Jumapili
ya 2 ya Kwaresima
1. Mwanzo 12: 1-4
|
2. 2 Timotheo 1: 8-10
|
3. Mathayo 17: 1-9
|
USIJISAHAU
“Kama umemsahau Mungu umejisahau.” Ni methali ya Kiswahili. Wakati
Yesu alipogeuka sura katika mlima Tabor Mtume Petro alijisahahu katika masuala mawili. Kwanza
alijisahau yeye na wenzake katika suala
la kusali. “Petro na wenzake walikuwa wameshikwa na usingizi, lakini walipoamka,
waliona utukufu wake na wale watu wawili wakisimama naye” (Luka 9: 32). Kuacha kusali ni kujisahau. Mtoto mmoja aliyeitwa John alikuwa
anajiandaa kusali sala za jioni
alipomuuliza mama yake, “Ni lini unanishauri niache kusali kama baba alivyoacha
kusali?”Mama alimweleza mtoto wake kuwa sala haina mambo ya likizo, haina
kustaafu. Sala haina kuhairisha.
Pili alijisahau katika suala la
kujenga vibanda. Petro alimwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri kwetu kukaa hapa;
tutajenga vibanda vitatu, kimoja chako, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.”
(Mathayo 17: 4). Juu ya mtume Petro Caro
Kardinali Maria Martini alikuwa na haya ya kusema. “Tilia maanani kutojipendelea kwake: vibanda ni kwa ajili ya Yesu, Musa
na Eliya, wakati mitume wanaweza kukaa
nje ambako ni wazi.” Ingawa mtume Petro akujipendelea hakujipenda au
alijisahau. Marcus Tullius Cicero
aliwahi kusema: “Sijawahi kusikia mtu
ambaye ni mzee sana akisahau alipozika pesa yake! Wazee hukumbuka
wanachokipenda: tarehe za kesi za madai, na majina ya wanaowadai na wadaiwa.”
Kama tunakumbuka tunachopenda tusiwasahau watu wengine hatuna budi kuwapenda.
Mfanyabiashara anaweza kujisahau.
Anatafuta pesa lakini hawezi kula vizuri au kulala mahali pazuri. Huko ni
kujisahau. Mvuvi anaweza kujisahau. Wakati anauza samaki anakula chakula bila
kitoweo. Fundi seremala wakati anatengeneza milango mizuri kwa ajili ya watu
wengine unakuta mlango wake una matundu makubwa ya kupitisha kichwa. Mfinyanzi
hulia kwenye kipande cha chungu. Ni methali ya Tanzania. Anayetengeneza vyungu
vya kupikia yeye anatumia kipande cha chungu kilichovunjika. Fundi cherehani
wakati anashonona mitindo mipya unakuta yeye anavaa nguo zilizochanika. Ni
kujisahau. Daktari wakati anahimiza watu wengine wamalize dozi yeye akiugua
anashindwa kumaliza dozi. Ni kujisahau. Unaweza kukuta mtu anauza baisikeli
wakati yeye hana baisikeli. Ni kujisahau. Mwalimu anayefundisha somo la
kuwekeza yeye hawekezi hata kidogo kuwekeza. Mwalimu anafundisha somo la
Mipango Mikakati wakati yeye hana hata diari. Ni kujisahau. Mlinzi anaweza
kujisahau. Unaweza ukagundua wizi umetokea mahali fulani lakini aliyesaidia
kufanikisha zoezi hilo la kuhujumu ni mlinzi. Mwindaji anakuwa muwindwa. Kuna
methali ya wahaya isemayo: Wanaolinda
vibuyu vya pombe ndio wanaovivunja. Mwanampotevu alijisahau kuwa Baba yake
ni Tajiri alikuwa tayari kujishibisha kwa r chakula cha nguruwe. Usijisahau
wewe ni Mwana wa Mungu. Umeumbwa kwa mfano na sura ya Mwenyezi Mungu.
USIMSAHAU
Yesu usimsahau. Mto ambao usahau chanzo chake utakauka. Ni methali
ya Yoruba. Yesu ni chanzo chako usimsahu. Kuna aliyesema: “Tukikutana na ukanisahau, haujapoteza chochote. Ukikutana na Yesu
Kristo na ukamsahau, umepoteza kila kitu.” Mateso, shida, visitufanye
tumsahau Yesu wa utukufu. Mtume Yohane
mmoja wa watatu aliandika: “Nasi tumeona
utukufu wake” (Yohane 1: 14). Petro aliandika: “tulikuwa mashahidi wenyewe tulioona kwa macho yetu utukufu wake” (2
Petro 1: 16). Hii ni kumbukumbu ya kugeuka sura. Mitume kabla ya kuimarishwa na
Roho Mtakatifu na kabla ya ufufuko walisahau Yesu wa utukufu, Yesu wa kugeuka
sura. Petro alimfuata kwa mbali. Petro alimkana Yesu. Yohane akikumbuka vizuri
Yesu wa utukufu alikuwa amesimama chini ya msalaba. Yakobo alikimbia. Usimsahau
Yesu wa kugeuka sura. Katika Misale ya Waumini Chapa ya kumi ya mwaka 2008
katika kituo cha kumi na tano tunasali hivi: “Twakushukuru, ee Yesu, kwa mateso yako, lakini twakushukuru hasa kwa
ufufuko wako, kwa kuwa huo ndio unaotupa hakika ya kuwa hatukuzaliwa kwa ajili
ya mateso na maumivu, bali kwa ajili ya heri ya milele.” Katika maneno haya
tunajifunza kuwa mateso hayana kauli ya mwisho. “Tuishi maisha yetu kama kwamba Kristo anakuja mchana huu,” alisema
Jimmy Carter.
Mtakatifu Thomas Aquinas aliweka
wazi lengo la Yesu kugeuka sura: “Wewe
uligeuka sura mlimani, na kadiri walivyoweza, wafuasi wako walitafakari utukufu
wako ee Kristo Mungu ili watakapokuona umesulubiwa waelewe kwamba mateso yako
yalikuwa ya hiari, na watangaze duniani kwamba Wewe ni kweli mng’aro wa Baba.”
Hapa tunajifunza kuwa Ijumaa Kuu inatangulia Jumapili ya Paska. Hapa
tunajifunza kuwa mtaka cha uvunguni sharti ainame. “Imetupasa kuingia katika
ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (Matendo ya Mitume 14:22).
Katika hadithi za Aesop kuna hadithi ya mbwa aliyeona sura yake
ikiakisiwa kwenye dimbwi la maji chini ya miguu yake. Ingawa alikuwa
ameshikilia mfupa, aliona wivu kuona mbwa kwenye dimbwi la maji akiwa na mfupa
mdomoni. Alifungua kinywa chake ili kumbwekea mbwa mwingine na kuweza
kumnyanganya mfupa. Utukufu kama wa Yesu wa kudumu ndio tunautafuta.
Usiache utukufu huu na kukimbilia mambo yanayopita. Usiache mtego ambao
umekamata ukaenda kuchungulia mtego uliotegwa.
USIWASAHAU
Watu wengine usiwasahau. Kusahau ni sawa na kutupa. Ni methali ya
Kiafrika. Usiwatupe wenzako. Ukisikia mtu anasema amewatupa ndugu zake. Ina
maana amewasahau. Petro alimwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri kwetu kukaa hapa;
tutajenga vibanda vitatu, kimoja chako, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.”
(Mathayo 17: 4). Mt. Petro alisahau
kuna watu wanawangoja chini ya Mlima. Alisahau
kuwa kuna mitume wenzake. Yesu Kristu
alitaka kuwaonesha kidogo utukufu ambao ni matokeo ya kubeba msalaba. Ijumaa Kuu kwanza, Jumapili ya Paska baadaye. Kula kutamu, kulima mavune. "Mavune" maana yake "
machofu". Utukufu huu ilibidi Mt. Petro
arudi chini ya mlima na wenzake waufanyie kazi.
Ukiona vyaelea vyaundwa.
“Petro hakulielewa bado neno hilo alipotamani kuishi na Kristo mlimani.
Amekuwekea hayo, Petro, baada ya kifo chako lakini sasa yeye mwenyewe
anakuambia: shuka kuangaika duniani, ukatumikie duniani, ukadharauliwe,
ukasulubiwe duniani.Uzima umeshuka ili kuuawa:Njia imeshuka ili isikie uchovu
wa duniani; chemichemi imeshuka ili kupata kiu;nawe wakataa kuteseka? “ (Mt. Augustino
Sermo 78,6: PL38,492-493;Lk9:33). Cha bure hakipatikani. Mtaka cha uvunguni
sharti ainame.
Kuwakumbuka watu wengine ni jambo
muhimu. Mwizi msalabani alitaka kukumbukwa (Luka 23:42). Wahaya
wana msemo husemao, "Maji yakichemka hayasahau ubaridi." Tusisahau makundi ya watu chini ya mlima,
wenye shida, wenye matatizo. Kuna
mgonjwa wa kutembelea chini ya mlima, kuna wafu wa kuzika chini ya mlima, kuna
mfungwa wa kutembelea chini ya mlima, kuna aliyeuchi ni wa kuvisha chini ya
mlima.
Mtoa ahadi asiwasahau wale aliowapa ahadi. Nasi katika maisha
tusiwasahau wengine. Ahadi tunazofanya
wakati wa matatizo na karaha, wakati wa matezo na masumbufu tunazisahau wakati
wa raha, wakati wa utulivu. Kukopa
harusi, kulipa matanga. Daktari alimwambia mgonjwa, “utapona lakini
unaumwa sana”. Mgonjwa alimjibu,
“Tafadhali, Daktari fanya kila unaloweza kuakikisha ninapona. Nikipona nitatoa milioni thelathini kwa ajili
ya ujenzi wa Hospitali mpya.” Miezi
michache baadaye mgonjwa huyo alipokuwa amepona kabisa daktari alimkumbusha
ahadi yake: “Ulisema ukipona utatoa msaada wa milioni thelathini?” Mgonjwa aliyepona alishangaa, “Kama nilisema
hivyo, nilikuwa mgonjwa kweli.” Mgonjwa
aliyepona alimsahau daktari.
Mwalimu usiwasahau wanafunzi ni wateja wako wanakutegemea uwape elimu.
Wanafunzi wanahitaji msaada toka kwa walimu kutokana na visa vifuatavyo:
Mwalimu wakati wanaandikisha wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza.
Mwalimu alimwambia mwanafunzi: “ Nitajie majina ya baba yako na mama yako.
Mwanafunzi alijibu.” Majina yao ni Dadi na Mami.” Katika kisa kingine mwalimu alimuuliza mwanafunzi:
“Taja vitu viwili ambavyo havikuwepo miaka mia moja iliyopita.” Mwanafunzi
alijibu: “Ni mimi na wewe.” Lakini binadamu si kitu. Mwalimu alimuuliza
mwanafunzi: “Mama mdogo kwa Kiingereza anaitwaje?” Mtoto alijibu: “Anaitwa –
minimum.” Na mama mkubwa anaitwaje?” mwalimu aliendelea kuuliza licha ya
mwanafunzi kukosea. Mwanafunzi alijibu anaitwa maximu.” Mwanafunzi alikosea.
Wanafunzi wanahitaji kusaidiwa.
Mwanasiasia usiwasahau wapiga kura wapo chini ya mlima wanakungoja.
Daktari,
nesi, mganga, muuguzi usiwasahau wagonjwa. Wagonjwa wana hofu zao wengine
hawaelewi. Kuna mtu mmoja alikuwa anatoka Hospitalini analia. Karibu na lango
palikuwa na mgonjwa anaingia akauliza kwa nini unalia. Mgonjwa akasema wamekata
kidole changu wakati wanatoa damu ili kuipima. Mgonjwa mwingine wa kiume
akashtuka na kusema: “Mimi itakuwaje maana naenda wapime mkojo.” Mchungaji usiwasahau kondoo wako. Wakristu msiwasahau wachungaji. Mtawala
usiwasahau wale unaowatawala. Mzazi
usiwasahau watoto wako. “Kuku mwenye vifaranga hamezi mnyoo.” Ni methali ya
kisukuma. Watoto msiwasahau wazazi wenu.
“Hujui kama unawapenda wazazi wako mpaka hapo wanapokufa.” Ni methali ya
Namibia.
Mwanandoa usimsahau mwenzi wako wa ndoa. Kula umbakizie. Mkumbuke. Usitake kwenda mbinguni peke yako. Ilikuwa
ni wakati wa roho kuingia mbinguni. Watu waligawanywa kulingana na hali zao za
maisha; hivyo, watu wa ndoa, watawa, mapadre, na watu wasio na miiito hiyo ya
ndoa, utawa na upadre walikusanywa pamoja. Lango la mbinguni lilikuwa na mlango
kwa kila hali ya maisha. Watu wa ndoa kwa mfano, walipaswa kuingia kupitia
mlango wa kwanza. Hata hivyo mwanamume mmoja ambaye ndoa yake iliishatenguliwa
kwenye mahakama ya serikali, zamu yake ya kuingia ilipowadia, alikuta kwamba
mlango haufunguki tena. “ Malaika”, alimwita mlinda mlango,
“Nimejaribu kufungua huuu mlango kwa ufunguo wangu, lakini haufunguki”. “Mke
wako yuko wapi ?” Malaika aliuliza. “Nilimpa talaka.” “Basi inabidi umtafute.”
“Lakini sijui aliko!” alijibu mwanaume. “Heri ungelijua”, alisema malaika.
“Lango la mbinguni kwa watu wa ndoa laweza kufunguliwa tu kwa funguo mbili’.
“Lakini mke wangu ana nini la zaidi?” aliuliza kwa uchungu. “Bwana”, malaika
akajibu, “ufunguo mwingine wa mlango anao yeye. Unahitaji ufunguo wake ili
mpate kuingia pamoja”. (Angalisho Katika Kanisa Katoliki hakuna talaka.
Panaweza kuwepo kutengana kwa muda. Au ndoa kubatilishwa kwa maana ya
kutangazwa ndoa haikuwepo ni null and void)
Wakopaji msiwasahau
waliowakopa. Isiwe kukopa arusi kulipa matanga. Tulio hai tuwakumbuke marehemu. Tuwaombee tusiwasahau.
HITIMISHO
Kumbuka kukumbuka. Kugeuka sura ni tukio linaloimarisha imani. “Tukio
hili liliimarisha imani ya Mitume hao watatu kwa Bwana wetu Yesu. Bwana alijua
kwamba imani yao itajaribiwa vikali sana baadaye watakapomwona bustanini katika
mahangaiko makubwa, na hasa atakapokuwa anateswa na kuuawa msalabani. Kwetu
sisi, hii ni nafasi ya kuiamsha upya imani yetu kwa Kristu Bwana wetu Msulubiwa
na Mfufuka, ambaye heri yake tunatumaini kuishiriki baadaye. Kulitafakari fumbo
hili kutujalie picha fulani ya heri hiyo ijayo.” (John Kabeya, Maisha ya Watakatifu, uk. 270). Yesu ni
mfariji mateso tunayopitia. Unaweza kumweleza mtoto sababu za kundugwa sindano nesi anapokuja kumdunga
sindano anakimbia kumwendea mama yake. Kufarijiwa hakuhitaji sababu bali kujua
kuna mfariji.
Kuwa na utamaduni wa kupiga picha. Piga picha ya utukufu wa Kristo.
Katika somo la kwanza tunaona utamaduni wa kupiga picha Mungu akamleta nje
Abramu, akasema: “Utazame mbinguni,
uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu. Akamwambia: Ndivyo uzao wako
utakavyokuwa. Abramu akamwamini Bwana” (Mwanzo 15: 5-6). Unapoomba kitu piga picha yake akilini.
Usimsahau Mungu katika kila kitu,
hata kabla na baada ya kula. Kuna kijana alimwambia mwenzake mbona haukusali
kabla ya kula. Mwenzake akamjibu hakuna haja mama anapika chakula kizuri sana.
Kusahau kusali ni kujisahau na kumsahau Mungu. Toa huduma nzuri ulipo. Mhudumu
katika hoteli moja alimwambia mteja. “Wewe na ni mara yako ya kwanza kuja
hapa.” Mteja aliuliza: “Unajuaje?” Mhudumu alijibu: “Hapa mteja anayekula
chakula harudi tena.” Huenda sababu mteja haudumiwi vizuri.