“Basi, kesheni, kwa
sababu hamjui siku wala saa” (Mathayo 25: 13) jmggyt
|
|
|
UTANGULIZI
Mafuta: Yanaweza kuwa na tafsiri nyingi. “Busara ni kama ufuta;
unaukaanga kadiri unavyokula” (Methali ya Batoro, Uganda). Taa zetu hazina budi
kuwa na mafuta. Mafuta ni busara. Kujiandaa ni busara. Pia mafuta yanaweza
kueleweka kama upendo hai. Ndio huo unaoleta tofauti baina ya wanawali
wapumbavu na wenye busara. Kadiri ya Mt. Augustino, “Mafuta yanamaanisha furaha.” Kufuatana na ukweli huo, “Mungu wako,
amekupaka mafuta, kwa mafuta ya furaha, kuliko wenzako” (Zaburi 45:8). Mafuta
kuwekwa kwenye vyombo ni furaha iliyotunzwa moyoni na kwenye dhamiri.
Taa: Taa inaweza kuwa na tafsiri nyingi. Taa ni imani. Taa ni
matendo mema. tKadiri ya Baba wa Kanisa Mt. Augustino: “Taa wanazobeba mikononi ni matendo yao
ambapo ilisemwa, ‘mwanga wenu uangaze mbele ya watu.’” (Mt 5:6).
Mabikira: Wanaojiandaa wanalinganishwa na mabikira watano wenye
busara na wale ambao hawajiandai wanalinganishwa na mabikira wapumbavu.
Bwana harusi: Ni Yesu. Yesu anakuja namna mbili. Anapomchukua mtu
mmoja. Namna ya pili atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Hakuna anayemjua
mjumbe wa kifo atakuja lini. Ni busara kila tufanyalo katika maisha tujiulize,
“Halafu?” Kama hadithi ya vijana wawili. Kijana mmoja alimuuliza mwingine.
“Utafanya nini ukikua?” “Nitachukua somo la biashara.” “Halafu?” “Nitatafuta
kazi.” “Halafu?” “Nitapata fedha nyingi kama mshahara.” “Halafu?” “Nitatafuta
msichana nioe” “Halafu?” “Nitakuwa na watoto.” “Halafu?” “Nitawalea watoto”
“Halafu?” “Nitakuwa babu?” “Halafu?” “Labda nitafanywa chifu.” “Halafu?”
“Nitatawala watu.” “Halafu?” “Nitazeeka.” “Halafu?” ““Halafu?”, halafu, halafu,
halafu usiulize zaidi ya hapo.” “Bila shaka uwe unafikiria kuwa siku moja
utakufa.” Lakini tumaini linabaki kuwa kifo sio nukta, sio kikomo, bali ni
alama ya mkato hadithi ya maisha inaendelea. Kutojiandaa ni kujiandaa Kutokuwa
katika wateule. Jiandae.
MAHUBIRI YENYEWE
“Ukinipa saa sita ili niukate mti, nitatumia
saa nne za awali kulinoa shoka langu,” alisema
Abrahamu Lincoln (1809-1865). Hiyo ni busara. Hayo ni mafuta katika taa.
Somo la meneno hayo ya Abrahamu ni kuwa kujiandaa kunatangulia mafanikio. Kwa
kushindwa kujiandaa, unajiandaa kushindwa. Kuna mambo ambayo yanawafanya watu
wasijiandae.
Kwanza ni kuwa katika eneo la
faraja. Ili ni eneo ambapo watu wanajiona wako salama, wamefarijika. Hawataki kujisumbua.
Kazi ya kweli ya kupigia debe ufalme wa mbinguni au maendeleo ni kuwasumbua
waliofarijika na kuwafariji waliosumbuka. Lazima kutoka katika eneo la faraja
ambalo linakufanya usifanye lolote la maana na kujiandaa. Ili kuleta mabadiliko ni lazima kuvunja uzio
na ukuta wa eneo la faraja inayokufanya kubweteka. Toka ndani ya sanduku.
“Faraja ni mtego wako mkubwa na kutoka katika eneo la faraja ni changamoto yako
kubwa,” alisema Manoj Arora. Katika Biblia tuna watu waliovunja ukuta wa eneo
la faraja ni Musa: “ Kwa nguvu ya imani, Musa alipofikia utu uzima, alikataa
kuitwa mwana wa binti Farao” (Waebrania 11: 24). Musa alikuwa kwenye eneo la
faraja la kuitwa mwana wa binti Farao. Mambo mawili yalimfanya kuacha eneo la faraja: nayo ni nguvu ya imani
na utu uzima.
Kuna nguvu ya imani. Katika kitabu cha maombi tunasali hivi:
“Iliwalazimu wanawali kuwa na taa, yaani, imani: Utuangaze kutumia imani kama
taa ya njia ya kweli katika maisha yetu ya kila siku.” Musa alitumia imani kama
taa nasi tutumie imani kama taa.
Kuna utu uzima. Wanawali wapumbavu hawakutenda kama watu wazima. Kuna
mwanaume alimuuliza mke wake utaweza kweli kwenda Dubai kuchukua mzigo wa
biashara bila kusumbuliwa na wanaume huko? Mwanamke alimjibu mume wake: “Mimi
ni mtu mzima.” Kuna kijana ambaye alihama kwa kaka yake akaanza kupanga nyumba.
Kaka yake alimuuliza utaweza kuyamudu maisha. Alimjibu: “Mimi ni mtu mzima.” Ni
utu uzima ambao unakufanya kung’amua
kuwa: mtegemea cha nduguye hufa akiwa maskini. Kuna kijana alikuwa anaenda
kuanza masomo chuo kikuu, mzazi akamwambia tusindikize hadi Dodoma. Alimjibu
mzazi: “Mimi ni mtu mzima. Hakuna haja ya kunisindikiza.” Mfalme alikuwa na
mtumishi ambaye alimdharau na kumuona kama mtoto. Siku moja alimpatia fimbo
akasema ukimuona mtu mzima ambaye hajiandai jua ni kama mtoto mpe fimbo hii.
Mtumishi alizunguka hakumpata mtu wa namna hiyo. Siku moja alisikia mfalme yupo
kitandani anaumwa sana kiasi cha kuchungulia kaburi. Alienda na kumuuliza:
ukifa huko unakokwenda umeishajitengenezea marafiki? Mfalme alisema: “Hapana.”
Mtumishi alimpa fimbo na kumwambia: “Wewe sio mtu mzima.”
Jambo la pili linalotufanya tusijiandae ni kusitasita. Kuna
mtu ambaye alisema: “Kusitasita ni chanzo cha matatizo yangu yote. Hata hivyo
sijui vizuri maana ya neno kusitasita kesho nitatazama maana yake kwenye
kamusi.” Kutojiandaa ni kujiandaa kushindwa. Ngoja ngoja huumiza tumbo. Asubuhi
ni wakati wa kuweka kipimo cha kasi utakayotumia. Kuna nguvu ya kufanya mambo
mapema. Kuna mtu aliyeambiwa kuna ng’ombe dume watatu kwenye zizi, ukiweza
kukamata mkia wa mmojawapo utapewa zawadi ya milioni mbili. Ng’ombe wa kwanza
kujitokeza alikuwa mkali, macho makali, mnene na wa kutisha. Mtu huyo akaogopa
kushika mkia wake. Wa pili kujitokeza alikuwa mkali zaidi na wa kutisha zaidi.
Mtu huyo akangoja wa tatu. Wa tatu alikuwa amekonda, hana nguvu. Mtu huyo
akasema nitashika mkia wa huyo. Bahati mbaya hakuwa na mkia. Alishindwa kufanya
mambo mapema. Adui ya nguvu ya mapema ni kusitasita.
Jambo la tatu ambalo linatufanya
tusijiandae ni mazoea mabaya. Kuna methali ya Tanzania isemayo, “Huwa nazaa
watoto namna hii, aliuawa na mimba ya tisa.” Mazoea yanaweza kupofusha macho
yetu, na kutufanya viziwi. Ukimtia chura kwenye maji moto ataruka ili atoke.
Lakini ukimtia kwenye maji baridi na kupasha joto pole pole. Chura hatajua ni
lini maji yamekuwa ya moto. Mazoea yanamfanya mtu hasishtuke. Mazoe ya kutenda mema yatakusaidia.
Jambo la nne linalotufanya tusijiandae ni inesha au
ubaridi au kingungumizi cha kuanza.
“Watu wengi hushindwa kwa sababu hawaanzi. Hawaishindi inesha. Hawaanzi,”
alisema Ben Stein. Jiulize umefikaje ulipo: kwa kuelea au kwa kupiga makasia.
Kama ni kwa kuelea utakuwa hauna mwelekeo na dira. Kama kwa kupiga makasia ina
maana unafanya kitu fulani. Palipo na inesha kuna kushindwa kuonesha hisia kali
au shauku. Hakuna bashasha. Inesha ni kutofanya lolote. Kuna hadithi ya fisi
aliyetoa kipande cha nyama kwenye sufuria. Kilikuwa ni cha moto. Kilimchoma
midomo. Fisi wenzake wakamwambia, “Tema.” Akawajibu. “Niteme utamu.” Wakazidi
kumshauri, “Meza.” Akawajibu, “Nimeze moto.” Huu ni ubaridi unaoletwa na kukosa
uamuzi.
Kujiandaa ni kujiandaa kushinda. Mwanamke
mmoja alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha kusindika nyama. Siku moja baada
ya kumaliza kazi zake pale kiwandani alienda katika chumba chenye freezer (cold
room) ambako nyama zilikuwa zikihifadhiwa kukagua baadhi ya bidhaa. Kwa bahati
mbaya wakati yupo kwenye hicho chumba katika harakati za hapa na pale akausukuma
mlango, ukajifunga. Hakukuwa na msaada wowote wa kuweza kuufungua mlango ule.
Alianza kulia na kupiga kelele za kuomba msaada wa kufungiliwa, lakini kelele
zake hazikuwa rahisi kusikika nje ya hicho chumba kidogo, na wafanyakazi wote
pale kiwandani walikuwa wameishaondoka. Masaa mawili baadae akiwa katika hali
ya kukaribia kukata roho kutokana na baridi kali iliyoko kwenye hicho chumba.
Ghafla mlinzi wa geti la kiwanda hicho alifungua mlango alimokuwamo yule
mwanamke. Alitahamaki kumkuta mwanamke yule katika hali ile mbaya.
Basi jitihada za kumpa huduma ya
kwanza kumpeleka hospitali ikafuata. Baada ya kutolewa hospitalini alipata
wasaa wa kumuuliza yule mlinzi ilikuwaje akafungua mlango wa cold room wakati
ilikuwa si ratiba yake na vile vile ilikua si kazi yake? Maelezo ya yule mlinzi
yakawa kama ifuatavyo:
''Nimefanya kazi kwenye hiki
kiwanda kwa miaka 38 sasa, mamia ya wafanyakazi wanatoka na kuingia kiwandani
lakini wewe peke yako kati ya wote ndiye uliyekuwa ukithubutu kunisalimia
asubuhi na kuniaga kila jioni unapoondoka kiwandani. Ulipokuja kazini asubuhi
ulinisalimia kama kawaida na kunijulia hali. Lakini baada ya kazi na wafanyakazi
kuanza kutoka kurudi, nilitegemea kusikia salamu yako, niliendelea kusubiri
lakini cha ajabu mpaka watu wote wakawa wametoka na wewe sikuona sura yako.
Nilianza kuingiwa na maswali mengi, na ndipo nikapata wazo la kuanza kuzunguka
maeneo yote ya kiwanda na baadae chumba baada ya chumba. Na ndipo nilipokukuta kwenye chumba cha barafu. Funzo ni kuwa
tenda mema kuna kesho. Ishi vizuri na kila mtu, mheshimu kila mtu bila kujali
hadhi yake, ukubwa wala udogo wake, kwani hujui kesho atakua wapi katika kuwa
sababu ya MSAADA kwako.
HITIMISHO: Maisha ya kikristo yanadai kazi, kuwa macho na kuwa tayari.