Saturday, April 30, 2016

KAZI NI HURUMA NA HUDUMA NI HURUMA



    

1. Mwanzo 1: 26-2:3
2. Wakolosai 3: 14-15, 17.23-24
3. Mt. 13: 54-58

               SIKUKUU YA YOZEFU MFANYAKAZI (Mei Mosi 2016 Kwa majimbo Kama Jimbo Kuu la Dar es Salaam na mengine kwa wengine tazama tafakari yangu ya Jumapili ya 6 ya Pasaka)

Mwalimu wa wanafunzi wadogo wa somo la dini aliwauliza wanafunzi. Kama ungeomba Mungu akupe sehemu ya masalia ya mtakatifu ungeomba nini? Mwanafunzi wa miaka kumi na miwili akasema, “Mimi ningeomba tone la jasho la Mt. Yozefu, ni jasho la heshima ya kazi, ni jasho la unyenyekevu kwa sababu kwa kutoa jasho aliweza kujilisha, kumlisha mtoto Yesu na kumlisha Bikira Maria.”

Leo ni sikukuu ya Mt. Yozefu Mfanyakazi. Heshima tunayompa Mt. Yozefu inaitwa, “Proto-dulia.” Inatangulia heshima kwa watakatifu wote ambayo ni “dulia.” Heshima kwa Bikira Maria ni “hyper dulia” yaani juu ya heshima kwa watakatifu wote. “Mt. Yozefu alikuwa mtu wa haki, mfanyakazi asiyechoka, mlinzi mkweli wa wale ambao amekabidhiwa awatunze. Kila mara alinde, akinge na kuziangazia familia,” alisema Mt. Papa Yohane Paulo II. Sikukuu ya Mt. Yozefu Mfanyakazi ilianzishwa na Papa Pius XII mwaka 1955 ili dhana ya kazi kuipa maana ya kikristo na kuwapa wafanyakazi mtu wa kuiga na mwombezi.  “Wafanyakazi na wale wote ambao wanafanya kazi katika hali za umaskini watakuwa na sababu ya kufurahi kuliko kuomboleza, kwa vile wanajambo linalofanana na Familia Takatifu katika kazi zao na shughuli zao”(Leo XIII).
Mama mwenye watoto kumi anaweza kuangaika akiwatafutia chakula wale washibe anawaonea huruma yeye akisha zeeka watoto kumi wanashindwa kumlisha mama yao. Wanakosa huruma. Kufanya kazi kwenye taasisi ni kuifikisha huruma ya Mungu maeneo ya kazi. Tuna mifano ya kuigwa ya mashujaa wa huruma. Kuna hadithi isemayo kuwa huko mbinguni Mtakatifu Petro aligundua watu wanazidi kuongezeka. Alipochunguza aligundua Mt. Yozefu alikuwa ametengeneza dirisha anawapitisha watu kuingia mbinguni. Akatishia kumfukuza mbinguni. Yozefu akasema, “Ukinifukuza naondoka na mke wangu na mtoto Yesu kama baba yake mlishi.” Mjadala ukaisha. Mt. Yozefu anawaonea huruma wengine kama alivyowaonea Yesu na Maria duniani.

Kazi ni huruma kwa  sababu inakuwezesha kufanya matendo ya huruma. Inakuwezesha kujitunza na kuitunza familia. Inakuwezesha kuwa mkarimu. Inakuwezesha kushiriki kazi ya ukombozi. Inakuweze sha kutoa zawadi.

Kazi ni kujifanyia matendo ya huruma. Kujihurumia ni kujionyesha moyo wa wema na upole. Ni kujitendea mema.  Kazi inakuwezesha kujitendea matendo ya huruma. Kipato kitokanacho na kazi kinakuwezesha kujitendea matendo ya huruma na kujiendeleza. Upendo huanzia nyumbani ingawa unatoka, una sifa ya kimisionari. Unapojivika unajitendea tendo la huruma. Unapojirisha unajitendea tendo la huruma. Yesu alisema nilikuwa na njaa ukanilisha. Ukiwa na njaa ukajilisha unajitendea tendo la huruma. “Mungu anampa kila ndege chakula, lakini hakitupi kwenye kiota,” alisema J.G. Holland. Mtume Paulo alikuwa na ujumbe mzito kwa wasiofanya kazi: “Asiyefanya kazi asile” (2 Wathesalonike 3:10). Ukifanya kazi unakula. Kazi inakuwezesha kujifanyia tendo la huruma la kula. Unapofanya kazi vizuri unajiongezea hadhi na heshima. KAMA UNAFIKIRI KUFANYA KAZI SI KAZI JARIBU KUACHA KAZI UONE KUPATA KAZI ILIVYO KAZI. Kumbe Usichezee kazi chezea mshahara.

Kazi ni huruma kwa Mungu. Kazi nzuri na yenye viwango vya juu na ubora wa hali ya juu inampa Mungu utukufu wake. “LOLOTE MFANYALO, LIFANYE KWA MOYO, KAMA KWAMBA MNAMFANYIA BWANA.” (Wakolasai 3:23). “ Hakuna jambo linaloonekana linachosha or linahumiza wakati unamfanyia Bwana kazi ambaye analipa vizuri, ambaye anakuzawadia hata kikombe cha maji baridi ambacho kinatolewa kwa upendo Wake,” alisema Mtakatifu Dominiko Savio. “Kazi chini ya viwango inamyima Mungu utukufu wake. Mhurumie Mungu. Haijalishi mkubwa wako wa kazi ni nani. Unamfanyia Mungu kazi. Kuwa na huruma usimfanyie kazi ya hovyo. Michelengelo alikuwa akichora michoro na kupanga rangi kwenye kona ya kikanisa cha Sistine ambayo ilikuwa haionekani aliulizwa na msaidizi wake kwa nini ameweka nguvu za ziada kwenye sehemu ya paa ambayo hakuna atakayeiona. Alijibu, “Mungu ataona.

Kazi ni huruma kwa watu wengine. Waendeshaji wa teksi Nairobi wanalala kwenye teksi wakitafuta matunzo ya familia. Kazi ni huruma kwa watu wengine.  Mwajiri alikuwa anazungumza na mwajiriwa mpya: “Kijana, hapa tuna rekodi ya kufanya yasiyowezekana na yaliyoshindikana.” Kijana: Ndiyo Kiongozi, nitajitahidi kuwa mfayanyakazi aliyeshindikana siku zote.” Kuwa mfanyakazi aliyeshindakana si kuwahurumia wengine.

Kufanya kazi ni kuvihurumia vizazi vijavyo. “Kula uwabakizie” Mzee wa mika 85 alikuwa akipanda miti ya miembe. Vijana walipita na kumuuliza katika umri huu unapanda miembe na unajua kuwa utakula amembe yake. Alijibu kwa muda nilioishi nimekuwa nikila maembe yaliyopandwa na watu wengine, na mimi napanda maembe kwa vizazi vijavyo.` 

Katika kazi yetu ya leo lazima tufikirie nyakati zijazo,” alisema Padre Adolph Kolping. “Vizazi vijavyo vituonee huruma vikitazama nyuma kuiona kazi tunayofanya leo. Tulifanya tulichoweza kwa kile tulichokuwa nacho,”alisema Mira Grant. Mtakatifu Yozefu Mume wa Bikira Maria na Baba mlishi wa Yesu alifikiria vizazi vijavyo. Kanisa Katoliki husali, “Ee Mungu Mwenyezi, toka mwanzo ulimkabidhi Mtakatifu Yozefu kazi ya kuyatunza mafumbo ya wokovu wa binadamu. Tunakuomba kwa maombezi yake ulijalie Kanisa lako liyatunze siku zote mafumbo yako yote…” Kutunza mafumbo ni kazi lakini ni huruma kwa vizazi vijavyo. Ni tendo la huruma kuviachia vizazi vijavyo urithi. Hawa watu hawawezi kukulipa.

Palikuwepo na msichana aliyejichukia kwa sababu alikuwa kipofu. Alimchukia kila mtu isipokuwa rafiki wake wa kiume. Alikuwepo kwa ajili yake kila mara. Alimwambia rafiki wake wa kiume. Nikiweza kuiona dunia nitakubali kuolewa na wewe. Siku moja mtu alijitolea na kumpa macho mawili. Aliweza kuona kila kitu na hata kumuona rafiki yake wa kiume. Rafiki yake alimuuliza, “Sasa unaweza kuiona dunia, je uko tayari kuolewa na mimi?” Yule msichana alimtazama rafiki yake wa kiume na kugundua alikuwa kipofu. Matundu ya mashimo ya macho yalimshtua. Wazo la kuyatazama maisha yake yote lilimfanya akate kuolewa na yeye. Rafiki yake wa kiume aliondoka kwa masikitiko na machozi. Alimwandikia ujumbe, “Tunza macho yako mpendwa wangu kabla hayajawa yako yalikuwa yangu.” Akili ya binadamu inafanya hivyo pale ambapo hadhi yetu inabadilika. Leo kabla ya kusema neno baya fikiria yule ambaye hawezi kuongea. Leo kama umechoka na kulalamika juu ya kazi unayoifanya mfikirie yule ambaye hana kazi. Kabla ya kulalamikia umbali unaoendesha gari, mfirikie yule anayetembea umbali huo kwa miguu.




Friday, April 22, 2016

UPENDO HAUFICHIKI, UPENDO UNAONEKANA



                                 
                                                     Jumapili ya 5 ya Paska
1.       Mdo 14: 21-27
2.       Ufu 21: 1-5a
3.       Yn 13: 31-33a.34-35
“Waliwaimarisha wafuasi roho na kuwatia moyo “ (Mdo 14: 22)
Hivyo watu wote watawatambua kuwa wafuasi wangu, mkipendana” (Yohane 13:34-35).
MUHTASARI
·         Upendo unaonekana katika ukaribu wa mioyo
·         Upendo unaonekana katika matendo na vipaumbele
·         Upendo unaonekana katika maneno ya kutia moyo
·         Upendo unaonekana katika kumbukumbu
·         Upendo unaonekana katika mahusiano
·         Upendo unaonekana katika zawadi au kutoa
·         Upendo unaonekana katika kusikiliza

Upendo unaonekana katika ukaribu wa mioyo. Palipo na upendo mioyo imekaribiana. Mioyo imeshibana. Wanaopendana ni wataalamu wa moyo. “Mtu yeyote anaweza kuwa mtaalamu wa moyo. Sharti pekee ni kumpenda mtu fulani,” alisema Angie Papadakis. Moyo wa Mtume Paulo na moyo wa Barnaba ilikuwa imekaribiana. Walipendana. Walishibana. Walikuwa wataalamu wa moyo. Jambo hilo linaonekana. Kuna methali ya Tanzania isemayo, nyumba hupakana lakini mioyo haipakani. Upendo unaonekana jinsi tunavyozungumza. Kwamba mioyo inapakana ni jambo linaloonekana kwa namna tunavyozungumza. Profesa alikuwa anatoa mafundisho juu ya haya hii: “Jibu pole hutuliza ghadhabu, bali neno kuhumiza huchochea hasira” (Mithali 15: 1). Profesa aliwauliza wanafunzi kwa nini tukiwa na hasira huwa tunapiga kelele au tunapaza sauti? Kwa nini watu wanapigiana kelele wanapokuwa na mfadhaiko? Mwanafunzi mmoja alijibu, ni kwa sababu tunapoteza utulivu wetu. “Lakini kwa nini upige kelele wakati mtu unayemwambia yupo karibu nawe?” aliuliza profesa. Wanafunzi walitoa majibu mbali mbali lakini hakuna jibu lililomridhisha profesa. Hatimaye alieleza hivi, “Watu wanapokasirikiana kuna umbali mrefu kati ya mioyo yao kisaikolojia. Ili kupunguza umbali wanapigiana kelele ili waweze kusikia. Jambo gani linatokea kama watu wanapendana? Hawapigiani kelele wanaongea kwa upole wananong’ezana, wanakaribiana palipo na upendo. Hatimaye hawahitaji hata kunong’onezana wanatazama. Ikitokea siku ukampigia kelele unayempenda   jua kuwa unaweka umbali kati yako na wewe. Jibu pole hutuliza hasira.
  
Kuna mambo mawili tu mtu hawezi kuficha: kwamba amelewa na kwamba anapenda,” alisema Antiphanes. Lakini yapo mambo mengi ambayo hayafichiki, chuki haifichiki ikifichika ni kama kuficha moto kwenye karatasi. Kuna methali isemayo mapenzi ni kikohozi hayafichiki. Upendo unaonekana bila kujali kama mtu ana ulemavu au la. “Upendo ni lugha ambao kiziwi anaweza kusikia; Upendo ni wimbo ambao mlemavu anaweza kucheza; upendo ni mapambazuko ambayo kipofu anaweza kuona,” alisema Ramesh Umadkat. Palipo na upendo mwenye ulemavu atachangamka hata akiwa na mguu mmoja anaweza kudansi. “Upendo unaonekaje? Una mikono ya kuwasaidia wengine. Una miguu ya kuharakisha kuwaendea wahitaji. Una macho ya kuona shida na hitaji. Una masikio ya kusikia kushusha pumzi kwa majonzi na mateso ya watu. Hivyo ndivyo upendo unavyofanana,”alisema Mtakatifu Augustino wa Hippo Afrika ya Kaskazini.
Biblia inathibitisha kuwa upendo haufichiki, unaonekana. “Amri mpya nawapeni: mpendane. Kama mimi nilivyowapenda, nanyi pia mpendane. Hivyo watu wote watawatambua kuwa wafuasi wangu, mkipendana” (Yohane 13:34-35). Watakatifu wengi walikuwa na haya ya kusema juu ya haya hizo. “Yeyote kati yenu asiwe na hali ya kawaida tu kwa jirani yake isipokuwa muendelee kupendana ninyi kwa ninyi katika Yesu Kristo” (Mtakatifu Inyasi wa Antiokioa). Upendo unampambanua mkristo. “Mmoja lazima amwone Mungu katika kila mmoja” (Mtakatifu Katharina Laboure). “Ninakwambia mambo haya, kuwaburudisha ninyi, huku nikisali kwamba kwa kuwa wote tumeumbwa kwa dutu ile ile, ambayo ina mwanzo lakini haina mwisho, tuweze kupendana sisi kwa sisi kwa upendo mmoja. Kwa wale wote wanaojitambua wenyewe wanajua kuwa ni watu wadutu moja isiyokufa” (Mtakatifu Antoni wa Misri).

Upendo unaonekana katika matendo na vipaumbele. Vijijini au mijini wanaposema fulani anampenda fulani ni kwa sababu mapenzi yanaonekana. Asubuhi anamtembelea. Mchana anamtendembela. Jioni anamtembelea. Usiku anamtembelea. Watu wanaanza kusema maneno. Hivyo hivyo anayempenda Mungu ataonekana kila mara anaenda Kanisani kila siku. Atasali sala za asubuhi. Yaani atakutana na Mungu kabla ya kukutana na shetani. Atakutana na Mungu kabla ya kukutana na mazingira ya maisha. Atazungumza na Mungu kabla ya kuzungumza na watu wengi. Anaungana na Mungu kabla ya kuungana na watu wengine. Atasikiliza sauti ya Mungu kabla ya kusikiliza sauti za watu wengine. Atasikiliza habari kutoka mbinguni kabla ya kusikiliza habari kutoka BBC. Ataliita jina la Yesu kabla ya kuita majina mengine madogo. Kwa macho ya imani atamuona Yesu kabla ya kujiona kwenye kioo. Atafagia moyo wake kabla ya kufagia uwanja wake unaozunguka nyumba. Upendo kwa Mungu unaonekana. Yesu kwa vile alimpenda Mungu baba alisali asubuhi na mapema. “Asubuhi na mapema, kabla ya kupambazuka, aliamka, akaondoka, na kwenda mahali pa nyika alikosali” (Marko 1: 35).

Upendo unaonekana katika maneno ya kutia moyo. Lililo moyoni ulimi huiba. Moyoni pakiwepo upendo ulimi utaiba utaonekana katika maneno. Upendo wa Barnaba na mtume Paulo ulionekana katika matendo na maneno. Tunaambiwa. “Waliwaimarisha wafuasi roho na kuwatia moyo “ (Mdo 14: 22).  Jina Barnaba linamaanisha mwana wa kutia moyo. Unapotia moyo ni upendo unaonekana. Tuna mifano ya watu mbali mbali ambao wamesema maneno ya kutia moyo. “Hapajakuwepo kamwe usiku au tatizo ambalo limeweza kushinda mapambazuko au matumaini,” alisema Bern Williams. Hata pakiwepo usiku wa matatizo ya namna gani kutakucha. Matatizo hayapigi bao matumaini. Kuna aliyesema, “Mungu huwapeleka watu katika maji marefu si kwa ajili ya kuwazamisha majini bali kuwatakasa,” alisema John Aughey. Matatizo yanatakasa mawazo hasi, mawazo taka na mtazamo taka yanapotafakiriwa katika mtazamo chanya. Mtu fulani alisema, “Watu wasio sahihi wanapokuacha mambo sahihi yanaanza kutokea.” Maneno hayo yanatia matumaini kwa yule aliyeachwa na watu ambao wasio sahihi.

Upendo unaonekana katika kumbukumbu. Mchungaji Rick Warren katika kitabu chake, Maisha Yanayoongozwa na Malengo alikuwa na haya ya kusema, “Upendo huacha kumbukumbu. Jinsi unavyowatendea watu wengine, siyo utajiri au mafanikio yako ndicho kitu kinachodumu unachoweza kuacha duniani.” Kama Mama Theresa alivvyosema, “Sivyo unavyotenda, lakini kiasi gani cha upendo unaweka katika tendo hilo ndilo jambo la muhimu sana.”

Upendo unaonekana katika mahusiano. Mahusiano mazuri kati ya mtume Paulo na Barnaba ni ushahidi wa upendo. Mchungaji Rick Warren katika kitabu chake, Maisha Yanayoongozwa na Malengo alikuwa na haya ya kusema, “Nimekuwa kando ya kitanda cha watu wengi wanaokuwa katika kufa, wanaposimama pembezoni mwa umilele, na sijasikia yeyote akisema, ‘Nileteeni vyeti vyangu! Nataka kuviona mara moja tena. Nionyeshe zawadi zangu, medali zangu, ile saa ya dhahabu niliyopewa.’ Maisha yanapokoma duniani, watu hawajizungushii vitu. Tunachotaka kitunzunguke ni watu – watu tuwapendao na tulio na uhusiano nao. Katika mahusiano mtu hataki kumhumiza bila sababu anayempenda. Wakati wa ibada ya ndoa mchungaji aliuliza kama kuna mtu ana la kusema dhidi ya wanandoa watarajiwa. Kimya kikuu na mshangao vilitawala pale ambapo mwanamke  aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma alienda mbele karibu na wanandoa amembeba mtoto. Bibi arusi alianguka na kuzirai. Mchungaji alimuuliza kama ana jambo lolote la kusema, “Hatusikii huko nyuma nimekuja mbele kusiliza vizuri wakiweka ahadi za ndoa.”

Upendo unaonekana katika zawadi au kutoa. Upendo unakufa unapouhodhi – unakua unapoutoa,” alisema Elbert Hubbard. Kuhodhi ni kukusanya mali au bidhaa na kuvirundika kwa matumizi binafsi. Katika kutoa tunawasaidia wengine. “Lengo letu kuu katika maisha haya ni kuwasaidia wengine. Na kama huwezi kuwasaidia, walau usiwaumize,” alisema Dalai Lama.
Upendo unaonekana katika kusikiliza. Weka hili katika kumbukumbu ya moyo wako: Hakuna mtu yeyote ambaye huwezi  kukosa kumpenda kama umesikiliza hadithi yake,” alisema Mary Lou Kownack. Ukimsikiliza utampenda. Mtume Paulo na Barnaba waliwatia watu moyo kwa sababu waliwasikiza. Tatizo kubwa siku hizi ni kutowasikiliza watu. “Barabara ya kuufikia moyo ni sikio,” alisema Voltaire. Unapomsikiliza mtu unagusa moyo wake. Kusikiliza ni kutoa huduma. “Kuwasikiliza wengine ni sehemu ya kwanza ya huduma ya kweli ya kikristo,” alisema Dietrich Bonhoeffer. Kusikiliza ni changamoto. “Yeye ambaye hamsikilizi tena ndugu yake muda mfupi atakuwa hamsikilizi Mungu,” alisema Dietrich Bonhoeffer.
  
Hitimisho
Upendo ni jambo la kujifunza. Kama watu wanajifunza kuchukia wanaweza kujifunza kupenda.”Hakuna mtu anayezaliwa akiwa anamchukia mtu mwingine kwa sababu ya rangi yake, historia yake, ama dini yake. Watu ni lazima wajifunze kuchukia, na kama wanaweza kujifunza kuchukia, wanaweza kufundishwa kupenda, kwa sababu upendo huja kiasili kwenye moyo wa binadamu kuliko chuki,” alisema Nelson Mandela (1918 – 2013).

Counter

You are visitor since April'08