Saturday, August 29, 2015

MOYONI UMEJAZA NINI?



                               

                                        Jumapili ya 22 ya Mwaka B

1. Kumb 4: 1-2, 6-8
2.  Yakobo 1: 17-18, 22, 27
3.  Mk 7: 1-8, 14-15, 21-23


“…Kwa maana kutoka ndani ya watu, kutoka mioyo yao, yanatoka mawazo mabaya; uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu, matusi, kiburi, upumbavu.Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi” (Marko 7: 15-23)

Mungu anapompima mtu, anaweka utepe kuzunguka moyo wake na si kichwa chake. Mwalimu wa shule ya wanafunzi wadogo wa elimu dini waliokuwa wakikutana Jumapili alikuwa akiwaambia watoto wadogo juu ya taji la utukufu na zawadi huko mbinguni kwa watu wema. Mwishoni mwa somo aliwauliza wanafunzi wa shule ya awali, “Nani atapata taji kubwa?” Palikuwepo na kimya, mtoto mmoja akainua mkono, “Mwenye kichwa kikubwa.” Tofauti na jibu hili Mungu haangalii ukubwa wa kichwa bali ukubwa wa moyo: moyo wenye upendo, ukarimu, mawazo safi, unyenyekevu.  “Kila mtu anaweza kupenda ua la waridi; lakini inahitaji moyo mkubwa kupenda jani,” alisema Askofu Fulton Sheen. Kila mtu anaweza kupenda chumvi lakini inahitaji moyo mkubwa kumpenda muuza chumvi. Kila mtu anaweza kupenda kinywaji kilichomo kwenye glasi, lakini inahitaji moyo mkubwa kuipenda glasi. Kila mtu anaweza kuchukia dhambi lakini inahitaji moyo mkubwa kumpenda mdhambi.

Kama hakuna adui ndani, adui wa nje hawawezi kukudhuru. Ni methali ya Kiafrika. Mawazo mabaya ni adui wa ndani. Wakiwemo moyoni adui wa nje anaweza kukudhuru. Yesu alitaja maadui kumi na wawili ambao wanaweza kuwa moyoni: “…Kwa maana kutoka ndani ya watu, kutoka mioyo yao, yanatoka mawazo mabaya; uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu, matusi, kiburi, upumbavu.Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi” (Marko 7: 15-23)

Mungu anatazama moyo na kuangalia moyoni. Tunapoimba Mungu hatazami midomo tu anatazama moyo. Tunapoimba Mungu hatazami kinanda tu anatazama moyo. Unapotoa sadaka Mungu hatazami pesa tu uliyotoa anatazama moyo. Kutoa ni moyo vidole huachia. Tunapomwabudu Mungu, Mungu anatazama moyo. Mtu anaposema nakupenda kwa moyo wote, hoja si kupenda kwa moyo wote hoja ni aina gani ya moyo. Watu wanapenda moyo unaojali. Watu hawajali unajua kiasi gani mpaka wanapojua unajali kiasi gani. Mioyo yetu ni kama sanduku tunatofautiana namna ya kujaza sanduku. Swali: moyoni umejaza nini? Wengine wanaweka mengi kwenye sanduku kama wanavyoweka mengi moyoni. Wengine wanaweka machache. Mwenyezi Mungu anaangalia moyoni:”…siangalii mambo kama wanavyoangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni” ( 1 Samueli 16: 7). Tunapozungumza maneno ni maelezo ya wazo. Kila mara unapoongea unachokifikiria na kinachokuwa moyoni kinakuwa kwenye gwaride watu wanaona.





Maneno yako ni madirisha ya moyo wako. Lililo moyoni ulimi huiba. “Kinywa hutaja yanayofurika moyoni” (Mathayo 12: 34). Ukisema, “asante” shukrani imefurika moyoni. Ukisema, “nakupenda” upendo umefurika moyoni. “Mtu mwema hutoa mema katika hazina njema ya moyo wake, na mtu mwovu hutoa maovu katika hazina mbovu ya moyo wake; kwa maana kutoka kinywa chake hunena yafurikayo moyoni” (Luka 6: 45).

Barua kutoka moyoni inawezwa kusomwa usoni. Ni methali ya Kiswahili. Uso wa mtu unaonesha kilichomo moyoni. Katika lugha ya kawaida tunatambua umuhimu wa moyo. Kuna mifano michache: Ana moyo mwepesi: ana huruma nyingi na mwepesi wa kumsamehe mtu aliyemkosea. Fulani ana moyo wa simba: ni shujaa; mjasiri mkubwa; haogopi kufanya jambo. Kipendacho moyo ni dawa (methali). Ana moyo mweupe: hana hila au nia mbaya. Suala la kupatana ni suala la moyo: “Moyo wa binadamu umeumba kupatanisha yanayokinzana,” alisema David Hume. Naye Harbert Hoover alikuwa na mawazo hayo aliposema: “Amani haifikiwi kwenye meza ya baraza au kwa mikataba, bali kwenye mioyo ya watu.”  Ni moyo unaopenda. “Moyo wa kupenda hausemeki.” Ni methali ya Kiswahili. Jicho halisau moyo ulichoona. Ni methali ya Kiafrika. Yote yakishasemwa wito ni moyoni jazeni mawazo mazuri.

MAWAZO YA UKARIMU, SADAKA NA HISANI: Moyo wa binadamu haupimwi kwa ukubwa wa pochi bali kwa ukubwa wa moyo wenyewe. Tunazungumzia moyo usiofungwa, ulio wazi. “Gereza baya sana litakuwa moyo uliofungwa,” alisema Mt. Yohane Paulo II.  Moyo uliojaa uchoyo ni moyo uliofungwa. Kilijochaa hufurika. Moyo ukijaa ukarimu, ukarimu utafurika. Moyo ukijaa mawazo ya sadaka, sadaka itafurika. Moyo ukijaa mawazo ya hisani, hisani itafurika. “Kuna tofauti kubwa sana kati ya zawadi na sadaka. Sadaka ni zawadi kujumlisha na upendo na kujumlisha na hulka ya mtoaji. Zawadi hutoka kwenye pochi; sadaka hutoka moyoni,” alisema Askofu Fulton Sheen. Kuna mtoto wa mitaani aliyekutana na Padre akamuuliza, “Padre gari lako ulinunua kwa shilingi ngapi?” Padre alijibu, “Sijui.” Mtoto akasema, “Unaendesha gari haujui bei yake.” Padre alimwelewesha mtoto, “Gari hili nilipewa na kaka yangu.” Mtoto alisema, “Ningekuwa na moyo kama kaka yako ningekununulia gari.” Hakusema, “Ningekuwa na ndugu kama huyo akaninunulia gari.” Mambo yote yanategemea moyo.Mtoto huyu wa mitaani alikuwa na moyo wa ukarimu. Kuna mtu aliyeenda kwa tajiri kuomba elfu tatu. Tajiri akampa elfu hamsini. Yule aliyeomba elfu tatu akashangaa na kusema, “Bwana Mkubwa, Chifu, Bosi! Mimi nimeomba elfu tatu wewe mbona umenipa hamsini.” Bwana huyo akasema, “Elfu tatu zinakutosha wewe kuomba lakini hazinitoshi mimi kutoa.”


MAWAZO SAFI, NIA SAFI, NDOTO SAFI
Hakimu wakati anahukumu kesi juu ya wizi. Alimuuliza mwizi: Je huwa hauoni aibu kuweka mkono kwenye mfuko wa mtu ili umwibie. Mwizi huyo alijibu: “Huwa nakuwa na aibu nisipokuta kitu chchote.” Moyoni mwa mwizi huyo yalijaa mawazo mabaya, mawazo ya wizi. Hayo si mawazo safi. Familia moja ilikuwa na mazoea ya kuwakaribisha wageni wakati wa Kumbukumbu za Kuzaliwa za Wanafamilia. Baba alimuomba mtoto wake wa miaka mitatu kuongoza sala kabla ya kula. Mtoto alisita. Baba alisema sema ambavyo mama huwa anasema siku kama hii: Mtoto alifanya ishara ya msalaba na kusema, “Mama huwa anasema, “Kwa nini tumewaalika watu wengi chakula hakitoshi.” Unaweza kujua mawazo ya mama huyo. Wazo lolote ambalo linaleta mwanga lifikirie. Wazo lolote ambalo ni wazo taka achana nalo. Wazo lolote ambalo ni wazo mgando achana nalo. Wazo lolote ambalo ni wazo giza achana nalo. “Ndugu, yaliyo kweli, matukufu, adili, yaliyo matakatifu, ya kupendeza nay a sifa njema, yote yanayohusiana na ukamilifu, tena masifu, hayo yafikirieni hasa” (Wafilipi 4:8). Mawazo ya upendo ni mawazo safi. “Palipo na upendo, hakuna giza (Methali ya Burundi). Mawazo ya kusaidia wengine ni mawazo safi. “Lengo letu la kwanza katika maisha haya ni kuwasaidia wengine. Kama huwezi kuwasaidia wengine usiwahumize,” alisema Dalailama.

Heri walio na moyo safi, maana hao watamowona Mungu” (Mathayo 5: 8).“Tunateka nyara kila fikra ipate kushuka na kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:5). “Ni nani atakayependa katika mlima wa Bwana?” Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, wala hakuapa kwa hila” (Zaburi 24 (23): 3-4).


MAWAZO YA UNYOFU, UAMINIFU NA UADILIFU
Kuna watu ambao hawawezi kusoma Biblia lakini wanaweza kusoma moyo wako. Kinachompendeza Mungu ni unyofu wa moyo. “Nawe wapendezwa na unyofu wa moyo; ndani ya moyo unanifundisha hekima” (Zaburi 51: 8). Mungu haangalii kwamba mtu amekujaribu na sketi fupi bali anaangali unyofu wako wa moyo. Mungu haangalii kwamba mtu aliacha pesa mezani zikakushawishi Mungu anaangalia unyofu wa moyo.

MAWAZO YA UCHESHI, UCHANGAMFU, FURAHA
“Moyo wenye furaha ni huduma nzuri sana tunayoweza kumpa Mungu,” alisema Marie Chaplain. “Moyo wenye furaha ni matokeo yasiyoepukika ya moyo unaowaka upendo,” alisema Mwenyeheri Mama Teresa wa Calcutta. Moyo unapodunda kwa ajili yaw engine unakuwa na furaha sana.

MASIFU, PONGEZI, SHUKRANI, MAPENDO
“Ujaze moyo wako wingi wa mapendo na shukrani, unapowaza jinsi kila siku neema ya Mungu inavyokuokoa katika mitego unayotegewa njiani na adui,” alisema Mt. Josemaria Escriva. Kipimo cha mtu sio ukubwa wa imani yake bali ukubwa wa upendo wake. Msichana mmoja alikuwa amempenda kijana mmoja mtanashati na mchaMungu. Malengo yao ilikuwa waje kuoana baada ya muda. Kijana alijitoa sana kwa binti huyu hadi wenzake wakamuona mjinga, lakini ukweli ni kuwa alimpenda msichana Yule kwa dhati. Alimtafutia kazi alipomaliza chuo, alimshauri kuhusu mipango ya maisha na alikua akimuombea kila alipopata nafasi ya kuomba. Siku moja binti alikua anasherehekea siku yake ya kuzaliwa…hivyo akaalika marafiki zake, na watu wengine muhimu akiwemo mpenzi wake. Wageni wote walifika kwa wakati isipokuwa yule kijana alichelewa kidogo…Hivyo msichana akatumia muda ule ambao mpenzi wake hajafika kuwaeleza wageni namna yule kijana alivyokuwa wa muhimu kwake. Akamsifia sana, akasema atamvalisha pete ya uchumba karibuni, na akasema siku hiyo ya Siku ya Kuzaliwa kwake anategemea zawadi kubwa sana kutoka kwa huyo mpenzi wa nafsi yake. Baadaye kijana akaingia na kuketi kwenye meza ya wageni wahemishimiwa. Muda wa zawadi ulipofika watu wakamtunza binti zawadi mbalimbali na kijana akawa wa mwisho. Hivyo wageni wote wakawa na hamu ya kutaka kujua zawadi aliyoleta hasa baada ya Yule msichana kumsifia sana kijana akaamka na kutoa mfuko…kila mtu akataka kujua kilichokua ndani ya mfuko…mara kijana akafungua mfuko na kutoa mkate! Lahula! Watu wote wakastaajabu na kusema, “Mkate?” Lakini kabla hajasema lolote kuhusu ule mkate, Yule msichana akaanza kulia..akapandwa hasira kwa kuwa mpenzi wake amemuaibisha! Akiwa analia kwa kwikwi, akamshika shati na kumvua tai yake, akamwagia juisi, kasha akauchukua ule mkate na kuutupa! Maskini Yule kijana akaukimbilia ule mkate na kuuokota. Kisha akarudi mezani na kusema, “Mtoto nakushukuru kwa yote..Huenda umenidharau kwa kuwa nimekuletea zawadi  hii ndogo kwenye siku yako muhimu kama hii. Lakini kama ungetambua thamani ya zawadi hii, usingefanya haya.” Kisha akafungua ule mkate na kutoa vitu viwili alivyovificha ndani ya mkate…Kwanza akatoa ufunguo wa gari, ambalo alikuwa amemnunulia mpenzi wake na alitaka amkabidhi siku hiyo ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa. Kisha akatoa pete ya uchumba na kusema “Nilimuomba Mungu anipe mwanamke atakayenipenda katika hali yoyote. Nilipanga leo nikuvalishe pete hii ili kuelekea ndoto yetu ya ndoa. Lakini kwa kuwa uliangalia nje, uliona mkate, badala ya pete hii ya thamani iliyokuwa ndani.Naamini mwanamke niliyemuomba kwa Mungu bado sijampata. Nashukuru kwa yote uliyonifanyia nimekusamehe, nawe naomba unisamehe kama nimekukwaza.” Kisha akachukua mkate wake, huyoo akaondoka. Msichana akaomba msamaha lakini alikuwa amechelewa. Fundisho usidharau kila mtu kwa kumtazama kwa nje. Mungu huangalia thamani ya kitu au mtu kwa ndani lakini wanadamu walio wengi huangalia nje. Wanaokudharau leo na kukuona mkate watagundua haukuwa mkate wa kawaida, kuna vingi vya thamani ndani mwako. Wote wanaokudharau leo, ipo siku watakusalimia kwa heshima.

Ujaze moyo wako masifu. Msichana huyo hakujaza moyo wake na masifu. “Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa  moyo, Mshukuruni Bwana kwa kinubi, kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Mwimbieni wimbo mpya, pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe” (Zaburi 33(32) 1: 1-3).


TUMUOMBE MUNGU ATUUMBIE MIOYO SAFI

Kuna mtu alikuwa anaulizia bei ya taulo. Mnunuzi: “ Taulo hiyo pale shilingi ngapi? Muuzaji: Laki mbili. Mnunuzi: Inasafisha hata dhambi! Muuzaji: kimya. Mnunuzi alishangaa bei ilikuwa juu. Taulo inaondoa maji haiondoi dhambi, inasafisha uchafu haisafishi makosa. Biblia inazungumzia hisopo inayosafisha. “Unisafishe kwa hisopo, nami nitakuwa safi; unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji” (Zaburi 51: 9). Hisopo ni mmea mdogo wenye vitawi vingi unaofaa kwa kunyunyuzia katika madhehebu ya kutakasa (Hesabu 19:18; Law 14;4; Rev 1: 9). Wahaya walikuwa na mimea ya kutumia kutakasa katika ibada za kitamaduni: orweza na orugoshora. Ni kama mmea wa hisopo. Sala yetu iwe kama ya mfalme Daudi alipotembelewa na nabii Nathani baada ya kutenda dhambi na Bathsheba: “Uniumbie moyo safi, ee Mungu; ufanye upya roho thabiti ndani yangu” (Zaburi 51: 12).



Thursday, August 13, 2015

MBINGU IANZIE DUNIANI




                  SHEREHE YA KUPALIZWA BIKIRA MARIA MBINGUNI
1.  1 Mambo ya Nyakati  15: 3-4, 15-16, 16: 1-2
2. 1 Kor 15: 54-57
3. Lk 11: 27-28

Leo tunasherehekea Sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria mbinguni. Alipalizwa hakupaa mbinguni. Ni Yesu alipaa mbinguni. Ukweli kuwa Bikira Maria alipazalizwa Mbinguni tunaupata katika Biblia kitabu cha Ufunuo, “Ishara kubwa ilionekana mbinguni, mwanamke amevikwa jua, mwezi ukiwa chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake” (Ufunuo 12:1).
 “Maria ameingia utukufu wa mbinguni, ameshirikishwa utukufu wa Mwanawe….Katika Maisha yake Maria alimfuata Mwanawe bila kumwacha hata alipokuwa msalabani. Sasa tunaona Mwana hamwachi mama yake, bali anamshirikisha utukufu wake” (MISALE YA WAUMINI, uk.871). Mwaliko leo ni kuwa mbingu ianzie duniani. Ni kama tunasema,  “Njia yote ya kwenda mbinguni ni mbinguni” (Canon Farrar). Chunga mawazo yako yanageuka kuwa maneno. Chunga maneno yako yanageuka kuwa matendo. Chunga matendo yako yanakuwa kuwa tabia. Chunga tabia yako inageuka desturi. Chunga desturi inageuka kuwa hatima yako.  “Nikichukua hatua ya kwanza nikiwa na wazo zuri, ya pili nikiwa na neno zuri, na ya tatu nikiwa na tendo zuri, niliingia mbinguni,” alisema Zoroaster.
Hata kama mbingu hauioni Mbingu ipo. Hauwezi kusema kwa vile Mungu simuoni Mungu hayupo. Kuna Profesa ambaye hakuamini kuwa Mungu yupo. Akiwa anawafundisha wanafunzi alimwambia mwanafunzi mmoja, “Ebu chungulia dirishani kama utamuona Mungu. Unaona nini?” Mwanafunzi akasema, “Naona miti nje. Naona majani. Naona watu. Naona magari.” Profesa kwa kujitapa akasema, “Nemekuambia Mungu hayupo.” Mwanafunzi mmoja akasema, “Profesa, ngoja mimi nimuhoji mwanafunzi mwenzangu.” Akaanza kumuhoji, “Unamuona Profesa?” Mwanafunzi mwenzako akasema, “Namuona.”  Anayehoji akazidi kuhoji, “Unaona mambo gani ya Profesa?” Mwanafunzi akajibu, “Naona shati, naona macho naona kichwa, naona viatu, naona mikono.” Mwanafunzi akaulizwa, “Je unaona akili yake.” Akajibu, “Sioni akili yake.” Mwanafunzi anayehoji akasema, “Hivyo profesa wetu hana akili kwa vile hauioni.” Katika mtazamo huo, hauwezi kusema kuwa hakuna mbingu kwa vile hauioni.
Papa Pius XII katika barua yake ya kipapa  Munificentissimus Deus aliandika hivi: “Mwishowe Bikira Maria asiye na doa, aliyekingwa na kila doa la dhambi ya asili, akishamaliza mwendo wa maisha yake duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbingu pamoja na mwili wake na pamoja na roho yake. Na alitukuzwa na Bwana kama Malkia wa ulimwengu, kwa sababu alikuwa amefanana sana na mwanawe, Bwana wa mabwana, na mshindi wa dhambi na mauti” (KKK Na. 966, LG 59).
SABABU ZA KUPALIZWA BIKIRA MARIA

1.      MUUNGANIKO NA MWANAWE
Mama na mwanawe, mwana na mama yake. “Bikira mwenye heri alitangulia katika safari yake ya imani akihifadhi kwa uaminifu muungano wake pamoja na Mwanawe mpaka msalabani, ambapo, kwa mpango wa Mungu  alisimama imara; aliteswa kikatili pamoja na Mwanawe wa pekee, na alijiunganisha kwa moyo wake wa kimama na sadaka yake. Alikubali kwa mapendo kuchinjwa kwa sadaka aliyoizaa mwenyewe. Mwishowe, alitolewa na Kristo mwenyewe akifa msalabani, kama Mama yake kwa mfuasi kwa maneno haya: “Mama, tazama Mwanao.”  (LG 58; KKK Na 964; Yoh 19: 26-27). Bikira Maria alipomchukua mimba Yesu aliunganika naye. Ilikuwa ni komunio yake ya kwanza. Akaenda kwa haraka kwenda kuunganika na Elizabeti. Unapounganika na Yesu nenda kwa haraka kuunganika na wengine.
2.      MFUASI WA KWANZA MATUNDA YA KWANZA YA UFUASI
Tunda la kwanza la kuwa mfuasi wa Yesu ni kushiriki maisha ya furaha mbinguni. Bikira Maria ni mfuasi wa kwanza wa Yesu. Hivyo alipata matunda ya kwanza ya kuwa mfuasi wa Yesu.  Katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki tunasoma hivi: “Kupalizwa kwa Bikira Maria Mtakatifu ni kushiriki kwa namna ya pekee ufufuko wa Mwanawe, na ni utangulizi wa ufufuko wa wakristo wengine” (KKK Na 966). Tunasoma katika Injili ya Luka: “Alipokuwa anasema hayo, mwanamke miongoni mwa watu alipaza sauti, akamwambia, “Heri tumbo lililokuchukua na maziwa uliyoyanyonya.” Naye akajibu, “Wenye heri hasa wasikiao neno la Mungu na kulishika” Luka 11: 27-28). Kwa Yesu wenye heri ni wale wasikiao neno la Mungu-yaani wafuasi. Kuwa mfuasi maana yake kusikia, kuishi na kuliweka katika vitendo neno la Mungu (Mt 12: 49-50). Wafuasi wa Kristu ni wake Yesu. Wa kwanza kuwa wake Yesu ni Bikira Maria na hivyo kupalizwa akiwa wa kwanza kama tunavyosoma katika somo la pili: “Kama wote hufa katika Adamu, vile wote watapata tena uzima katika Kristo. Lakini kila mmoja kwa zamu yake; wa kwanza ni Kristo; baadaye walio wa Kristo…” (1 Kor 15: 23).
MAMBO YA KUFANYA ILI MBINGU IANZIE DUNIANI
Kwa kawaida mambo huanzia mbali. Kuna methali ya Wahaya isemayo, “Atakayekula chakula kweli unamugundua wakati wa kunawa mikono.” Namna ya kula inaazia mbali. Ndoa haianzii wakati wa kufunga ndoa. Ndoa inaanzia mbali. Kila Nyumba ni shule ya maisha ya ndoa. Mtoto wa kiume anajifunza maisha ya ndoa nyumbani. Vilevile mbingu inaanzia duniani. Maisha ya mbinguni hayanyeshi kama mvua yanaanzia mbali. Mbingu inaanzia dunia. Yesu aliyepaa kwenda mbinguni amesema, “Mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:20).
  1. HUDUMA-TUNDA LA UPENDO NI HUDUMA
Bikira Maria alienda kwa Elizabeti kuanzisha “Kliniki” ndogo nyumbani kwa Zakaria amhudumie Elizabeti. Na namna hii Bikira Maria anakuwa mhudumu na muuguzi wa kwanza katika ustaarabu wa kikristu. Huduma yake ni changamoto kwetu. Katika kutoa huduma hauitajiki moyo wa “fulani atafanya.” “Tendo lolote la Wema ambalo naweza kumtendea mwanangu, afadhali nilitende sasa, kwa sababu sitapitia njia hii tena”, alisema Stephen Grellet. Tenda wema huende zako. Wema hauozi. Tujue kuwa: “Tunda la upendo ni huduma. Tunda la huduma ni amani” Mama Theresia wa Calcutta.
Siku ya hukumu Yesu kama Jaji anaweza kusema, Nilikuwa na njaa mlianzisha vikundi na vyama vya kusaidia waathirika mkajadili njaa yangu. Lakini hamkunipa chakula. Nilikuwa gerezani mkaenda Kanisani kuniombea na wala hamkunitembelea. Nilikuwa uchi mkajadili maadili ya kutembea uchi, hamkunipa nguo. Nilikuwa mgonjwa mkapiga magoti na kumshuru Mungu kwa kuwapa afya njema. Nilikuwa sina nyumba mahali pa kulala, mkanielezea kuna nyumba ya upendo wa Mungu lakini hamkunijengea nyumba. Nilikuwa mkiwa na mpweke mkaniacha nijiombee mimi mwenyewe. Mlionekana watakatatifu na karibu na Mwenyezi Mungu lakini bado nina njaa, niko mpweke na nina baridi sina nyumba. Ni katika msingi huu tunasema imani lazima itafsiriwe katika matendo. Imani na matendo havitenganishwi ni kama mate na ulimi.
  1. HARAKA KATIKA KUTENDA MEMA
Malaika Gabrieli alimjulisha Mama wa Yesu, Maria kuwa Elizabeti, jamaa yake, amepata mimba ingawa ni mzee na sasa ni mwezi wa sita yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa (Lk.1:36). Baada ya kujua hilo, tunaambiwa Maria alifunga safari akaenda kwa haraka. Hakusitasita, hakuhairisha. Alimthamini Elizabeti. Alienda kwa haraka. Wengine husema haraka haraka haina baraka . Lakini katika mazingira kama haya: ngoja ngoja huumiza tumbo. Philimus mtu wa kusitasita alitembea siku moja kupitia kijijini. Alikutana na omba omba maskini aliyemwomba sadaka. Alitaka kumsaidia omba omba na kusema, “ndiyo, nitakusaidia baadaye.”Alipita karibu na Kanisa, alikumbuka kuwa hajasali sala zake. Alijiambia, “nitasali baadaye”. Alipoendelea na safari alikutana na bibi kikongwe ambaye alimwambia, ‘tafadhali naomba umpeleke mtoto wangu mgonjwa hospitalini. Niko peke yangu na hakuna mtu yoyote wa kunisaidia.” “Ndiyo,” Philimus alijibu, “Nitakusaidia, lakini nitakusaidia baadaye.” Baada ya kuachana na bibi huyo kikongwe alipata ajali ya kugongwa na gari na kufa papo hapo. Roho yake ikapelekwa bahari ya moto. Wakati akiungua, alimwomba Malaika, “Tafadhali nipe tone la maji.” “Ndiyo” Malaika alimwambia, “Nitakupa maji baadaye”. Halafu malaika alimwacha. Alipomwona malaika mwingine, Philimus alimsihi, “Nitoe kwenye huu moto.” “Ndiyo,” Malaika alisema kwa haraka, “Nitakutoa baadaye” Halafu  na malaika huyo alimwacha. Aliposihi malaika wengine, Philimus  alipata jibu lile lile, “Ndiyo, baadaye…” Kadiri alivyoendelea kuungua motoni alitambua kuwa Mungu husitasita kwa wale ambao husitasita. 
Kusitasita ni kuchelewesha mambo. Kuchelewa ni kupoteza muda. Kumbuka muda ni mali. Zaidi ya hayo kila dakika iendayo kwa Mungu hairudi. Tunasitasita labda kwa vile tunangojea mambo yawe mazuri. Lakini kumbuka, “Mvua ilikuwa hainyeshi Nuhu alipoanza kujenga safina,” alisema Howard Ruff.
  1. WAKIKUSIFU MSIFU MUNGU
Maria mama wa Yesu aliposifiwa na Elizabeti alimsifu Mungu. Alizabeti alisema hivi, “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa” (Luka 1:42). Maria mama wa Yesu alimsifu Mungu. “Moyo wangu wamtukuza Bwana, na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu” (Luka 1:46-47). Maria mama wa Yesu hakujisifu na kujisifia. Alimsifu Mungu. Alimhimidi Mungu. Alimtukuza Mungu.  Elizabeti ni mfano wa kuigwa watu wa familia yako wakifanya vizuri, wakibarikiwa wasifu. Katika mambo yanayomuhumiza mwanamke ni mme wake kuwasifia wanawake wengine mbele yake bila kumsifia yeye na kwa mwanaume ni hivyo hivyo. Kuna mwanaume aliyemwambia mke wake, haupiki vizuri kama mama yangu. Naye mke wake alimjibu. “Na wewe hauna pesa kama baba yangu.”
Wakikusifu una kila sababu ya kumsifu Mungu kama Maria mama wa Yesu alivyofanya.  Kwanza ni Mungu wetu anayetoa. Mungu ndiye mpaji. Mungu ndiye mgawa mafungu. Maria mama wa Yesu alineemeshwa na Mungu na aliposifiwa alikuwa amembeba mwokozi mimbani. Pili tunamcha au tunamuogopa. Waogope wasiomuogopa Mungu. Tatu, kumsifu Mungu ni kuzuri na ni vema kama asemavyo mtunga Zaburi. “Msifuni BWANA; maana ni vema kumwimbia Mungu wetu, maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri” (Zaburi 147:1).  Nne kusifu ni jambo la lazima na la kimaumbile. Mara ngapi katika uwanja wa mpira yanatoka bila breki maneno ya mshangao na ya kusifia kama lo, la-la-la-la mchezo ukichezwa vizuri. Ndivyo ilivyo katika uwanja wa dini kumsifu Mungu ni jambo la lazima la kimaumbile. Tano, tunampenda Mungu. Unaweza kusifia bila kupenda lakini hauwezi kupenda bila kusifia.
  1. JIBARIKI KWA MANENO
Maria mama wa Yesu alijisambazia baraka pia. “Vizazi vyote vitaniita mwenye heri” (Luka 1:48). Alijiambia maneno mazuri katika utenzi wake. Maneno hayo yaliumuumba anaitwa mama mwenye sifa na mama msaajabivu. Neno alibariki tu linaumba, linampa mtu sura mpya. Ni kweli alivyosema Edward Thorndike, “Rangi ufutika, hekalu huharibika, ufalme huanguka, lakini maneno ya hekima hudumu.” Maneno ya Mama wa Yesu yamedumu. Jibariki kwa maneno. Kuna msichana aliyekuwa na umri wa kuolewa msichana pekee kwa wazazi wake. Alijibariki wakati wa kusali. Alisema kuwa hatajiombea yeye mwenyewe atamuombea mama yake. Sala yake ilikuwa hii. “Ee Mwenyezi Mungu mpe mama yangu mkwe mzuri wa sura na tabia.” Kwa sala hii msichana huu alijasambazia baraka, yaani kuwa na mme mzuri wa sura na tabia. Kwa mama yake ni mkwe, kwake ni mme wake.  Panda mbegu za maneno mazuri ya kujibariki. Biblia inatoa wito huo. “Hata aliye dhaifu na aseme: ‘mimi pia ni shujaa” (Yoeli 3:10). Hata aliye masikini na aseme: Mimi ni tajiri. Hata aliye na akili za wastani aseme: Mimi nina akili nyingi sana. Hata na aliye na uzuri wa wastani aseme: Mimi ni mzuri sana. Anayejipenda atajiambia maneno hayo.
  1. UKIPATA SHUKURU
“Mungu amekupa zawadi ya sekunde 86,400 siku ya leo, je umetumia sekunde moja kusema, “Mungu Nakushukuru,” alisema William A. Ward. Ukitaka kupata miujiza shukuru kwa dogo ulilopata. “Shukuru kwa zawadi ndogo ndipo utaweza kupata zawadi kubwa.” (Thomas à Kempis).Mkumbuke Mungu. Hakuna haja ya kujidai sana sote ni “CHAKUPEWA.” “Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa?” (1 Wakorintho 4:7).   Kuna methali isemayo, “Aliyekupa wewe kiti ndiye aliyenipa mimi kumbi.” Na aliye na kidogo akitumie kupata kikubwa.
Soma zaburi ya 100, “Pitieni milango yake ya hekalu lake kwa shukrani, ingieni katika nyua zake kwa sifa. Mshukuruni na kulisifu jina lake.” (Zaburi 100: 4) Unapopitia mlango wa kanisa pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa duka la magari pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa Supermarket pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa benki, pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa Hospitali pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa ofisi, pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa duka, pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa gereji, pitieni kwa shukrani.Unapoingia kwenye sehemu ya kuegesha magari, ingieni kwa shukrani. Fikiri na Shukuru. Unapopita kwenye mlango wako nyumba pitieni kwa shukrani. Unapoelekea kwenye chumba cha kulala, pitieni kwenye mlango kwa shukrani. Milionea wanaotajwa katika Biblia walikuwa ni watu wa shukrani.
  1. KUWA MMISIONARI WA UPENDO
Kama upendo wako hauwezi kupaa kwenda kuwatumikia wengine, una Mbawa ambazo zimevunjika. Upendo huanzia nyumbani. Umisionari uanzie mahali ulipo, kwenye jumuiya yako. Usikoke moto kwa mama wa kambo wakati kwa mama yako moto umezimika.
Juu ya Umisionari, Mama Theresia wa Calcutta alikuwa na haya ya kusema:
“Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda. Huko aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elizabeth. (Lk.1:39-40). Mara Knistu alipoingia katika maisha yake, ona alivyofunga safari na kwenda kwa haraka kumtoa kwa wengine. Na namna gani anafanya hili. Na kwa kutenda tena kama mtumishi mnyenyekevu, akiosha, kusafisha na kupika kwa ajili ya binamu yake mzee. Masista wa Shirika letu wanaitwa Wamisionari wa Upendo (Missionaries of Charity) na kila mara ninasema kuwa Maria yeye mwenyewe alikuwa “mmisionari wa Upendo”. Mmisionari ni mtu anayetumwa kupeleka upendo wa Mungu kwa wengine; na mmisionari wa upendo anafanya hili kupitia matendo ya upendo, kama huduma za kiupendo na za kiunyenyekevu ambazo Maria alitoa kwa Elizabeth.
HITIMISHO: Mtaka cha uvunguni sharti ainame. Kuingia mbinguni hakuna njia ya mkato. Mtu mmoja wa  Ireland ambaye alikuwa amelewa na alikuwa anapenda pombe sana siku moja aliulizwa na Baba Paroko, “Mwanangu unategemea utaendaje mbinguni?” Mtu huyo alijibu, “Hilo ni jambo rahisi sana! Nitakapofika kwenye mlango wa mbingu, nitafungua mlango na kufunga. Nitafungua mlango na kufunga. Nitaendelea kufanya hivyo mpaka Mtakatifu Petro atakapokasirika na kusema, “Mike! Ingia ndani au Utoke hapo mlangoni.!’ Hivyo nitaingia mbinguni kwa urahisi. Mtaka cha uvunguni sharti ainame. Kwenda mbinguni kunahitaji kufanyiwa kazi.

Counter

You are visitor since April'08