Saturday, August 12, 2017

AMINI MPAKA UNAAMINI


             



             Jumapili ya 19 ya Mwaka A



  “Ewe mwenye imani haba mbona uliona shaka” (Mathayo 14:31)



1. Fal 19:9a, 11-13a

2. Rum 9: 1-5

3.    Mt 14: 22-33



Kwanza kuamini mpaka kuamini ni kuonyesha au kutangaza nia. Penye nia pana njia. Mtume Petro alipoona Yesu anatembea juu ya maji alionesha nia ya yeye kutaka kutembea juu ya maji. Petro alimwambia Yesu: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.” Petro alitangaza nia. Alionesha nia. Siku moja niliambatana na mchungaji kwenda kwenye yadi ya magari kumsaidia kuchagua gari zuri. Tulipofika pale tuliona magari mengi, tukaingia ndani na kuyakagua: Mark II, Toyota Corolla, Suzuki, Rava 4, Pick up, kutaja machache. Baada ya masaa mawili ya kukagua na kutazama nilimwambia, “Naomba tuchague sasa gari ambalo utanunua.”  Alinijibu: “Kusema kweli sina hata shilingi.” Nilimwambia: “Kwa nini usumbufu wote huu.” Alinijibu: “Namwonyesha Mungu nia yangu.” Onesha nia. Ukitaka kununua shamba hata kama huna hela, ulizia bei kwanza, kagua viwanja vilipo. Sala yetu iwe kama ya kijana mmoja kwenye Biblia, “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu” (Marko 9: 24). Petro kwa upande mmoja alikuwa na kuamini na kwa upande mwingine alikuwa na kutoamini. Kutangaza nia tu hakutoshi.

Pili, kuamini mpaka unaamini si kutazama dhoruba imebeba nini mtazame anayeibeba dhoruba. Kwenye ziwa, Yesu haamrishi mawimbi kutulia ili kumwonesha Petro kuwa si ghadhabu ya upepo iliyomtia katika hatari bali ukosefu wa imani,” alisema Mtakatifu Yohane Chrysostomu. Tunasoma hivi katika Injili: “Lakini alipouona upepo akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana niokoe” (Mt 14: 30). Petro ana ujasiri na woga. Anaanza vizuri, anaona dhoruba na kuogopa. Anakosa imani. Usimwambie Yesu nina tatizo kubwa. Liambie tatizo Mungu wangu ni mkubwa nitashinda. Yesu anabeba makubwa kuliko dhoruba. Kuna hadithi juu ya mbwa na tembo. Wanyama wote walibeba mimba wakati ule ule. Baada ya miezi mitatu mbwa alijifungua. Na baada ya miezi mitatu mingine alibebea mimba na kujifungua tena. Mara ya tatu alibeba mimba na kujifungua. Hapo tembo hajajifungua. Mbwa akamuuliza tembo: "Una hakika umebeba mimba ?" Tembo akamwambia mbwa : "Mimi nimebeba tembo sikubeba kambwa kadogo. Mtoto wangu anapozaliwa anatingisha ardhi. Akipita barabarani watu wanangoja apite na wanamstaajabia."  Yesu amebeba makubwa. Usijisumbue na kesho imebeba nini. Shughulika na anaye ibeba kesho



Tatu, kuamini mpaka unaamini kunahitaji hatua ya kwanza. Ukitembea kwa imani piga hatua ya kwanza. “Imani ni kupanda ngazi ya kwanza hata kama hauoni ngazi zote,” alisema mchungaji Dk. Martin Luther King Jr. Unapopiga hatua ya kwanza umeamini mpaka ukaamini. Petro alimjibu Yesu: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.” Akasema, Njoo. Hakusema maneno mengi bali: N-j-o-o. Petro alishindwa kutembea kwa imani juu ya bahari. Alikuwa na imani ya kumtoa kwenye mtumbwi hakuwa na imani ya kumfanya atembee juu ya bahari. Walau alijaribu kupiga hatua ya kwanza. .



Wana wa Israeli walipovuka bahari ya shamu inasemekana maji hayakutoa nafasi iliyowazi kwanza mpaka mtu mmoja alipoingia majini na kupiga hatua ya kwanza. Kwa macho ya mwili huyu mtu aliona maji. Kwa macho ya imani aliona njia kavu baharini. Yesu alipowambia wakoma kumi waende wajioneshe kwa makuani. Walikuwa hawajapona walipona walipokuwa wanapiga hatua kwenda mbele. Kwa kuona walikuwa bado na ukoma lakini walitembea kwa imani. Walipokuwa wanatembea walitakasika, walipona. Mungu anapoona umepiga hatua, anajua kuwa mtu huyu anatembea kwa imani. “Imani si kujaribu kuamini jambo bila ya kuzingatia ushahidi: imani ni kujaribu kufanya jambo bila kuzingatia matokeo,” alisema Sherwood Eddy.



Nne, kuamini mpaka unaamini ni kutumaini kuwa Yesu atajitokeza. Katika kilele cha dhoruba Yesu alijitokeza. Katika kilele cha hatari, katika upeo wa wasiwasi Yesu alijitokeza. Anakuja wakati ambapo hategemewi kabisa. Mitume walifikiri ni mzuka wakauotea mbali. Yesu ni Mkombozi wakubariki. Ni Mkombozi tunayeweza kumkimbilia. Alifanya kile ambacho binadamu hawezi kufanya. Alitembea juu ya maji. Vile ambavyo hatuwezi kufanya tumuachie yeye. Wakati tunapozama kwenye bahari ya matatizo tulie kwa sauti: “Bwana utuokoe !”



Kuna mtu ambaye aliota ndoto alikuwa anatembea kando ya bahari kwenye mchanga. Akiwa na furaha alipotazama nyuma aliona nyayo za watu wawili. Wakati wa shida na matatizo alipotazama nyuma aliona nyayo za mtu mmoja. Alimuuliza Yesu: maana yake nini? Yesu alimwambia kuwa wakati wa furaha wanakuwa pamoja wanaambatana pamoja. Mtu huyo alidadisi: “Mbona wakati wa shida naona nyayo zangu peke yangu?” Yesu alimwambia kuwa wakati wa shida anakuwa amembeba mgongoni. Ndiyo maana anaona nyayo za mtu mmoja.



Tano, kuamini mpaka kuamini ni kuwa na sala za mishale wakati wa hatari. Hizi ni sala fupi. Sala fupi hufika mbinguni (Methali ya Kidachi). Petro alilia kuomba msaada kwa maneno machache tu: “Bwana, Niokoe!” (Mt 14:30). Ilikuwa sala tosha na ya kueleweka. Sala fupi inaweza kutolewa wakati wowote mahali popote. Mbali na sala rasmi na ndefu; tujitahidi kutunga sala zetu baada ya kuona ile ya petro, jaribu hii kabla kuanza safari, “Bwana, tusaidie tusafiri vema.” Unapokuwa na hasira sema: “Bwana, nisaidie niwe mvumilivu,” unapokuwa na mambo mengi ya kufanya, Sali: “Bwana, panga siku yangu.” Jaribu hii unapokuwa mezani “Ahsante Bwana kwa chakula hiki.”“Tusisali sala ndefu, zinazotutoa nje lakini tusali sala fupi iliyo na mapendo kamili. Tusali kwa niaba ya wasio sali.  Tuwakumbuke, kama tunataka kuweza kupenda, lazima tuweze kusali!”(Mama Teresa wa Calcutta). Kuna ambao radi ikipiga wanasali: “Yesu na Maria.” Kuna wengine wanasema kile kilichojaa moyoni: “Panya amedondokea kwenye sufuria.”

Counter

You are visitor since April'08