|
|
|
“Kuzomewa kunasikika sana kuliko
kushangiliwa,” alisema Lance Armstrong.
Kama wewe umezomewa, umesemwa, umekataliwa na watu kumbuka Mungu wetu ni
Mungu wa fursa nyingine, nafasi nyingine, Mungu hajakukataa. “Nachukulia kukataliwa kama mtu anayepiga
vuvuzera masikioni mwangu kuniamsha ili kuendelea na safari badala ya kurudi
nyuma,” alisema Sylivester Stallone. Katika maisha tunkumbana na visa vya
kukataliwa. Ombi la kazi kukataliwa. Ombi la kuongezewa mshahara kukataliwa.
Ombi la uchumba kukataliwa. Hoja zako kwenye mkutano kukataliwa. Maoni yako
kukataliwa. Lakini Mungu hajakukataa.
Katika Biblia tunasoma: “Mara
hapo wafuasi wake walirudi na wakashangaa kumkuta anasema na mwanamke” (Yohane
4: 27). Mwanamke huyu alikuwa Msamaria. Alienda kuchota maji saa sita mchana
kwenye Kisima cha Yakobo. Alijitahidi kukwepa wanawake wengine. Historia yake
ilikuwa mbaya. Alikwepa majungu. Alikwepa kuyoshewa kidole. Alikwepa watu.
Alikuwa na wanaume watano kabla na aliyekuwa naye wakati huo hakuwa mme wake.
Wafuasi wa Yesu walishangaa kumkuta anaongea na mwanamke wa aina hii. Licha ya
kukataliwa na wasamaria ni kama alikuwa amekataliwa na wafuasi wa Yesu. Kisa
hiki kinatupa mafundisho yafuatayo.
Saa ambayo haumtafuti Yesu. Yeye anakutafuta. “Nilikubali
wanikaribie watu wasioniuliza kitu, wanipate wale wasionitafuta” (Isaya 65:1). Yesu
alimtafuta mwanamke huyu kumpa habari njema ya wakovu. Ni kama mchungaji mwema
anayeacha kondoo tisini na tisa na kwenda kumtafuta kondoo aliyepotea. Yesu
alimpata Zacchaeus na sio Zacchaeus aliyempata Yesu. Yesu alimtafuta Saulo
(Paulo). Sio Paulo aliyemtafuta Yesu. Wakati tunapomtafuta Mungu naye
anatutafuta.
Katika ubaya wako kuna uzuri. Mwanamke huyu Msamaria aliacha mtungi
wake na kwenda kuwaita watu wamuone Yesu. Wamuone yule aliyemwambia aliyotenda.
Wamuone Masiya. Mkwepaji watu anakuwa mtangazaji na habari njema. Kuna hadithi
juu ya mitungi miwili ya kutekea maji. Muuza maji alikuwa anabeba mitungi hiyo
miwili. Mmoja ulikuwa mtungi usio na ufa. Mtungi wa pili ulikuwa na nyufa tatu.
Kila mara maji katika mtungi wenye nyufa yalimwagika. Mchota maji alilipwa pesa
kidogo sababu hiyo. Mtungi wenye nyufa kila mara ulisononeka na kuwa na huzuni
ukimwambia mteka maji kuwa unamfanya kupata kiasi kidogo cha fedha unamwaga
maji njiani. Mteka maji aliuwaambia mtungi. Usijidharau. Sijakukataa. Tazama
nyuma kila unapomwaga maji, unamwagilia maua ya bwana wangu na yanafanya sehemu
hii ipendeze. Katika ubaya wa mtungi huu palikuwepo na uzuri. Yesu aligundua
nyufa kwenye moyo, dhamira ya mwanamke Msamaria kisiwani.
Ukibadilika Mungu anakurudishia heshima ya kusikilizwa. Kadiri
Bwana Yesu alivyongea na mwanamke mwanamke huyo alibadilika katika kumtabua
Yesu ni nani. Kwanza alimuita wewe, baadaye Myahudi, baadaye Bwana au Sir,
baadaye nabii na hatimaye Masiya. Kubadilika huku kunaakisi na kubadilika
kimtazamo. Mwanamke huyo alipokimbia kutoa habari kwa watu aliowakwepa
tunaambiwa: “Katika mji ule Wasamaria wengi walimsadiki kwa sababu ya neno la
mwanamke yule aliyeshuhudia” (Yohane 4:39). Wasamaria walianza kuamini neno la
mwanamke huyo. Kama unasimama kuongea watu wanasema wewe kaa chini au msimpe
kipaza sauti. Heshima yako Mungu anaweza kuirudisha. Jambo la msingi ni
kubadilika na kuacha ubaya.
Kukataliwa ni changamoto. “Watu wema wanapokufikiria kuwa wewe ni
mtu mbaya, unakuwa na moyo wa kusaidia watu wabaya. Unawaelewa,” alisema Criss
Jami. Usijidharau kwa vile watu wengine wamekudharau. Wewe sio bidhaa mbovu.
Wewe si takataka. Wewe ni mpakwa mafuta kwa vile ulibatizwa. Inashangaza buibui
anavyotengeneza utando wa kukamata wadudu lakini yeye hakamatwi. Inasemekana
mwili wake unatoa mafuta ambayo hutiririka miguuni na kulainisha anapopita.
Yeyote aliyebatizwa ana upako wa Roho Mtakatifu, ule uwezo wa kukwepa maovu.
Lakini shida hatutumii uwezo huo. Ni kama stima au umeme. Watu wengi wanatumia
stima au umeme kuona tu. Lakini unaweza kutumiwa kunyoshea nguo, kupikia,
viwandani, kwenye runinga, simu, video kutaja matumizi machache.
Haujakataliwa. Mungu anakujua kwa jina. “Nitafanya na hilo neno
uliloniomba, kwa maana umepata upendeleo wangu, na kwamba nakujua kwa jina
lako” (Kutoka 33:17). Mungu anakupenda kama kwamba ni wewe peke yake duniani.
Ukikataliwa kumbuka wewe si wa kwanza kukataliwa. Yesu alikataliwa na watu wa
kijijini kwake. “Hakuna nabii mwenye kukubaliwa mjini mwake” (Luka 4:24).
ULICHOPATA KWA IMANI KITAPOTEA UKIKUFURU: Kutajwa kwa shamba na
kisima cha Yakobo (Yn 4: 6) kunafunua ukweli huo. “Njiani alifika mji wa
Samaria uitwao Sikari, karibu na Shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yozefu.
Pale palikuwa na kisima cha Yakobo.” (Yn 4: 5-6). Kisima cha Yakobo kilikuwa
karibu na Mlima Gerizimu. Yohana anataja mahali hapo penye Kisima, “kukumbusha
mababu walichopata kwa imani kwa Mungu, wayahudi walikipoteza kwa kukufuru
kwao,” alisema Baba wa Kanisa Theophyl. Ukiomba kupata kazi usikufuru. KAZI NI
MBAYA UKIWA NAYO.