Jumapili ya 6 ya Paska
1. Mdo 10: 25 –
26.34-35.44-48
|
2. 1 Yoh 4: 7-10
|
3. Yn 15: 9 -17
|
Utangulizi
Yesu alisema, “ninyi mu rafiki zangu.” “Urafiki
wa kweli haupaswi kuficha kile unachofikiria” (Mt Jerome). Rafiki ni yule
anayekuonya wewe kama Yesu. Urafiki ni ndoa ya roho. “Hakuna rafiki mwenye upendo mkubwa
zaidi kuliko yule aliye tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”
Nitajie rafiki yako, nami nitakwambia
ulivyo. Huo ni msemo wa wataalamu wa saikolojia. Ndege wa bawa moja huruka
pamoja. Marafiki wengi huwa na kitu kinachowaunganisha kama kupenda aina fulani
ya mchezo kama mchezo wa mpira, mchezo wa ngumi. Pengine huwa wanaunganishwa na
kupenda au kutenda mazuri au kutenda mabaya. Kuwa na marafiki sio hoja au
sababu ya msingi maishani. Hoja je urafiki huo ni wa kujenga au kubumoa maana
na majambazi wana marafiki zao majambazi. Urafiki wa kweli lazima uunganishwe
na matendo mazuri. Mafanikio katika kuwa na marafiki si suala tu la kuwapata marafiki wa kweli ni
suala la wewe kuwa mwandani wa kweli , mwenzi wa kweli, rafiki wa kweli.
Urafiki wa kweli unazo sifa nyingi.
Urafiki wa kweli una sifa ya upendo. Upendo ulio mkubwa na upendo uliokomaa.
Bwana Yesu alibainisha sifa hii aliposema, “Hakuna rafiki mwenye upendo mkubwa
zaidi kuliko yule aliye tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”
(Yohane 15:13). Yeye aliwaita binadamu rafiki zake na akawa tayari kutoa uhai
wake kwa ajili ya watu, akawaonyesha namna ya kuishi vyema: Hakuna Paska bila
Ijumaa Kuu, yaani mtaka cha uvunguni sharti ainame. Baada ya dhiki faraja.
Upendo wa
marafiki ni vazi linalovutia upendo huo ukiwa ni upendo uliokomaa. Upendo
uliokomaa upo katika misingi hii: unamhitaji mtu kwa sababu unampenda.
Unapendwa kwa sababu unapenda. Unamhitaji mtu akusaidie sababu unampenda sio
sababu unamhitaji. Huo ndio upendo uliokomaa. Lakini kuna binadamu wanaopenda
mali na kutumia watu bila kuwa na upendo wa kweli kwao. Bali wanawahitaji tu.
Huo sio upendo uliokomaa. Upendo ambao haujakomaa upo katika mtazamo potofu:
Unampenda mtu sababu unamhitaji. Ukiwa na shida ndipo unampenda mtu atakayeweza
kukusaidia. Huo ni upendo wa kitoto ambao haujakomaa.
Marafiki wa kweli ni watu ambao wanajua
mapungufu yako, lakini hujivunia sifa zako nzuri. Marafiki wa kweli ni wale
wanaokufahamu vizuri kama nyuma ya viganja vyao lakini bado wanakupenda. Katika
msingi huu kuna msemo wa kiswahili usemao, “ mhesabu visa pendo haliwezi.”
Rafiki wa kweli haweki kumbukumbu ya makosa. Usichotaka kutendewa usimtendee
mwenzako. Rafiki wa kweli ni yule anayekupenda licha ya kasoro zako na
anakusaidia kurekebisha kasoro hizo. Zaidi ya hayo, marafiki wa kweli ni watu
ambao hawawezi kusema lolote nyuma ya mgongo wako ambalo hawawezi kusema mbele
yako.Watu ambao wameshiriki pamoja nawe katika furaha na karaha. Watu ambao
wamekuimarisha wakati wa shida. Akufaaye katika dhiki au shida ndiye rafiki wa
kweli.
Sifa ya pili ya urafiki wa kweli ni
kusameheana. Alikuwa ni Henry Ward Beecher aliyetuandikia maneno ya hekima
kuhusu marafiki kusameheana: “Kila mtu anapaswa kutunza kaburi la usawa wa kadiri ambalo ndanimo atazika makosa ya
rafiki zake” Kusamehe ni sharti kubwa la kusamehewa. Wakristu wanajua hilo
maana katika sala ambayo huwa wanaisali kila siku na imeandikwa katika Biblia
wanasema, “Utusamehe makosa yetu kama tunavyowasemehe waliotukosea.” Tunahitaji
kujenga utamaduni na siasa za kusameheana katika Afrika ila bara la Afrika
lisonge mbele hasa wakati huu ambapo limefunikwa na vita huko Darful, mizozo ya
kisiasa huko Zaire, kunyosheana kidole huko Zimbabwe kati ya chama tawala na
vyama vya upinzani maana hata katika siasa hatuna budi kuwa na marafiki wa
kweli ingawa tumezoea kusikia kuwa katika siasa hakuna rafiki wa kudumu na adui
wa kudumu. Lakini tunaweza kuwa na marafiki wa kudumu tukizingatia sifa za urafiki
wa kweli ambazo ni upendo uliokomaa, kusameheana, kuheshimiana, mawasiliano na
maneno matamu yaliyo ya kweli.
Mawasiliano na maneno matamu vinaendana
katika kudumisha urafiki. Mawasiliano ni muhimu. Magugu huziba njia ambayo
haitumiki. Usipomtembelea rafiki yako na kuwasiliana ni kama kwamba magugu
yataziba njia ambayo haitumiki. Juu ya
maneno matamu, Yoshua mwana wa Sira anatuasa, “ Maneno matamu yatamrudishia mtu
rafiki, na midomo yenye neema itamwongezea
wamsalimio (Ybs.6:5) Katika kutumia maneno matamu utakwepa kumhukumu
rafiki yako mpaka umevaa viatu vyake. Yaani kujiweka katika nafasi yake na
kujiuliza “Je kama angekuwa mimi ningefanyaje?”
URAFIKI
WATAKA MOYO
Jiulize aina ya
urafiki ulio nao. Je, huo ni urafiki ama utumwa? Urafiki ambao kwa miezi nenda
miezi rudi ni kupokea ujumbe wa simu wa
tafadhali nipigie. Huenda urafiki wa namna hiyo ni utumwa. Urafiki wa kila
mara niwekee pesa kwenye simu huenda ukawa utumwa. Kwa msingi huu urafiki
wataka moyo. Urafiki wataka uvumilivu, umakini na busara. “Yataka moyo kuwa
rafiki wa kweli. Inabidi kusamehe mengi, kusahau mengi, kuvumilia mengi,”
alisema Anna Robertson Brown. Kuna watu wawili waliokuwa wanamjadili tajiri
aliyefilisika. Mmoja akasema, “Tangia afilisike, nusu ya rafiki wake
hawamtembeli tena, hawamjulii hali tena.” Mwingine akauliza habari juu ya nusu
ya rafiki wake wengine. Mwenzake akamjibu: “Hawajui kama amefilisika.” Biblia
yasema: “Kuna rafiki aliye mwenzi wa mezani, wala hatadumu karibu nawe siku ya
taabu yako (Yoshua bin Sira 6:10). Rafiki katika taabu huyo ni rafiki wa kweli.
Kuna aina tatu
za marafiki: marafiki kwa sababu fulani, marafiki wa msimu na marafiki wa
daima. Marafiki kwa sababu fulani ni wale ambao wana lengo fulani. Labda
wanataka kusaidiwa kupata kazi. Kazi ikipatikana urafiki unawekwa kwenye kaburi
la sahau. Kuna marafiki wa msimu ambao labda wanajitokeza wakati wa kampeini
kama wewe ni mwanasiasa, kuna ambao wanajitokeza wakati wa kuvuna kama wewe ni
mkulima, kuna ambao wanajitokeza mwishoni mwa mwezi unapopata mshahara kama
wewe ni mfanyakazi. Marafiki wazuri ni wale wa nyakati zote ikinyesha mvua wapo
likiangaza jua wapo. Tunaweza kuwazungumzia kwa namna nyingine. Kuna makundi
matatu ya marafiki: kuna ambao ni kama chakula, bila wao huwezi kuishi; wale
ambao ni kama dawa, ambayo unahitaji mara chache; na ambao ni kama ugonjwa
ambao hauhitaji.
Wenzi wa ndoa
kama sio marafiki ndoa hiyo inaweza kuwa mashakani au kuwa kama wagonjwa kwenye
chuma cha wagonjwa mahututi. “Sio ukosefu wa upendo, bali ukosefu wa urafiki
unaofanya ndoa zisiwe na furaha,” alisema Friedrich Nietzsche. Unahitaji kuwa
rafiki wa kweli. Rafiki wa kweli ni rafiki ambaye ni mwaminifu. “Rafiki
mwaminifu ni hifadhi imara; aliyempata amepata hazina” (Yoshua bin Sira 6:14).
Rafiki wa kweli anapewa sifa zifuatazo katika Biblia: hazina, hifadhi imara,
dawa ya uzima na mwaminifu.
Jina lako liko
salama mdomoni mwa rafiki wa kweli. “Watu wanapokupenda, namna wanavyotamka
jina lako ni tofauti. Unajua jina lako liko salama midomoni mwao,” alieleza
Jess C. Scott. Kwa kawaida kuna vitu au malengo yanayowaunganisha marafiki.
Katika msingi mwanafalsafa wa Kigiriki Aristotle alisema: “Urafiki ni roho moja
inayoishi katika miili miwili.”
Urafiki wataka
moyo kwa vile unagharimu. Tafakari mazungumzo haya: “Nasikia rafiki yako Tamson
ameoa tena. “ “Ndiyo ameoa. Amekuwa rafiki yangu mpendwa. Arusi zake
zimenigharimu pesa. Ilibidi ninunue zawadi mara tatu. Kwa vile alifunga ndoa
mara tatu baada ya kufiwa na wake zake mara mbili. Pia ilibidi kununua mashada
ya maua mara mbili kuweka kaburini.” Urafiki unagharimu. Unaweza kupoteza
urafiki hata katika kukopa. Kuna mtu aliyemwambia rafiki yake. “Brown
alijitolea kunikopa.” Aliulizwa: “Je, ulichukua pesa toka kwake.” Jibu
lilikuwa: “Hapana. Urafiki wetu ni mzuri sana sitaki kuupoteza kwa kukopa kopa
baadaye kushindwa kurudisha.”
Swali linabaki
kama urafiki wataka moyo unawezaje kujipatia rafiki wa kweli. Kitabu cha Yoshua
bin Sira kinapendekeza njia tatu. Kwanza tumia maneno matamu. “Maneno matamu
yanaongeza rafiki” (Yoshua bin Sira 6: 5). Pili, Umpate wakati wa shida au
majaribu. Rafiki wakati wa shida ndiye rafiki wa kweli. “Ukijipatia rafiki, umpate
katika majaribu” (Yoshua bin Sira 6: 7). Tatu, omba na kusali na kuwa na
mahusiano mazuri na Mungu atakupa rafiki wa kweli. “Nao wamchao Bwana
watampata” (Yoshua bin Sira 6:16). Yote yakiisha semwa: urafiki wataka moyo.
Urafiki wataka subira, uvumilivu, ukarimu, moyo wa kusamehe na kuwa makini.