MISA YA USIKU
1.
Isa 9: 2-7
|
2.
Tit. 2: 11-14
|
3.
Lk 2: 1-14
|
UTANGULIZI
Yesu anapoingia vivuli
vinatoweka. Alizaliwa usiku ili kufukuza giza. Ili afukuze giza tumpe nafasi.
Krismasi ni Kristu Kwanza.
MAHUBIRI YENYEWE
Krismasi ni zaidi ya
mti wa Krismasi. Krismasi ni zaidi ya kadi za Krismasi. Krismasi ni zaidi ya
likizo. Krismasi ni zaidi ya kubadilishana zawadi. Krismaisi ni zaidi ya kula
vizuri na kunywa sana . Krismasi ni zaidi ya kuuuza na kununua. Krismasi ni
zaidi ya kununua nguo mpya. Kuna mwanaume mmoja alikuwa anakoa sana Kanisani
siku ya Krismasi. Tulipomaliza adhimisho la Misa nilimuuliza mke wake, “Mbona
mmeo alikuwa anakoa sana Kanisani.” Nilijibiwa na huyo mama, “Yeye ni kawaida
yake siku ya Krismasi akinunua suti mpya.”
Tunapokimbizana kusherehekea Krismasi tujiulize, nini chanzo cha haya
yote? Krismasi ni Kristu kwanza. Krismasi ni sherehe ya kuadhimisha siku ya
kuzaliwa Yesu Kristu kama wakristo wanavyoamini. “Krismasi ni Kristu, Kristu wa
haki na upendo, wa uhuru na amani,” alisema Francis J. Spellman. Tukumbuke kuwa
Yesu Kristo mwana wa Maria alipozaliwa alikosa nafasi katika nyumba ya wageni.
Je, atabanana katika moyo wako na wageni wengine? Je atakosa nafasi katika moyo
wako. Kama kwako Krismasi ni Kristu kwanza hatakosa nafasi katika moyo wako
kama alivyokosa nafasi katika nyumba ya wageni.
Tunasoma hivi katika Biblia: “Walipokuwa
wakikaa huko, siku zake za kuzaa zilitimia, (Maria) akamzaa mwanawe, mzaliwa wa
kwanza. Akamzungushia vitambaa, akamlaza horini, kwa maana walikosa kupata
nafasi katika nyumba ya wageni” (Luka 2:7). Hakukuwa na chumba katika Nyumba ya
wageni. Nyumba ya wageni ni hoteli. Inamaanisha ni sehemu yoyote ambayo msafiri
aliweza kukirimiwa. Hakukuwa na chumba kwa ajili ya Yesu katika Bethlehemu
ikiwa ndiyo ishara ya kukataliwa Yerusalemu. Kushughulikia likizo ya Krismasi
tukamsahau Yesu ni kumyima nafasi moyoni ambao ni kama nyumba ya wageni.
Tukiitazama Krismasi kwa miwani ya
kubadilishana zawadi, “Krismasi imejikita katika kubadilishana zawadi: zawadi
ya Mungu kwa binadamu-Mtoto wake; na zawadi ya binadamu kwa Mungu pale
tunapojitoa kwa Mungu kwanza,” alisema Vance Havner. Krismasi ni zawadi toka
kwa Mungu ambayo mtu hawezi kuifanya iwe yake binafsi bila kumshirikisha
mwingine. Mshirikishe mwingine habari njema za Yesu Kristu.
Tukitazama Krismasi kwa miwani ya mti wa
Krismasi, ni zaidi ya mti wa Krismasi. “Yeye asiye na Krismasi moyoni mwake
hawezi kuikuta chini ya mti,” alisema Roy L. Smith. Chini ya miti nyingi ya
Krismasi tarehe 25 Desemba patakuwepo na zawadi nyingi. Katika mti wa Kalvari
msalabani palikuwepo na zawadi moja lakini inazijumlisha zawadi zote- zawadi ya
Mungu kwetu ya mwana wake wa pekee Yesu Kristu. Tunapochukua zawadi toka mtini
wa Krismasi tukumbuke zawadi kubwa Yesu Kristu katika mti wa msalaba. Krismasi
ni Kristu kwanza.
Tukiitazama Krismasi kwa miwani ya upendo,
“Kuna upendo wakati wa Krismasi kwa sababu Krismasi ilitokana na upendo. Moyo
huu wa upendo na kumtukuza Mungu ubaki ukiwaka,” alisema Joseph Emms Seagram
(1841 - 1919) mwingereza raia wa Canada
na mwanasiasa. Natamani moyo huu wa Krismasi tungeutia katika chupa za
marashi na kutumia marashi haya kila siku. Kila siku ifanye Krismasi katika
familia yako kwa kuwapulizia watu marashi ya maneno ya upendo. Namna hii
Krismasi itakuwa ni Kristu Kwanza kwa vile tunaweka katika matendo upendo wake.
Kuna mpiga picha siku ya Krismasi ambaye wakati anapiga picha alikuwa karibu
sana na mishumaa inayowaka shati lake lilichomwa na moto. Watu walizima moto
huo. Mchungaji mmoja alianzia katika tukio hilo kuhubiri. Akisema, “Kuna mmoja
wetu ambaye amewaka moto kwa ajili ya Kristu.” Nasi tuwake moto kwa ajili ya
Kristu si katika kuchoma nguo bali tuwake moto wa mapendo. Yesu alikuja kuishi pamoja nasi ili baadaye
tuweze kuishi naye mbinguni. Hivyo, tumtangulize tunapoadhimisha Sherehe ya
Krismasi.
KRISMASI
NI UPENDO KWA VITENDO
“Krismasi…ni upendo kwa
vitendo,” alisema Dale Evans Rogers (1912-2001) mchezaji cinema wa kike,
mwimbaji na mtunzi wa nyimbo. Nakubaliana na maneno ya mtunzi huyo. Krismasi
sio kisingizio cha watu kulewa, Krismasi sio kisingizio cha walinzi wanaolinda
mali ya umma kutofanya kazi. Krismasi sio kisingizio cha watu kutapanya hovyo
pesa na kukosa kubana matumizi. Krismasi si kisingizio cha baadhi ya wazazi
kuwapokea watoto wa shule waliokuja likizo kwa shingo upande. Krismasi sio
kisingizio cha kuchanganyikiwa. Krismasi ni wakati wa kufanya matendo ya
upendo. Krismasi sio tu kipindi cha kufungua zawadi ni kipindi cha kuwafungia
wengine zawadi. Krismasi ni upendo kwa vitendo. Krismasi ni sherehe ya kuzaliwa
Bwana wetu Yesu Kristu. Alizaliwa kuokomboa ulimwengu. Ni jambo la upendo.
Kila mfuasi wa Kristu
hata mwanasiasa anatakiwa siku ya Krismasi kufanya matendo ya upendo. Papa
Benedict XVI Kiongozi wa juu kabisa katika Kanisa Katoliki katika kitabu chake,
“Mungu ni Upendo,” aliandika, “ni
lazima upendo uhuishe maisha yote ya walei, na kwa hiyo uhuishe pia kazi zao
zote za siasa, ziwe pia kazi zao za ‘upendo kijamii.” Upendo pia utawale siasa.
Siasa ikiwa kazi ya upendo kijamii Krismasi inakuwa ni upendo kwa vitendo. Hii
ndiyo maana ya Krismasi. Mama Tereza wa Calcutta (1910-1997) mshindi wa zawadi
ya Nobel 1979 alikuwa na mawazo kama haya aliposema: “Ni Krismasi kila
unapomruhusu Mungu awapende wengine kupitia kwako…ndiyo, ni Krismasi kila siku
unapompa tabasamu ndugu yako na kumpa mkono wa salamu.”
Juu ya kuzaliwa Yesu
Kristu tunasoma hivi katika Biblia:
“Walipokuwa wakikaa huko, siku zake za kuzaa zilitimia, (Maria) akamzaa
mwanawe, mzaliwa wa kwanza. Akamzungushia vitambaa, akamlaza horini, kwa maana
walikosa kupata nafasi katika nyumba ya wageni” (Luka 2:7). Yesu alinyimwa
nafasi katika nyumba ya wageni. Tunapokosa kutenda matendo ya upendo kwa
vitendo tunamunyima Yesu nafasi mioyoni
mwetu siku ya Krismasi. “Krismasi ni kipindi cha kuwasha moto wa ukarimu
ukumbini, na miale ya upendo moyoni,” Washington Irving. Bila kufanya hivyo ni
kumunyima Yesu nafasi moyoni. Krismasi ni kipindi cha kuonesha ukarimu na
kusamehe.
Krismasi si wakati wa
watu kugombana na kutumia mabavu. Kufanya hivyo ni kumunyima Yesu Kristu nafasi
mioyoni. Kuna insha iliyoandikwa na Mkurugenzi wa California Department of Mental Hygiene akionya: “Kipindi cha
Krismasi kinajulikana kinasifika kwa msongo wa mawazo na matendo zaidi ya
matumizi ya mabavu kuliko kipindi chochote cha mwaka.” Krismasi tofauti na
ujumbe huo hakina budi kuwa kipindi cha kumwinua Yesu Kristu badala ya kuinua
matumizi ya mabavu maana yeye alitetea amani. “Amani dunia itadumu,
tutakapoiishi Krismasi kila siku,” alisema Helen Steiner Rice.
Hali ya hewa ya Krismasi
haina budi kuwa ya upendo. Mtoto mmoja aliyepewa sanamu za kuchezea.
Alilalamika kwa mama yake. Mimi naonyesha upendo kwa sanamu hizi lakini zenyewe
hazionyeshi upendo. Yesu Kristu kwa kuzaliwa tuonyeshe upendo kwake. Kipimajoto
cha upendo ni upendo kwa jirani zetu. Upendo kwa jirani lisiwe suala la
Krismasi bali suala la maisha. Tusingoje Krismasi kupeana zawadi. Krismasi huwe
utamaduni wa maisha. “Nitaiheshimu Krismasi moyoni mwangu, na kujaribu kuitunza
mwaka mzima wote,” alisema Charles Dickens. Huwezi kupenda chumvi bila kupenda
muuzaji wa chumvi. Huwezi kupenda Krismasi bila kumpenda Kristu. Benjamin
Franklin alisema: “Watu wengi wanasheherekea siku ya Kuzaliwa Kristu! Wachache
kweli, wanashika maagizo yake!” Ndugu msomaji nakutakia furaha ya Krismasi
ambayo ni matumaini; roho ya Krismasi ambayo ni amani; moyo wa Krismasi ambao
ni upendo kwa vitendo