SHEREHE YA KUPALIZWA BIKIRA
MARIA MBINGUNI
1. 1 Mambo ya Nyakati 15: 3-4, 15-16, 16: 1-2
|
2. 1 Kor 15: 54-57
|
3. Lk 11: 27-28
|
Leo tunasherehekea
Sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria mbinguni. Alipalizwa hakupaa mbinguni. Ni
Yesu alipaa mbinguni. Ukweli kuwa Bikira Maria alipazalizwa Mbinguni tunaupata
katika Biblia kitabu cha Ufunuo, “Ishara kubwa ilionekana mbinguni, mwanamke
amevikwa jua, mwezi ukiwa chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili
juu ya kichwa chake” (Ufunuo 12:1).
“Maria ameingia utukufu wa mbinguni,
ameshirikishwa utukufu wa Mwanawe….Katika Maisha yake Maria alimfuata Mwanawe
bila kumwacha hata alipokuwa msalabani. Sasa tunaona Mwana hamwachi mama yake,
bali anamshirikisha utukufu wake” (MISALE YA WAUMINI, uk.871). Mwaliko leo ni
kuwa mbingu ianzie duniani. Ni kama tunasema,
“Njia yote ya kwenda mbinguni ni mbinguni” (Canon Farrar). Chunga mawazo
yako yanageuka kuwa maneno. Chunga maneno yako yanageuka kuwa matendo. Chunga
matendo yako yanakuwa kuwa tabia. Chunga tabia yako inageuka desturi. Chunga
desturi inageuka kuwa hatima yako.
“Nikichukua hatua ya kwanza nikiwa na wazo zuri, ya pili nikiwa na neno
zuri, na ya tatu nikiwa na tendo zuri, niliingia mbinguni,” alisema Zoroaster.
Hata kama mbingu
hauioni Mbingu ipo. Hauwezi kusema kwa vile Mungu simuoni Mungu hayupo. Kuna
Profesa ambaye hakuamini kuwa Mungu yupo. Akiwa anawafundisha wanafunzi
alimwambia mwanafunzi mmoja, “Ebu chungulia dirishani kama utamuona Mungu.
Unaona nini?” Mwanafunzi akasema, “Naona miti nje. Naona majani. Naona watu.
Naona magari.” Profesa kwa kujitapa akasema, “Nemekuambia Mungu hayupo.”
Mwanafunzi mmoja akasema, “Profesa, ngoja mimi nimuhoji mwanafunzi mwenzangu.”
Akaanza kumuhoji, “Unamuona Profesa?” Mwanafunzi mwenzako akasema,
“Namuona.” Anayehoji akazidi kuhoji,
“Unaona mambo gani ya Profesa?” Mwanafunzi akajibu, “Naona shati, naona macho
naona kichwa, naona viatu, naona mikono.” Mwanafunzi akaulizwa, “Je unaona
akili yake.” Akajibu, “Sioni akili yake.” Mwanafunzi anayehoji akasema, “Hivyo
profesa wetu hana akili kwa vile hauioni.” Katika mtazamo huo, hauwezi kusema
kuwa hakuna mbingu kwa vile hauioni.
Papa Pius XII katika
barua yake ya kipapa Munificentissimus Deus aliandika hivi:
“Mwishowe Bikira Maria asiye na doa, aliyekingwa na kila doa la dhambi ya
asili, akishamaliza mwendo wa maisha yake duniani, aliinuliwa katika utukufu wa
mbingu pamoja na mwili wake na pamoja na roho yake. Na alitukuzwa na Bwana kama
Malkia wa ulimwengu, kwa sababu alikuwa amefanana sana na mwanawe, Bwana wa
mabwana, na mshindi wa dhambi na mauti” (KKK Na. 966, LG 59).
SABABU
ZA KUPALIZWA BIKIRA MARIA
1.
MUUNGANIKO
NA MWANAWE
Mama
na mwanawe, mwana na mama yake. “Bikira mwenye heri alitangulia katika safari
yake ya imani akihifadhi kwa uaminifu muungano wake pamoja na Mwanawe mpaka
msalabani, ambapo, kwa mpango wa Mungu
alisimama imara; aliteswa kikatili pamoja na Mwanawe wa pekee, na
alijiunganisha kwa moyo wake wa kimama na sadaka yake. Alikubali kwa mapendo
kuchinjwa kwa sadaka aliyoizaa mwenyewe. Mwishowe, alitolewa na Kristo mwenyewe
akifa msalabani, kama Mama yake kwa mfuasi kwa maneno haya: “Mama, tazama
Mwanao.” (LG 58; KKK Na 964; Yoh 19:
26-27). Bikira Maria alipomchukua mimba Yesu aliunganika naye. Ilikuwa ni
komunio yake ya kwanza. Akaenda kwa haraka kwenda kuunganika na Elizabeti.
Unapounganika na Yesu nenda kwa haraka kuunganika na wengine.
2.
MFUASI
WA KWANZA MATUNDA YA KWANZA YA UFUASI
Tunda la kwanza la kuwa mfuasi wa Yesu ni kushiriki
maisha ya furaha mbinguni. Bikira Maria ni mfuasi wa kwanza wa Yesu. Hivyo
alipata matunda ya kwanza ya kuwa mfuasi wa Yesu. Katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki tunasoma
hivi: “Kupalizwa kwa Bikira Maria Mtakatifu ni kushiriki kwa namna ya pekee
ufufuko wa Mwanawe, na ni utangulizi wa ufufuko wa wakristo wengine” (KKK Na
966). Tunasoma katika Injili ya Luka: “Alipokuwa anasema hayo, mwanamke
miongoni mwa watu alipaza sauti, akamwambia, “Heri tumbo lililokuchukua na
maziwa uliyoyanyonya.” Naye akajibu, “Wenye heri hasa wasikiao neno la Mungu na
kulishika” Luka 11: 27-28). Kwa Yesu wenye heri ni wale wasikiao neno la
Mungu-yaani wafuasi. Kuwa mfuasi maana yake kusikia, kuishi na kuliweka katika
vitendo neno la Mungu (Mt 12: 49-50). Wafuasi wa Kristu ni wake Yesu. Wa kwanza
kuwa wake Yesu ni Bikira Maria na hivyo kupalizwa akiwa wa kwanza kama
tunavyosoma katika somo la pili: “Kama
wote hufa katika Adamu, vile wote watapata tena uzima katika Kristo. Lakini
kila mmoja kwa zamu yake; wa kwanza ni Kristo; baadaye walio wa Kristo…” (1 Kor
15: 23).
MAMBO
YA KUFANYA ILI MBINGU IANZIE DUNIANI
Kwa kawaida mambo
huanzia mbali. Kuna methali ya Wahaya isemayo, “Atakayekula chakula kweli
unamugundua wakati wa kunawa mikono.” Namna ya kula inaazia mbali. Ndoa
haianzii wakati wa kufunga ndoa. Ndoa inaanzia mbali. Kila Nyumba ni shule ya
maisha ya ndoa. Mtoto wa kiume anajifunza maisha ya ndoa nyumbani. Vilevile
mbingu inaanzia duniani. Maisha ya mbinguni hayanyeshi kama mvua yanaanzia
mbali. Mbingu inaanzia dunia. Yesu aliyepaa kwenda mbinguni amesema, “Mimi nipo
pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:20).
- HUDUMA-TUNDA LA UPENDO NI HUDUMA
Bikira Maria alienda
kwa Elizabeti kuanzisha “Kliniki” ndogo nyumbani kwa Zakaria amhudumie
Elizabeti. Na namna hii Bikira Maria anakuwa mhudumu na muuguzi wa kwanza
katika ustaarabu wa kikristu. Huduma yake ni changamoto kwetu. Katika kutoa huduma hauitajiki moyo wa
“fulani atafanya.” “Tendo lolote la Wema ambalo naweza kumtendea mwanangu,
afadhali nilitende sasa, kwa sababu sitapitia njia hii tena”, alisema Stephen
Grellet. Tenda wema huende zako. Wema hauozi. Tujue kuwa: “Tunda la upendo ni
huduma. Tunda la huduma ni amani” Mama Theresia wa Calcutta.
Siku ya hukumu Yesu
kama Jaji anaweza kusema, Nilikuwa na njaa mlianzisha vikundi na vyama vya
kusaidia waathirika mkajadili njaa yangu. Lakini hamkunipa chakula. Nilikuwa
gerezani mkaenda Kanisani kuniombea na wala hamkunitembelea. Nilikuwa uchi
mkajadili maadili ya kutembea uchi, hamkunipa nguo. Nilikuwa mgonjwa mkapiga magoti
na kumshuru Mungu kwa kuwapa afya njema. Nilikuwa sina nyumba mahali pa kulala,
mkanielezea kuna nyumba ya upendo wa Mungu lakini hamkunijengea nyumba.
Nilikuwa mkiwa na mpweke mkaniacha nijiombee mimi mwenyewe. Mlionekana
watakatatifu na karibu na Mwenyezi Mungu lakini bado nina njaa, niko mpweke na
nina baridi sina nyumba. Ni katika msingi huu tunasema imani lazima itafsiriwe
katika matendo. Imani na matendo havitenganishwi ni kama mate na ulimi.
- HARAKA KATIKA KUTENDA MEMA
Malaika Gabrieli alimjulisha Mama wa Yesu, Maria kuwa Elizabeti, jamaa
yake, amepata mimba ingawa ni mzee na sasa ni mwezi wa sita yeye ambaye watu
walimfahamu kuwa tasa (Lk.1:36). Baada ya kujua hilo, tunaambiwa Maria alifunga safari akaenda kwa haraka.
Hakusitasita, hakuhairisha. Alimthamini Elizabeti. Alienda kwa haraka. Wengine
husema haraka haraka haina baraka . Lakini katika mazingira kama haya: ngoja
ngoja huumiza tumbo. Philimus mtu wa kusitasita alitembea siku moja kupitia
kijijini. Alikutana na omba omba maskini aliyemwomba sadaka. Alitaka kumsaidia
omba omba na kusema, “ndiyo, nitakusaidia baadaye.”Alipita karibu na Kanisa,
alikumbuka kuwa hajasali sala zake. Alijiambia, “nitasali baadaye”.
Alipoendelea na safari alikutana na bibi kikongwe ambaye alimwambia, ‘tafadhali
naomba umpeleke mtoto wangu mgonjwa hospitalini. Niko peke yangu na hakuna mtu
yoyote wa kunisaidia.” “Ndiyo,” Philimus alijibu, “Nitakusaidia, lakini
nitakusaidia baadaye.” Baada ya kuachana na bibi huyo kikongwe alipata ajali ya
kugongwa na gari na kufa papo hapo. Roho yake ikapelekwa bahari ya moto. Wakati
akiungua, alimwomba Malaika, “Tafadhali nipe tone la maji.” “Ndiyo” Malaika
alimwambia, “Nitakupa maji baadaye”. Halafu malaika alimwacha. Alipomwona
malaika mwingine, Philimus alimsihi, “Nitoe kwenye huu moto.” “Ndiyo,” Malaika
alisema kwa haraka, “Nitakutoa baadaye” Halafu
na malaika huyo alimwacha. Aliposihi malaika wengine, Philimus alipata jibu lile lile, “Ndiyo, baadaye…”
Kadiri alivyoendelea kuungua motoni alitambua kuwa Mungu husitasita kwa wale
ambao husitasita.
Kusitasita ni
kuchelewesha mambo. Kuchelewa ni kupoteza muda. Kumbuka muda ni mali. Zaidi ya
hayo kila dakika iendayo kwa Mungu hairudi. Tunasitasita labda kwa vile
tunangojea mambo yawe mazuri. Lakini kumbuka, “Mvua ilikuwa hainyeshi Nuhu alipoanza kujenga safina,” alisema Howard
Ruff.
- WAKIKUSIFU MSIFU MUNGU
Maria mama wa Yesu
aliposifiwa na Elizabeti alimsifu Mungu. Alizabeti alisema hivi, “Umebarikiwa
wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa” (Luka 1:42). Maria
mama wa Yesu alimsifu Mungu. “Moyo wangu wamtukuza Bwana, na roho yangu
imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu” (Luka 1:46-47). Maria mama wa Yesu hakujisifu
na kujisifia. Alimsifu Mungu. Alimhimidi Mungu. Alimtukuza Mungu. Elizabeti ni mfano wa kuigwa watu wa familia
yako wakifanya vizuri, wakibarikiwa wasifu. Katika mambo yanayomuhumiza
mwanamke ni mme wake kuwasifia wanawake wengine mbele yake bila kumsifia yeye
na kwa mwanaume ni hivyo hivyo. Kuna mwanaume aliyemwambia mke wake, haupiki
vizuri kama mama yangu. Naye mke wake alimjibu. “Na wewe hauna pesa kama baba
yangu.”
Wakikusifu una kila
sababu ya kumsifu Mungu kama Maria mama wa Yesu alivyofanya. Kwanza ni Mungu wetu anayetoa. Mungu ndiye
mpaji. Mungu ndiye mgawa mafungu. Maria mama wa Yesu alineemeshwa na Mungu na
aliposifiwa alikuwa amembeba mwokozi mimbani. Pili tunamcha au tunamuogopa.
Waogope wasiomuogopa Mungu. Tatu, kumsifu Mungu ni kuzuri na ni vema kama
asemavyo mtunga Zaburi. “Msifuni BWANA; maana ni vema kumwimbia Mungu wetu,
maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri” (Zaburi 147:1). Nne kusifu ni jambo la lazima na la
kimaumbile. Mara ngapi katika uwanja wa mpira yanatoka bila breki maneno ya
mshangao na ya kusifia kama lo, la-la-la-la mchezo ukichezwa vizuri. Ndivyo
ilivyo katika uwanja wa dini kumsifu Mungu ni jambo la lazima la kimaumbile.
Tano, tunampenda Mungu. Unaweza kusifia bila kupenda lakini hauwezi kupenda
bila kusifia.
- JIBARIKI KWA MANENO
Maria mama wa Yesu
alijisambazia baraka pia. “Vizazi vyote
vitaniita mwenye heri” (Luka 1:48). Alijiambia maneno mazuri katika utenzi
wake. Maneno hayo yaliumuumba anaitwa mama mwenye sifa na mama msaajabivu. Neno
alibariki tu linaumba, linampa mtu sura mpya. Ni kweli alivyosema Edward
Thorndike, “Rangi ufutika, hekalu huharibika, ufalme huanguka, lakini maneno ya
hekima hudumu.” Maneno ya Mama wa Yesu yamedumu. Jibariki kwa maneno. Kuna
msichana aliyekuwa na umri wa kuolewa msichana pekee kwa wazazi wake.
Alijibariki wakati wa kusali. Alisema kuwa hatajiombea yeye mwenyewe atamuombea
mama yake. Sala yake ilikuwa hii. “Ee Mwenyezi Mungu mpe mama yangu mkwe mzuri
wa sura na tabia.” Kwa sala hii msichana huu alijasambazia baraka, yaani kuwa
na mme mzuri wa sura na tabia. Kwa mama yake ni mkwe, kwake ni mme wake. Panda mbegu za maneno mazuri ya kujibariki.
Biblia inatoa wito huo. “Hata aliye dhaifu na aseme: ‘mimi pia ni shujaa”
(Yoeli 3:10). Hata aliye masikini na aseme: Mimi ni tajiri. Hata aliye na akili
za wastani aseme: Mimi nina akili nyingi sana. Hata na aliye na uzuri wa
wastani aseme: Mimi ni mzuri sana. Anayejipenda atajiambia maneno hayo.
- UKIPATA SHUKURU
“Mungu amekupa zawadi
ya sekunde 86,400 siku ya leo, je umetumia sekunde moja kusema, “Mungu
Nakushukuru,” alisema William A. Ward. Ukitaka kupata miujiza shukuru kwa dogo
ulilopata. “Shukuru kwa zawadi ndogo ndipo utaweza kupata zawadi kubwa.”
(Thomas à Kempis).Mkumbuke Mungu. Hakuna haja ya kujidai sana sote ni
“CHAKUPEWA.” “Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na
ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa?” (1 Wakorintho
4:7). Kuna methali isemayo, “Aliyekupa
wewe kiti ndiye aliyenipa mimi kumbi.” Na aliye na kidogo akitumie kupata
kikubwa.
Soma zaburi ya 100,
“Pitieni milango yake ya hekalu lake kwa shukrani, ingieni katika nyua zake kwa
sifa. Mshukuruni na kulisifu jina lake.” (Zaburi 100: 4) Unapopitia mlango wa
kanisa pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa duka la magari pitieni kwa
shukrani. Unapopita mlango wa Supermarket pitieni kwa shukrani. Unapopita
mlango wa benki, pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa Hospitali pitieni
kwa shukrani. Unapopita mlango wa ofisi, pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango
wa duka, pitieni kwa shukrani. Unapopita mlango wa gereji, pitieni kwa
shukrani.Unapoingia kwenye sehemu ya kuegesha magari, ingieni kwa shukrani. Fikiri
na Shukuru. Unapopita kwenye mlango wako nyumba pitieni kwa shukrani.
Unapoelekea kwenye chumba cha kulala, pitieni kwenye mlango kwa shukrani.
Milionea wanaotajwa katika Biblia walikuwa ni watu wa shukrani.
- KUWA MMISIONARI WA UPENDO
Kama upendo wako hauwezi
kupaa kwenda kuwatumikia wengine, una Mbawa ambazo zimevunjika. Upendo huanzia
nyumbani. Umisionari uanzie mahali ulipo, kwenye jumuiya yako. Usikoke moto kwa
mama wa kambo wakati kwa mama yako moto umezimika.
Juu ya Umisionari, Mama
Theresia wa Calcutta alikuwa na haya ya kusema:
“Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda. Huko aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elizabeth. (Lk.1:39-40). Mara Knistu alipoingia katika maisha yake, ona alivyofunga safari na kwenda kwa haraka kumtoa kwa wengine. Na namna gani anafanya hili. Na kwa kutenda tena kama mtumishi mnyenyekevu, akiosha, kusafisha na kupika kwa ajili ya binamu yake mzee. Masista wa Shirika letu wanaitwa Wamisionari wa Upendo (Missionaries of Charity) na kila mara ninasema kuwa Maria yeye mwenyewe alikuwa “mmisionari wa Upendo”. Mmisionari ni mtu anayetumwa kupeleka upendo wa Mungu kwa wengine; na mmisionari wa upendo anafanya hili kupitia matendo ya upendo, kama huduma za kiupendo na za kiunyenyekevu ambazo Maria alitoa kwa Elizabeth.
“Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda. Huko aliingia katika nyumba ya Zakaria, akamsalimu Elizabeth. (Lk.1:39-40). Mara Knistu alipoingia katika maisha yake, ona alivyofunga safari na kwenda kwa haraka kumtoa kwa wengine. Na namna gani anafanya hili. Na kwa kutenda tena kama mtumishi mnyenyekevu, akiosha, kusafisha na kupika kwa ajili ya binamu yake mzee. Masista wa Shirika letu wanaitwa Wamisionari wa Upendo (Missionaries of Charity) na kila mara ninasema kuwa Maria yeye mwenyewe alikuwa “mmisionari wa Upendo”. Mmisionari ni mtu anayetumwa kupeleka upendo wa Mungu kwa wengine; na mmisionari wa upendo anafanya hili kupitia matendo ya upendo, kama huduma za kiupendo na za kiunyenyekevu ambazo Maria alitoa kwa Elizabeth.
HITIMISHO:
Mtaka
cha uvunguni sharti ainame. Kuingia mbinguni hakuna njia ya mkato. Mtu mmoja wa
Ireland ambaye alikuwa amelewa na alikuwa anapenda pombe sana siku moja
aliulizwa na Baba Paroko, “Mwanangu unategemea utaendaje mbinguni?” Mtu huyo
alijibu, “Hilo ni jambo rahisi sana! Nitakapofika kwenye mlango wa mbingu,
nitafungua mlango na kufunga. Nitafungua mlango na kufunga. Nitaendelea kufanya
hivyo mpaka Mtakatifu Petro atakapokasirika na kusema, “Mike! Ingia ndani au
Utoke hapo mlangoni.!’ Hivyo nitaingia mbinguni kwa urahisi. Mtaka cha uvunguni
sharti ainame. Kwenda mbinguni kunahitaji kufanyiwa kazi.