Tuesday, December 31, 2013

SHEREHE YA MARIA MTAKATIFU MAMA WA MUNGU


 
                                                  1 JANUARI  2014

UTANGULIZI

Ukweli muhimu sana kuhusu Bikira Maria ni kuwa yeye ni Mama wa Mkombozi. Ukweli huu sio heri kubwa pekee kwa Bikira Maria bali ni ufunguo wa heri nyingine. “Maria...anafahamika kuwa kweli Mama wa Mungu na wa Mkombozi. Yeye mwenyewe alikombolewa kwa ajili ya mastahili ya mwanawe tena kwa namna ya pekee. Aliangaliwa na Baba kama binti yake mpenzi, na Mwana kama Mama mheshimiwa, na Roho Mtakatifu kama hekalu lake.”  Bikira Maria ni Mama wa Mungu sio kwa jina tu bali amemzaa Yesu ambaye ni Mungu. Kuna maswali ya kujiuliza, namna gani Mungu, ambaye hana mwanzo wala mwisho na Muumba wa vyote, anaweza kuwa na Mama hapa duniani? Je inawezekanaje, Yesu ambaye ana Baba mbinguni lakini bila Mama huko mbinguni awe na Mama duniani lakini bila Baba duniani?

NAFASI YA BIKIRA MARIA KATIKA BIBLIA

Ili Bikira Maria awe Mama wa Mungu kweli mambo mawili ni lazima: Kwanza lazima awe Mama halisi wa Yesu; na Pili ni kuwa Yesu aliyemzaa ni Mungu. Kama hayo yote ni hivyo, Maria ni Mama wa Mungu kweli.

1) BIKIRA MARIA NI MAMA HALISI WA YESU

Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maanaMungu amekujalia neema, Na hivi: Utapata mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu” (Lk.l :30-31). “Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, Mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. (Mt. 1: 18). “Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristu, ambaye, mintarafu ubinadamu wake, alikuwa mzao wa Daudi” (Rom. 1:3). “Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, Bikira atachukua mimba, atajifungua mtoto wa kiume na kumwita jina lake Immanueli” (Isaya 7:14). Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadhaa wa kadhaa, na Maria Mama yake Yesu, na ndugu zake” (Mate. 1: 14).

2) YESU NI MUNGU NA BIKlRA MARIA NI MAMA WA MUNGU

Hapo mwanzo, Neno aliwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu, tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu” (Yoh. 1: 1-2). “ ... naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele : Amina” (Rom. 9:5). “Muwe na msimamo uleule aliokuwa nao Kristo Yesu: Yeye, kwa asili, alikuwa daima Mungu; lakini hakufikiri kwamba kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania kwa nguvu. Bali, kwa hiari yake mwenyewe, aliachilia hayo yote, akajitwalia hali ya mtumishi akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama mwanadamu” (Fil. 1 :6-7). “Mitume nao walikiri kuwa Yesu ni Mungu-Mtu:” Thoma akamjibu, “Bwana wangu na Mungu wangu” (Yoh. 20:28). “Malaika akamjibu, Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, na Mwana wa Mungu” (Lk. 1 :35). “Mimi ni nani hata Mama wa Bwana wangu afike kwangu?” (Lk. 1 :43). Kristo huitwa “Bwana”Yahwe. Neno hili Bwana katika Agano la Kale lilitumika kwa ajili ya Mungu tu. Kwa ajili ya hayo, mwinjili amwitapo Kristo kwa jina la Bwana ataka kudokeza kwamba ..huyo Kristo ni Mungu. “Mungu alimtuma mwanae aliyezaliwa na mwanamke” (Gal. 4:4). Huyo Mwana wa Mungu ni Mwana wa mwanamke. Huyo Mwana wa Mungu, pia ni Mwana wa Maria.

MAPOKEO

Ingawa Kanisa la Mwanzoni katika karne ya kwanza liliamini kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, fundisho hilo lilikuwa halijatangazwa rasmi. Alitokea Askofu Nestorius mtu mwenye majivuno kutoka Constantinople aliyeanza kufundisha kuwa Bikira Maria si Mama wa Mungu Theotokos, bali Mama wa Kristu-Christokos, mtu tu wa Nazareti. Mafundisho haya yalizua kasheshe. Yalizua mgongano. Yalizua mgogoro ulioliweka Kanisa Katoliki hatarini. Mwaka 431 uliitishwa Mtaguso wa Ephesus uliopinga vikali uzushi wa Nestorius. Askofu Mkuu wa Alexander Mt. Sirilo alifungua Mtaguso tarehe 22 Juni 431, ulioitishwa kwa ruhusa ya Papa Celestine I. Katika duru ya kwanza ilisomwa barua iliyomwondolea Nestorius cheo chake. Usiku wa tamko hilo, kadiri ya wanahistoria barabara zilijaawatu waliopaza sauti na kusema “Hagia Maria Theotokos” yaani Mtakatifu Maria, Mama wa Mungu.’ Mafundisho yaliyothibitishwa na Mtaguso wa Ephesus yalikuwa katika barua ya Mt. Sirilo iliyosomwa katika duru ya kwanza. Mt. Sirilo alifundisha hivi: “Nashangaa sana ninapoona wakristu wanaogopa kumwita Bikira Maria ‘Mama wa Mungu’: Mbona Rabbi wetu YESU Kristu ni Mungu? Bikira Maria ndiye aliyemzaa. Atakosaje tena kuitwa “Mama wa Mungu”.3 Hoja iliyotolewa kupinga kuwa Bikira Maria si Mama wa Mungu ni kwamba Kristu anaitwa Mungu sababu ya Umungu wake. Lakini umungu huu haukuanzia kwa Bikira Maria. Hivyo Bikira Maria asiitwe Mama wa Mungu. Hii ilikuwa hoja ya Nestorius. Mt. Sirilo alijibu kama ifuatavyo: “Katika kila mtu kuna sehemu mbili: mwili na roho. Sehemu hizi mbili zaungana na hazitengani katika kumfanya mtu. Mwili wa mtu umezaliwa na mama yake, lakini roho haikuzaliwa na mama yake, ila ilitoka kwa Mungu, ikaumbwa naye. Japo mambo ni hivyo mama aliyezaa mwili haitwi Mama wa Mwili, ila Mama wa mtu mzima, kwa sababu mwili na roho ya mtu vikisha ungana, vyashikamana kwa kufanya mtu mmoja. Ndiyo sababu Mama, aitwa Mama wa mtu yule yule. Vivyo hivyo, ndani ya Yesu mna sehemu mbili, Umungu na Ubinadamu, kwani Yesu ni Mungu kweli na mtu kweli. Basi, wakati wa umwilisho, Ubinadamu na Umungu viliungana kabisa, vikawa MUNGU-MTU, au Mkombozi. Na Mungu-Mtu huyu akaitwa jina jipya, YESU KRISTU. Kwa hivi, Bikira Maria, aliyezaa ubinadamu wa Yesu aweza kuitwa Mama wa Mungu kwa sababu mwanaye YESU ni Mungu kweli, na kwa sababu, ndani ya YESU, Ubinadamu na Umungu havitengani, ila vyashikamana kwa kufanya Mkombozi mmoja, ndiye YESU.’’  Fumbo juu ya YESU Kristu, muungano wa Umungu na Ubinadamu ulimaanisha katika Mtaguso wa Ephesus kuwaUmungu na Ubinadamu haviwezi kutengana . Yesu Kristu ni Mungu-Mtu “Mwanga kutoka kwa Mwanga, Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli, aliyezaliwa bila. kuumbwa, mwenye Umungu mmoja na Baba ... ’’5

Mt. Germanus wa Constantinople (+720) alimwita Maria “Mahali pa kuishi pa Mungu” Mt. Jerome alimwita: “Hekalu la Mwili wa Bwana.” Martin Luther, hata baada ya kujiengua kutoka Kanisa Katoliki, alikiri kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Alisema hivi: “Hakuna jambo kubwa zaidi ya hili kuwa (Bikira Maria) alipata kuwa Mama wa Mungu; ambalo kwalo zinatoka zawadi (heri) kubwa na nyingi ambazo amepewa yeye ...”

MAISHANI

1. WAJIBU WA KUTETEA UHAI

Bikira Maria ni Mama wa Uhai. Eva alikuwa kwa watu sababu ya kifo na kupitia kwake kifo kiliingia duniani. Maria amekuwa sababu ya uhai kwetu. Ni kwa sababu hii Mwana wa Mungu amekuja duniani. “Lakini pale dhambi ilipoongozeka, neema iIiongezeka zaidi” (Rom. 5:20). Wakati kifo kilipoingia, uhai uliingia, ili kuchukua nafasi ya kifo, kufutilia mbali kifo kilichotufikia kwa njia ya mwanamke. Kristu amekuja kwetu kupitia mwanamke na amekuwa kwetu uhai. Eva kwa kutotii kwake alitenda dhambi, Bikira Maria alitii. Utiifu wake unaonekana pale ilipotangazwa kuwa Mungu, uhai wa milele, atashuka toka mbinguni azaliwe katika mwili.” Kumbe hatuna budi kutetea uhai tukiiga mfano wa Bikira Maria ambaye ni Mama wa uhai, kupitia kwake uhai umeingia na sio kama Eva wa kwanza ambapo kupitia kwake kifo kiliingia. Je kupitia kwetu kifo kinaingia? Je tunatetea maisha ya watoto ambao hawajazaliwa? Mwaka 1985, mimba 1,588,600 zilitolewa huko Amerika.

 Na Canada mimba 62,291 zilitolewa.!” Hii ni mifano michache ya utamaduni wa kifo. Na Mungu hapendezwi na utamaduni huu, utamaduni wa kuua na kwa lugha ya kidiplomasia “Kutoa mimba” Biblia yatwambia “Wasio na hatia na wenye haki usiwaue” (Kut. 23:7). Watoto tumboni mwa Mama zao hawana hatia. Wana haki ya kuishi. Papa Yohane Paulo II ametunga sala ya watetezi wa uhai wa mtoto. “Ee Mama Bikira Mtukufu, uliyeonja fumbo kuu la umama kwa jinsi tofauti kabisa na akina mama wengine duniani wakati imani yako ilikuwezesha kulipokea Neno la Mungu, mwili wako ulijiandaa kuwa ni mahali penye rutuba nzuri kwa ajili ya kuuchukua mwili wake wa kibinadamu. Ee Mama ambatana nasi basi iii tuzidi kukiri heshima ya kila binadamu. Utujalie sote utambuzi wazi, lakini hasa kwao wanaume na wanawake waliopewa wito wa heshima ya kuwa wazazi, ili daima wawe ni “mahali patakatifu kwa uhai” kwa njia ya muujiza wa kuzaa, wito waliokabidhiwa na Mungu kwa msingi wa ukweli na upendo wao mwaminifu na moyo wa utunzaji mwaminifu. Amina” (Papa Yohane Paulo II).

2. UNYENYEKEVU

“Maria alimpendeza Mungu kwa ubikira wake, lakinialichukua mimba kwa unyenyekevu wake” (Mt. Bemado). Unyenyekevu umejengwa juu ya upendo. Ndiyo maana Bwana wetu Yesu Kristu alisema “Mkinipenda mtazishika amri zangu”. Bikira Maria alimpenda Mungu Ni kwa upendo huu alikuwa tayari kunyenyekea na kuchukua mimba Mkombozi. Hatuna budi kujinyenyekeza, mbele ya Bwana. “Unyenyekevu ni mama wa fadhila nyingi sababu utii, uchaji, ibada, uvumilivu kiasi, upole, amani vyatokana na unyenyekevu. Yeye ambaye ni mnyenyekevu hutii kila mtu, ni mwema kwa wote, ni mtiifu kwa kila mtu, hamchukizi wala kumuudhi yeyote”. (Mt. Thoma wa Killanova).12” .Kinyume cha unyenyekevu ni majivuno. Mwenye majivuno ni kilema hatari sana, hufikiri ameisha wasili kwenye kikomo cha safari. Na mwenye unyenyekevu hujua kuwa duniani tu wageni duniani tu wasafiri. Mambo bado. Majivuno ni kilema hatari sana “Majivuno yaliwabadili malaika wakawa mashetani. Unyenyekevu huwafanya watu wawe malaika” (Mt. Augustino)13 Bikira Maria ni mfano wa kuigwa katika unyenyekevu. Bikira Maria alimpendeza Mungu kwa unyenyekevu wake kama Mt. Ambrosio anavyotwambia “Oneni: Unyenyekevu gani: Anajiita mwenyewe mtumishi wa Mungu saa ile ile anapochaguliwa naye awe mama mzazi wa Mungu Mwana. Anapashwa habari kwamba atakuwa mkubwa ajabu, lakini hana majivuno hata kidogo.”

 

HITIMISHO

Mungu alimpa Bikira Maria wito wa kuwa Mama wa Mungu. Alimtafuta Bikira Maria, kuanza kizazi kipya, kurekebisha mambo kukarabati palipoharibika, Mungu alitaka Eva wa pili afanye kile Eva wa kwanza alichokataa kufanya mpaka kifo kikaingia. Tunapoanza mwaka mpya, tukumbuke kuwa Mungu “anatutafuta”, ili kurekebisha mambo ambayo hayakwenda vizuri mwaka uliopita. “Anatutafuta tukarabati palipoharibika. Hatuna budi kuitikia wito. Hatuna budi kunyenyekea “Bwana anataka nini kwako, ila kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako” (Mika.6:8). Ili kurekebisha pale ambapo hapakwenda vizuri mwaka uliopita, hatuna budi kusali sala ya Mt. Fransisko wa Asisi kila mara: “Ee Bwana, nifanye chombo cha amani yako. Panapokuwa chuki, niruhusu nipande mapendo. Panapokuwa na maumivu, iwepo huruma. Panapokuwa na mashaka, imani ipatikane. Panapokuwa kukata tamaa, yawepo matumaini. Panapokuwa huzuni, ipatikane furaha. Ee Bwana Mungu, naomba.  Nisitafute sana kutulizwa, bali kutuliza. Nisitafute kufahamika, bali kufahamu. Nisitafute kupendwa, bali kupenda. Maana kwa kutoa tunapokea, Kwa huruma tunahurumiwa,

 

Counter

You are visitor since April'08