JUMAPILI YA 32 YA MWAKA C
“Kwani
Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, maana kwa sababu yake wote wanaishi”
(Lk 20: 38).
1. 2 Makabayo
7: 1-2.9-14
|
2. 2 Thess 2:
16-3:5
|
3. Lk 20:
27-38
|
Meli ikianza
safari yake toka Kisumu hadi mwanza Tanzania wale walioko Kisumu
wanasema meli imeenda. Wale walioko Tanzania wanaoiona kwa mbali
wanasema meli imekuja. Mtu akiaga dunia tunasema “Ameenda.” Walioko mbinguni au
toharani wanasema, “Amekuja.” Hivyo kifo
sio kituo bali ni koma. KWETU KIFO SIO
UKUTA NI MLANGO. Kwetu kifo sio kizuizi bali ni daraja. Mbio za sakafuni
huishia ukingoni. Mbio zetu haziishii ukutani bali tunapitia zinafika mlangoni
na tunapita.
Hadithi ikiwa nzuri sana kwenye gazeti inakatizwa na
chini yake yanaandikwa maneno itaendelea toleo lijalo. Mtu anapoaga dunia maisha yake yanaendelea toleo lijalo. Toleo Lijalo ni motoni,
mbinguni au toharani. Kuna mshika kipenga aliyeaga
dunia akaenda motoni. Huko alikuta uwanja mzuri sana
na watu wamejipanga kucheza mpira alifurahi sana . Timu mbili ziliingia yeye akashika
kipenga. Wachezaji wakasalimiana na kushika nafasi zao. Yeye mshika kipenga
akauliza: “Mpira wapi?”. Aliambiwa huku ndio maana kunaitwa motoni. “The hell
of it” ni kwamba hakuna mpira. Motoni ni
kama una hamu ya chakula na hauwezi ukala. Kuna kitu kinakosekana.
MZAHAA JUU YA KIFO NA MAISHA BAADA YA KIFO: “Ukristo kwa kiini chake
ni dini ya ufufuko. Dhana ya ufufuko iko kwenye kitovu chake. Ukiondoa ufufuko,
ukristo unauharibu,” alisema John R. W. Stott.
Mungu wetu si Mungu wa wafu ni Mungu wa walio hai. Masadukayo kidini
walikuwa mahafidhina na hawakupokea mafundisho yaliyokuwa nje ya vitabu vya
kwanza vya Agano la Kale. Waliyakataa mafundisho juu ya ufufuko, malaika na
pepo wabaya. Mara kwa mara Yesu alibishana nao. Kusema kweli kifo si nukta bali
ni alama ya mkato maisha yanaendelea. Kule
mbinguni hapakuwepo kuoa au kueolewa. Tutaishi kama malaika. Tumefanywa kidogo
chini ya malaika (Zaburi 8:6).
Masadukayo
walifanya mzahaa juu ya kifo na maisha baada ya kifo. Walifikiri kifo ni mwisho
wa safari. Walifikiri kifo ni kikomo. Walifikiri kifo ni kituo. Walijiuliza
kama “Alichokiunganisha Mungu mwanadamu
hasitenganishe.” Kwa nini sasa Mungu atenganishe mbinguni?” Walimuuliza
swali Yesu lenye mtego. Walitazamana. Walikonyezana. Wakasema tumumweza.
Walimuuliza kama mambo mazuri yatakuwa huko. Kuna wengine labda wanafanya mzaha
kama huo. Wanauliza kama kuwa mbinguni ni
sherehe nani watakuwa wanapika? Kuni hizo zitatoka msitu upi? Jiko litakuwa
wapi? Ni aina gani ya pombe zitakuwa huko? Mafarisayo walikuwa kama chura ambaye alikuwa anabishana na kusema hakuna
nchi kavu dunia yote ni maji. Ni kama watoto wawili mapacha waliokuwa kwenye
tumbo la mama yake mmoja alipozaliwa mwingine alilia sana na kusema kaka yangu ameaga dunia. Wote
wakakutana duniani.
MASADUKAYO WALIFIKIRIA MAMBO YA KARIBU
Tunafikiri mambo
ya karibu. Sala zetu ni za mambo ya karibu na sio za mambo ya mbali sana . Watoto shuleni
wanafikiria maksi. Pengie tunafikiria kesho. Mtu anaenda kufanya mkataba
anafikiria atakavyomdanya mtu. Hafikirii kesho itakuwaje.
MUNGU WA IBRAHIMU NI MUNGU WAKO NA WA JAMAA YAKO
ALIYEKUFA
Abrahamu anaitwa
“Rafiki wa Mungu,” (Isaya 41:8), “Mtumishi wa Mungu” (Zaburi 105:6) Mungu
alimbadili Abrahamu anaweza kukubadili wewe. Abramu alimdanganya Farao na
kusema Sarai si mke wake (Mwanzo 11: 10 – 20) Sasa Mungu wetu ni Mungu wa Ibrahimu. Isaka
alidanganya hakusema kuwa Rebeka ni mke wake maana alikuwa mzuri sana . (Mwanzo 26: 6-10)
Yakobo aliiba haki ya Esau (Mwanzo 27: 1 – 29). Walikuwa wameoa wanawake wazuri
sana . Mungu
aligeuza maisha yao
anaweza kugeuza maisha yako. Na Mungu akaitwa Mungu wa Kamau, Mungu wa Onyango,
Mungu wa Kilonzo, Mungu wa Mutua, Mungu wa Anna. Ibrahimu alikuwa baba wa
imani.
MAISHA
BAADA YA MAISHA
Katika tamaduni
za kiafrika mtu akiwa anaomboleza anamwambia marehemu amsalimie jamaa zake
walioaga dunia. Anasema: Nisalimie babu yangu, nisalimie nyanya yangu.
Nisalimie mjomba wangu. Nisalimie mama mdogo. Mfano wa majina: immortality of
name: mjukuu anapewa jina la babu. Mtoto wa kike anapewa jina la nyanya yake. Tunataka
jina la mtu liendelee kutajwa. Immortality of fame: Tunataka sifa ya mtu iishi
milele. Tunajenga sanamu za ukumbusho. Kuna immortality of influence: Jina la
baba linawapa watoto ushawishi. Immortality of power: Tunataka mamlaka
yaendelee kwa kuanzisha mashirika ya kutoa msaada. Nyerere Foundation.
Aliyeanzisha zawadi ya Nobel Prize.
KIFO SIO NUKTA NI ALAMA YA MKATO
Kifo kipo katika
miguu tunatembea nacho. Ndivyo isemavyo methali moja ya kiafrika. Sio tu kwamba tunatembea nacho katika miguu
tu pengine tunasafiri nacho katika vyombo vya majini, angani na
barabarani. Hadithi inapokuwa tamu
kwenye gazeti au runinga hukatizwa na chini yake maneno “Itaendelea Toleo
Lijalo,” huandikwa. Maisha ya marehemu waliokufa ni hadithi ambayo itaendelea toleo lijalo.
Toleo lijalo ni huko mbinguni, toharani
au motoni.
Katika adhimisho
la misa huwa tunasali: “Tunasikitika kwa
sababu tunajua kwamba lazima tutakufa, lakini tunatulizwa kwa kuwa alituhaidia
uzima wa milele. Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu.
Nayo makao ya hapa duniani yakishabomolewa, tunapata makao ya milele mbinguni.” Sayansi inatwambia kuwa hakuna kitu chochote
katika maumbile, hata chembe ndogo inaweza kupotea kabisa kabisa. Maumbile
hayajui kutokuwepo, yanachokijua ni mabadiliko. Ukweli huu wa kisayansi
unahimarisha imani yetu katika kuendelea kuishi katika maisha ambayo
yamegeuzwa. Kusema kweli kifo ni
kudondoka kwa ua ili tunda liweze kukomaa. Kuna maisha baada ya kifo. Kuna
maisha baada ya maisha. Katika somo la
kwanza saba wako mbinguni na saba wa kufikirika wa Injili wako mbinguni. Katika
somo la kwanza tunasoma hivi: “Karibu na kukata roho, akasema, “Ewe mpotovu,
unatuondoa uzima wa sasa, lakini Mfalme wa ulimwengu atatufufua sisi, tunaokufa
kwa ajili ya amri zake, naye atatupatia tena maisha ya uzima wa milele” (2
Wamakabayo 7: 9).
NAMNA
GANI?
Ingawa kifo huja mara moja tu kwa kila mtu,
swali linabaki ni kifo cha namna gani ? Baadhi ya wakristu husali na kumuomba
Mungu wafe kifo chema. Sala yao huwa hivi, “Na kifo cha ghafla na
kisichotazamiwa, utuopoe, Ee Bwana.”
Masadukayo walisumbuliwa na swali la namna gani baada ya ufufuko mpaka
walitambulikana hivi: “ndio watu wanaokana ufufuko wa wafu” (Lk 20: 27).
Masadukayo walikuwa ni tabaka la kikabila kati ya Wayahudi wa Palestina
wakiwemo kati yao familia za kikuhani, wamiliki wa ardhi na wafanyabiashara
matajiri – ambao bila shaka walikuwa wazaliwa wa watawala wa kihasmonea. Jina
lao linatokana na jina la Zadoki kuhani mkuu wa mfalme Daudi (2 Sam 19: 12) na
walihesabiwa katika kundi lao makuhani wengi sana katika Israeli. Wao
walishikilia kwa nguvu mafundisho ya Torati na kuyaacha kando mafundisho makuu yasiyokuwamo humo. Matokeo yake
walikataa ufufuko na uwepo wa malaika.
Katika masuala ya imani namna gani tunamwachia Mungu.
Juu ya namna
gani ya kwanza hakuna anayemjua mjumbe
wa kifo atakuja lini. Ni busara kila tufanyalo katika maisha tujiulize,
“Halafu?” Kama hadithi ya vijana wawili. Kijana mmoja alimuuliza mwingine.
“Utafanya nini ukikua?” “Nitachukua somo la biashara.” “Halafu?” “Nitatafuta
kazi.” “Halafu?” “Nitapata fedha nyingi kama mshahara.” “Halafu?” “Nitatafuta
msichana nioe” “Halafu?” “Nitakuwa na watoto.” “Halafu?” “Nitawalea watoto” “Halafu?”
“Nitakuwa babu?” “Halafu?” “Labda nitafanywa chifu.” “Halafu?” “Nitatawala
watu.” “Halafu?” “Nitazeeka.” “Halafu?” ““Halafu?”, halafu, halafu, halafu
usiulize zaidi ya hapo.” “Bila shaka uwe unafikiria kuwa siku moja utakufa.”
Lakini tumaini linabaki kuwa kifo sio nukta, sio kikomo, bali ni alama ya mkato
hadithi ya maisha inaendelea.
KWA NINI?
Masadukayo
walijishughulisha na namna gani walipomuuliza swali Yesu la mtego. “Atakuwa mke wa nani?” Yesu
alijishughulisha na “kwa nini?” Badala ya masadukayo kuleta mtanziko halisi,
wanajaribu kuonesha upuuzi wa mahubiri ya Yesu juu ya ufufuko wa miili. Yesu
analiondoa swali kutoka kwenye uwanja wa kuchekesha na kulifanya kauli nzito
kuhusu ufufuko na kupaa kwake mwenyewe mbinguni na vile vile hatima ya
ubinadamu na ukamilisho wa historia ya binadamu. Jibu la kwa nini ya Yesu
kwanza Mungu wetu ni Mungu wa walio hai: “Kwani Mungu si Mungu wa wafu, bali wa
walio hai, maana kwa sababu yake wote wanaishi” (Lk 20: 38).
Pili dini ya
kikristo ni dini ya ufufuko. Ukiondoa ufufuko unafuta dini ya kikristu.
Kutokana na Pasaka wakristo inabidi wawe watu wa matumaini, watu wa ukweli,
watu wa amani, na watu wa kutenda mema. “Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi,
Kristo naye hakufufuka na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana
maana na imani yetu haina maana…Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa
kutoka wafu.” (1 Wakorintho 15: 13-20).
Kifo
Kiwe Zawadi
Kuna methali ya
Ujerumani isemayo hastahili kuishi anayeishi kwa ajili yake tu. Binadamu wengi
wako tayari kufia imani, kufia mtu, kufia dini, kufia shirika na kufia familia.
Hawaishi kwa ajili yao
nafsi zao tu. Ukiwafia wengine, unakifanya kifo kiwe zawadi kwa wengine. Ipo misingi
ya kumfanya mtu amfie mwingine au alifie shirika, kampuni, au dini. Yesu
aliifia dunia Yesu alifia watu kama Kayafa
alivyotabiri ili waneemeke, waokoke. “Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri
Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.” (Yohane 18: 14). Yesu
alikufa kwa ajili ya watu. Jambo la kujiuliza ni unafia nini? Kutokana na neno
kufa tuna neno kufia yaani kupigana kwa namna zote ili kutetea kitu au jambo
fulani. “Ni baraka kufia jambo fulani, sababu unaweza kwa urahisi kufia bure,”
alisema Andrew Young. Kuwafia wengine hakuhitaji kujipendelea. Mtu
anayejipendelea hafikiri kama kuna wengine duniani
anajiona kitinda mimba duniani. Unapowafia wengine unafanya kifo chako zawadi
kwa kizazi kijacho au watu wengine.
Kuna methali isemayo, “kifo kinafuta kila kitu isipokuwa ukweli.”
Kifo hakifuti ukweli wa maneno yetu na matendo yetu. Wakati wa kufani maneno
yetu yawajenge tunaowaacha nyuma. Kuna mchungaji ambaye alikuwa anafanyiwa jubileo
ya miaka 40 katika uchungaji. Alikuwa mgonjwa sana . Aliombwa kusema neno. Mwanzoni
alikataa.Baada ya kuombwa kuzungumza alisema, “Afya ni mali .” Aliketi chini. Wakristu
waliomba ufafanuzi. Aliamka na kusema. “Afya ni mali . Afya yangu si nzuri. Ni mbaya
sana . Nyinyi
mmechangia afya yangu kuwa mbaya.” Mchungaji huyo hakumwingiza Mungu katika
ugonjwa wake. Kama Ayubu angetulia katika Mungu, “Bwana ametoa Bwana ametwaa
jina lake litukuzwe .” Baada ya miezi miwili aliaga
dunia. Kifo chake kiliwaacha waliopaswa kumpa huduma wakisutwa na dhamiri. Kifo
chake hakikuwa zawadi kwa wengine. Kufa ni lazima, kama
biblia isemavyo, “Kwa kila kitu kuna majira, na wakati kwa kila jambo
duniani:…kuna…wakati wa kufa” (Mhubiri 3: 2), swali unakufa je? Yesu akiwa
kufani aliwasamehe watesi wake. Kifo chake kilikuwa ni zawadi kwa watesi,
walipata zawadi ya msamaha.
Juu ya kufanya
vifo vyetu viwe zawadi, Henri J.M.Nouwen alikuwa na haya ya kusema, “Namna gani
tunafanya vifo vyetu zawadi kwa wengine? Mara nyingi maisha ya watu
yanaharibiwa, yanadhuriwa au kuwa na majeraha maisha yao yote kwa vifo vya jamaa au marafiki zao.
Lazima tufanye tuwezalo ili kukwepa ili.Tunapokuwa kufani tunalowaambia wale
ambao wako karibu nasi, iwe kwa kusema au kuandika ni muhimu. Tunapowashukuru,
kuwaomba msamaha kwa makosa yetu na kuwasamehe kwa ya kwao na kuwaonesha nia ya
kutaka waendelee na maisha yao
bila kusutwa na dhamiri lakini wakikumbuka neema za maisha yetu basi vifo vyetu
vinakuwa zawadi kweli.”
Hasara kubwa si kifo bali kinachokufa ndani mwetu. “Kifo si hasara
kubwa sana
katika maisha yetu. Hasara kubwa sana
ni kile kinachokufa ndani mwetu wakati tunaishi,” alisema Normani Cousins mtunga
insha na mwariri wa Amerika (1912 –
1990). Wakati tunaishi kuna mambo ambayo yanaweza kufa kama
shauku, moyo wa kutoa, moyo wa kujitoa, uchaji kwa Mungu, utii, usafi wa moyo.
Vikifa ni hasara kubwa.