Saturday, November 5, 2016

KIFO SIO NUKTA NI ALAMA YA MKATO

                                 
                                                        JUMAPILI YA 32 YA MWAKA C
“Kwani Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, maana kwa sababu yake wote wanaishi” (Lk 20: 38).
1.  2 Makabayo 7: 1-2.9-14
2.  2 Thess 2: 16-3:5
3.  Lk 20: 27-38

Meli ikianza safari yake toka Kisumu hadi mwanza Tanzania wale walioko Kisumu wanasema meli imeenda. Wale walioko Tanzania wanaoiona kwa mbali wanasema meli imekuja. Mtu akiaga dunia tunasema “Ameenda.” Walioko mbinguni au toharani wanasema, “Amekuja.”  Hivyo kifo sio kituo bali ni koma. KWETU KIFO SIO UKUTA NI MLANGO. Kwetu kifo sio kizuizi bali ni daraja. Mbio za sakafuni huishia ukingoni. Mbio zetu haziishii ukutani bali tunapitia zinafika mlangoni na tunapita.
Hadithi ikiwa nzuri sana kwenye gazeti inakatizwa na chini yake yanaandikwa maneno itaendelea toleo lijalo. Mtu anapoaga dunia maisha yake yanaendelea toleo lijalo. Toleo Lijalo ni motoni, mbinguni au toharani. Kuna mshika kipenga aliyeaga dunia akaenda motoni. Huko alikuta uwanja mzuri sana na watu wamejipanga kucheza mpira alifurahi sana. Timu mbili ziliingia yeye akashika kipenga. Wachezaji wakasalimiana na kushika nafasi zao. Yeye mshika kipenga akauliza: “Mpira wapi?”. Aliambiwa huku ndio maana kunaitwa motoni. “The hell of it” ni kwamba hakuna mpira. Motoni ni kama una hamu ya chakula na hauwezi ukala. Kuna kitu kinakosekana.
MZAHAA JUU YA KIFO NA MAISHA BAADA YA KIFO: “Ukristo kwa kiini chake ni dini ya ufufuko. Dhana ya ufufuko iko kwenye kitovu chake. Ukiondoa ufufuko, ukristo unauharibu,” alisema John R. W. Stott.  Mungu wetu si Mungu wa wafu ni Mungu wa walio hai. Masadukayo kidini walikuwa mahafidhina na hawakupokea mafundisho yaliyokuwa nje ya vitabu vya kwanza vya Agano la Kale. Waliyakataa mafundisho juu ya ufufuko, malaika na pepo wabaya. Mara kwa mara Yesu alibishana nao. Kusema kweli kifo si nukta bali ni alama ya mkato maisha yanaendelea.  Kule mbinguni hapakuwepo kuoa au kueolewa. Tutaishi kama malaika. Tumefanywa kidogo chini ya malaika (Zaburi 8:6).
Masadukayo walifanya mzahaa juu ya kifo na maisha baada ya kifo. Walifikiri kifo ni mwisho wa safari. Walifikiri kifo ni kikomo. Walifikiri kifo ni kituo. Walijiuliza kama “Alichokiunganisha Mungu mwanadamu hasitenganishe.” Kwa nini sasa Mungu atenganishe mbinguni?” Walimuuliza swali Yesu lenye mtego. Walitazamana. Walikonyezana. Wakasema tumumweza. Walimuuliza kama mambo mazuri yatakuwa huko. Kuna wengine labda wanafanya mzaha kama huo. Wanauliza kama kuwa mbinguni ni sherehe nani watakuwa wanapika? Kuni hizo zitatoka msitu upi? Jiko litakuwa wapi? Ni aina gani ya pombe zitakuwa huko? Mafarisayo walikuwa kama chura ambaye alikuwa anabishana na kusema hakuna nchi kavu dunia yote ni maji. Ni kama watoto wawili mapacha waliokuwa kwenye tumbo la mama yake mmoja alipozaliwa mwingine alilia sana na kusema kaka yangu ameaga dunia. Wote wakakutana duniani.
MASADUKAYO WALIFIKIRIA MAMBO YA KARIBU
Tunafikiri mambo ya karibu. Sala zetu ni za mambo ya karibu na sio za mambo ya mbali sana. Watoto shuleni wanafikiria maksi. Pengie tunafikiria kesho. Mtu anaenda kufanya mkataba anafikiria atakavyomdanya mtu. Hafikirii kesho itakuwaje.

MUNGU WA IBRAHIMU NI MUNGU WAKO NA WA JAMAA YAKO ALIYEKUFA
Abrahamu anaitwa “Rafiki wa Mungu,” (Isaya 41:8), “Mtumishi wa Mungu” (Zaburi 105:6) Mungu alimbadili Abrahamu anaweza kukubadili wewe. Abramu alimdanganya Farao na kusema Sarai si mke wake (Mwanzo 11: 10 – 20) Sasa  Mungu wetu ni Mungu wa Ibrahimu. Isaka alidanganya hakusema kuwa Rebeka ni mke wake maana alikuwa mzuri sana. (Mwanzo 26: 6-10) Yakobo aliiba haki ya Esau (Mwanzo 27: 1 – 29). Walikuwa wameoa wanawake wazuri sana. Mungu aligeuza maisha yao anaweza kugeuza maisha yako. Na Mungu akaitwa Mungu wa Kamau, Mungu wa Onyango, Mungu wa Kilonzo, Mungu wa Mutua, Mungu wa Anna. Ibrahimu alikuwa baba wa imani.
 MAISHA BAADA YA MAISHA
Katika tamaduni za kiafrika mtu akiwa anaomboleza anamwambia marehemu amsalimie jamaa zake walioaga dunia. Anasema: Nisalimie babu yangu, nisalimie nyanya yangu. Nisalimie mjomba wangu. Nisalimie mama mdogo. Mfano wa majina: immortality of name: mjukuu anapewa jina la babu. Mtoto wa kike anapewa jina la nyanya yake. Tunataka jina la mtu liendelee kutajwa. Immortality of fame: Tunataka sifa ya mtu iishi milele. Tunajenga sanamu za ukumbusho. Kuna immortality of influence: Jina la baba linawapa watoto ushawishi. Immortality of power: Tunataka mamlaka yaendelee kwa kuanzisha mashirika ya kutoa msaada. Nyerere Foundation. Aliyeanzisha zawadi ya Nobel Prize.
KIFO SIO NUKTA NI ALAMA YA MKATO
Kifo kipo katika miguu tunatembea nacho. Ndivyo isemavyo methali moja ya kiafrika.  Sio tu kwamba tunatembea nacho katika miguu tu pengine tunasafiri nacho katika vyombo vya majini, angani na barabarani.  Hadithi inapokuwa tamu kwenye gazeti au runinga hukatizwa na chini yake maneno “Itaendelea Toleo Lijalo,” huandikwa. Maisha ya marehemu waliokufa  ni hadithi ambayo itaendelea toleo lijalo. Toleo lijalo ni huko mbinguni,  toharani au motoni. 
Katika adhimisho la misa huwa tunasali: “Tunasikitika kwa sababu tunajua kwamba lazima tutakufa, lakini tunatulizwa kwa kuwa alituhaidia uzima wa milele. Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakishabomolewa, tunapata makao ya milele mbinguni.”  Sayansi inatwambia kuwa hakuna kitu chochote katika maumbile, hata chembe ndogo inaweza kupotea kabisa kabisa. Maumbile hayajui kutokuwepo, yanachokijua ni mabadiliko. Ukweli huu wa kisayansi unahimarisha imani yetu katika kuendelea kuishi katika maisha ambayo yamegeuzwa. Kusema kweli kifo ni kudondoka kwa ua ili tunda liweze kukomaa. Kuna maisha baada ya kifo. Kuna maisha baada ya maisha. Katika somo la kwanza saba wako mbinguni na saba wa kufikirika wa Injili wako mbinguni. Katika somo la kwanza tunasoma hivi: “Karibu na kukata roho, akasema, “Ewe mpotovu, unatuondoa uzima wa sasa, lakini Mfalme wa ulimwengu atatufufua sisi, tunaokufa kwa ajili ya amri zake, naye atatupatia tena maisha ya uzima wa milele” (2 Wamakabayo 7: 9).
NAMNA GANI?
 Ingawa kifo huja mara moja tu kwa kila mtu, swali linabaki ni kifo cha namna gani ? Baadhi ya wakristu husali na kumuomba Mungu wafe kifo chema. Sala yao huwa hivi, “Na kifo cha ghafla na kisichotazamiwa, utuopoe, Ee Bwana.”  Masadukayo walisumbuliwa na swali la namna gani baada ya ufufuko mpaka walitambulikana hivi: “ndio watu wanaokana ufufuko wa wafu” (Lk 20: 27). Masadukayo walikuwa ni tabaka la kikabila kati ya Wayahudi wa Palestina wakiwemo kati yao familia za kikuhani, wamiliki wa ardhi na wafanyabiashara matajiri – ambao bila shaka walikuwa wazaliwa wa watawala wa kihasmonea. Jina lao linatokana na jina la Zadoki kuhani mkuu wa mfalme Daudi (2 Sam 19: 12) na walihesabiwa katika kundi lao makuhani wengi sana katika Israeli. Wao walishikilia kwa nguvu mafundisho ya Torati na kuyaacha kando mafundisho  makuu yasiyokuwamo humo. Matokeo yake walikataa ufufuko na uwepo wa malaika.  Katika masuala ya imani namna gani tunamwachia Mungu.
Juu ya namna gani ya kwanza  hakuna anayemjua mjumbe wa kifo atakuja lini. Ni busara kila tufanyalo katika maisha tujiulize, “Halafu?” Kama hadithi ya vijana wawili. Kijana mmoja alimuuliza mwingine. “Utafanya nini ukikua?” “Nitachukua somo la biashara.” “Halafu?” “Nitatafuta kazi.” “Halafu?” “Nitapata fedha nyingi kama mshahara.” “Halafu?” “Nitatafuta msichana nioe” “Halafu?” “Nitakuwa na watoto.” “Halafu?” “Nitawalea watoto” “Halafu?” “Nitakuwa babu?” “Halafu?” “Labda nitafanywa chifu.” “Halafu?” “Nitatawala watu.” “Halafu?” “Nitazeeka.” “Halafu?” ““Halafu?”, halafu, halafu, halafu usiulize zaidi ya hapo.” “Bila shaka uwe unafikiria kuwa siku moja utakufa.” Lakini tumaini linabaki kuwa kifo sio nukta, sio kikomo, bali ni alama ya mkato hadithi ya maisha inaendelea.
KWA NINI?
Masadukayo walijishughulisha na namna gani walipomuuliza swali Yesu la mtego. “Atakuwa mke wa nani?” Yesu alijishughulisha na “kwa nini?” Badala ya masadukayo kuleta mtanziko halisi, wanajaribu kuonesha upuuzi wa mahubiri ya Yesu juu ya ufufuko wa miili. Yesu analiondoa swali kutoka kwenye uwanja wa kuchekesha na kulifanya kauli nzito kuhusu ufufuko na kupaa kwake mwenyewe mbinguni na vile vile hatima ya ubinadamu na ukamilisho wa historia ya binadamu. Jibu la kwa nini ya Yesu kwanza Mungu wetu ni Mungu wa walio hai: “Kwani Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, maana kwa sababu yake wote wanaishi” (Lk 20: 38).
Pili dini ya kikristo ni dini ya ufufuko. Ukiondoa ufufuko unafuta dini ya kikristu. Kutokana na Pasaka wakristo inabidi wawe watu wa matumaini, watu wa ukweli, watu wa amani, na watu wa kutenda mema. “Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yetu haina maana…Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu.” (1 Wakorintho 15: 13-20).
Kifo Kiwe Zawadi
Kuna methali ya Ujerumani isemayo hastahili kuishi anayeishi kwa ajili yake tu. Binadamu wengi wako tayari kufia imani, kufia mtu, kufia dini, kufia shirika na kufia familia. Hawaishi kwa ajili yao nafsi zao tu. Ukiwafia wengine, unakifanya kifo kiwe zawadi kwa wengine. Ipo misingi ya kumfanya mtu amfie mwingine au alifie shirika, kampuni, au dini. Yesu aliifia dunia Yesu alifia watu kama Kayafa alivyotabiri ili waneemeke, waokoke. “Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.” (Yohane 18: 14). Yesu alikufa kwa ajili ya watu. Jambo la kujiuliza ni unafia nini? Kutokana na neno kufa tuna neno kufia yaani kupigana kwa namna zote ili kutetea kitu au jambo fulani. “Ni baraka kufia jambo fulani, sababu unaweza kwa urahisi kufia bure,” alisema Andrew Young. Kuwafia wengine hakuhitaji kujipendelea. Mtu anayejipendelea hafikiri kama kuna wengine duniani anajiona kitinda mimba duniani. Unapowafia wengine unafanya kifo chako zawadi kwa kizazi kijacho au watu wengine.

Kama unawafia wengine ukitoka haja kubwa kiache choo katika hali ya usafi maana wewe si wa mwisho kukitumia, wewe si kitinda mimba. Ukimaliza kidato cha nne usiharibu dawati au viti vya kukalia maana wewe si wa mwisho au kitinda mimba. Ukiviacha katika hali nzuri unawafia wengine. Fikiria kizazi kijacho. Kifie kizazi kijacho. Usimalize raslimali za dunia maana wewe si kitinda mimba duniani. Jitoe kwa ajili ya wengine. “Unatoa kidogo unapotoa kutoka katika mali yako, lakini unatoa zaidi unapojitoa wewe mwenyewe,” alisema Kahlil Gibran.
 Kuna methali isemayo, “kifo kinafuta kila kitu isipokuwa ukweli.” Kifo hakifuti ukweli wa maneno yetu na matendo yetu. Wakati wa kufani maneno yetu yawajenge tunaowaacha nyuma. Kuna mchungaji ambaye alikuwa anafanyiwa jubileo ya miaka 40 katika uchungaji. Alikuwa mgonjwa sana. Aliombwa kusema neno. Mwanzoni alikataa.Baada ya kuombwa kuzungumza alisema, “Afya ni mali.” Aliketi chini. Wakristu waliomba ufafanuzi. Aliamka na kusema. “Afya ni mali. Afya yangu si nzuri. Ni mbaya sana. Nyinyi mmechangia afya yangu kuwa mbaya.” Mchungaji huyo hakumwingiza Mungu katika ugonjwa wake. Kama Ayubu angetulia katika Mungu, “Bwana ametoa Bwana ametwaa jina lake litukuzwe.” Baada ya miezi miwili aliaga dunia. Kifo chake kiliwaacha waliopaswa kumpa huduma wakisutwa na dhamiri. Kifo chake hakikuwa zawadi kwa wengine. Kufa ni lazima, kama biblia isemavyo, “Kwa kila kitu kuna majira, na wakati kwa kila jambo duniani:…kuna…wakati wa kufa” (Mhubiri 3: 2), swali unakufa je? Yesu akiwa kufani aliwasamehe watesi wake. Kifo chake kilikuwa ni zawadi kwa watesi, walipata zawadi ya msamaha.
Juu ya kufanya vifo vyetu viwe zawadi, Henri J.M.Nouwen alikuwa na haya ya kusema, “Namna gani tunafanya vifo vyetu zawadi kwa wengine? Mara nyingi maisha ya watu yanaharibiwa, yanadhuriwa au kuwa na majeraha maisha yao yote kwa vifo vya jamaa au marafiki zao. Lazima tufanye tuwezalo ili kukwepa ili.Tunapokuwa kufani tunalowaambia wale ambao wako karibu nasi, iwe kwa kusema au kuandika ni muhimu. Tunapowashukuru, kuwaomba msamaha kwa makosa yetu na kuwasamehe kwa ya kwao na kuwaonesha nia ya kutaka waendelee na maisha yao bila kusutwa na dhamiri lakini wakikumbuka neema za maisha yetu basi vifo vyetu vinakuwa zawadi kweli.”

 Hasara kubwa si kifo bali  kinachokufa ndani mwetu. “Kifo si hasara kubwa sana katika maisha yetu. Hasara kubwa sana ni kile kinachokufa ndani mwetu wakati tunaishi,” alisema Normani Cousins mtunga insha na mwariri wa  Amerika (1912 – 1990). Wakati tunaishi kuna mambo ambayo yanaweza kufa kama shauku, moyo wa kutoa, moyo wa kujitoa, uchaji kwa Mungu, utii, usafi wa moyo. Vikifa ni hasara kubwa. 

Counter

You are visitor since April'08