JUMAPILI YA 2 YA MWAKA
“Tazameni, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu”
(Yohane 1: 29)
1. Isa 49: 3. 5-6
|
2. 1 Kor
1: 1-3
|
3. Yn 1:
29-34
|
SIFA YA KONDOO NI UPOLE NA UNYENYEKEVU
Kuna watu ambao wanaweza kupinga
kuwa Yesu hasiitwe Mwana Kondoo kwa vile katika kitabu cha Ufunuo 5:5 anaitwa
Simba wa Yuda, “Kisha mmoja wa wale
wazee akaniambia, ‘Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, chipukizi wa Daudi,
ameshinda.” Katika maneno ya nabii Yeremia tunamwona Yesu Mwanakondoo
mnyenyekevu, “Nami nilikuwa kama kondoo mpole anayepelekwa machinjoni; sikujua kuwa
njama walizozifanya zilikuwa dhidi yangu.” (Yeremia 11: 19)
SIFA YA KONDOO NI KUTOKUWA NA HILA, UBAYA NA KOSA
Yesu ni mwanakondoo hasiyekuwa na
hila, ubaya, wala kosa, kama tunavyosoma
katika biblia. “Lakini hamkukombolewa
kwa vitu vyenye kuharibika: kwa fedha na dhahabu; bali kwa damu tukufu ya
Kristo, ambaye alikuwa kama mwanakondoo asiye
na dosari wala doa.” (1 Petro 1:19) “Yeye
hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake.” (1
Petro 2:22) Kabla ya Kukomunika maneno “Mwana Kondoo wa Mungu,” yanatajwa mara
nne katika Ibada ya Misa. Kwanza yanatajwa
mara tatu katika sala ya Mwana Kondoo. “Mwana Kondoo wa Mungu huondoaye dhambi
za dunia, utuhurumie. Mwana Kondoo wa Mungu huondoaye dhambi za dunia,
utuhurumie. Mwana Kondoo wa Mungu huondoaye dhambi za dunia, utujalie amani.
Kabla ya kumuomba Mungu atujalie amani tunaomba atuhurumie. Kwa sababu gani?
Amani ni tunda la moyo usio na hila, usio na udanganyifu, usio na doa, usio na
kasoro. Hatuwezi tukawa na amani kama kuna
dhambi mioyoni mwetu. Minyoo inaingiaje kwenye tunda. Unakuta tunda lina tundu
na katikati kuna munyoo mkubwa. Umetoka nje ama ndani. Umetoka ndani. Ua
linapochanua ndipo hapo mayai yanatagwa. Mdudu anakua wakati tunda linakua.
Shida inatokea wakati watoto wakiwa wadogo wanasikia mazungumzo ya watu
wakubwa. Wanasikia kuwa watu wa kabila hili ni wabaya. Uovu unakua na mtoto.
Matokeo yake ni ukosefu wa amani. Je tunapanda mbegu ipi?
Jina hili la heshima
linadokeza mateso ya Yesu na kifo chake
msalabani (Isa 19: 36; 53:7). Jina hili Mwanakondoo limerudiwa na Yohane mara
29.
SIFA YA KONDOO NI KUVUMILIA
Kufa kikondoo maana yake
kuvumilia shida bila malalamiko. Mwokozi Yesu alikufa kikondoo. “Alidhulumiwa na kuteswa, lakini alivumilia
kwa unyenyekevu, bila kutoa sauti hata kidogo. Alikuwa kama mwanakondoo
apelekwaye machinjoni, kama kondoo akaavyo
kimya anapokatwa manyoya. Hakutoa sauti hata kidogo.” (Isaya 53: 7) Ni yeye
aliyesema ukipigwa shavu moja la kulia
geuza la kushoto. Yeye hakugeuza la kushoto tu aligeuza mwili mzima. Lakini
bado alikuwa na kadi nyingine kadi ya kumtumia Roho Mtakatifu. Maadui zake
walifikiri ameshindwa. Matumaini yake aliyaweka kwa Mungu, hakimu mwenye haki. “Yeye
hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake.
Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali
aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu
mwenye haki.” (1 Petro 2: 22) Ili
kuimarisha umoja wa wakristu tunahitaji kuvumiliana na kupendana. MUNGU NI HAKIMU MWENYE HAKI.
SIFA YA MWANAKONDOO NI KUWA SADAKA YA UPATANISHO
Katika jamii nyingi za kiafrika
kondoo hutumiwa katika kupatanisha watu. Nabii Isaya 11: 1-9 alitabiri ufalme
wa amani utakaoletwa na Yesu ambaye ni mwanakondoo wa Mungu. “Mbwa mwitu
ataishi pamoja na mwanakondoo, chui watapumzika pamoja na mwanambuzi. Ndama na
wanasimba watakuja pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.” (Isaya 11:6) Ili kupatana lazima tuangalie yale yanayotuunganisha. Mwanamke
mmoja na Bwana wake walifarakana. Waliamua kutengana. Wakawa wanaishi sehemu
zilizokuwa mbali. Siku moja mwanaume alirudi kwenye hilo jiji akiwa katika shughuli zake. Akaamua
kwenda kwenye makaburi kutembelea kaburi la mtoto wake. Akiwa amesimama kwenye
kaburi hilo
alisikia hatua za mtu anayetembea au mtitimo wa miguu ya mtembeaji. Aliogeuka
alimuona mke wake waliyetengana. Wote walikuwa na hamu ya kutembelea kaburi.
Badala ya kupeana migongo waligeuka na kukumbatiana. Walipatana. Walipatanishwa
na kifo cha mtoto wao. Tuangalie yale yanayotupatanisha na sio
yanayotutenga. Tusisitize yanayotupatanisha na sio yanayotutenga.
Naomba umtazame mwenzako machoni.
Huyo uliyemtazama Yesu alimfia. Mwanakondoo wa Mungu alichinjwa kwa ajili yake.
Huyo anayemtazama Mungu anamfahamu kwa jina. Mwanakondoo wa Mungu yupo tayari
kuondoa dhambi zake. Huyo anayemtazama ni mtu. Huyu anayemtazama ana thamani
kubwa kiasi cha Yesu kumfia. Huyo unayemtazama sio takataka. Mungu haumbi
takataka Yesu amemwaga damu kwa ajili yake. Huyu unayemtazama sio mtumba. Mungu
haumbi mtumba. Yesu Mwanakondoo hakuchinjwa kwa ajili ya mtumba. Huyu unayemtazama
sio kivuli au photocopy. Mungu haumbi vivuli au photocopy Mungu anaumba watu.
Huyo unayemtazama ni Yesu. Huyo ni binadamu. Huyo ni zaidi ya Mkenya ni
binadamu. Ni mwana Adamu. Ni mwana wa Mungu. Mkatoliki ni zaidi ya Mkatoliki ni
mwana wa Mungu. Mwanglikani ni zaidi ya Mwanglikani ni mwana wa Mungu. Huyo
uliyemtazama na huyo ambaye nabii anamzungumzia katika kitabu cha Isaya, “Mwenyezi-Mungu, ambaye aliniita tangu
tumboni mwa mama ili nipate kuwa mtumishi wake.” (Isaya 49:5)
SIFA YA MWANAMBUZI WA WATU NI KUBEBESHWA LAWAMA
Wayahudi walikuwa na desturi ya kufanya toba kwa Mungu.
Siku ya kufanya toba walimutwisha mbuzi mmoja makosa yao yote na dhambi zao
zote na kumfukuzia mbali na kumnyoshea mbuzi huyo kidole kuwa makosa sasa yote
ni yako. Tabia ya kuwalaumu wengine inalinganishwa na kumnyoshea mbuzi kidole
(scapegoat complex). Huko India watu walijaza mtumbwi makosa ya watu kiishara
na kuweka mtumbwi huo katika mto Ganges . Namna hiyo watu walitumaini kutakaswa
dhambi zao.
“Akiishamaliza kufanya malipizi ya patakatifu, ya hema ya kukutania, na
ya altare, atamleta yule beberu aliye mzima. Haruni atamwekea mikono yote
miwili juu ya kichwa chake, na kuungama juu yake makosa yote ya wana wa
Israeli, maovu yao yote, na dhambi zao zote. Akiisha kuyaweka hivyo juu ya kichwa cha huyo beberu, atampeleka
jangwani kwa mkono wa mtu mmoja aliye hapo tayari, na huyo beberu atajichukulia
makosa yao yote mpaka huko mahali palipo jangwa. Atamwachia mbuzi jangwani”
(Mambo ya Walawi 16: 20 -22).
Tabia ya namna hiyo inajitokeza katika familia. Unakuta
kuna mtu katika familia ambaye anatwishwa makosa ambayo hakuyatenda. Glasi
ikivunjika, ndugu wakigombana, fedha ikiota mbawa kama ndege na kuruka na kupotea,
pakiwepo na mafuriko ya madeni yeye anasingiziwa kuwa ndiye chanzo cha
matatizo. Katika hali mbaya ya uchumi dunia nzima kuna watu ambao wanaweza
kuwalaumu wengine kuwa wanawaroga ndio maana biashara yao imekwama. Katika
sehemu zenye ukame kijiografia ndiko kuna hadithi za wachawi wa mvua. Watu
wanadiriki kuwalaumu wengine kuwa wanaroga mvua isinyeshe. Mtu msafi
anapochafua hewa watu humlalamikia mtu mchafu kati yao . Ni methali ya Yoruba.
Ni mchezo ule ule wa Adamu na Eva wa kulalamikia nyoka na mazingira.
Ukweli ungawa
unauma lazima kukubali ukweli ulivyo na kurekebisha palipo na kasoro zilizo
ndani ya uwezo wetu kurekebisha. Ukweli unatutaka tuwajibike kwa makosa yetu,
tuwajibike kwa maamuzi yetu na tubebe misalaba yetu badala ya kuwatwisha wengine
misalaba yetu. Badala ya kuwalaumu wengine tuwakomboe wengine. Hakuna ambaye
anapika nyama iliyooza na kuitia kwenye mdomo wa rafiki yake na kusema mdomo
wako unanuka.
Watu wakishatenda dhambi na kufanya makosa wanatafuta “mwanambuzi” wa
kubebesha lawama badala ya kuungama. Wanatafuta mchawi ni nani? “Utafutaji wa
mbuzi anayebebeshwa dhambi ni safari rahisi kati ya safari zote za uwindaji,”
alisema Dwight D. Eisenhower.
Lazima tumlaumu mwizi kwanza kabla ya kumwambia mwenye mali
kuwa mali yake aliitunza vibaya. Ni methali ya Nigeria . Samaki wengi hula watu
lakini ni nyangumi tu anayelaumiwa. Ni methali ya Jamaica . Methali hizo
zinahusu lawama na kuwanyoshea wengine kidole. Nyani haoni kundu lake. Ni
methali ya Kiswahili. Nyani haoni makalio yake. Methali hii inamaanisha kuwa
mtu yuko tayari kuona makosa yaw engine na hata kuwalaumu lakini haoni
makosa yake. Yuko tayari kuona kipande kidogo cha mchanga kwenye jicho la mwenzake
lakini haoni jiwe kubwa katika jicho lake. Mwafunzi ambaye alikuwa anakuwa wa
kwanza miaka mingi darasani alipokuwa wa pili kwenye mtihani wa kufunga mwaka
aliulizwa na mwalimu wake kwa nini amekuwa wa pili alisema kuwa hata watu
mashuhuri wamekuwa wa pili. Mwalimu alitaka mwanafunzi atoe mfano. Mwanafunzi
alisema, "George Washington alikuwa Rais wa kwanza wa Amerika, alikuwa wa
kwanza katika vita, wa kwanza katika kuleta amani, wa kwanza kuchukua nafasi
kubwa katika mioyo ya Waamerika lakini alioa mjane, katika hilo alikuwa wa
pili." Mwanafunzi hakutoa sababu zake zinazomhusu ambazo zilimfanya arudi
nyuma.
SIFA
YA MWANAMBUZI WA WATU NI KUSINGIZIWA
Mtu mmoja alikua karamuni na wakwezake pamoja na mkewe na rafikize
wakati wa chakula yulemtu akaweka pilipili nyingi kwenye chakula chake kwaajili
ya tamaa alipo kula ghafla akaaza kuwashwa akatulia kimya akisikilizia maumivu
mara machozi yakaanza kumtiririka
machonig,baba mkwe akamuliza unalia nini akamjibu natafakari wema wa mungu
namatendo yake yaajabu ,mkewe na wote walio kuako karamuni walimsifu sana
kuaameguswa ,laki kwakua yule bwana na
mkewe walikua wana kula katika saani moja mkewe naye akanaza kutokwa machozi
mama yake akamsifia binti yake kua nayeamjua mungu lakini binti akasema chakula
kina pilipili nyingi,sasa watu wote walitambua kilichokua kina mliza yule bwana
kua nipilipili akapatwa naaibukubwa sana.Fundisho
tukubali matokeo ya makosa yetu wala tusimsingizie mtu wala mungu.mungu haonekani bali yeye
anatuona sisi.
Katika masuala ya maadili kuna ambao wanasingizia
wazazi hao kwa kushindwa wao kuishi ipasavyo. Mlevi anaweza kumsingizia mjomba
wake na kusema nimemfanana na mjomba wangu yeye alikuwa akilewa chakali kila
siku.
ILI MWANAKONDOO WA MUNGU
ATUJALIE AMANI TUFANYE NINI?
Gari likigongana na gari lingine gari
linapelekwa kwenye gereji au karakana. Mkristu akigongana na Shetani anaenda
kwa Yesu. Tufanye nini? Kwanza: Usilipe uovu kwa uovu: uwe mkweli kwa
nafsi yako.Usipokuwa mkweli kwa nafsi yako hauwezi kujua. Mara unasikia mtu
analalamika. Wananionea. Hasemi yeye amewatendea kosa lipi. Amenipiga. Hasemi
kwa nini amepigwa.Tuwe wakweli kwa nafsi zetu. Pili: Tutakieni amani. “Neema na amani kutoka
kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi” (1 Wakorintho 1: 3).
Tatu: Kuwa na shukrani katika kila hali