Friday, December 26, 2014

GHARAMA YA KUMFUATA KRISTU




                                         SIKUKUU YA MT.STEFANO SHAHIDI
                                                         26 Desemba 2013

1.       Mate 6: 8-10, 7: 54 -59
2.        Mt 10: 17-22
 UTANGULIZI
 Jana ilikuwa “Birthday” ya Yesu Kristu. Leo ni Birthday ya Mtakatifu Stefano shahidi. Ni kuzaliwa kwa Mtakatifu Stefano. Lakini ni kuzaliwa kwake mbinguni. Sikukuu ya Mtakatifu Stefano inavumbua mbivu na mbichi katika kumfuata Yesu Kristu. Ili tuzaliwe mbinguni hatuna budi kulipa gharama. Jana Bwana alizaliwa duniani ili Stefano azaliwe mbinguni. Jana aliingia duniani ili Stefano aweze kuingia mbinguni.
  
GHARAMA YA KUMFUATA KRISTU
  
MSAMAHA
 Stefano aliwasamehe wauaji wake. Alisema, “Bwana, usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii” (Matendo 7:60). Msamaha ni gharama ya kumfuata Yesu Kristu. Watu hujiandaa kusamehe lakini walio wengi hawajiandai kusamehewa. Je kama unasemehewa unapokea msamaha? Bwana Yesu alipokuwa kufani msalabani alisema maneno saba msalabani: Neno la kwanza ni: “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya,” (Luka 23: 34). “Kufanya makosa ni jambo la kibinadamu, kusamahe ni jambo la kimungu,” Alisema Alexander Pope (1688-1744) mshairi wa Uingereza. Lakini tujue kuwa kuendelea kutenda makosa bila kuacha ni jambo la kishetani. Yesu alivyowasamehe waliomkosea alifanya jambo la kimungu. Hakutaka kutwika uwezo wake wa kukumbuka mzigo mzito wa mambo yaliyopita. Kama yeye alifanya hivyo kwa nini sisi tunabeba mizigo mizito ya mambo mabaya tuliyotendewa.
 William Shakespeare aliandika hivi katika kazi yake iitwayo, “The Tempest,” “Prospero, alipopewa nafasi kuwaadhibu wale waliomwondoa katika nafasi yake kama mfalme, alisema, ‘Tusitwishe mzigo mzito kumbukumbu zetu kwa jambo zito ambalo limepita.” Kununa kwetu hakubadili historia. Kukasirika kwetu hakubadili historia. Kulaani hakubadili historia. Kutukana hakubadili historia. Kusamehe kunabadili historia maana hakuongezi idadi ya watu wabaya lakini kulipiza kisasi kunaongeza idadi ya watu wabaya.

Bwana Yesu ni kioo cha jamii na familia katika kutoa msamaha. Aliwatetea waliomfanyia mabaya kuwa hawakujua. Wanafamilia wajifunze toka kwa Yesu kusameheana. Maneno “nisamehe” yawe kama kiitikio katika familia. Familia ni shule ya kwanza ya kujifunza kusamehe na kupokea msamaha. Wazazi ni walimu wa kwanza wa somo la msamaha. Kama pametokea ugomvi, msamaha ufuate kama asubuhi inavyofuata usiku. Ugomvi huanza kwa kutokubali kosa na kuomba msamaha. Mfano, mtu mmoja alimwambia mwenzake, “ulitenda kosa.” Mwenzake alijibu, “sikutenda kosa.” Ugomvi ulianza na marafiki hao wawili walikasirikiana. Mmoja baadaye alisema, “Samahani naomba unisamehe.” “Na mimi naomba nisamehe pia,” alisema mwenzake. Ugomvi ulimalizika, kwa sababu ya maneno machache ya upendo.
 Kuomba msamaha na kukubali kupokea msamaha ni tiba. Karl Menninger, daktari bingwa wa magonjwa ya akili kama kichaa alisema kuwa kama angeweza kuwafanya wagonjwa kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili kuamini kuwa dhambi zao zimesamehewa, asilimia 75 ya wao wangetoka wamepona siku inayofuata. Mzee Joe alikuwa kufani kwenye kitanda cha mahuti. Kwa muda wa miaka mingi alikuwa hapatani na Bill, ambaye zamani alikuwa mmoja wa marafiki zake. Akitaka kunyosha mambo yake kabla ya kuaga dunia alimtuma Bill waongee na kumaliza mambo. Bill alipofika, Joe alimwambia kuwa anaogopa kwenda mbinguni akiwa na kinyongo naye. Kwa kusita na kwa kujikaza Joe aliomba msamaha kwa mambo aliyoyasema na kuyatenda. Alimwaakikishia Bill kuwa amemsamehe kwa makosa yote aliyomtendea. Mambo yote yalionekana kwenda vizuri mpaka hapo Bill alipojiandaa kuondoka. Alipokuwa anatoka chumbani, Joe alimuita, “Lakini kumbuka, nikipona, haya yote niliyosema hayana maana wala uzito.”

KUSALI
Mtakatifu Stefano aliinua macho juu. Alisali. Mashaka yanatazama nyuma. Wasiwasi unatazama kila upande lakini imani inatazama juu. Tunasoma katika Biblia, “Waliendelea kumpiga Stefano kwa mawe huku akiwa anasali: “Bwana Yesu ipokee roho yangu!” (Matendo 7:59). Kusali ni gharama ya kumfuata Yesu Kristu.
Sala ni jiwe linalojenga msingi wa nyumba ya ndoa. Hoja ya msingi sio kusali tu bali kusali pamoja. Mtume Paulo anawaasa, “Mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikra moja.” (1 Petro 3:8). Familia ambayo haisali ni familia iliyoasi. Mwanzo wa kuteleza kwa familia ni kudharau sala hasa sala za pamoja. Kusali hakuishii katika kusali pamoja nyumbani. Wanafamilia hawanabudi kwenda kusali pamoja Kanisani pia. Katika suala la kwenda Kanisani kusali Bwana hasimwachie Bibi yake. Hasiseme, “Sali kwa niaba yangu.” Huko mbinguni hatasema, “nenda kwa niaba yangu.”  Mbinguni ni pa wote wanaume na wanawake. Hakuna anayekunywa dawa kwa niaba ya mgonjwa. Kila mtu anawajibu wa kufanyia kazi wokovu wake.
 Mbinguni si pa jinsia moja tu. Sio kama mtoto Veronika alivyofikiri. Veronika mtoto wa miaka mitano alimuuliza mama yake, Jancita, “Mama, je wanaume huwa hawaendi mbunguni?” “Huwa wanaenda mbinguni.” Alijibiwa mtoto. Mama alitaka kujua kwa nini swali kama hilo linaulizwa. “Kwa nini Veronika unauliza kama wanaume wanaenda mbinguni.?” Alidadisi mama. “Ni kwa vile sijawahi kuona picha za malaika wenye ndevu.” “Wanaume huwa wananyolewa ndevu kabla ya kwenda mbinguni.” Alimjibu mama. Nguvu ya sala ya pamoja tunaiona katika maisha ya Tobia na Sara. “Tobia aliondoka kitandani, akamwambia mkewe, ‘Inuka,dada, tumwombe Bwana atuonee huruma na kutukinga salama.’ Sara akainuka. Tobia akaanza kusali: ‘Utukuzwe ee Mungu wa wazee wetu…Uwe na huruma kwake na kwangu utufikishe uzeeni pamoja!” (Tobiti 8:7) Tobia alifikia umri wa miaka mia moja ishirini na saba. Alifikia uzee pamoja na Sara.
 Tuwabebe wengine katika sala. Kubeba ni kuchukua mkononi, begani au kichwani. Ni kusaidia kwa kutoa mahitaji ya lazima. Tunaweza kusema anawabeba wazazi na kuwasimamia katika mahitaji yao yote. Yesu alipokuwa amefadhaika aliomba Mungu Baba ambebe. Tuwabebe wengine katika sala tuwalete kwa Yesu
 Tuwabebe katika sala watu wa makabila mengine na mataifa mengine. Filipo na Andrea wayahudi “waliwabeba” wagiriki kuwapeleka kwa Yesu (Yohane 12: 20-21). Tuwabebe watu wa makabilia mengine tuwapeleke kwa Yesu.  Hawa Wagiriki walikuwa wanatafuta na wanaangaika. Mtanzania ambebe Mkenya katika sala. Mkenya ambebe Mtanzania katika sala. Mkikuyu ambebe Mjaluo katika sala. Mjaluo ambebe Mkikuyu katika sala. Mkikuyu ambebe Mkalenjini katika sala. Mkalenjini ambebe Mkikuyu katika sala. Tuwabebe wenzetu katika sala. Mtakatifu Monica alimbeba mtoto wake Augustini katika sala. Augustini akabadilika. Ni huyu alisema, “Jinsi nilivyo ni zawadi ya Mungu kwangu. Jinsi nitakavyokuwa ni zawadi yangu kwa Mungu.”
 UNYENYEKEVU
Biblia yasema, “Akapiga magoti akalia kwa sauti kubwa” (Matendo 7:60). Kupiga magoti ni ishara ya unyenyekevu. Gharama ya kumfuata Yesu Kristu ni kunyenyekea. Kuna sababu nyingi za kunyenyekea. Kwanza sisi ni cha kupewa. “Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa?” 1 Kor.4:7. Mungu ametupa vipaji mbalimbali. Kuna kipaji cha lugha, kipaji cha mehesabu, kipaji cha uandishi, kipaji cha kuimba, kipaji cha kutibu na kipaji cha kucheza mpira. Lakini si busara kuwadharau wengine kwa vile unakipaji fulani. Wewe umepewa. Ya nini kujivunia kana kwamba hukupewa? Palikuwepo na Profesa aliyekuwa anavushwa na mvuvi kwenye mto. Wakiwa katikati ya mto, Profesa alimuuliza mvuvi, “Wewe mvuvi unajua kusoma?” Mvuvi alijibu, “Profesa sijui kusoma.” Profesa alisema, “Kama ni hivyo robo ya maisha yako imepotea.” Profesa aliuliza tena, “Wewe mvuvi unajua kuandika?” Mvuvi alijibu, “Profesa sijui kuandika.” Profesa alisema, “Kama ni hivyo nusu ya maisha yako imepotea.”Profesa aliuliza tena, “Wewe mvuvi unajua kuhesabu?” Mvuvi alijibu, “Profesa sijui kuhesabu.” Profesa alisema, “Kama ni hivyo umepoteza robo tatu ya maisha yako.” Wakati wanaendelea na safari upepo mkali ulianza kuvuma. Mvuvi alimuuliza Profesa, “Profesa unajua kuogelea.” Profesa alijibu, “Sijui kuogelea.” Mvuvi alisema, “Maisha yako yote yamepotea.”
 Kinyume cha unyenyekevu ni majivuno na kiburi. “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu.” (Mithali 11: 2)  Unyenyekevu sio kujidharau. Ni kukubali vipaji na uwezo ulio nao na kutambua kuwa hautoki kwako bali unapitia kwako unatoka kwa Mungu. USIJIVUNE SANA KINAKUDANGANYA KIOO. Dhambi ya kwanza kutendeka mbinguni ni majivuno. Lucifer aliangushwa toka mbinguni sababu ya majivuno. “Jinsi gani ulivyoporomoshwa toka mbinguni, wewe uliyekuwa nyota angavu ya alfajiri. Jinsi gani ulivyoangushwa chini, wewe uliyeyashinda mataifa!” (Isaya 14: 12) Chini ya kila kosa kuna majivuno.
 Kadili tumbili anavyopanda juu ndivyo makalio yanazidi kuonekana. Kadili tunavyopanda juu hatuna budi kunyenyekea. Hawezi kusema kama mtu fulani hayupo dunia itaacha kuzunguka kwenye mhimili wake. Itazunguka. Mlima uliaibisha kichuguu mpaka vyote viwili viliponyenyekeshwa na nyota. Mwembe ukiwa na miembe unakuwa umeinama. Ni unyenyekevu. Mwembe usio na maembe hauinami. Unyenyekevu ni mama wa wokovu “...alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe...” (Wafilipi  2: 8-10). 

Counter

You are visitor since April'08