MATENDO SABA YA
KIROHO YA HURUMA
MWAKA B
Jumapili ya Huruma ya Mungu
1. Matendo 2: 42 - 47
2. 1 Petro 1: 3-9
3. Yohane 20: 19 – 31
UTANGULIZI
Mojawapo ya neno muhimu sana
katika lugha ya Kiswahili ni neno huruma. Huruma inashikilia mambo mengi
yasiharibike: upendo, umoja, mshikamano, msamaha na amani. “Ukitaka watu wengine wawe na furaha,
huruma iweke katika matendo. Ukitaka kuwa na furaha huruma iweke katika
matendo,” alisema Dalai Lama. Biblia yasema: “Heri walio na huruma, maana
watahurumiwa” (Mathayo 5:7). Hii ni heri pekee ambapo unavuna ulichopanda. “Mwenye
huruma ni yule aliye na huzuni moyoni; anahesabu mateso ya wengine kama mateso
yake, na anahuzunishwa na maombolezo yao kama ya kwake,” alisema Remigius Baba
wa Kanisa. Hapa haki na huruma vinaungana, kimojawapo kinapaswa kuchanganyikana
na kingine; haki bila huruma ni ukatili; na huruma bila haki ni ziada kwa hiyo
anatoka kwenye heri ya haki na kuiendea nyingine ya huruma. “Huruma sio katika
kutoa sadaka tu, bali katika kila dhambi ya ndugu, tunapochukuliana mizigo
alisema Baba wa Kanisa Jerome. “Mungu anafurahishwa sana na hisia zetu za
kufadhili watu wote, atatoa huruma yake kwa walio na huruma tu,” alisema Hilary. “Mwanzoni zawadi inaonekana kulingana
na kilichotolewa; lakini kusema kweli ni zaidi sana; kwa vile huruma ya
kibinadamu na huruma ya kimungu haviwezi kulinganishwa,” alisema Mtakatifu
Yohane Chrysostom. Aliyenacho atapewa zaidi.
Watu katika uwanja wa kiuchumi
wanazungumzia kununua hisa katika makampuni sisi tunazungumzia kununua hisa za
huruma maana Mungu ni tajiri katika huruma (Dives in Misericordia) . “Lakini Mungu
ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, hata, ingawa
tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa
neema ya Mungu nyinyi mmeokolewa.” (Waefeso 2: 4-5) Watu wote wanahitaji huruma
masikini na matajiri. Huruma sio kwa matajiri tu kama methali ya Kiyahudi
inavyotoa kejeli, “Mahakama ina huruma
kubwa sana iwapo mshitakiwa ni tajiri sana.” Leo tunasherehekea Jumapili ya
Huruma ya Mungu. Ibada ambayo imeenezwa na Mt. Faustina wa Poland baada ya
kutokewa na Bwana wetu Yesu Kristu.
MAANA YA NENO HURUMA
Kadiri ya “Kamusi ya Maana na
Matumizi,” huruma ni moyo wa imani. Ni moyo wa kupenda kumsaidia mwenye shida.
Mfano, “Niliingiwa na huruma nikampa mwombaji fedha za kununulia chakula.”
Kuelewa maana ya neno huruma tunaweza kutumia neno la Kilatini, “Misericordia.”
Neno hili lina maneno mawili: cordia ambapo yanatoka maneno kama kadiolojia
Kiingereza cardiology maana yake taaluma ya moyo; cardiac arrest maana yake
shtuko la moyo; cardiac maana yake – a kuhusu moyo; cardiac musle maana yake
msuli moyo. Neno “miseri” linamaanisha mateso na shida. Misercordia
linaamanisha kuwa na moyo ambao huko tayari kuteseka kwa ajili ya wengine, kuwa
na moyo ambao unateseka kwa ajili ya wenye shida. Moyo wa Yesu ni moyo wa namna
hii. Huruma ni kiini cha kusamehe. Kuna matendo saba ya kiroho ya huruma.
1. KUFUNDISHA WASIOJUA
Yesu Alimfundisha Mtume Thoma
Hasiyejua ana shida. Ukimfundisha
unatatua shida. Mtume Thoma aitwaye Didymus “Pacha,” alikuwa hajui kweli juu ya
ufufuko wa Yesu na haamini. Yesu alipowatokea wanafunzi wake alimwambia Thoma,
“Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni
mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini.” (Yohane 20: 27) Yesu alimfundisha Thoma
aitwaye Didymus kwa kutumia USHAHIDI. Thomas alielewa, akasema, “Bwana wangu na
Mungu wangu.” (Yohane20: 28) Aliamini katika ubinadamu wa Yesu Kristu na Umungu
wa Yesu Kristu. Katika Kanisa Katoliki ni Msimamizi wa Wanasayansi wanaofanya
utafiti. Katika Litania ya Moyo Mtakatifu wa Yesu tunasali, “Moyo wa Yesu,
zinamokaa hazina za hekima na elimu,” “Utuhurumie.” Alimpa elimu juu ya ufufuko
wake Thomas. Hilo ni tendo la huruma. “Kutokujua kutokujua kwako ni ugonjwa wa
kutokujua,” alisema A.A. Alcott. Hao wanahitaji kufundishwa.
Umuhimu wa Kufundisha
Tunapata changamoto la
kuwafundisha wasiojua. Kuna methali ya Kichina isemayo, “Nipe samaki nitakula
siku moja. Nifundishe kuvua nitakula maisha yangu yote.” Kufundisha mtu namna
ya kupata chakula ni zaidi ya kumpa chakula ambacho atakula siku moja. Ni tendo
la kubwa la huruma. Atakula chakula siku zote za maisha yake. Kwa walimu kuwa
na huruma kwa mwanafunzi wako “A,” na “B,” siku moja mmoja wao atarudi chuoni
hapo kuwa profesa. Kuwa na huruma kwa mwanafunzi wako, “C,” siku moja atarudi
hapo na kuwajengea mahabara ya mamilioni.
Mtu ambaye hajui jambo fulani ni
mbumbumbu. Kuna ambao wanajua kuwa hawajui hao ni wanyenyekevu hao ni wazuri
kwa kufundishwa. Kuna wajuaji hao ni wenye majivuno. wanajifanya kuwa wanajua
kila kitu. Hao wanahitaji kufundishwa kwanza umuhimu wa unyenyekevu. Kuna ambao
wanajua kuwa hawajui lakini wana woga. Watie moyo wawe na moyo mkuu wasiogope.
Mfano Mwalimu Denis Mapunda alimuuliza mwanafunzi aitwaye Aristides Swala,
“Nani aliandika Biblia?” Mwanafunzi mwenye hofu alijibu, “Sio mimi mwalimu!”
Kuna msemo wa Amerika husemao, “Kitu chenye bei kubwa sana hapa duniani ni
ujinga.” Ukisaidia kumfundisha mjinga unatoa msaada mkubwa sana.
Tufundishe Neno la Mungu
Ni vizuri tuwafundishe wenzetu
ambao hawajui neno la Mungu yaani Biblia. “Maandiko yote matakatifu yameandikwa
kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufunidishia ukweli, kuonya,
kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili, ili mtu
anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila kazi njema.” (2
Timotheo 3: 16-17) Mwanamke kijana alipojifungua mtoto wake wa kwanza alitaka
kutangaza habari njema juu ya kujifungua kwake mtoto kwa rafiki yake. Alituma
ujumbe wa simu ya mkono. “Isaya 9:6” Rafiki yake hakuwa na mazoea ya kusoma
biblia. Hivyo baada ya kupata ujumbe huo alimwambia mmbe wake Tereza
amejifungua mvulana ana uzito wa ratili 9 na aunsi 6. Lakini kwani wamemuita
Isaya?” Hakujua kuwa maneno ya Isaya 9:6 “ Maana mtoto amezaliwa kwa ajili
yetu, tumepewa mtoto wa kiume.” Mtu wa namna hii anahitaji kufundishwa neno la
Mungu.
Tufundishe Kumjua Mungu
Hasiyekujua hakuthamini. “Watu
wangu wameangamia kwa kutonijua, maana wewe kuhani umekataa mafundisho.” (Hosea
4: 6) Hatuna budi kuwafundisha watu kumjua Mungu. Katika Katekismu ya Kanisa
Katoliki tumefundishwa kuwa, “Mungu alituumba ili tumjue, tumpende ili baadaye
tuishi naye milele yote.”
2. KUSHAURI WENYE MASHAKA
Kutoa ushauri ni tendo la huruma.
Yesu anaitwa “Mshauri wa Ajabu” (Isaya 9:6). Bikira Maria Mama wa huruma
anaitwa, “Mama wa Shauri Jema,” katika Litania ya Bikira Maria. Hatuna budi
kuwaiga katika kutoa ushauri kwa wengine. Yesu alipowatokea wanafunzi wake
alimwambia Thoma, “Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono
wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini.” (Yohane 20: 27) Yesu
alimshauri Mtume Thoma Mwenye Mashaka. Kutokana na masha ya mtume Thoma tuna
nahau ya Kiingereza, “doubting Thomas,” mtu ambaye hukataa kuamini mpaka
amepata ushahidi wa mambo. Ni mtu mwenye kushuku au mwenye mashaka.
Tobiti alimuasa Tobia kuomba
ushauri: “Omba ushauri kwa watu wenye busara, wala usidharau kwa watu wenye
busara, wala usidharau shauri lenye kufaa.” (Tobiti 4:18) Mtu mwenye mashaka au
anayefanya jambo baya kuna upande wa mambo ambao hajaona mshauri. Mtu mmoja
aitwaye Tendewa alimpa ushauri mlevi mmoja juu ya namna ya kuacha kunywa pombe.
“Je unaweza kuniambia namna ya kufanya ili niache kunywa pombe?” Mlevi
aliuliza. Tendewa alisema, “Ni rahisi kama kufungua mikono yako au viganja
vyako.” Mlevi alidai kupata maelezo zaidi na kuahidi kutokunywa tena. Tendewa
alimfafanulia, “Nitakuonyesha namna ya kufanya. Ukiwa na glasi yenye pombe kali
fungua mikono yako au viganja vyako kabla ya kunywa. Na hautalewa tena.”
3. KUONYA WADHAMBI
Kuna methali ya kiafrika isemayo,
“Nilisema,” anamzidi, “Nilinyamaza.” Anayeona uovu ukitendeka akaonya kwa
kusema anamzidi yule anayeona uovu akakaa kimya. Mungu wetu ni Mungu mwenye
huruma. Hakai kimya anaonya. “…niliwaonya vikali wazee wao nilipowatoa katika
nchi ya Misri, na nimeendelea kuwaonya wanitii mpaka siku hii ya leo. Lakini
wao hawakunitii, wala hawakunisikiliza.” (Yeremia 11:7-8)
Tuwe Tayari Kupokea Maonyo
“Ukiona bibi kizee anakimbia
usiulize kuna nini na wewe kimbia.” Methali ya Jamaica. Kuna mambo mengi katika
maisha yanayotuonya. Lazima tupokee maonyo. Bwana anatuasa,
Basi, ewe mtu, nimekuweka kuwa
mlinzi wa Waisraeli. Utakaposikia neno kutoka kwangu utawapa onyo langu.
Nikikwambia mtu mwovu: ‘Wewe mtu mwovu hakika utakufa; lakini wewe husemi
chochote ili kumwonya yule mtu mwovu aachane na mwenendo wake; mtu huyo hakika
atakufa kwa kosa lake; walakini nitakudai wewe kifo chake. Lakini ukimwonya
mwovu aachane na mwenendo wake, naye haachani na mwenendo wake mbaya, yeye
atakufa kwa kosa lake; lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako. (Ezekiel 33:
7-9)
4. KUVUMILIA MABAYA
Mvumilivu hula mbivu.
“Tunamwamini Yesu ni wazi kwa sababu hakushuka toka msalabani” (General Booth).
Alivumilia. Mtume Paulo anatuasa, “Mwe na msimamo uleule aliokuwanao Kristo
Yesu” (Fil 2:5) Chenye mwanzo kina mwisho. Mateso, taabu vyote vina mwisho.
Subira na saburi ni fadhila muhimu sana. Wafipa wana methali isemayo, “Mzigo
uchukuao kichwani hukulemea siku moja tu.” Mvumilivu hula mbivu lakini
akivumilia sana hula mbovu. Zinaiva na kuwa mbovu. Yesu alivumilia akiwa na mpango
“B,” yaani wa kumtuma Roho Mtakatifu. Hatuna budi matatizo mengine kuyatafutia
uvumbuzi yaliyo katika uwezo wetu na yale ambayo hayamo katika uwezo wetu
tumwachie Mungu.
5. KUSAMEHE MAKOSA BILA KUSITA
Kusamehe makosa ni tendo la
huruma. Yesu alisisitiza sana hitaji la kuwasamehe wengine. “Kisha Petro
akamwendea Yesu, akamwuliza, ‘Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi?
Mara saba?’ Yesu akamjibu, ‘Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba.’”
(Mathayo 18:21” Kusamehe mara sabini na saba kunamaanisha kusamehe kila mtu
kila mara. “Ni wazi kuwa sharti hili la kiukarimu la msamaha haliondoi masharti
ambayo hayana upendeleo ya haki. Ikieleweka vizuri haki ina malengo ya msamaha.
Hakuna mahali popote katika ujumbe wa Injili ambapo msamaha au huruma kama
kiini chake humaanisha kujiigiiza katika kutenda maovu, kujiigiza katika
kashfa, kutia wengine hasara au kutukana wengine. Katika hali yoyote ile
kufanya malipizi kwa ajili ya maovu na kashfa, kufidia hasara na kufanya
malipizi ya matukano ni masharti ya msamaha,” Alisema Papa Yohane Paulo wa Pili
katika barua yake ya mwaka 1980 yenye kichwa cha habari, “Dives in
Misericordia,” yaani “Tajiri katika Huruma.” (Namba 14)
6. KUFARIJI WANAOTESEKA
Mungu wetu ni mfariji. “Mungu
hatufariji ili tufarijike tu bali tufanywe wafariji,” alisema hayo John Henry
Jewett.
Kuwa na Ufundi wa Kufariji
Tunahitaji kuwa na ufundi wa
maneno ya kufariji. Yesu aliwafariji mitume alipotokea kwao, aliwaambia, “Amani
kwenu! Alipokwisha sema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao
wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana.” (Yohane 20: 19-20) Yesu aliwaonyesha
mikono. Kama mke wako anateseka kisaikolojia muoyeshe unavyompenda. Kama mme
wako anateseka Kisaikolojia muonyeshe unavyompenda.
Fariji kwa Kulia na Wanaolia
Tufariji wanaoteseka. Mtume Paulo
alituasa, “Furahi pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia.”
(Waroma 12: 15). Yesu alilia Lazaro alipokufa. Alilia na wanaolia.
Fariji kwa Kutumia Tiba ya
Kuongea
Kuongea ni tiba. Kama una
sononokeko na simanzi kuongea ni tiba. Kama una mfadhaiko kuongea ni tiba.
Muulize mtu maswali ambayo hayambani mtu kutoa jibu la ndoa au hapana bali
kuelezea. Kuna mitume wawili waliokuwa wanaenda Emmaus walikuwa wamekata tamaa.
Yesu aliwauliza maswali mawili yanayohitaji majibu marefu ili waongee. Swali la
Kwanza: “Mnazungumza nini huku mnatembea?” (Lk 24: 17). Swali la Pili: “Mambo
gani?” (Lk 24: 19) Mitume hawa walikuwa wenye huzuni. Yesu aliwatia moyo
waongee. Kuongea ni tiba na kutia mtu moyo aongee kunahitaji ufundi katika
kuuliza maswali.
7. KUWAOMBEA WAZIMA NA WAFU
Kuwaombea Wazima
Kuwaombea wazima ni tendo la
huruma. Yesu aliwaombea wanafaunzi wake:
“Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya
jina lako ulionipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi
tulivyo mmoja.” (Yohane 17: 11)
Wazazi hawana budi kuwaombea
watoto hao. Mtakatifu Monica alimuombea mtoto wake Augustini akabadilika na
kuwa mtakatifu. Watoto hawana budi kuwaombea wazazi wao. Hatuna budi kuwaombea
viongozi wetu. Unaweza kutumia Kanuni ya Vidole.
Kidole gumba kinasimama badala ya
jamaa zako. Waombee. Kidole cha shahada kinasimama badala ya walimu na walezi.
Waombee wazazi ambao ni walimu wa kwanza na waombee walimu wote. Kidole cha
kati kinasimama badala ya viongozi wote wa kidini na wa serikali. Kidole cha
pete kinasimama badala ya wale waliodhaifu kama wagonjwa waombee. Kidole cha
kadogo kinasimama badala ya wewe. Jiombee.
Kuwaombea Wafu
Hadithi inapokuwa tamu katika
gazeti hukatizwa na chini yake maneno “Itaendelea Toleo Lijalo” huandikwa.
“Toleo lijalo” kwa marehemu waliolala ni mbinguni au toharani (Purgatorio) au
motoni. Kama wako toharani hatuna budi kuwaombea. Tuna msingi ya kuwaombea wafu
katika biblia: 2 Makabayo 12: 39-45; Mathayo 5: 25-26; Mathayo 12:32. Mtakatifu
Monika kabla ya kifo chake alimwambia Mt. Augustino na kaka yake: “Muuzike
mwili huu popote pale! Msijisumbue na chchote kwa ajili yake! Ninachowaombea ni
kunikumbuka katika altare ya Bwana popote pale mtakapokuwa.” Tuwakumbuke
marehemu katika altare ya Bwana.