“Kila tendo la Neno aliyetwaa
mwili ni fundisho kwetu,” alisema Mt. Augostino. Alhamisi Kuu ya Kwanza Yesu
alifanya matendo saba katika kuwaosha miguu mitume wake. Matendo saba hayo ni
somo la kujifunza. Bwana Yesu na mitume wake walikuwa katika chumba cha Karamu
ya mwisho kinachoitwa Cenaculum. Hiki
kilikuwa ni chumba cha kulia chakula cha jioni (cena) kilichokuwa orofani katika nyumba. Kwa kawaida matendo makuu
yanayokumbukwa Siku ya Alhamisi Kuu ni kuwekwa Sakramenti ya Ekaristi, Daraja
Takatifu na amri ya Bwana ya Mapendo ya kidugu. Lakini kuna utajiri mwingine
uliojificha katika matendo saba ya kuwaosha miguu mitume kama tunavyosoma
katika Injili ya Yohane: “…aliinuka kutoka mezani, akaweka kanzu yake kando, akatwaa kitambaa cha kitani,
akajizungushia kiuononi. Kisha akatia maji katika chombo, akaanza kuiosha miguu
ya wafuasi na kuifuta kwa kitambaa alichojizungushia” (Yohane 13: 3-5).
ALIINUKA KUTOKA MEZANI
Mazuri huachwa kwa ajili ya
mazuri zaidi. Ni fundisho la kwanza tunalolipata katika tendo la kwanza la Yesu
Alhamisi Kuu ya Kwanza. Bwana Yesu na wafuasi wake walikuwa hawajamaliza mlo wa
jioni. Aliacha mazuri mezani. Fundisho alilotaka kulitoa lilikuwa zuri zaidi.
Fundisho kuhusu ukuu wa huduma. Ilikuwa ni fursa nyingine ya kumtafakarisha
Yuda Iskarioti ajue kuwa tunda la huduma ni amani na pia hasilipe wema kwa
ubaya. Lakini yote kwa Yuda Iskarioti ilikuwa kama kupiga ngoma ikiwa
imezamishwa majini. Ukweli unabaki kuwa mazuri yanaachwa kwa ajili ya mazuri
zaidi. Kama unaweza kumsaidia mtu muda wa kupumzika baada ya chakula sio muhimu
kiasi cha kutotoa huduma muhimu kwa wenye shida. John Wesley alisema: “Fanya
mazuri yote kadiri uwezevyo, kwa vitendea kazi vyote uwezavyo, kwa njia zote
uwezavyo, mahali pote uwezavyo, kwa watu wote uwezavyo, kwa kiasi uwezacho.” Mazuri
huachwa kwa ajili ya mazuri zaidi. Kuna methali ya Tanzania isemayo: Jambo
linalomfanya mwanamwali alie huwa halipo kwa mme wake bali nyumbani anakotoka.
Inabidi kuwaacha wazazi na kuambatana na mme wake. Anaacha mazuri kwa ajili ya
mazuri zaidi. Anawaacha wazazi ili naye awe mzazi awe na familia yake.
Pili kuinuka kwa Yesu toka mezani
ni muhitasari wa umwilisho wake. Alitoka
mbinguni na kuacha mazuri ambayo sikio halijawahi kusikia. Aliacha mazuri
ambayo jicho halijawahi kuona. Neno alitwaa mwili. Tunaalikwa tuinuke. Maneno
yetu yageuke kuwa matendo. Yachukue mwili. Yasibaki maneno tu.
Tatu kadiri ya rejeo chini ya ukurasa
katika Biblia ya Kiafrika, kuinuka kwa Yesu kutoka mezani ni dokezo la ufufuko. Kuinuka ni
fursa ya kuvuta watu kwake. Alisema: “nitakapoinuliwa nitawavuta watu wengi
kwangu.”
AKAWEKA KANZU YAKE
KANDO
Bwana wetu Yesu Kristu aliweka
kando vazi la utukufu wake. Mtume Paulo anaweka wazi ukweli huu: “Muwe nao moyo
aliokuwa nao Kristo Yesu, ambaye ijapokuwa alikuwa namna ya Mungu, hakuchukulia
kwamba kuwa sawa na Mungun lilikuwa jambo la kushikamana nalo. Bali alijishusha
mwenyewe” (Wafilipi 2: 6-7). Kumbuka vazi lake walilipigia kura. Bila shaka
lilikuwa vazi zuri. Lilikuwa vazi la heshima. Aliliweka kando. Aliweka cheo
chake kando. Ni mwaliko wa kuweka cheo kando na utukufu kando ili
kutumikia.Palikuwepo na mwandishi mashuuri wa Kihindi aliyeitwa Suryakant
Thripathi. Jina lake maarufu aliitwa Nirala kwa sababu maandishi yake yote
yalikuwa na jina Nirala. Nirala alipenda sana kucheza na watoto. Siku moja
alikuwa anacheza na watoto mitaani. Watu ambao walikuwa hawajawahi kumuona uso
kwa uso walimtembelea. Walimuuliza Nirala mwenyewe bila kumjua: “Tafadhali
unaweza kutuonesha nyumba ya Nirala. Tumekuja kumtembelea.” Nirala aliwaambia
wangoje atawaonesha nyumba yake baadaye kidogo. Aliendelea kucheza na watoto na
baada ya kumaliza aliwaambia kuwa yeye ndiye Nirala. Wageni walishangaa na
kumuuliza: “Kwa nini ukutwambia mapema tulipokuuliza.” “Wakati huo sikuwa
Nirala mwandishi,bali mcheza na watoto.” Unapocheza na watoto kuwa kama mtoto.
Cheo chako kibadilike kulingana na mazingira. Tunasoma katika Biblia: “Kwa
wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu
wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu (1 Wakorintho 9:22). Kuna wimbo
unasema: “Nimefufuka nab ado ningali pamoja nanyi..”
AKATWAA KITAMBAA CHA KITANI
Alitwaa umbo la mtumishi. Watumwa
na watumishi huko Uyahudi enzi za Yesu walijulikana kama: “Watu
wa Taulo.” Alichukua cheo cha mtumishi. Tendo hilo lilikuwa ni utabiri wa
mateso na kifo chake. “Kabla ya kusulubiwa msalabani alivuliwa nguo Zake, na
alipokufa aliwekwa kwenye nguo ya kitani,” alisema Mtakatifu Augustino. Tunaposhawishiwa
kufikiria juu ya jina letu, shahada zetu, nafasi yetu, haki zetu, ubora wetu,
hadhi yetu, ukuu wetu, mafanikio yetu, sifa zetu, fahari yetu, uwezo wetu
tupige picha ya Bwana Yesu anachukua taulo. Katika taasisi na mashirika
matatizo yanaweza kujitokeza kwa vile mtu fulani hakupewa nafasi yake. Watu
wakubwa ukubwa wao unaweza kutotambuliwa vizuri. Lakini kuna ukubwa wa aina
moja, ukubwa wa utumishi. Papa anaitwa “Mtumishi wa Watumishi.” Usijiulize
watumishi wangapi wanakutumikia bali jiulize watumishi wangapi wanakutumukia.
Ibn Batuta, Mwanafalsafa na mfanyabiashara wa Afrka Magharibi alisema: “Tukifa
msitutafute katika makuburi yaliyopakwa chokaa na marumaru, bali mtutafute
katika mioyo ya watu tuliowatumikia.”
AKAJIZUNGISHIA
KIUNONI
Bwana Yesu Kristo aliuzungushia
Umungu wake taulo ya ubinadamu aliouchukua toka kwa Bikira Maria. Kuzungusha taulo kiunoni kunadokeza utayari
na wepesi wa kufanya kazi. Kumbuka bahati huwaendea walio tayari. Giuseppe
Garibaldi alisema: “Nipe mkono ulio tayari
badala ya ulimi ulio tayari.” Yesu hakuwa tayari kwa maneno alikuwa tayari kwa
matendo. Matendo yana kauli kuliko maneno. “Safari ya kwenda mbinguni ni kazi
ngumu ambayo kila mmoja hana budi kujifunga mkanda ili aitekeleze, kwani
kinyume na hapo ipo hatari ya kuishia mlangoni tu,” alisema Samweli Waiti
Ndugwa. Jifunge mkanda utumikie.
KISHA AKATIA MAJI KATIKA CHOMBO
“Kanisa lina maji na machozi,
maji ya ubatizo na machozi ya kutubu,” alisema Mtakatifu Ambrose. Maji ni
kimiminiko. Kutia maji chomboni kutukumbushe vimiminiko viwili: maji yatakasayo
na machozi ya toba. Kadiri duniani panavyokuwepo na dhambi ndivyo tunavyohitaji
kufanya toba. Mapdre ni vyombo vya kutakasa watu katika Sakramenti ya
Upatanisho. Machozi ya toba yana nguvu: “Machozi kama ya Daudi huzima hata moto
wa Jehanumu,” alisema Mtakatifu Chrysostomu. Sikitiko timilifu ni sifa ya toba
ya kweli. “Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote,
na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza” (Yoeli 2: 12). “ Kama ukiwa
mbele ya mahakama ya kibinadamu baada ya hukumu kupitishwa, ukilia na
kuomboleza, kwa kulia kwako hautabadili hukumu kamwe, lakini mbele ya baraza la
kimungu utabadili hukumu kama kutoka ndani ya moyo wako utalia kwa ajili ya
kupata huruma,” alisema Mtakatifu Chryosostomu.
AKAANZA KUIOSHA MIGUU YA WAFUASI
Kuna aliyesema kuwa: “Kukaa
majini si kutakata.” Yesu alipoosha miguu ya wafuasi wake si wote walitakatata.
Nanyi mmekuwa safi lakini si nyote. Ni maneno ya Yesu. Yuda Iskarioti hakuwa
safi. Alikuwa na mpango wa kumsaliti Yesu. Kukaa majini si kutakata. Samaki
anakaa majini lakini ngozi yake si safi. Samaki anakaa majini lakini lazima
kumuosha kabla ya kumla. Tunalazimika kutumia Sakramenti ya Upatanisho ili
tupate neema ya utakaso. Kusali sala kunatupa neema ya msaada si neema ya
utakaso. Tunahitaji neema hizo zote. Kuna methali ya Kidachi isemayo: “Rafiki
akimuosha rafiki yake wote hutakata.” Ni vizuri marafiki wakasahishashana. “Kila
mtu anapaswa kutunza kaburi la usawa wa kadiri ambalo ndanimo atazika makosa ya
marafi wake. Tukumbuke kuwa: “Urafiki ni kama pesa, rahisi kuzipata kuliko
kuzitunza,” alisema Samuel Butler. Yuda Iskarioti hakutunza urafiki wake na
Yesu. Alimsaliti Yesu. Kutenda dhambi ni kumsaliti Yesu kwa vipande thelathini
vya fedha. Wanandoa hawana budi
kusahihishana. Kuna methali ya Tanzania isemayo: “Viganja viwili ni kwa ajili
ya kuoshana.”
NA KUIFUTA KWA KITAMBAA ALICHOJIZUNGUSHIA
Yesu alitumia raslimali zake za kibinadamu
kuwahudumia wengine. Tutumie raslimali tulizonazo kuwatumikia wengine. “Upendo
una mikono kuwasaidia wengine. Upendo una miguu kuharakisha kuwasaidia masikini
na wahitaji. Upendo una macho kuona mahangaiko na shida za wengine. Upendo una
masikio kusikiliza kilio na sauti za huzuni za watu. Namna hiyo ndivyo upendo
ulivyo,” alisema Mt. Augustino wa Hippo.
Huduma ni gharama ya ufuasi. Tulipe huduma hiyo. Upendo ni
gharama ya ufuasi tulipe gharama hiyo. Yesu ametupa mfano wa unyenyekevu, mfano
wa upendo, mfano wa huduma, mfano wa undugu na mfano wa utume.