JUMAPILI YA 7 YA MWAKA A
1. Law 19: 1-2. 17-18
|
2. 1 Kor 3: 16-23
|
3. Mt. 5: 38-48
|
Mmesikia ya kuwa imenenwa, ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’ Mimi
lakini nawaambieni, msibishane na mtu mbaya” (Mt 5: 38).
Mzee Joe alikuwa kufani kwenye kitanda
cha mahuti. Kwa muda wa miaka mingi alikuwa hapatani na Bill, ambaye zamani
alikuwa mmoja wa marafiki zake. Akitaka kunyosha mambo yake kabla ya kuaga
dunia alimtuma Bill waongee na kumaliza mambo. Bill alipofika, Joe alimwambia
kuwa anaogopa kwenda mbinguni akiwa na kinyongo naye. Kwa kusita na kwa
kujikaza Joe aliomba msamaha kwa mambo aliyoyasema na kuyatenda.
Alimwaakikishia Bill kuwa amemsamehe kwa makosa yote aliyomtendea. Mambo yote
yalionekana kwenda vizuri mpaka hapo Bill alipojiandaa kuondoka. Alipokuwa
anatoka chumbani, Joe alimuita, “Lakini kumbuka, nikipona, haya yote niliyosema
hayana maana wala uzito.”
“Jicho
kwa jicho” mtazamo huo utawaacha watu wengi
wakiwa vipofu. “Jino kwa jino” mtazamo huo utawaacha watu wengi wakiwa
vibogoyo. Kisasi
kilicho bora ni kusahau. Ndivyo isemavyo methali ya Kiswahili. Lakini kisasi
kilicho bora zaidi ni kusamehe. Na pia
kisasi kilichobora zaidi ni kutokuwa kama yule aliyekufanyia jambo baya ili
pasiwepo watu wabaya wawili, yeye aliyekufanyia ubaya na wewe unayeshindwa
kujibu ubaya kwa wema. Nelson Mandela alikuwa na haya ya kusema juu ya kusamehe
waliomtendea vibaya: “Nilivyotembea
kutoka mlangoni nakuelekea lango ambalo likuwa natokea na kwenda kwenye uhuru
wangu, nilijua kuwa kama nisingeacha ukali wangu na chuki nyuma yangu,
ningeendelea kuwa gerezani.” Kusamehe
ni kumfungua mfungwa utagundua mfungwa ni wewe. Kabla ya kusamehe unakuwa
kwenye gereza la chuki na kulipiza kisasi. Kumbuka chuki umchoma anayeitunza. “Msamaha ni manukato ambayo ua huacha
kwenye kisigino kilicholikanyaga,” alisema Mark Twain. Kutosamehe ni kurudi
nyuma. Nakubaliana na Libba Bray aliyesema: “Hatuwezi kurudi nyuma. Tunaweza tu
kwenda mbele.”
Msamaha ni Dawa
Kutosamehe ni Sumu
“Kutosamehe ni kama kunywa dawa ya panya na kungoja ili panya afe,” alisema
Anne Lamott. Naye Nelson Mandela alikuwa na mawazo hay ohayo aliposema: “Chuki
ni kama kunywa sumu ukitumaini kuwa itawaua adui zako.” Kuomba
msamaha na kukubali kupokea msamaha ni tiba. Karl Menninger, daktari bingwa wa
magonjwa ya akili kama kichaa alisema kuwa kama
angeweza kuwafanya wagonjwa kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili kuamini kuwa
dhambi zao zimesamehewa, asilimia 75 ya wao wangetoka wamepona siku inayofuata.
Zawadi nzuri ya kumpa adui yako ni msamaha
Kabla hatujasamehe hatutulii. Kumsamehe mtu hakubadili yaliyopita
bali kunabadili yajayo. Kunabadili mahusiano mabaya yanakuwa mazuri, kunabadili
fikra hasi zinakuwa chanya. Kunatibu vidonda vya chuki. Kwa mtazamo huo, zawadi
nzuri ya kumpa adui yako ni msamaha.
Mshangaze adui yako kwa kumpa zawadi ya msamaha. Zawadi hiyo itakumbukwa
na kuzunguziwa vizazi hata vizazi. Ni zawadi ambayo Yesu aliwapa waliomtesa na
kumtundika msalabani. Ni zawadi ambayo Stefano katika kitabu cha matendo ya
mitume, aliwapa waliomua. Ni zawadi ambayo Papa Yohane Paulo II alimpa Ali Agca
ambaye alimpiga risasi. Ni zawadi ambayo Josephina Bakhita wa Sudani aliwapa
waliomuuza utumwani. Kuna umuhimu wa kusamehe, lakini kuna umuhimu wa kuwa
tayari kupokea msamaha. Ishara ya kuwa mtu amepokea msamaha ni kutokurudia
kosa. Zipo hatua nyingi katika za kupokea msamaha na kusamehe.
Kwanza anayepaswa kusamehewa
lazima atambue kosa lake. Na kosa kubwa ni kutokutambua kosa. Pili kutubu na
kuungama ni muhimu katika hatua za kupokea msamaha. Mtume Paulo anatuasa,
“Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele na matusi. Acheni kila uovu!
Mwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe nyinyi kwa njia ya Kristo”
(Waefeso 4: 31-31). Kuwa na hasira na
uhasama, chuki, kelele na matusi ni kuamua kujiweka kwenye gereza la kujitakia.
Kama kusamehe ni muujiza basi tuna uwezo wa
kufanya huo muujiza. Msamaha si jambo la mzaha. Mwalimu aliwauliza wanafunzi wa
darasa la kwanza, “Kabla ya kumpa mtu msamaha mtu anatakiwa kufanya nini?”
Mwanafunzi akajibu, “Kwanza mtu afanye kosa.”
Mwalimu alitegemea mwanafunzi ajibu, “Kwanza
lazima atambue kosa lake.” Tunazungumzia msamaha katika mazingira ambapo kosa
limetendeka.
Kwa kawaida ni vizuri kupasha
moto chakula lakini si vizuri kupasha moto wa kumbukumbu ya mabaya
uliyotendewa. Kama Nelson Madiba Mandeka angepasha moto kumbukumbu ya mabaya
aliyotendewa hasingezungumzia kusameheana baada ya kukaa gerezani kwa kipindi
cha zaidi ya miaka ishirini na tano. Kusamehe ni tendo la kibinadamu, mbwa
hawezi kutafakari juu ya kumsamehe mbwa mwenzake. Tendo la kusamehe ambalo ni
la kibinadamu linainuliwa na kuwa la kimungu. Zipo faida nyingi za kusamehe.
Kusamehe kunaleta amani ya moyoni. Kusamehe kunaleta mwanga katika maisha yetu.
Mungu sio
Adui wa Adui Zako
Martin Niemoller alitoka katika
gereza la Hitler akisema, “Ilininchukua muda mrefu kujifunza kuwa Mungu sio
adui wa adui zangu. Na sio adui wa
maadui zake.” Kama unapenda watu wakupende nawe uwapende. Injili ya leo
inatutaka tuwapende adui zetu: “Mmesikia kwamba imenenwa, ‘umpende jirani yako,
na umchukie adui yako.’ Mimi lakini nawaambieni, wapendeni adui zenu, waombeeni
wanaowadhulumu…” (Mathayo 5:43-44). Adui mpende. Ni methali ya Kiswahili.
Usimchukie hasidi au adui yako. Adui zetu yafaa kuwachukulia makosa yao watutendeavyo. Huenda
wakatubu na kuacha uovu wao. Tunaaswa na methali ya Kiswahili, Adui aangukapo mnyanyue. Ni methali
nyingine ya Kiswahili kuhusu kumpenda adui na kumtendea mema. Ni ubinadamu
kumsaidia adui yako akiwa na shida. “Tunapowachukia
maadui wetu tunawapa uwezo juu yetu: uwezo juu ya usingizi wetu, hamu yetu ya
chakula, shinikizo letu la damu, afya yetu na furaha yetu.” (Dale Carnegie)
“Jinsi miti yote inavyojulikana kwa vivuli vyake, ndivyo hivyo watu wazuri
wanajulikana kwa maadui wao.” (Methali ya Kichina).
Masharti ya msamaha
“Usiposamehe uhalifu unatenda uhalifu.”
“Anayesamehe anapata ushindi.” “Anayesamehe anamaliza ugomvi.” “Hasiyejua
kusamehe hasitegemee msamaha.” Hizo ni baadhi ya methali toka makabila
mbalimbali katika Afrika. Msamaha una nafasi katika tamaduni za kiafrika.
Kusamehe makosa ni tendo la huruma. Yesu alisisitiza sana
hitaji la kuwasamehe wengine kama tunavyosoma
katika Biblia “Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, ‘Je, ndugu yangu
akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?’ Yesu akamjibu, ‘Sisemi mara saba
tu, bali sabini mara saba.’” (Mathayo 18:21” Kusamehe mara sabini na saba
kunamaanisha kusamehe kila mtu kila mara. Kunamaanisha kusamehe bila kikomo.
Lakini kutoa msamaha na kusamehe kuna masharti yake.
Sharti la kusamehewa ni kusamehe.
Katika sala ya Baba yetu (Mathayo 6: 9-13) ambayo ina maombi saba ni ombi moja
lililo na masharti. “Utasamehe makosa yetu kama
tunavyowasamehe waliotukusea.” (Mathayo 6: 12) Maombi mengine kama
“Utupe leo mkate wetu wa kila siku,” “Usitutie vishawishini,” hayana masharti. Ukitaka Mungu akusamehe
samehe wale waliokukosea. Samehe mtu mbaya aliyekukosea ili pasiwepo watu
wabaya wawili: yule aliyekukosea na wewe ambaye hukutoa msamaha.
Sharti lingine la msamaha ni kuweka
makosa katika kaburi la sahau. Samehe na sahau. Kuna baadhi ya watu ambao
hupamba methali ifuatayo katika nyumba zao. “Kwangu uingie lakini kumbuka
mabaya uliyonitendea.” Methali kama hiyo haionyeshi msamaha. Kila mmoja anabidi
awe na “kaburi dogo,” la kuzika makosa ya wale waliomkusea. Kuna Mzee mmoja alikuwa
mgonjwa sana .
Alikuwa kufani akichungulia kaburi. Alimuita mchungaji ampatanishe na jirani
yake kusudi akifa Mungu awe tayari kumsamehe kwa vile naye anasamehe. Basi
Mchungaji aliwapatanisha. Wakasameheana. Lakini jirani yake alipojiandaa kurudi
nyumbani mgonjwa huyo katika kitanda cha mauti alisema, “Mapatano haya yana
maana iwapo nitakufa, kama sitakufa usikanyage
kwangu.” Mgonjwa huyu alikuwa hajasamehe. Alikuwa anatunza kinyongo.
Sharti lingine la msamaha ni
kutokujiingiza katika kutenda maovu. Hakuna mahali popote katika ujumbe wa
Biblia ambapo msamaha au huruma kama kiini
chake humaanisha kujiigiiza katika kutenda maovu, kujiigiza katika kashfa,
kutia wengine hasara au kutukana wengine. Katika hali yoyote ile kufanya
malipizi kwa ajili ya maovu na kashfa, kufidia hasara na kufanya malipizi ya
matukano ni masharti ya msamaha.
Lakini katika maisha tunakuta vizuizi
na vikwazo vya kutoa na kupokea msamaha. Kutokuwa tayari kutubu makosa na
kubadilika ni kikwazo katika kupokea msamaha. Mtu anafanya kosa na hayuko
tayari kubadili nia na kumgeukia Mungu. Kumsamehe mtu ambaye hayuko tayari
kutubu ni kama kuchora picha kwenye maji.
Kikwazo kingine ni moyo mgumu. Moyo mgumu ni moyo unaotunza chuki. Lakini chuki
humchoma anayeitunza. Zaidi ya hayo, kukata tamaa, kukataa ukweli ulio wazi, visingizio, kuficha ukweli wa mambo,
ni vikwazo na vizuizi katika kutoa na kupokea msamaha. Lakini hatuna budi kutambua ukweli huu,
kisasi kilicho bora ni kusamehe.
Samehe
na Sahau
“Naweza kusamehe, lakini siwezi
kusahau” ni namna nyingine ya kusema “Siwezi kusamahe”, alisema Henry Ward
Beecher. Bwana wetu Yesu Kristu alisamehe na kusahau. Jambo ambalo linamtofautisha
shahidi wa kweli na shahidi bandia (wa uongo) ni moyo wa kusamehe. Sifa kubwa
ya wafiadini na mashahidi ni moyo wa kusamehe. Mtakatifu Stefano alilia kwa
sauti kubwa: “Bwana usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii” (Matendo 7:60). Katika
kila msamaha kuna upendo. Kusamahe ni kuchagua kupenda. Kusamehe ni chaguo
bora. Neno la kwanza la Yesu msalabani ni neno la msamaha: Baba
uwasamehe kwa vile hawajui watendalo.
Yesu hakulipa kisasi cha jicho kwa
jicho au jino kwa jino. “Sheria ya zamani “jicho kwa jicho – inaacha kila mtu
akiwa kipofu,” Martin Luther King anatukumbusha. Mtu akikosa na mwingine
aliyetendewa vibaya akakataa kata kata kutoa msamaha panakuwepo na watu wabaya
wawili. Kama mtu mbaya akikukosea msamehe,
pasije pakawepo watu wawili wabaya. Methali ya kichina inaweka bayana ukweli
huu, “Yeye anayetaka kulipa kisasi itambidi kuchimba kaburi mbili.” Kulipa
kisasi ni kumkomoa mtu, lakini ni zaidi ya hapo ni kujikomoa, kwa sababu “Yule
ambaye hawezi kuwasamehe wengine anaharibu daraja ambalo lazima avuke yeye
mwenyewe; kwa sababu kila mtu anahitaji kusamehewa,” jambo hili aliliweka
vizuri Thomas Fuller. Tendo la Yesu kusamehe waliomkosea ni changamoto kwetu.
Wasamehe
Wanafamilia
Baba fulani alikuwa anamwambia siri
mtoto wake. “Kila mara mama yako na mimi tunapokuwa na mabishano huwa nina neno
la mwisho.” “Huwa unafanya nini?” aliuliza mtoto kwa mshangao, “Ni rahisi”,
alitabasamu mzee, “Naomba msamaha”. Msamehe mama yako ambaye hataki uwe mtu
mzima. Msamehe baba yako ambaye ni mlevi. Msamehe dada yako ambaye hakuheshimu.
Msamehe mama mkwe mwenye wivu. Msamehe mke wako kwa usumbufu wake. Msamehe
mzazi wako kwa kukusahau.
Wasamehe
Marafiki Zako
“Ni rahisi kumsamehe adui kuliko
kumsamehe rafiki yako,” alisema Austin Malley. Msamehe rafiki yako licha ya
kasoro zake. Msamehe rafiki yako ambaye alikuacha ukiwa na upweke wakati wa
shida. Msamehe rafiki yako ambaye hatimizi ahadi. Msamehe rafiki yako ambaye
anajifanya kuwa hamjuani mbele ya watu.
Msamehe rafiki yako ambaye hakukutendea haki. “Kila mtu anapaswa kutunza kaburi la usawa wa kadiri, ambalo ndani ndimo
atazika makosa ya rafiki zake,” alituasa Henry Ward Beecher.
Ujisamehe
Wewe Mwenyewe
Kama ambavyo hauwezi kuwapenda wengine
kama hujipendi, hauwezi kuwasamehe wengine kama
wewe mwenyewe hujisamehe. Ujisamehe kwa kutopokea ushauri na kwa kukosa la
jiwe. Ujisamehe kwa kukosa ujasiri, ujisamehe kwa hofu isiyo na msingi.
Ujisamehe kwa kukerwa na yale yasiyokuhusu. Ujisamehe kwa ya kwako kuyaweka
chumbani na ya wengine sebuleni. Jisamehe kwa kutoona lako. Jisamehe kwa kubaki
na labda. Jisamehe kwa kusherekea vita na kulilia amani.
Kwa
Nini Yesu Aliomba Baba Awasamehe Wakati Yeye Angesamehe?
Mtakatifu Bernard analo jibu:
“Alimwomba Baba, siyo kwa sababu yeye asingeweza kuwasamehe, bali ili
atufundishe kuwaombea wanatukosea”. Mtawa huyo alizidi kusema: “Ee jambo la
ajabu! Anapaza sauti, samehe; wanapaza sauti, msulubishe”. Hii ni changamoto
kwetu. “Mtazame Mungu wako msalabani;
ona anavyowaombea walimsulubisha; na halafu ukatae kumsamehe ndugu yako aliyekukosea!
“Alitoa changamoto Mtakatifu Augustino.