Jumatatu
ya Juma la 32
“Mitume wakamwambia Bwana, ‘Tuongezee
Imani” (Luka 17: 5)
Imani kidogo
yaweza kufanya mambo makubwa. Ni ukweli unaoendana na ujumbe wa methali ya
Kiswahili, Kidogo kidogo kamba ukatika. Nguvu ya mbegu haitegemei ukubwa au
udogo wake inategemea uhai uliofichwa katika mbegu hiyo. Kuna nguvu ambayo
imefichwa ndani mwako. Yesu aliwaambia mitume: “Mngekuwa na imani kiasi cha
punje ya haradali, mngeuambia mforsadi huu, ‘Ng’oka, kapandikizwe baharini, nao
ungewatii” (Luka 17:6). Kama ni hivyo unahitaji kujiamini kuwa utaweza
kufanikiwa katika maisha. Kwa imani na kujiamini ndege imevumbuliwa. Kwa imani
na kujiamini simu za mkononi zimegunduliwa. Kwa imani na kujiamini utalaamu wa
kutengeneza runinga umefunuliwa.
Mitume
walipoomba kuongezewa imani, Yesu hakusema nimewaongezea imani. Hakuahidi
kuwaongezea imani. Ni kama aliwaambia anza na mlicho nacho, kidogo huvuta
kikubwa, kidogo huzaa kikubwa, laini huzaa ngumu. Walikuwa kama mfanyabiashara
asemaye nina pesa kidogo sana
ngoja iwe nyingi ndipo nianze kufanya biashara. Je, itaongezekaje bila
kuzalisha, kuuza na kununua? Walikuwa kama mkulima asemaye nina mbegu lakini
hazitoshi nitalima nikiwa na mbegu za kutosha. Anza na ulicho nacho. Hawezi
kusema sina pesa yote ya kujenga na kumalizia nyumba. Anza kujenga na pesa
uliyo nayo. Ili kuwa na zaidi anza na ulicho
nacho. Aliyenacho ataongezewa ndivyo
Bwana Yesu alivyofundisha.
Mitume walitaka
imani yao ikomae na iwe thabiti. “ni kwa
kuamini peke yake ndiko imani hukomaa na kuwa thabiti,” aliandika Baba
Mtakatifu Benedikto XVI katika kitabu “Mlango wa Imani.” Mitume wengi walikimbia Yesu alipokamatwa.
Huu ni ushahidi wa imani ambayo si thabiti na ambayo haijakomaa. Imani ambayo
si thabiti inakuwa na mashaka mengi wakati wa shida na matatizo. Ni katika msingi huu mitume waliomba
waongezewe imani. Baba anapomchukua mtoto wake mdogo wa kike na kumzungusha
hewani, mtoto anacheka na kufurahi kwa vile anaamini na ana imani katika baba yake. Ingawa anajikuta
katika hali ambayo si ya kawaida kama miguu kuwa juu na kichwa chini umbali wa
futi nne kutoka sakafuni. Haogopi kwa vile anamwamini baba yake. Hii ndiyo
imani ambayo ni thabiti na iliyokamaa ambayo hatuna budi kuwa nayo kwa Baba wa
mbinguni. J. Hudson Taylor alimwandikia
mke wake wakati mgumu akiwa anafanya kazi ya China Inlanda Mission, “Tuna centi
ishirini na tano na ahadi zote za Mungu.”
Ni maneno ya mtu mwenye thabiti katika shida.