Saturday, May 9, 2015

URAFIKI WA KWELI




                                                         Jumapili ya 6 ya Paska

1. Mdo 10: 25 – 26.34-35.44-48
2.  1 Yoh 4: 7-10
3.  Yn 15: 9 -17

 Utangulizi

Yesu alisema, “ninyi mu rafiki zangu.” “Urafiki wa kweli haupaswi kuficha kile unachofikiria” (Mt Jerome). Rafiki ni yule anayekuonya wewe kama Yesu. Urafiki ni ndoa ya roho. “Hakuna rafiki mwenye upendo mkubwa  zaidi kuliko yule aliye tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”

Nitajie rafiki yako, nami nitakwambia ulivyo. Huo ni msemo wa wataalamu wa saikolojia. Ndege wa bawa moja huruka pamoja. Marafiki wengi huwa na kitu kinachowaunganisha kama kupenda aina fulani ya mchezo kama mchezo wa mpira, mchezo wa ngumi. Pengine huwa wanaunganishwa na kupenda au kutenda mazuri au kutenda mabaya. Kuwa na marafiki sio hoja au sababu ya msingi maishani. Hoja je urafiki huo ni wa kujenga au kubumoa maana na majambazi wana marafiki zao majambazi. Urafiki wa kweli lazima uunganishwe na matendo mazuri. Mafanikio katika kuwa na marafiki si  suala tu la kuwapata marafiki wa kweli ni suala la wewe kuwa mwandani wa kweli , mwenzi wa kweli, rafiki wa kweli.

Urafiki wa kweli unazo sifa nyingi. Urafiki wa kweli una sifa ya upendo. Upendo ulio mkubwa na upendo uliokomaa. Bwana Yesu alibainisha sifa hii aliposema, “Hakuna rafiki mwenye upendo mkubwa  zaidi kuliko yule aliye tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yohane 15:13). Yeye aliwaita binadamu rafiki zake na akawa tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya watu, akawaonyesha namna ya kuishi vyema: Hakuna Paska bila Ijumaa Kuu, yaani mtaka cha uvunguni sharti ainame. Baada ya dhiki faraja.

Upendo wa marafiki ni vazi linalovutia upendo huo ukiwa ni upendo uliokomaa. Upendo uliokomaa upo katika misingi hii: unamhitaji mtu kwa sababu unampenda. Unapendwa kwa sababu unapenda. Unamhitaji mtu akusaidie sababu unampenda sio sababu unamhitaji. Huo ndio upendo uliokomaa. Lakini kuna binadamu wanaopenda mali na kutumia watu bila kuwa na upendo wa kweli kwao. Bali wanawahitaji tu. Huo sio upendo uliokomaa. Upendo ambao haujakomaa upo katika mtazamo potofu: Unampenda mtu sababu unamhitaji. Ukiwa na shida ndipo unampenda mtu atakayeweza kukusaidia. Huo ni upendo wa kitoto ambao haujakomaa.

Marafiki wa kweli ni watu ambao wanajua mapungufu yako, lakini hujivunia sifa zako nzuri. Marafiki wa kweli ni wale wanaokufahamu vizuri kama nyuma ya viganja vyao lakini bado wanakupenda. Katika msingi huu kuna msemo wa kiswahili usemao, “ mhesabu visa pendo haliwezi.” Rafiki wa kweli haweki kumbukumbu ya makosa. Usichotaka kutendewa usimtendee mwenzako. Rafiki wa kweli ni yule anayekupenda licha ya kasoro zako na anakusaidia kurekebisha kasoro hizo. Zaidi ya hayo, marafiki wa kweli ni watu ambao hawawezi kusema lolote nyuma ya mgongo wako ambalo hawawezi kusema mbele yako.Watu ambao wameshiriki pamoja nawe katika furaha na karaha. Watu ambao wamekuimarisha wakati wa shida. Akufaaye katika dhiki au shida ndiye rafiki wa kweli.

Sifa ya pili ya urafiki wa kweli ni kusameheana. Alikuwa ni Henry Ward Beecher aliyetuandikia maneno ya hekima kuhusu marafiki kusameheana: “Kila mtu anapaswa kutunza kaburi la usawa  wa kadiri ambalo ndanimo atazika makosa ya rafiki zake” Kusamehe ni sharti kubwa la kusamehewa. Wakristu wanajua hilo maana katika sala ambayo huwa wanaisali kila siku na imeandikwa katika Biblia wanasema, “Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasemehe waliotukosea.” Tunahitaji kujenga utamaduni na siasa za kusameheana katika Afrika ila bara la Afrika lisonge mbele hasa wakati huu ambapo limefunikwa na vita huko Darful, mizozo ya kisiasa huko Zaire, kunyosheana kidole huko Zimbabwe kati ya chama tawala na vyama vya upinzani maana hata katika siasa hatuna budi kuwa na marafiki wa kweli ingawa tumezoea kusikia kuwa katika siasa hakuna rafiki wa kudumu na adui wa kudumu. Lakini tunaweza kuwa na marafiki wa kudumu tukizingatia sifa za urafiki wa kweli ambazo ni upendo uliokomaa, kusameheana, kuheshimiana, mawasiliano na maneno matamu yaliyo ya kweli.

Mawasiliano na maneno matamu vinaendana katika kudumisha urafiki. Mawasiliano ni muhimu. Magugu huziba njia ambayo haitumiki. Usipomtembelea rafiki yako na kuwasiliana ni kama kwamba magugu yataziba njia ambayo haitumiki.  Juu ya maneno matamu, Yoshua mwana wa Sira anatuasa, “ Maneno matamu yatamrudishia mtu rafiki, na midomo yenye neema itamwongezea  wamsalimio (Ybs.6:5) Katika kutumia maneno matamu utakwepa kumhukumu rafiki yako mpaka umevaa viatu vyake. Yaani kujiweka katika nafasi yake na kujiuliza “Je kama angekuwa mimi ningefanyaje?”


URAFIKI WATAKA MOYO

Jiulize aina ya urafiki ulio nao. Je, huo ni urafiki ama utumwa? Urafiki ambao kwa miezi nenda miezi rudi ni kupokea ujumbe wa simu wa  tafadhali nipigie. Huenda urafiki wa namna hiyo ni utumwa. Urafiki wa kila mara niwekee pesa kwenye simu huenda ukawa utumwa. Kwa msingi huu urafiki wataka moyo. Urafiki wataka uvumilivu, umakini na busara. “Yataka moyo kuwa rafiki wa kweli. Inabidi kusamehe mengi, kusahau mengi, kuvumilia mengi,” alisema Anna Robertson Brown. Kuna watu wawili waliokuwa wanamjadili tajiri aliyefilisika. Mmoja akasema, “Tangia afilisike, nusu ya rafiki wake hawamtembeli tena, hawamjulii hali tena.” Mwingine akauliza habari juu ya nusu ya rafiki wake wengine. Mwenzake akamjibu: “Hawajui kama amefilisika.” Biblia yasema: “Kuna rafiki aliye mwenzi wa mezani, wala hatadumu karibu nawe siku ya taabu yako (Yoshua bin Sira 6:10). Rafiki katika taabu huyo ni rafiki wa kweli.
Kuna aina tatu za marafiki: marafiki kwa sababu fulani, marafiki wa msimu na marafiki wa daima. Marafiki kwa sababu fulani ni wale ambao wana lengo fulani. Labda wanataka kusaidiwa kupata kazi. Kazi ikipatikana urafiki unawekwa kwenye kaburi la sahau. Kuna marafiki wa msimu ambao labda wanajitokeza wakati wa kampeini kama wewe ni mwanasiasa, kuna ambao wanajitokeza wakati wa kuvuna kama wewe ni mkulima, kuna ambao wanajitokeza mwishoni mwa mwezi unapopata mshahara kama wewe ni mfanyakazi. Marafiki wazuri ni wale wa nyakati zote ikinyesha mvua wapo likiangaza jua wapo. Tunaweza kuwazungumzia kwa namna nyingine. Kuna makundi matatu ya marafiki: kuna ambao ni kama chakula, bila wao huwezi kuishi; wale ambao ni kama dawa, ambayo unahitaji mara chache; na ambao ni kama ugonjwa ambao hauhitaji.
Wenzi wa ndoa kama sio marafiki ndoa hiyo inaweza kuwa mashakani au kuwa kama wagonjwa kwenye chuma cha wagonjwa mahututi. “Sio ukosefu wa upendo, bali ukosefu wa urafiki unaofanya ndoa zisiwe na furaha,” alisema Friedrich Nietzsche. Unahitaji kuwa rafiki wa kweli. Rafiki wa kweli ni rafiki ambaye ni mwaminifu. “Rafiki mwaminifu ni hifadhi imara; aliyempata amepata hazina” (Yoshua bin Sira 6:14). Rafiki wa kweli anapewa sifa zifuatazo katika Biblia: hazina, hifadhi imara, dawa ya uzima na mwaminifu.
Jina lako liko salama mdomoni mwa rafiki wa kweli. “Watu wanapokupenda, namna wanavyotamka jina lako ni tofauti. Unajua jina lako liko salama midomoni mwao,” alieleza Jess C. Scott. Kwa kawaida kuna vitu au malengo yanayowaunganisha marafiki. Katika msingi mwanafalsafa wa Kigiriki Aristotle alisema: “Urafiki ni roho moja inayoishi katika miili miwili.”
Urafiki wataka moyo kwa vile unagharimu. Tafakari mazungumzo haya: “Nasikia rafiki yako Tamson ameoa tena. “ “Ndiyo ameoa. Amekuwa rafiki yangu mpendwa. Arusi zake zimenigharimu pesa. Ilibidi ninunue zawadi mara tatu. Kwa vile alifunga ndoa mara tatu baada ya kufiwa na wake zake mara mbili. Pia ilibidi kununua mashada ya maua mara mbili kuweka kaburini.” Urafiki unagharimu. Unaweza kupoteza urafiki hata katika kukopa. Kuna mtu aliyemwambia rafiki yake. “Brown alijitolea kunikopa.” Aliulizwa: “Je, ulichukua pesa toka kwake.” Jibu lilikuwa: “Hapana. Urafiki wetu ni mzuri sana sitaki kuupoteza kwa kukopa kopa baadaye kushindwa kurudisha.”


Swali linabaki kama urafiki wataka moyo unawezaje kujipatia rafiki wa kweli. Kitabu cha Yoshua bin Sira kinapendekeza njia tatu. Kwanza tumia maneno matamu. “Maneno matamu yanaongeza rafiki” (Yoshua bin Sira 6: 5). Pili, Umpate wakati wa shida au majaribu. Rafiki wakati wa shida ndiye rafiki wa kweli. “Ukijipatia rafiki, umpate katika majaribu” (Yoshua bin Sira 6: 7). Tatu, omba na kusali na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu atakupa rafiki wa kweli. “Nao wamchao Bwana watampata” (Yoshua bin Sira 6:16). Yote yakiisha semwa: urafiki wataka moyo. Urafiki wataka subira, uvumilivu, ukarimu, moyo wa kusamehe na kuwa makini.

Counter

You are visitor since April'08