NOELI USIKU
1. Isa 9: 1-6
|
2. Tit 2: 11-14
|
3. Lk 2: 1-14
|
“Zawadi kubwa sana maishani ni
kukumbukwa,” alisema Ken Venturi. Siku ya Krismasi tunampa zawadi kubwa sana
mtoto Yesu zawadi ya kumkumbuka. Siku ya Krismasi tunampa zawadi kubwa sana
Bikira Maria zawadi ya kumkumbuka. Siku ya Krismasi tunampa zawadi kubwa sana
Mtakatifu Yozefu zawadi ya kumkumbuka. Siku
ya Krismasi tunalipa hori zawadi kubwa sana alipozaliwa mtoto Yesu zawadi ya
kulikumbuka. Hatumkumbuki meneja wa Nyumba ya Wageni aliyewanyima nafasi.
Tunasoma hivi katika Biblia: “Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua
ikawadia, akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto,
akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni” (Luka 2: 6
-7). Kuna mambo saba ya kukumbukwa siku ya Krismasi.
Kwanza, Mtoto Yesu anapewa zawadi kubwa sana zawadi ya kukumbukwa. Kuna
aliyemuuliza mtoto, “je umepata kile ulichohitaji katika Krismasi hii?” Mtoto
alijibu sikupata kila nilichohitaji na kila nilichotegemea. Lakini hata hivyo siku
ya leo siyo siku yangu ya kuzaliwa ni siku ya kuzaliwa Yesu Kristu.” Ni vizuri watoto watambue kuwa Krismasi siyo
siku yao ya kuzaliwa (labda kama mtoto alizaliwa tarehe 25/Desemba naye atakuwa
anasherekea siku yake ya kuzaliwa) ni siku ya Kuzaliwa Yesu Kristu. Tatizo
tunaweza kutekwa na kile kinachouzwa na kununuliwa tukamsahau yule
aliyesababisha vitu vyenye maneno: “Heri ya Krismasi” viuzwe. Naye ni Yesu.
Maneno ya kutakiana heri: Heri Krismasi; Baraka ya Krismasi; Furaha ya Krismasi
yatukumbushe juu ya Yesu ambaye ni baraka kwa dunia. Kwa sababu yake kuna
mabadiliko. Wafuasi wa Yesu wanafanya mengi ya maendeleo. Kuna Hospitali
zimejengwa na madhehebu ya Kikristu. Vyuo vimejengwa kwa sababu Yesu alikuja.
Inasikitisha kadi za Krismasi zinapokuwa hazina mchoro au “picha” ya Yesu.
Krismasi bila Yesu ni bure.
Pili, Bikira Maria Mama wa Yesu anapewa zawadi kubwa sana ya kukumbukwa:
Hakuna Krismasi bila Mama Maria Mama wa Yesu Kristo. “Hapa hakuwepo mkunga,
hapakuwepo wasiwasi uliojaa huruma wa wanawake; alimvisha Yesu nguo za kitoto,
yeye akiwa mama na mkunga,” alisema Mtakatifu Jerome. Ni kama “Mkunga” na “Nesi”
katika Agano Jipya. Jambo kubwa na zuri sana ambalo baba anaweza kuwafanyia
watoto ni kumpenda mama yao. Na jambo kubwa ambalo tunaweza kumfanyia Yesu
mkombozi wetu ni kumpenda mama yake. Tuwaenzi wakina mama, tuwaheshimu wakina
mama. Uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Titi la mama li tamu, jingine halishi hamu.
Mama ni mama ajapokuwa rikwama, hata akiwa na upungufu ni mama. Mama hamkani
mwanawe japo awe kilema. Kuna watu ambao hutaka kulinganisha wakina mama. Mama
wa Yesu hawezi kulinganishwa na mwanamke yeyote. Kuna Bwana mmoja aliyemwambia
mke wake: “Chakula unachopika sio kitamu kama chakula mama yangu alikuwa
anatupikia.” Mwanamke naye akamjibu: “Ni sawa, lakini hata mshahara wako ni
mdogo ukilinganisha na mshahara baba yangu alikuwa anapata.”
Bikira Maria ni MAMA. Tafakari neno “MAMA.” Herufi ya Kwanza “M”
inasimama badala ya Milioni ya vitu alivyokupa mama. “A” asante. Anastahili asante
kwa mamilioni ya vitu alivyokupa. Waluhya wa Kenya
wana methali isemayo: “Nyama choma haiwezi kuwa tamu sana ukasahau aliyeichoma.” Mama Maria
anastahili asante
kwa kukubali kumzaa mkombozi Yesu. “M” inasimama badala ya “Malezi” Mama analea
mimba na analea mtoto. Mama Maria alilea mimba, mtoto Yesu akiwa tumboni. “A”
inasimama badala ya “Adabu,” onyesha adabu kwa mama.
Tatu, Mtakatifu Yozefu anapewa
zawadi kubwa sana ya kukumbukwa: Jina Yozefu linatokana na neno la kiebrania lenye maana:
na aniongezee mwingine. Papa Leo XIII alikuwa na
haya ya kusema juu ya Mtakatifu Yozefu, “Mtoto aliyekuwa anatishiwa na wivu wa
mfalme alimkinga asiuawe na alimtafutia mahali pa kukimbilia; katika shida za
safari na katika makali ya ukimbizi alikuwa daima mwenzi na msaada, mtetezi wa
Bikira na Yesu.” Yozefu anakumbukwa kama baba mwema. Changamoto kwa
wanaume ni kukumbukwa na watoto kama baba mwema. “Natumaini nakumbukwa na
watoto wangu kama baba mwema,” alisema Orson scott Card.
Nne, Nguo za kitoto
alizovikwa Yesu zinapewa zawadi kubwa ya kukumbukwa: Siku ya Krismasi tunazipa
zawadi kubwa sana nguo za kitoto alizovikwa mtoto Yesu, tunazikumbuka. “Yeye aliyevisha
dunia yenye uzuri wa aina mbalimbali alivikwa nguo za kawaida za kitani, ili
tuweze kupokea vazi zuri sana; yeye ambaye vitu vyote vimafanyika, mikono yake
na miguu vinakunjwa ili mikono yetu
iinuliwe kwa kila kazi tuifanyayo, na miguu yetu iongozwe katika njia ya amani,”
alisema Baba wa Kanisa Bede. Tukumbuke vazi tulilovishwa tulipobatizwa.
Tano, Horini alipowekwa mtoto Yesu panapewa zawadi kubwa sana ya
kukumbukwa: “Anafungiwa mahali padogo pa hori baya, ambaye kiti chake
kilikuwa mbinguni, ili atupe chumba cha kutosha katika furaha za ufalme wa
mbinguni. Yeye ambaye ni mkate wa
mbinguni analazwa horini, ili atushibishe kama wanyama walivyokuwa
wanashibishwa,” alisema Baba wa Kanisa Bede. Kuingia horini ilibidi mtu
kuinama, ishara ya unyenyekevu. Alitaka watakaoingia waingie kwa mtindo wa
unyenyekevu. Horini alipozaliwa Yesu alizungukwa na wanyama. Kwa wayahudi
wanyama kama ilivyo kwa Wamasai walikuwa ni ishara ya utajiri. Bwana Yesu
alizungukwa na ishara ya utajiri kuonesha alikuja kututajirisha. Katika
kupambana na umaskini ni vizuri hilo likasisitizwa vinginevyo tunaweza
kuwaprogramu watu kuwa maskini (Umaskini wa kiroho ni muhimu lakini ulalahoi si
muhimu). Ingawa watakatifu wengi wametokea “Slum” hatuwezi “kuendekeza” slums
ili tuwapate watakatifu.
Sita, Bethlehemu alipozaliwa Yesu panapewa zawadi kubwa sana ya
kukumbukwa. Hapo pamejengwa Kanisa. Bethlehemu maana yake ni nyumba ya mkate. Yeye
aliyejitambulisha kama Mkate alizaliwa mahali penye maana ya Nyumba ya Mkate. “Ee
Bethlehemu nchini Yudea, wewe si mdogo kamwe kati ya miji maarufu ya Yudea;
maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu Israeli” (Mathayo 2:
6). Changamoto: “Kama Kristu anazaliwa mara elfu moja Bethlehemu na si katika
moyo wako, umepotea milele yote,” alisema Angelus Silesius (1624-1677). Umuhimu
wa mtu si mahali anapokaa na mahali anapotokea, au mahali alipozaliwa. Baraka
Obama Rais wa Amerika ametokea Kijiji cha Kogelo huko Kisumu lakini sasa ni
Rais wa Amerika. Hakutoka New York. Hakutokea Tel Aviv. Hakutokea London. Yesu
hakutokea jiji la Yerusalemu. Alizaliwa Bethlehemu. Alitokea Nazareti, kijiji
kilichodharauliwa sana kama tunavyosoma katika Biblia “Naye Nathanaeli
akamwuliza Filipo, “Je kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia,
“Njoo uone” (Yohane 1: 46).
Saba, usiku mtulivu na mtakatifu unapewa zawadi kubwa sana ya kukumbukwa.
Kipindi cha Krismasi unaimbwa wimbo ambao umevuta nyoyo za watu “Silent Night”
ambao umetafsiriwa kwa Kiswahili: Usiku mkuu! Usiku Mtakatifu! Uko utulivu;
Bikira amezaa Mwana, Mtoto Mtakatifu ni Bwana; Alale amanini, Alale amanini.”
Wimbo huu unazungumzia ukimya, utulivu, ukuu na utakatifu wa usiku alipozaliwa
Yesu. Utulivu huu na ukimya huo ni wito wa kuwa na utamaduni wa kuwa kimya na
kutulia. Wakati wa vita ya kwanza ya dunia Krismasi ya mwaka 1914 vikosi vyote
vilivyokuwa vinapigana viliweka silaha chini na kuimba wimbo wa “Silent Night.” Kelele za bunduki
zilisimamishwa. Lakini pongezi ingekuwa kama kelele hizo zingesimamishwa siku
zote na sio usiku tu wa Krismasi. Utamaduni wa kutochafua hewa kwa kelele
lisiwe suala la Krismasi tu. “Tunahitaji kumtafuta Mungu, na hapatikani katika
kelele na kutotulia. Mungu ni rafiki wa ukimya. Tazama viumbe – miti, maua,
nyasi vinakua katika ukimya; tazama nyota, mwezi na jua vinafanya mambo katika
ukimya.. Tunahitaji ukimya kuweza kugusa nyoyo za watu,” alisema Mama Tereza wa
Calcutta.
Kila mtu ajiulize anakumbukwa kwa
lipi na atakumbukwa kwa lipi. Tenda wema huende zako wema hauozi. Tunasoma
katika Biblia. “Habari kuhusu tukio hilo iliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu
mbele ya mfalme” (Esta 2:23). Matendo yako mazuri yataandikwa katika kitabu cha
“Guiness” cha Mungu.
Kijana mwenye umri wa miaka kumi
na nane alienda karibu na Ghala la Dawa na kutoa kreti ya soda aitumie kufikia
kwenye sanduku la kupigia simu. Alisimama juu ya kreti ya soda na kubonyeza vitufe
(buttons) za namba saba. Mmiliki wa Ghala ya Dawa alisikiliza mazungumzo:
Kijana alisema, “Mama unaweza kunipa kazi ya kukata nyasi kwenye uwanja wako?
Mama huyo alijibu, “Tayari nina mtu anayekata nyasi katika uwanja.” Kijana
alisema, “Mama nitaka nyasi kwenye uwanja nusu ya gharama ya mtu anayekata
nyasi katika uwanja wako.” Mama huyo alijibu, “Ninaridhika na kazi anayoifanya
mfanyakazi wangu.” Kijana akionesha uvumilivu alisema, “Mama, nitafagia njia na
vinjia katika eneo lako lote bure.” Mama
huyo alijibu kwa mkato, “Hapana, nashukuru.” Akiwa amevaa tabasamu, kijana huyo
alimaliza mazungumzo. Mmiliki wa Ghala ya Dawa alisema, “Kijana nimependa
mtazamo wako juu ya kazi nataka nikupe kazi.” Kijana alijibu kwa ufupi, “Hapana,
nashukuru.” Mmiliki wa Ghala ya Dawa alimjibu, “Lakini ulikuwa unaomba sana
upewe kazi.” Kijana alisema, “Nilikuwa nataka kujua kipimajoto cha kazi kikoje,
kama mama ninayemfanyia kazi anaridhika na ananikumbuka kama mchapakazi.” Ndugu
utakumbukwa kama Yozefu – Mfanyakazi? Ndugu utakumbukwa kama Bikira Maria –
Mama mkimya aliyeweka yote moyoni? Ndugu utakumbukwa kama mtoto Yesu aliyekua
katika umbo na hekima?