NOELI USIKU
1. Isa 9: 1-6
|
2. Tit 2: 11-14
|
3. Lk 2: 1-14
|
“Wanashangilia mbele yako, kama
wanavyoshangilia wavunaji” (Isaya 9: 2)
“Mara jeshi kubwa la mbinguni
wakawa pamoja na malaika wakimsifu Mungu, na kusema: Utukufu kwa Mungu juu, na
amani duniani kwa watu aliopendezwa nao,” (Luka 2: 13-14)
UTANGULIZI
Kuna aliyemuuliza mtoto, “je
umepata kile ulichohitaji katika Krismasi hii?” Mtoto alijibu sikupata kila
nilichohitaji na kila nilichotegemea. Lakini hata hivyo siku ya leo siyo siku
yangu ya kuzaliwa ni siku ya kuzaliwa Yesu Kristu.” Ni vizuri watoto watambue kuwa Krismasi siyo
siku yao ya kuzaliwa (labda kama
mtoto alizaliwa tarehe 25/Desemba naye atakuwa anasherekea siku yake ya
kuzaliwa lakini siyo Krismasi) ni siku ya Kuzaliwa Yesu Kristu. Tatizo tunaweza
kutekwa na kile kinachouzwa tukamsahau yule aliyesababisha vitu vyenye heri ya
Krismasi viuzwe. Naye ni Yesu. Maneno ya kutakiana heri: Heri Krismasi. Baraka
ya Krismasi. Furaha ya Krismasi yatukumbushe juu ya Yesu ambaye ni baraka kwa
dunia. Kwa sababu yake kuna mabadiliko. Wafuasi wa Yesu wanafanya mengi ya
maendeleo. Kuna Hospitali zimejengwa na madhehebu ya Kikristu. Kuna mashule,
mazahanati, vyuo na misaada mingi kwa watu walionamatatizo vinavyofanywa na
wafuasi wa Yesu. Krismasi itukumbushe wema aliotenda Yesu na awe mfano wa
kuigwa.
Kote duniani madhehebu mengi ya
Kikristo yanasherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristu. Sherehe hii inajulikana kama
Krismasi, Noeli, Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Yesu Kristu, mhasisi wa dini ya
Kikristu. Krismasi ni vigelegele sio kelele. “Mara jeshi kubwa la mbinguni
wakawa pamoja na malaika wakimsifu Mungu, na kusema: Utukufu kwa Mungu juu, na
amani duniani kwa watu aliopendezwa nao,” (Luka 2: 13-14. Hakuna mtu anayependa
Krismasi imkute kifungoni au jela. Taarifa ambazo huwa tunazipata toka zahanati
na hospitalini ni kuwa wakati wa Krismasi wagonjwa wanapungua wadini. Hakuna
ambaye anapenda Krismasi imkute wadini. Lakini ugonjwa haubishi hodi na hauna
kalenda. Kipindi cha Krismasi ni kipindi cha kufurahi. Mtume Paulo
anatukumbusha, “ Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena:
furahini!” (Wafilipi 4:4).
MAHUBIRI YENYEWE
“Kwa kawaida Krismasi huonekana
kuwa ni likizo yenye kelele: litakuwa ni jambo zuri kwetu kuwa na ukimya
kidogo…kuwa kimya ili uweze kusikia upole wa Mungu,” alisema Papa Fransisco
Kiongozi wa Kanisa Katoliki. Methali ya Kiswahili inasema yote: kelele nyingi
ni makeke (vishindo). Kelele nyingi haziwezi kutimiza chochote na huwa ni
usumbufu tu kwani kelele nyingi ni sawa na vishindo. Methali hii hutuonya dhidi
ya kupayuka. Kelele za muziki wa kusumbua jirani nyumbani, kelele za muziki
kwenye matatu, kelele za bunduki, kelele za milio ya simu kwenye sehemu za
ibada, kelele kwenye sehemu za starehe vinaharibu heshima ya Krismasi.
Kelele ni uchafu. Ni uchafuzi wa
mazingira kupiga kelele. “Kelele zote ni uchafu. Kuza tabia ya utulivu katika
katika maneno, katika mawazo yako na katika hisia zako. Kwa kawaida zungumza
kwa sauti ya chini,” alisema Elbert
Hubbard (1856-1915) mhariri na mwandishi
wa Amerika. Kelele ni kama maji taka.
Vigelegele ni kama maji safi. Ukimya ni kama maji salama. Kelele zinakosa sifa
moja kubwa sifa ya utulivu na ukimya. Vigelegele ni matokeo ya ukimya na kuwaza
matendo makuu. Kelele si matokeo ya ukimya bali ukosefu wa ukimya. Nyota
hazipigi kelele. Ni methali ya Ireland. Watu ambao ni nyota au mashuhuri
hawapigi kelele. Mama wa Yesu Maria aliyatafakari katika ukimya matendo makuu
ya Mungu Krismasi ya kwanza. “Naye Maria akatunza mambo hayo yote akiyawaza
moyoni mwake” (Luka 2:19). Aliyatafakari kwa mwanga wa maandiko ya Agano la
Kale.
Krismasi ni kipindi cha aina yake
cha kumtafuta Mungu. “Tunahitaji kumtafuta Mungu, na hapatikani katika kelele
na kutotulia. Mungu ni rafiki wa ukimya. Tazama viumbe – miti, maua, nyasi
vinakua katika ukimya; tazama nyota, mwezi na jua vinafanya mambo katika
ukimya.. Tunahitaji ukimya kuweza kugusa nyoyo za watu,” alisema Mama Tereza wa
Calcutta. Kipindi cha Krismasi unaimbwa wimbo ambao umevuta nyoyo za watu
“Silent Night” ambao umetafsiriwa kwa Kiswahili: Usiku mkuu! Usiku Mtakatifu!
Uko utulivu; Bikira amezaa Mwana, Mtoto Mtakatifu ni Bwana; Alale amanini,
Alale amanini.” Wimbo huu unazungumzia ukimya, utulivu, ukuu na utakatifu wa
usiku alipozaliwa Yesu. Utulivu huu na ukimya huo ni wito wa kuwa na utamaduni
wa kuwa kimya na kutulia. Wakati wa vita ya kwanza ya dunia Krismasi ya mwaka
1914 vikosi vyote vilivyokuwa vinapigana viliweka siraha chini na kuimba wimbo
wa “Silent Night.” Kelele za bunduki
zilisimamishwa. Lakini pongezi ingekuwa kama kelele hizo zingesimamishwa siku
zote na sio usiku tu wa Krismasi. Utamaduni wa kutochafua hewa kwa kelele
lisiwe suala la Krismasi tu.
Kadiri ya Kamusi ya Karne ya 21
kelele ni sauti kubwa sana. Kelele ni hali ya kutokuwa na utulivu; fujo,
ghasia, rabsha, nyange, ngenga, chachawizo. Penye kelele kuna kutosikilizana.
Penye kelele kuna kutoheshimiana. Penye kelele kuna kukasirikiana. Penye kelele
hakuna mshikamano. Penye kelele hakuna utaratibu. Tukumbuke methali ya
Kiswahili. Kelele za mpangaji hazimnyimi usingizi mwenye nyumba. Ni kama
methali isemayo: Kelele za mwenye nyumba hazimkatazi mgeni kulala. Ni ushauri
kuwa mtu mwenye nia ya kutimiza jambo fulani, hagutushwi na lawama, shutuma au
malalamiko ya watu wengine wanaonuia kumkatisha tamaa.
Kelele za mlango hazininyimi
usingizi. Ni methali ya Kiswahili. Mtu anapoamua kulala hajishughulishi na mlio
au kelele za mlango kufungwa na kufunguliwa. Tunapoendelea na kazi zetu
tusiwajali watu wenye kutuambia maneno ya upuuzi nay a kutuharibia wakati wetu.
Tunapaswa kuwapuuza watu kama hao. Macho ya chura hayamnyimi ng’ombe kunywa
maji.
Krismasi ni kipindi
cha kupiga vigelegele na si kelele. Kigelegele ni sauti ya kushangilia
inayofanywa katika arusi kwa kuchezesha ulimi mdomoni. Lakini ulimi lazima
uwekewe utaratibu usije ukachafua mazingira kwa kelele. Mbwa anapendwa na wengi
sababu muda mwingi anatingisha mkia badala ya ulimi. Kupiga kelele na kusema
kwa sauti ya juu ni ushahidi tosha kuwa mtu hana pointi au nguvu ya hoja.
Nakubaliana na mwanafalsafa wa Kifaransa
na mwandishi Michel de Montaigne (1533-1592) aliyesema: “yeye anayejenga hoja
yake kwa kelele na amri anaonyesha kuwa hoja yake ni dhaifu.” Kuna watoto
wawili ambao walikuwa wanajidai juu ya uwezo wa mama zao. Mmoja akasema: mama
yangu anaweza kutoa hotuba bila kusoma karatasi. Mwingine akasema: mama yangu
anaweza kutoa hotuba bila kufikiria. Kutoa hotuba bila kufikiria ni kupiga
kelele. Ukweli unabaki Krismasi ni vigelegele si kelele.
KRISMASI NI KUTAJIRISHANA
“Yeye amejitoa mwenyewe kwa ajili yetu” (Tito
2: 14)
Hakuna ambaye ni maskini kiasi
cha kutokuwa na chochote cha kutoa na hakuna ambaye ni tajiri kiasi cha
kutohitaji lolote. Krismasi imepambwa na ukarimu. “Krismasi, mwanangu, ni
upendo kwa vitendo. Kila mara tunapopenda, kila mara tunapotoa, ni Krismasi,”
alisema Dale Evans. Sura ya Krismasi ni sura ya ukarimu. Kutumiana zawadi.
Kutumiana kadi za heri ya Krismasi. Watoto kununuliwa nguo. Watu wazima
kununuliana nguo. Watoto wawili wadogo walikuwa wamemtembelea babu yao siku
tatu kabla ya sikukuu ya Krismasi. Usiku walipiga magoti upandeni mwa kitanda
kusali sala za usiku . Mdogo kiumri alipaza sauti kadiri ya mapafu yake
yalivyomruhusu “Naomba nipate baisikeli mpya. Naomba nipate baisikeli mpya.
Naomba nipate baisikeli mpya. Naomba nipate baisikeli mpya…” Kaka yake
alimwambia mbona unaomba kwa sauti ya juu sana Mungu sio kiziwi anasikia. Mtoto
mdogo alijibu. Mungu anasikia lakini babu yangu atakeyeninunulia baisikeli
anajifanya kutosikia. Kipindi cha Krismasi ni kipindi cha kuwasikiliza watoto.
Tutajirishane kwa kusikilizana. Kuna methali ya Nigeria isemayo: “Sikiliza na
utasikia sauti ya hatua ya mchwa.” Sikiliza mwili wa mwenzako unaongea. Hasira,
upendo, huruma vinaonekana kwenye mwili.
Itakuwa makosa makubwa kuadhimisha Krismasi
bila kumtaja Kristo, kuuza kadi za Krismasi bila kuandikwa jina Kristo. “Nilifunga
zawadi zangu za Krismasi kwenye karatasi za kufungia zawadi lakini nilitumia
karatasi ambazo si sahihi zilikuwa na meneno: Heri ya Kuzaliwa. Sikutaka
kuzipoteza nikaongeza neno Yesu,” alisema Demetri Martin.
Jina hilo Kristo wakati wa
Krismasi linatajirisha wengi. Biblia yasema “Katika Kristo Yesu mmetajirika
katika yote, katika kila neno na kila utambuzi” ( 1 Wakorintho 1:5). Yesu
alikuja kututajirisha. Ikumbukwe vipimo vya utajiri si pesa tu. Yesu anaitwa
mshauri wa ajabu. Ametutarisha kwa maneno ya ushauri katika Biblia. Nawe toa
ushauri wa kutajirisha wengine. Tusitoe ushauri ambao hauwezekani. Hapo zamani
kadiri ya hadithi za Aesop panya walikuwa na mkutano namna ya kumkwepa paka.
Panya mmoja akatoa wazo kuwa tumfunge kengele shingoni paka akikaribia tutajua
kuwa anakaribia. Panya huyo mdogo kwa umri alipigiwa makofi nakushangiliwa.
Panya mkubwa akauliza. “Hilo ni wazo zuri lakini nani atamfunga paka kengele?” “Inawezekana tatizo la paka kwa panya
lingekwisha kama paka angefungwa kengele. Taabu ni kumpata panya wa kuifanya
kazi hiyo. Na panya watakuwa wajinga sana kama watadhani kuwa paka watajifunga
wenyewe kengele shingoni,” alisema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa
rais wa kwanza wa Tanzania.
Ukarimu uonekane katika kurudisha wema. Ukitendewa wema rudisha wema
hili kama au mnyororo wa wema usikatike. Mtu akiokota kitu chako akakuletea mpe
zawadi. Mwanamke mmoja alipoteza begi lake wakati ananua vitu vya Krismasi.
Mvulana mdogo mwaminifu aliokota begi hilo na kumrudishia mwanamke huyo.
Alipotazama kwenye mfuko wake alisema: Kuna jambo la kushangaza katika begi
langu palikuwepo noti moja ya shilingi elfu moja ya Kenya sasa nakuta noti 20
za shilingi hamsini hamsini.” Mtoto huyo alijibu haraka. Hiyo ni kweli.
Niliwahi kuokota begi la mwanamke mwingine lakini hakuwa na pesa ndogo ndogo ya
kunipa zawadi kama shukrani hivyo nimeamua kupata fedha ndogo ndogo wewe
utaamua unanipa kiasi gani. “Krismasi ni
kufanya jambo la ziada kwa ajili ya mwingine,” alisema Charles M. Schulz
Krismasi sio kipindi cha kuwaibia wengine ni kipindi cha kuwapatia
wengine. Jaji aliyewatembelea wafungwa siku ya Krismasi alimuuliza mfungwa:
wewe ulifanya kosa gani? Mfungwa alisema Nilifanya manunuzi ya vitu vya
Krismasi mapema sana?” Jaji alisema hilo sio kosa. Lakini mapema ya saa ngapi
ulifanya manunuzi hayo?” Mwizi huyo alisema: “Kabla duka alijafunguliwa. Huyu
alidokoa. Huyu aliiba.
“Krismasi ni kipindi cha kuwasha moto wa ukarimu katika ukumbi, na miale
ya joto la ukarimu moyoni,” alisema Washington Irving. Wanafamilia wape muda wako. Muda ni mali.
Kuwa nao. Siku hizi muda wa baba na mama kukaa na watoto wao ni mdogo. Wanakuwa
shuleni. Wakienda likizo za Krismasi wanawekewa mwalimu wa kuwafundisha. Wape
muda watoto wako. Krismasi sio kipindi cha kutapanya hovyo. Wengine wanatapanya
hovyo mpaka wanatumia karo za watoto wao. Krismasi sio mwisho wa maisha kuna
kesho.