Saturday, March 18, 2017

UMEBEBA NINI?


                                            
                                                               Jumapili ya 3 ya Kwaresima
1.       Kut 17: 3-7
2.       Rum 5: 1-2, 5-8
3.       Yn 4: 5-42
 
                               “Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda” (Yohane 4:27).
Masomo ya leo yanahusu wabebaji. Musa alibeba fimbo. Mwanamke Msamaria alibeba mtungi na Habari Njema baadaye. Mitume walibeba chakula. Yesu alibeba maji ya uzima.  Bwana Yesu alibeba Teolojia aliyozungumza juu yake na mwanamke Msamaria ambaye hakuwa malaika alikuwa na hadithi yake.
Mwanamke Msamaria alibeba mtungi. “Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda” (Yohane 4:27). “Nakuuliza na kujiuliza: ‘Nini mtungi wako wa moyoni, ambao unakuelemea, ambao unakuweka mbali na Mungu? Tuuweke kando kidogo na mioyo yetu tusikilize sauti ya Yesu akitupa maji ya aina nyingine, maji mengine yanayotuleta karibu na Bwana,” alisema Papa Fransisko.  Mwanamke huyu alikuwa kama mtungi wenye nyufa.
Kuna hadithi juu ya mchota maji. Alikuwa akichota maji na kuyapeleka kwa mfalme. Alitumia mitungi miwili. Mtungi mmoja ulikuwa na nyufa. Hivyo maji yalimwagika njiani. Mtungi huo ulilalamika kwa maana ulifikishwa nyumbani bila chochote. Mtungi mwingine ulifikishwa nyumbani umejaa maji. Mchota maji aliuambia mtungi uliokuwa unalalamika. Tazama nyuma yako maua yanayopendeza. Nilipanda mbegu za maua njiani baada ya kuona kuwa una nyufa na umekuwa ukizimwagalia. Mungu anaweza kutumia nyufa zetu kutoa jambo zuri. Bwana Yesu alitumia nyufa za mwanamke huyu Msamaria kutoa jambo zuri, mahubiri juu ya Maji ya Uzima.
Mwanamke Msamaria alibeba aibu. Alikuja kuchota maji saa sita ili kukwepa maneno na macho ya watu. Kisima kilikuwa mahali pa kukutana na mahali pa ufunuo wa mambo. Ilikuwa ni sehemu ya jumuiya kukutana. Maji yalichotwa asubuhi sana na jioni. Wanawake na wasichana walikusanyika kisimani. Palikuwepo muda wa kubadilishana habari: nani alikuwa anachumbiwa, nani alizaa nje ya ndoa, nani anauza sana sokoni, nani amejifungua mtoto, nani anaiba waume za watu. Walifua nguo zao karibu na maeneo hayo na kunyesha mifugo. Ni katika kisima Rebecca na Rachel walipata wachumba wao: Isaka na Yakobo. Palikuwepo na mkono wa Mungu katika wanandoa hawa (Mwanzao 24: 10-67;  29: 1-14). Kisimani ni sehemu ya ufunuo. Hagar mwenye mimba alipata ufunuo kisimani (Mwanzo 16: 1-14)
Mwanamke msamaria alibeba maswali. “Injili inamwonesha Yesu akikutana na Mwanamke Msamaria huko SIkari, karibu na kisima cha zamani ambapo mwanamke alienda kuchota maji kila siku…Yesu alihitaji kukutana na mwanamke Msamaria ili kufungua moyo wake: alimuomba maji ili kuleta kwenye mwanga kiu cha mwanamke. Mwanamke anahamasika kwa kukutana huku. Anamuuliza Yesu maswali kadhaa ya msingi ambayo sote tunayabeba moyoni, lakini mara nyingi hatuyajali. Sisi nasi pia tunayo maswali mengi ya kuuliza, lakini hatuna ujasiri wa kumuuliza Yesu! Kwaresima ndugu zangu ni fursa ya kujitazama ndani na kuelewa mahitaji yetu ya kweli kabisa ya kiroho, na kuomba msaada wa Bwana katika sala,” alisema Papa Fransisko (Malaika, Machi 23, 2014). Mwanamke Msamaria alikuwa na ujasiri wa kumuuliza Yesu maswali. Kuuliza si ujinga: “Je, wewe uliye Myahudi, unaniomba mimi niliye mwanamke Msamaria, maji ya kunywa?” (Yohane 4:9); “Bwana, huna chombo cha kutekea, na kisima ni kirefu; utapataje maji ya uzima?” (yohane 4:11); “Je, wewe  u mkubwa kuliko baba yetu Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe, na wanawe, na wanyama wake wakanywa maji yake?” (Yohane 4: 12); “Bwana, nipe maji hayo, nisione tena kiu, wala nisifike tena hapa kuteka maji” (Yohane 4:15).
Mwanamke Msamaria alibeba Habari Njema. Alienda mjini na kuwaambia watu: “Njoni mtazame mtu aliyeniambia yote niliyotenda. Labda huyu ni MAsiya?” (Yohane 4: 29). Watu walitoka mjini. Mwanamke anakuwa mfuasi na mmisionari. Watu wa mjini wanakuja kwa Yesu kufuatia neno lake pasipo kuhitaji ishara. Nasi tubebe Habari Njema.
Mwanamke alibeba maneno ya sifa: Alimwita kwanza Yesu Myahudi. Baadaye alimwita Bwana. Halafu alimwita nabii. Hatimaye alimwita Masiya. Tunapotoa sadaka ya vitu tumpe Mungu pia sadaka ya maneno.“Mtolee Bwana maneno ya kitubio” (Hosea 14:3). Mwanamke huyu alitoa sadaka ya maneno.
Mitume walibeba chakula: “Rabbi kula (Yohane 4:30);” Chakula ni picha nyingine ya uzima wa milele. Kama mwanamke alivyoshinda kutoelewa kwake kuhusu kuabudu, sasa wafuasi wanaalikwa waache kutoelewa kwao kuhusu chakula na kanuni za usafi. Kama chakula kinavyoliwa kwa kushirikiana, vivyo hivyo Mungu anashirikisha zawadi ya uzima wake wa kimungu kwa binadamu.
Mitume walibeba chuki bila sababu: Katika hadithi ya Mwanamke Msamaria Injili inasema kuwa  wafuasi walishangaa kuwa Bwana wao alikuwa anaongea na mwanamke huyu. Lakini Bwana ni mkubwa kuliko chuki yao bila sababu, ndiyo maana hakuogopa kumhutubia mwanamke: huruma ni kubwa zaidi ya maamuzi mbele (chuki bila sababu). Lazima tujifunze jambo hili vizuri! Huruma ni kubwa zaidi ya chuki bila sababu, na Yesu ni mwenye huruma sana! Sana!” alisema Papa Fransisko wakati wa Sala ya Malaika Machi 23, 2014.
Musa alibeba fimbo. “Bwana akamjibu Musa, “…ukachukue mkononi ile fimbo uliyopiga nayo mto” (Kutoka 17:5).  Kila ulicho nacho Mungu anaweza kukibariki kikasaidia kuleta muujiza. Mungu alimuuliza Musa kabla ya hapa: Una nini? Musa alisema nina fimbo. Mungu alisema inatosha. Cheti chochote ulicho nacho Mungu anaweza kukitumia kukubariki.
Yesu alibeba maji ya uzima: Yesu Kristo anambeba Roho wa Mungu anayeonjeka katika Ekaristi (Ufunuo 21: 6; 22:17).

Counter

You are visitor since April'08