mtoto aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hii ni nini kwa watu wengi kama hawa?” (Yohane 6: 8). Mtu anaweza kusema hili haliwezekani kwa vile raslimali ni chache. Licha ya uchache wa raslimali Yesu alifanya muhujiza. Katika somo la kwanza tunaona uchache wa raslimali mikate ya shayiri ishirini (2 Wafalme 4: 42). Lakini Elisha akasisitiza, “Uwape watu, ili wale, kwa kuwa Bwana asema hivi: Watakula na kusaza.” (2 Wafalme 4: 42).
VIRUTUBISHO VYA KUTATUA MATATIZO
 Kama Kwamba Umepata
Yesu  akawaambia, Waketisheni  Watu” (Yohane 6: 10).  Yesu aliwataka watu wakae mkao wa kula chakula “kama kwamba” chakula kimeishapatikana. Muujiza wa kuongeza mikate ulikuwa haujafanyika lakini Yesu alitenda kama kwamba. Kuna wakristu katika parokia moja hapa Tanzania walimuomba padre Jumapili iliyokuwa inafuatia iwe siku ya kuomba kupata mvua. Wakristu hao walishangazwa na padre aliposema hayuko tayari kufanya maombi ya kuomba mvua kwa vile wakristu hawakwenda na miavuli ya kujikinga na mvua. Suala la kuwa na miavuli linadokeza maana ya “kama kwamba.” Yesu aliwambia wakoma kumi waende wajioneshe kwa makuhani kama kwamba wamepona. Bikira Maria aliwaambia watumishi: lolote atakalowambieni fanyeni “kama kwamba” Yesu amekubali.
Piga picha ya kile unachokitaka. Bila shaka Bwana Yesu Kristu alipiga picha ya muujiza, picha ya ongezeko la samali wawili na mikate mitatu.  Suala la kupiga picha ni muhimu ili ufanikiwe. “Akamleta (Abramu) nje akasema:Utazame mbinguni, uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu.Akamwambia: Ndivyo uzao wako utakavyokuwa” (Mwanzo 15:5). Mungu alisisitiza umuhimu wa kupiga picha.
Shukuru Usikufuru
“Yesu akaitwaa mikate, akashukuru” (Yohane 6: 11). Shukrani inabadili “hakitoshi” kuwa “kinatosha.” Shukrani inabadili kidogo kuwa kikubwa. Kushukuru ni kuomba tena.
Mshirikishe Yesu
Mipango bila kumshirikisha Yesu haina mafanikio ya kimihujiza. Filipo mwanahesabu hakumweka Yesu katika hesabu zake. Alisema dinari mia mbili kugawa kwa wanaume elfu tano haitoshi. Angesema dinari mia mbili  kujumlisha na Yesu na kugawa kwa wanaume elfu tano watoto na wanawake inatosha. Katika mipango yako mshirikishe Yesu. Katika hesabu zako mshirikishe Yesu.
Kidogo Kivute Kikubwa
Mungu wetu ni Mungu anayehitaji mchango wako. Mchango wa samaki wawili na mikate mitano ni kidogo kilichovuta kikubwa. Mungu anahitaji upige hatua ya kwanza. Katika hadithi za Kiyahudi ambazo hazikuandikwa katika Biblia kuna hadithi isemayo: Musa alipopiga maji yake na fimbo katika Bahari Nyekundu maji hayakugawanyika wana wa Israeli wapiti bali mtu wa kwanza ulitangulia na kuingia majini ndipo maji yakagawanyika. Piga hatua ya kwanza.
Tafakari maneno ya Mtakatifu Josemaria Escriva: “Omnia possibilia sunt credenti – yote yawezekana kwake yule anayesadiki. Hayo ni maneno ya Kristu. Vipi wewe huwezi kumwambia kama walivyosema mitume: adauge nobis fidem - utuongezee imani.” Nelson Mandela aliyekuwa mstari wa mbele kuleta uhuru wa walio wengi Afrika Kusini jambo ambalo lilionekana kama ndoto, alisema, “Kwa kawaida jambo linaweza kuonekana haliwezekani mpaka linapofanyika.” Ndani ya neno kisichowezekana kuna neno wezekana. Ndani ya neno lisilowezekana kuna neno wezekana.

                                                

Counter

You are visitor since April'08