Jumapili ya 22 ya Mwaka B
1. Kumb 4: 1-2, 6-8
|
2. Yakobo 1: 17-18, 22, 27
|
3. Mk 7: 1-8, 14-15, 21-23
|
“…Kwa maana kutoka ndani ya watu, kutoka mioyo yao, yanatoka mawazo
mabaya; uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu,
matusi, kiburi, upumbavu.Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi”
(Marko 7: 15-23)
Mungu anapompima mtu, anaweka
utepe kuzunguka moyo wake na si kichwa chake. Mwalimu wa shule ya wanafunzi
wadogo wa elimu dini waliokuwa wakikutana Jumapili alikuwa akiwaambia watoto
wadogo juu ya taji la utukufu na zawadi huko mbinguni kwa watu wema. Mwishoni
mwa somo aliwauliza wanafunzi wa shule ya awali, “Nani atapata taji kubwa?”
Palikuwepo na kimya, mtoto mmoja akainua mkono, “Mwenye kichwa kikubwa.”
Tofauti na jibu hili Mungu haangalii ukubwa wa kichwa bali ukubwa wa moyo: moyo
wenye upendo, ukarimu, mawazo safi, unyenyekevu. “Kila mtu anaweza kupenda ua la waridi; lakini
inahitaji moyo mkubwa kupenda jani,” alisema Askofu Fulton Sheen. Kila mtu
anaweza kupenda chumvi lakini inahitaji moyo mkubwa kumpenda muuza chumvi. Kila
mtu anaweza kupenda kinywaji kilichomo kwenye glasi, lakini inahitaji moyo
mkubwa kuipenda glasi. Kila mtu anaweza kuchukia dhambi lakini inahitaji moyo
mkubwa kumpenda mdhambi.
Kama hakuna adui ndani, adui wa
nje hawawezi kukudhuru. Ni methali ya Kiafrika. Mawazo mabaya ni adui wa ndani.
Wakiwemo moyoni adui wa nje anaweza kukudhuru. Yesu alitaja maadui kumi na
wawili ambao wanaweza kuwa moyoni: “…Kwa
maana kutoka ndani ya watu, kutoka mioyo yao, yanatoka mawazo mabaya;
uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, choyo, ukorofi, hila, ufisadi, wivu, matusi,
kiburi, upumbavu.Maovu hayo yote yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi” (Marko
7: 15-23)
Mungu anatazama moyo na kuangalia
moyoni. Tunapoimba Mungu hatazami midomo tu anatazama moyo. Tunapoimba Mungu
hatazami kinanda tu anatazama moyo. Unapotoa sadaka Mungu hatazami pesa tu
uliyotoa anatazama moyo. Kutoa ni moyo vidole huachia. Tunapomwabudu Mungu,
Mungu anatazama moyo. Mtu anaposema nakupenda kwa moyo wote, hoja si kupenda
kwa moyo wote hoja ni aina gani ya moyo. Watu wanapenda moyo unaojali. Watu
hawajali unajua kiasi gani mpaka wanapojua unajali kiasi gani. Mioyo yetu ni
kama sanduku tunatofautiana namna ya kujaza sanduku. Swali: moyoni umejaza
nini? Wengine wanaweka mengi kwenye sanduku kama wanavyoweka mengi moyoni.
Wengine wanaweka machache. Mwenyezi Mungu anaangalia moyoni:”…siangalii mambo
kama wanavyoangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje,
lakini mimi naangalia moyoni” ( 1 Samueli 16: 7). Tunapozungumza maneno ni
maelezo ya wazo. Kila mara unapoongea unachokifikiria na kinachokuwa moyoni
kinakuwa kwenye gwaride watu wanaona.
Maneno yako ni madirisha ya moyo
wako. Lililo moyoni ulimi huiba. “Kinywa
hutaja yanayofurika moyoni” (Mathayo 12: 34). Ukisema, “asante” shukrani
imefurika moyoni. Ukisema, “nakupenda” upendo umefurika moyoni. “Mtu mwema
hutoa mema katika hazina njema ya moyo wake, na mtu mwovu hutoa maovu katika
hazina mbovu ya moyo wake; kwa maana kutoka kinywa chake hunena yafurikayo
moyoni” (Luka 6: 45).
Barua kutoka moyoni inawezwa
kusomwa usoni. Ni methali ya Kiswahili. Uso wa mtu unaonesha kilichomo moyoni.
Katika lugha ya kawaida tunatambua umuhimu wa moyo. Kuna mifano michache: Ana
moyo mwepesi: ana huruma nyingi na mwepesi wa kumsamehe mtu aliyemkosea. Fulani
ana moyo wa simba: ni shujaa; mjasiri mkubwa; haogopi kufanya jambo. Kipendacho
moyo ni dawa (methali). Ana moyo mweupe: hana hila au nia mbaya. Suala la
kupatana ni suala la moyo: “Moyo wa binadamu umeumba kupatanisha
yanayokinzana,” alisema David Hume. Naye Harbert Hoover alikuwa na mawazo hayo
aliposema: “Amani haifikiwi kwenye meza ya baraza au kwa mikataba, bali kwenye
mioyo ya watu.” Ni moyo unaopenda. “Moyo
wa kupenda hausemeki.” Ni methali ya Kiswahili. Jicho halisau moyo ulichoona. Ni methali ya Kiafrika. Yote yakishasemwa
wito ni moyoni jazeni mawazo mazuri.
MAWAZO YA UKARIMU, SADAKA NA HISANI: Moyo wa binadamu haupimwi kwa
ukubwa wa pochi bali kwa ukubwa wa moyo wenyewe. Tunazungumzia moyo
usiofungwa, ulio wazi. “Gereza baya sana litakuwa moyo uliofungwa,” alisema Mt.
Yohane Paulo II. Moyo uliojaa uchoyo ni
moyo uliofungwa. Kilijochaa hufurika. Moyo ukijaa ukarimu, ukarimu utafurika.
Moyo ukijaa mawazo ya sadaka, sadaka itafurika. Moyo ukijaa mawazo ya hisani,
hisani itafurika. “Kuna tofauti kubwa sana kati ya zawadi na sadaka. Sadaka ni
zawadi kujumlisha na upendo na kujumlisha na hulka ya mtoaji. Zawadi hutoka
kwenye pochi; sadaka hutoka moyoni,” alisema Askofu Fulton Sheen. Kuna mtoto wa
mitaani aliyekutana na Padre akamuuliza, “Padre gari lako ulinunua kwa shilingi
ngapi?” Padre alijibu, “Sijui.” Mtoto akasema, “Unaendesha gari haujui bei
yake.” Padre alimwelewesha mtoto, “Gari hili nilipewa na kaka yangu.” Mtoto
alisema, “Ningekuwa na moyo kama kaka yako ningekununulia gari.” Hakusema,
“Ningekuwa na ndugu kama huyo akaninunulia gari.” Mambo yote yanategemea
moyo.Mtoto huyu wa mitaani alikuwa na moyo wa ukarimu. Kuna mtu aliyeenda kwa
tajiri kuomba elfu tatu. Tajiri akampa elfu hamsini. Yule aliyeomba elfu tatu
akashangaa na kusema, “Bwana Mkubwa, Chifu, Bosi! Mimi nimeomba elfu tatu wewe
mbona umenipa hamsini.” Bwana huyo akasema, “Elfu tatu zinakutosha wewe kuomba
lakini hazinitoshi mimi kutoa.”
MAWAZO SAFI, NIA SAFI, NDOTO SAFI
Hakimu wakati anahukumu kesi juu
ya wizi. Alimuuliza mwizi: Je huwa hauoni aibu kuweka mkono kwenye mfuko wa mtu
ili umwibie. Mwizi huyo alijibu: “Huwa nakuwa na aibu nisipokuta kitu chchote.”
Moyoni mwa mwizi huyo yalijaa mawazo mabaya, mawazo ya wizi. Hayo si mawazo
safi. Familia moja ilikuwa na mazoea ya kuwakaribisha wageni wakati wa
Kumbukumbu za Kuzaliwa za Wanafamilia. Baba alimuomba mtoto wake wa miaka
mitatu kuongoza sala kabla ya kula. Mtoto alisita. Baba alisema sema ambavyo
mama huwa anasema siku kama hii: Mtoto alifanya ishara ya msalaba na kusema,
“Mama huwa anasema, “Kwa nini tumewaalika watu wengi chakula hakitoshi.”
Unaweza kujua mawazo ya mama huyo. Wazo lolote ambalo linaleta mwanga
lifikirie. Wazo lolote ambalo ni wazo taka achana nalo. Wazo lolote ambalo ni
wazo mgando achana nalo. Wazo lolote ambalo ni wazo giza achana nalo. “Ndugu,
yaliyo kweli, matukufu, adili, yaliyo matakatifu, ya kupendeza nay a sifa
njema, yote yanayohusiana na ukamilifu, tena masifu, hayo yafikirieni hasa”
(Wafilipi 4:8). Mawazo ya upendo ni mawazo safi. “Palipo na upendo, hakuna giza
(Methali ya Burundi). Mawazo ya kusaidia wengine ni mawazo safi. “Lengo letu la
kwanza katika maisha haya ni kuwasaidia wengine. Kama huwezi kuwasaidia wengine
usiwahumize,” alisema Dalailama.
“Heri walio na moyo safi, maana hao watamowona Mungu” (Mathayo 5:
8).“Tunateka nyara kila fikra ipate kushuka na kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:5).
“Ni nani atakayependa katika mlima wa Bwana?” Ni nani atakayesimama katika
patakatifu pake? Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, asiyeiinua nafsi yake
kwa ubatili, wala hakuapa kwa hila” (Zaburi 24 (23): 3-4).
MAWAZO YA UNYOFU, UAMINIFU NA UADILIFU
Kuna watu ambao hawawezi kusoma Biblia lakini wanaweza kusoma moyo
wako. Kinachompendeza Mungu ni unyofu wa moyo. “Nawe wapendezwa na unyofu
wa moyo; ndani ya moyo unanifundisha hekima” (Zaburi 51: 8). Mungu haangalii
kwamba mtu amekujaribu na sketi fupi bali anaangali unyofu wako wa moyo. Mungu
haangalii kwamba mtu aliacha pesa mezani zikakushawishi Mungu anaangalia unyofu
wa moyo.
MAWAZO YA UCHESHI, UCHANGAMFU, FURAHA
“Moyo wenye furaha ni huduma
nzuri sana tunayoweza kumpa Mungu,” alisema Marie Chaplain. “Moyo wenye furaha
ni matokeo yasiyoepukika ya moyo unaowaka upendo,” alisema Mwenyeheri Mama
Teresa wa Calcutta. Moyo unapodunda kwa ajili yaw engine unakuwa na furaha
sana.
MASIFU, PONGEZI, SHUKRANI, MAPENDO
“Ujaze moyo wako wingi wa mapendo
na shukrani, unapowaza jinsi kila siku neema ya Mungu inavyokuokoa katika
mitego unayotegewa njiani na adui,” alisema Mt. Josemaria Escriva. Kipimo cha
mtu sio ukubwa wa imani yake bali ukubwa wa upendo wake. Msichana mmoja alikuwa
amempenda kijana mmoja mtanashati na mchaMungu. Malengo yao ilikuwa waje kuoana
baada ya muda. Kijana alijitoa sana kwa binti huyu hadi wenzake wakamuona
mjinga, lakini ukweli ni kuwa alimpenda msichana Yule kwa dhati. Alimtafutia
kazi alipomaliza chuo, alimshauri kuhusu mipango ya maisha na alikua akimuombea
kila alipopata nafasi ya kuomba. Siku moja binti alikua anasherehekea siku yake
ya kuzaliwa…hivyo akaalika marafiki zake, na watu wengine muhimu akiwemo mpenzi
wake. Wageni wote walifika kwa wakati isipokuwa yule kijana alichelewa
kidogo…Hivyo msichana akatumia muda ule ambao mpenzi wake hajafika kuwaeleza
wageni namna yule kijana alivyokuwa wa muhimu kwake. Akamsifia sana, akasema
atamvalisha pete ya uchumba karibuni, na akasema siku hiyo ya Siku ya Kuzaliwa
kwake anategemea zawadi kubwa sana kutoka kwa huyo mpenzi wa nafsi yake.
Baadaye kijana akaingia na kuketi kwenye meza ya wageni wahemishimiwa. Muda wa
zawadi ulipofika watu wakamtunza binti zawadi mbalimbali na kijana akawa wa
mwisho. Hivyo wageni wote wakawa na hamu ya kutaka kujua zawadi aliyoleta hasa
baada ya Yule msichana kumsifia sana kijana akaamka na kutoa mfuko…kila mtu
akataka kujua kilichokua ndani ya mfuko…mara kijana akafungua mfuko na kutoa
mkate! Lahula! Watu wote wakastaajabu na kusema, “Mkate?” Lakini kabla hajasema
lolote kuhusu ule mkate, Yule msichana akaanza kulia..akapandwa hasira kwa kuwa
mpenzi wake amemuaibisha! Akiwa analia kwa kwikwi, akamshika shati na kumvua
tai yake, akamwagia juisi, kasha akauchukua ule mkate na kuutupa! Maskini Yule
kijana akaukimbilia ule mkate na kuuokota. Kisha akarudi mezani na kusema,
“Mtoto nakushukuru kwa yote..Huenda umenidharau kwa kuwa nimekuletea
zawadi hii ndogo kwenye siku yako muhimu
kama hii. Lakini kama ungetambua thamani ya zawadi hii, usingefanya haya.”
Kisha akafungua ule mkate na kutoa vitu viwili alivyovificha ndani ya
mkate…Kwanza akatoa ufunguo wa gari, ambalo alikuwa amemnunulia mpenzi wake na
alitaka amkabidhi siku hiyo ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa. Kisha akatoa pete ya
uchumba na kusema “Nilimuomba Mungu anipe mwanamke atakayenipenda katika hali
yoyote. Nilipanga leo nikuvalishe pete hii ili kuelekea ndoto yetu ya ndoa.
Lakini kwa kuwa uliangalia nje, uliona mkate, badala ya pete hii ya thamani
iliyokuwa ndani.Naamini mwanamke niliyemuomba kwa Mungu bado sijampata.
Nashukuru kwa yote uliyonifanyia nimekusamehe, nawe naomba unisamehe kama
nimekukwaza.” Kisha akachukua mkate wake, huyoo akaondoka. Msichana akaomba
msamaha lakini alikuwa amechelewa. Fundisho usidharau kila mtu kwa kumtazama
kwa nje. Mungu huangalia thamani ya kitu au mtu kwa ndani lakini wanadamu walio
wengi huangalia nje. Wanaokudharau leo na kukuona mkate watagundua haukuwa
mkate wa kawaida, kuna vingi vya thamani ndani mwako. Wote wanaokudharau leo,
ipo siku watakusalimia kwa heshima.
Ujaze moyo wako masifu. Msichana
huyo hakujaza moyo wake na masifu. “Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo, Mshukuruni Bwana kwa kinubi, kwa
kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Mwimbieni wimbo mpya, pigeni kwa ustadi
kwa sauti ya shangwe” (Zaburi 33(32) 1: 1-3).
TUMUOMBE MUNGU ATUUMBIE MIOYO SAFI
Kuna mtu alikuwa anaulizia bei ya
taulo. Mnunuzi: “ Taulo hiyo pale shilingi ngapi? Muuzaji: Laki mbili. Mnunuzi:
Inasafisha hata dhambi! Muuzaji: kimya. Mnunuzi alishangaa bei ilikuwa juu.
Taulo inaondoa maji haiondoi dhambi, inasafisha uchafu haisafishi makosa.
Biblia inazungumzia hisopo inayosafisha. “Unisafishe kwa hisopo, nami nitakuwa
safi; unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji” (Zaburi 51: 9). Hisopo ni
mmea mdogo wenye vitawi vingi unaofaa kwa kunyunyuzia katika madhehebu ya
kutakasa (Hesabu 19:18; Law 14;4; Rev 1: 9). Wahaya walikuwa na mimea ya
kutumia kutakasa katika ibada za kitamaduni: orweza na orugoshora. Ni kama mmea
wa hisopo. Sala yetu iwe kama ya mfalme Daudi alipotembelewa na nabii Nathani
baada ya kutenda dhambi na Bathsheba: “Uniumbie
moyo safi, ee Mungu; ufanye upya roho thabiti ndani yangu” (Zaburi 51: 12).