Jumapili ya 2 ya Majilio
1. Isaya 40: 1-5, 9-11
|
2. 2 Peter 3: 8-14
|
3. Marko 1: 1-8
|
Barabara ya maisha ambayo haina
fadhila ni barabara ambayo haikunyoka. “Dhahabu yote iliyoko chini au kwenye
ardhi haitoshi katika kubadilishana na fadhila,” alisema Plato. Fadhila
ni kama unyenyekevu, subira, ukarimu, msamaha, upole. Kama hayo yapo katika
maisha ni kuwa barabara ni tambarare. Kinyume chake ni tabia mbaya, uovu au vilema kama majivuno, uvivu, uchoyo na hasira.
Kama hivyo vipo barabara ya maisha ina mabonde. Mbeuzi mmoja yaana mtu mwenye
tabia ya kudharau mambo nyakati za Dk
Johnson alichukulia msimamo kuwa hakuna
tofauti kati ya fadhila na tabia mbaya au kilema. Dk. Johnson alipopata habari hizo alisema: “Mtu
wa namna hiyo akitoka kwenye nyumba yetu
hesabu kama vijiko vimekamilika.” Lakini barabara ya maisha inaweza kuwa na
milima. Fadhila ikizidi kupita kiasi au kupindukia ni milima.
Wito wa Injili ya Marko ni: “Itengenezeni
njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake” (Marko 1: 3). Kunyosha mapito ni kufikia
mabonde ya vilema na kushusha milima ya kuzidisha fadhila kupindukia, ili tuwe
na tambarare ya fadhila. Hivyo unavyojiandalia Krismasi andaa njia kukutana na
Njia. Yesu Kristu ni Njia. Ni fadhila yenyewe. Fadhila inasimama katikati ya
kasoro na ziada kupindukia. Fadhila ya busara inasimama katikati ya uzembe na
ulaghai. Busara ikizidi sana ni ulaghai. Upungufu, dosari katika masuala ya
busara ni uzembe. Hapana hakuna utafiti unafanyika. Ukarimu ni fadhila ambayo
inasimama katikati ya uchoyo na kutapanya hovyo. Krismasi tunayoingojea sio kipindi cha
kutapanya hovyo. Wengine wanatapanya hovyo mpaka wanatumia karo za watoto wao.
Unyenyekevu unasimama
katikati ya majivuno na kujidhalilisha. Majivuno ni bonde. Unyenyekevu ni
tambarare. Kujidhalilisha ni mlima. Unyenyekevu ukizidi kupindukia ni
kujidhalilisha. Fadhila ya ujasiri inasimama katikati ya ujasiri wa
kipumbavu au ujasiri bila busara na woga. Ugumu ni namna ya kupima ni hapa
busara inapohitajika. Woga ni bonde. Ujasiri bila busara ni mlima.
“Anaamrisha mabonde yafukiwe, vilima na milima
kusawazishwa, kuonesha kuwa kanuni ya fadhila haipungukiwi uzuri na wala
haivuki na kupita kiasi,” alisema Baba wa Kanisa Gregory wa Nyassa. Bonde na milima vinaonyesha kuzidisha na
kuharibu fadhila ama kupunguza na kuharibu fadhila. Mfano wa bonde la ukarimu
ni uchoyo. Mlima wa ukarimu ni kutapanya hovyo.Bonde katika barabara ya
unyenyekevu ni majivuno. Mlima katika barabara ya unyenyekevu ni kujidhalilisha.
Kinachoitajiwa ni tambarare yaaani ukarimu, unyenyekevu na ujasiri
Bonde
|
Tambarare
|
Mlima
|
Uchoyo
|
Ukarimu
|
Kutapanya Hovyo
|
Woga
|
Ujasiri
|
Ujeuri/uchokozi/Kutojali
|
Majivuno
|
Unyenyekevu
|
Kujidhalilisha
|
Ulevi
|
Kiasi
|
Kutojali afya
|
Uzembe
|
Busara
|
Ulaghai
|
Kukosa Subira
|
Subira
|
Kutojali
|
Tambarare ya Subira
Subira inasimama
katikati ya kukosa subira na hali ya kutojali. Kuna methali za Kiswahili
zinazosisitiza tuwe na fadhila ya subira: Subira ni ufunguo wa faraja. Subira
huzaa mwana mwema. Subira huvuta heri. Kukosa subira ni bonde. Subira ni
tambarare. Hali ya kutojali tena ni mlima. Nyosheni njia. Mwanafalsafa wa
Kigiriki Aristotle alisema, “Mizizi ya subira ni michungu, lakini tunda lake ni
tamu.” Inasemwa mvumilivu hula mbivu akivumilia sana anakula chungu. Subira
ikizidi ni hali ya kutojali. Kukosa subira ni tabia ya watoto. Wanachotaka
wanataka wakipate haraka: kama ni baisikeli ya kuchea, kompyuta ya kuchezea,
pipi, andazi. Mtume Petro anatuhimiza tuwe na subira: “Lakini, wapenzi, msilisahau
neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama
siku moja. Bwana hakawii kutimiza ahadi yake” ( 2 Petro 3: 10). Mtume Paulo
anatutaka tuwe na subira kwa vile Mungu wetu ni Mungu wa Subira. Ufisadi
unaweza kutokana na kutokuwa na subira: unataka kuwa na gari zuri sasa, nyumba
nzuri sasa, simu ya gharama sasa. Subira ni kutofia madogo ya sasa, unangoja
makubwa. Kuna mtu aliyekuwa na mazungumzo na Mungu, “Bwana nimekuwa nikishangaa
juu ya muda. Miaka elfu moja kwako ni kama nini?” Mungu alimjibu, “Kwangu miaka
elfu moja ni kama sekunde moja.” Mtu
huyo aliuliza, “Je kuhusu pesa? Dola milioni moja kwako ni kama nini?” Mungu
alimjibu, “Kwangu dola milioni moja ni kama shilingi moja.” Mtu huyo alifurahi
sana na kuwa na shauku na kusema, “Bwana unaweza kunipa hiyo shilingi moja?”
Mungu akamwambia, “Hakuna shida, lakini utangoja sekunde moja.” Jua kwa Mungu
sekunde moja inaweza kuwa kama miaka elfu moja. Dhambi za kukosa subira ni nyingi. Kuiba ni dhambi ya kukosa subira
badala ya kufanya kazi mtu anachukua njia fupi ambazo zinamfupisha kiroho. Uzinzi
na uasherati ni dhambi za kukosa subira. Kipindi cha kungoja Krismasi ni
kipindi cha kujifunza somo la subira.
Tambarare ya Ujasiri
Juu ya ujasiri Nelson Mandela
alikuwa na haya ya kusema: “Nimejifunza
maishani kwamba ujasiri maana yake si ukosefu wa woga; bali ni ushindi dhidi ya
woga, na kwamba shujaa si yule ambaye hana woga; bali ni yule anayeushinda woga.”
Khruschchev aliposimama na kutoa
shutuma zake dhidi ya utawala wa Stalini katika ukumbi wa Congress, mtu mmoja
alisema, “Ulikuwa wapi Komredi Khruschchev wakati watu wasiokuwa na hatia
walipochinjwa ?”Khruschchev alinyamaza kwa muda na kutazama watu kwa makini na
kusema: “Yule aliyesema hayo asimame tafadhali”. Watu ukumbini walishikwa na
wasiwasi, mahangaiko na fadhaa, hakuonekana wa kujitingisha wala kujikuna.
Ndipo baadaye Khruschchev aliposema: “Yeyote uwaye sasa hivi unajibu, nilikuwa
katika hali uliyomo sasa”.
Tambarare ya Ukarimu
“Unaweza kutoa bila kupenda
lakini hawezi kupenda bila kutoa,” alisema, Robert Louis Stevenson. Kuna mtu
aliyeenda kwa tajiri kuomba elfu tatu. Tajiri akampa elfu hamsini. Yule
aliyeomba elfu tatu akashangaa na kusema, “Bwana Mkubwa, Chifu, Bosi! Mimi
nimeomba elfu tatu wewe mbona umenipa hamsini.” Bwana huyo akasema, “Elfu tatu
zinakutosha wewe kuomba lakini hazinitoshi mimi kutoa.” Hivyo kutoa ni moyo
vidole huachia. Uchoyo ni adui wa ukarimu. Mweheshimiwa Rais Mwai Kibaki alitoa
maneno ya hekima juu ya uchoyo. Alisema, “Uongozi ni fursa ya kuyaboresha
maisha ya wengine. Sio fursa ya kuridhisha uchoyo wa mtu.” Kusema kweli maneno
kwenye kanga au leso za wanawake yanasema, yote. Kula unibakizie. Ni ukarimu
kuwabakizia wengine. Uchoyo ni chanzo cha kuzika haki. Uchoyo hauna malipo.
Tambarare ya Unyenyekevu
Somo la unyenyekevu tunalipata
toka mahali pengi. Nyota hazilifuniki jua. Nyota hazishindani na mwanga wa jua.
Nyota zinatupa somo la unyenyekevu. “Unyenyekevu unamaanisha mambo mawili.
Kwanza, ni uwezo wa kujikosoa…Sifa ya pili ni kuwaruhusu wengine wang’ae,
kuwakubali wengine, kuwawezesha na kuwafanya wawe na uwezo,” alisema Cornel
West mwanafalsafa wa Amerika aliyezaliwa 1953. Kama ambavyo huwezi kuzuia nyota
sizing’ae hauwezi kuzuiwa using’ae ingawa unawezwa kucheleweshwa.
Kunyenyekea ni kumfanyia mtu
kitendo kinachoonyesha heshima kubwa. Ni kutii.Kadiri ya Kamusi ya Karne ya 21
nyenyekea maana yake ni kuwa mtiifu sana
kwa matarajio ya kupata kitu fulani. Unyenyekevu ni kukubali nafasi Mungu
aliyokupa iwe ya kiti cha mbele au ya kiti cha nyuma. Unyenyekevu una faida
nyingi. “Hakuna kitu kinachomweka mtu mbali na mkono wa shetani kama
unyenyekevu,” alisema Jonathan Edwards. Pia unyenyekevu huzaa fadhila nyingine.
“Unyenyekevu ni mzizi, mama, nesi, msingi, na kiungo cha fadhila zote,” alisema
Mtakatifu Yohane Chrysostom (347 – 407). Unyenyekevu unatambulika katika mambo
ya kila siku. Kufanya kazi ndogo ndogo kwa mtu mkubwa ni unyenyekevu. Balozi
toka nchi ya kigeni alimtembelea zamani Rais wa Amerika Abraham Lincoln
akamkuta anang’arisha viatu vyake. “Nini hii, Rais unapaka dawa viatu vyako
wewe mwenyewe?” Rais alimjibu, “Ndiyo, wewe huwa unapaka vya nani?” Zaidi ya
hayo kuwa tayari kushukuru ni ishara ya unyenyekevu. “Maneno nakushukuru ni
sala nzuri sana ambayo mtu yeyote anaweza kusali. Naisali sala hiyo mara
nyingi. Maneno nakushukuru yanabainisha shukrani isiyo na kifani, unyenyekevu
na kuelewa,” alisema Alice Walker mshairi wa Amerika aliyezaliwa mwaka 1944.
Yote yakishasemwa, nakubaliana na Mignon McLaughlin (1913 -1983) mwandishi wa
Amerika, aliyesema, “Mtu mwenye majivuno anaweza kujifunza unyenyekevu, lakini
atajivunia unyenyekevu huo.” La msingi nyenyekea ule vya Mungu. Upate neema ya
Mungu. Ili Mungu akuinue lazima kunyenyekea.