Jumapili ya 28 ya
Mwaka A
“Atayafuta machozi katika nyuso za watu wote na kuwaondolea watu wake
aibu duniani kote” (Isaya 25:8).
“Yesu ambaye
hakutoa machozi kamwe asingeweza kufuta machozi yangu,” alisema Mchungaji
Charles H. Spurgeon. Yesu anafuta machozi sababu naye alitoa machozi. Yesu
alimlilia Lazaro. Yesu aliilia Yerusalemu. Yesu alitokwa machozi Gethsamane. Yesu
Kristu tunayemfuata ni Bwana anayefuta machozi. Unabii wa Isaya unaweka hilo
wazi, “Atayafuta machozi katika nyuso za watu wote na kuwaondolea watu wake
aibu duniani kote” (Isaya 25:8). Yesu alifuta machozi ya Petro. Yesu alifuta
machozi ya waombolezaji. Yesu alifuta machozi ya jamaa zake Lazaro.
Mtakatifu Ambrose alisema, “Katika Kanisa kuna maji na
machozi: maji ya Ubatizo na machozi ya Kitubio.” Lakini kuna aina mbalimbali za
machozi. Kuna machozi ya kusingiziwa. Kuna machozi ya kurubuniwa. Kuna machozi
ya kufiwa. Kuna machozi ya mpendwa kuwa mbali. Kuna machozi ya kukataliwa. Kuna
machozi ya kutopata mchumba. Kuna machozi ya kutozaa. Kuna machozi ya kupoteza.
Kuna machozi ya ahadi zilizovunjwa. Kuna machozi ya kusemwa. Kuna machozi
kukata tamaa. Kuna machozi ya mateke ya shukrani ya Punda. Kuna methali
isemayo; “Ninaotibu vidole ni ndio wanaoiba viazi vyangu.” Nyingine inasema:
Nyuki anashukuriwa kwa kuchomwa moto. “Machozi ni maneno ambayo moyo huwezi
kueleza,” alisema Loretta Lynn. Mtu akishindwa kueleza huzuni kwa maneno
anaueleza kwa machozi. “Machozi ni lugha ya kimya ya huzuni,” alisema Voltaire.
Lakini Yesu anafuta machozi.
Kuna hadithi juu
ya Malaika aliyetumwa na Mungu kwenda duniani na kurudi na kitu cha thamani
kubwa. Aliruka kwenda chini duniani na kutafuta toka ncha moja hadi ncha
nyingine. Aliokota kipande cha dhahabu lakini aliona hakina uzuri wa kutosha
kwa ajili ya Mfalme. Aliona lulu isiyo na doa bado aliona haina uzuri wa
kutosha kwa ajili ya Mfalme. Malaika aliendelea kutafuta kila mahali. Hatimaye
alisijia mtu aliyetoa mguno wa kulia. Alikuwa ni mtu ambaye alikuwa amepiga
magoti anasali, akibwaga moyo wake kwa Mungu akiomba msaada na msamaha. Malaika
alijiambia, “Ee, ndiyo kitu chenyewe.” Malaika alimshika mkono mtu huyo na
kuweza kudaka chozi moja kati yam atone ya machozi yaliyokuwa yanabubujika. Alienda
mbinguni kwa moyo wa ushindi na kumkabidhi Mungu chozi akimwambia: “Chozi ni
jambo la thamani sana duniani.” Tumeona watu wengi wakibubujikwa machozi labda
tunafikiri ni kitu cha kawaida. Machozi ni lugha Mungu anayoelewa. Machozi yako
yamerokodiwa. Kumbukumbu ya machozi yako zimetunzwa.
Kuna watu ambao
wamekuwa na mvua za machozi. Hasira inaweza kugeuka machozi. Huzuni unaweza
kugeuka machozi. Kuna ambao wana machozi lakini wanayaficha. “Nilimdanganya
kila mtu kwa tabasamu langu kubwa kwa miaka na miaka. Sikumwonesha mtu yeyote
machozi yangu,” alisema Francine Chiar.
Namna gani
atafuta machozi? Ataondoa kifuniko cha uchungu kwenye macho ya akili.
“Ataliondoa wingu la huzuni lililowafunika watu wote, kifuniko cha uchungu juu
ya mataifa yote” (Isaya 25: 7). Yesu ataondoa pazia kwenye macho ya akili.
Ingawa tunasema macho hayana pazia, macho ya akili yanaweza kuwa na pazia. Kuna
vitu ambavyo labda hauelewi. Tunasema, “La kuvunda halina ubani.” Yesu anaondoa
kifuniko kwenye macho yetu ya akili. La kuvunda lina ubani. Alimfufua Lazaro.
Unasema, “Kwa nini mimi Mungu?” Yesu anaondoa kifuniko kwenye macho yako ya
akili. Katika maisha yake utagundua kuwa “Hakuna Jumapili ya Paska” bila
“Ijumaa Kuu.”Namna hiyo anafuta machozi.
Kama umepoteza jamaa yako Yesu atafuta
machozi. Namna gani? Tajiri mmoja mwenye pesa kama serikali alikuwa na shamba
kubwa na zuri la maua.
Alilikabidhi kwa mtu mwingine alitunze aliyependa maua
na alifahamu aina mbalimbali za maua.
Ilikuwa ni furaha ya mtu huyu kumwagilia miche ya maua
wakati wa ukame, kuweka fito za kutumika kama
mihimili ya mashina laini, kukinga mimea dhidi ya upepo na baridi na dhidi ya
wadudu na wanyama wahaaribifu. Asubuhi moja mtunza bustani aliamka na shauku
isiyokuwa ya kawaida. Baadhi ya maua yake mazuri
yalikuwa yamekaribia kutoa maua.
Alitegemea kuwa yatakuwa katika hali nzuri yakiwa kamili. Kwa mshangao
unaohumiza aligundua kuwa moja ya maua
yake mazuri limechumwa kutoka kwenye shina lake. Akijaa hasira na masikitiko
aliwaendea wafanyakazi wengine kwenye shamba, akitaka kujua aliyemwibia hazina
yake. Aliwapitia mmoja baada ya mwingine kila mmoja akisema kuwa hana hatia, na
aliwaamini. Hata hivyo moyo wake ulikuwa na masikitiko kwa kupoteza au lake zuri.
Hatimaye mmoja wa wahudumu alimpa angalisho: “Nilimuona Bwana wa Shamba
akitembea asubuhi hii katika bustani ya maua.
Nilimuona akichuma ua na kulibandika kwa
pini kwenye koti lake. Mtunza bustani ya maua
alipata liwazo kusikia kuwa Bwana wa Shamba ndiye amechuma ua. Alifurahi
kusikia kuwa Bwana amependezwa na hilo
ua. Alitabasamu kisirisiri kwa kulipoteza akijua kuwa limempendeza Bwana.
Waliotutoka ni maua
yaliyompendeza Bwana. Tunasoma katika kitabu cha ufunuo, “Andika! Heri watu
ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana. Naye Roho asema ‘Naam!
Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata” (Ufunuo
14: 13).
Kulia na kutoa
machozi kunategemea unatazamaje mambo? Kuna mtoto ambaye alipoteza shilingi mia
moja. Mzee mmoja alimkuta akilia barabarani. Alimuuliza, “Kwa nini unalia?”
Mtoto huyo alisema, “Nimepoteza shilingi mia moja.” Mzee huyo akatoa shilingi
mia moja na kumpa. Jambo la kushangaza mtoto aliendelea kulia sana na kupiga moyowe. Mzee akashangaa na
kumuuliza, “Mbona baada ya kukupa shilingi mia moja umelia sana.” Mtoto akasema, “Sasa hivi ningekuwa
nimefikisha shilingi mia mbili.” Mtoto huyu alikuwa na shida ya uchoyo. Penye
kilio sababu ya uchoyo Yesu anafuta machozi akipendekeza kutupilia mbali uchoyo
na kugawana. Alisema nilikuwa na kiu ukanipa maji ya kunywa, nilikuwa na njaa,
ukanilisha.
Machozi ya toba
Mtakatifu Ambrose alisema, “Katika Kanisa kuna maji na
machozi: maji ya Ubatizo na machozi ya Kitubio.” Kutubu ni kudondosha machozi
ya toba. Mtakatifu Petro alipotubu alitokwa na mchozi ya toba (Luka 22: 61).
Katika Injili ya Marko tunaambiwa, “Tubuni na kuiamini Habari Njema” (Marko 1:
15). Kutubu ni kubadili mwelekeo na uelekeo, njia na dira, msimamo na mtazamo.
Kubadili mwelekeo kunaendana na maumivu kiasi cha kutoa machozi ya toba. Kutubu
ni kuikimbia dhambi. Nilimuuliza Mkristu mmoja baada ya kuungama dhambi, “Sasa
unajionaje?” Aliniambia, “Padre kabla ya kuungama dhambi nilikuwa mdhambi
anayeikimbilia dhambi, sasa ninaikimbia dhambi.” Kutubu ni kuikimbia dhambi na
kumkimbilia Yesu Kristo. Tunaambiwa, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu
umekaribia” (Marko 1: 15). Yesu ni ufalme wa Mungu wenyewe. Yuko karibu kama mdomo na pua.
Tulie na
Wanaolia
“Wale ambao
hawajateseka hawajui mateso ya wengine,” ndivyo isemavyo methali ya Haiti.
Kuna watu wanaoteseka wanahitaji kuwafariji. Wakimbizi wanateseka wanahitaji
kuliliwa. Wasio na makazi wanateseka wanahitaji wa kuwalilia. Kwa kawaida jicho
moja likiingiwa na mchanga linajililia lenyewe jicho la pili halilii. Binadamu
hatuna budi kuwa kinyume na jicho hili.
Hatuwezi kusema kila jicho lijililie lenyewe. Ndio maana mtume Paulo anatuasa,
“Lieni pamoja nao waliao.” (Warumi 12:15) Yesu mwenyewe alilia na waliomlilia
Lazarus. “Basi Yesu alipomwona analia, na wale wayahudi waliofutana naye
wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, akasema, “Mmemweka wapi?
Wakamwambia, ‘Bwana, njoo utazame.’ Yesu akalia machozi.” (Yohane 11: 33-35)
Yesu hakulia tu machozi alitoa msaada.
Kuna watu ambao
wanabeba misalaba ya chuma ambayo siyo ya kujitakia yaani mateso makubwa
maishani. Kuna ambao wanabeba misalaba ya kijitakia mfano kuna kijana wa miaka
thelathini aliyemua baba yake na mama yake. Baada ya kutolewa hukumu aliulizwa
kujitetea. Akasema naomba mnipunguzie miaka maana mimi ni mwana yatima sina baba sina mama. Huu ni msalaba wa kujitakia sio kwa
sababu ya Yesu.
Kuna watu ambao
wanapata mateso juu ya mateso tulie nao. Yaani tuwafariji na kuwasaidia. Kuna
ambao wanakwepa mvua lakini wanaagukia mtoni. Tufarijianeni. Watu wengi wana
matatizo. Watu wasio na matitizo ni wale waliozikwa makaburini. Kulia na
wanaolia ina maana ya kujiweka katika nafasi ya wenye matatizo, kuingia katika
viatu vyao na kufikiria kama ingekuwa wewe. Licha ya hayo machozi yana nguvu.
Kulia na wanaolia ni namna ya kuwafariji wanaolia. Kuna ambao wanabeba misalaba
ya kutukanwa na kudharauliwa. “Vidonda vya maneno ni vibaya sana kuliko vidonda vya upanga.” Methali ya
Kiarabu Tusiwadharau watu na kuwatukana kwa vile wanatoka kabila fulani au eneo
fulani. Badala ya kuwatukana tuwasaidie.
Katika maisha ya
kawaida ya kila siku mtoto wakati mwingine huwasiliana kwa kulia. Machozi yana
nguvu. Mtoto anayelia huwafanya wazazi wajiulize kuna jambo gani? Penye shida
mtoto husaidiwa. Hiyo ni nguvu ya machozi. Mzee Mwambarikutu aliulizwa, “Nguvu gani katika dunia hii ilikufanya
umrudie mke wako wakati watu wote walijua mke wako alikuwa amekukosea,”
Alijibu, “Nguvu ya machozi – sikuweza kuvumilia kulia kwake.” Machozi yana
nguvu. Hata maji yakimwagika yanaweza kuzoeleka kama
kuna wanaokulilia yaani wanaokuonea huruma na kutafuta suluhisho. Ili maji yazoeleke lazima pawepo na “Kulia na wanaolia.” Lazima
watu wakulilie yaani wakuonee huruma na kukusaidia ambapo hauwezi kujisaidia
mwenyewe.
Unahitaji
washauri na wafariji wenye nguvu na sio duni. Ayubu aliwaambia marafiki zake
wafariji duni “Mambo kama hayo nimeyasikia
mengi: nyinyi ni wafariji duni kabisa!” (Ayubu: 16:2.) Mfalme Daudi katika
Biblia alikumbana na washauri duni na wafariji duni: “Wanitembeleapo husema
maneno matupu; wanakusanya mabaya juu yangu, na wafikapo nje huwatangazia
wengine. Wote wanichukiao hunong’onezana juu yangu; wananiwazia mabaya ya
kunidhuru. Husema: “Maradhi haya yatamuua; hatatoka tena kitandani mwake!” Hata
rafiki yangu wa moyo niliyemwamini, rafiki ambaye alishiriki chakula changu,
amegeuka kunishambulia!” (Zaburi 41: 6 -9)
Fariji kwa Kutumia Tiba ya Kuongea
Kuongea ni tiba.
Kama una sononokeko na simanzi kuongea ni
tiba. Kama una mfadhaiko kuongea ni tiba.
Muulize mtu maswali ambayo hayambani mtu kutoa jibu la ndoa au hapana bali
kuelezea. Kuna mitume wawili waliokuwa wanaenda Emmaus walikuwa wamekata tamaa.
Yesu aliwauliza maswali mawili yanayohitaji majibu marefu ili waongee. Swali la
Kwanza: “Mnazungumza nini huku mnatembea?” (Lk
24: 17). Swali la Pili: “Mambo gani?” (Lk 24: 19) Mitume hawa walikuwa wenye
huzuni. Yesu aliwatia moyo waongee. Kuongea ni tiba na kutia mtu moyo aongee
kunahitaji ufundi katika kuuliza maswali. Yesu alifuta machozi ya wafuasi wa
Emmaus atafuta ya kwako.
Mfariji mwenye
nguvu anayekulilia, atakukumbuka, akiwa na uwezo atakusaidia. “Kristu alilia: binadamu ajililie mwenyewe.
Kwa nini Kristu alilia, alitaka kuwafundisha watu kulia,” alisema Augustini wa
Hippo aliyeishi karne ya tano huko Afrika ya Kaskazini. Nasi hatuna budi kulia. Tulie kwa sababu ya
makosa yetu. Hapa tutoe machozi ya toba kama
Simon Petro. “Bwana akageuka na
kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: “Leo
kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Hapo akatoka nje, akalia sana.” (Luka 22: 61-62)
Petro alijutia mabaya aliyomtendea Yesu kwa kumkana. Alitoa machozi ya toba.
Tujutie mabaya tuliowatendea wengine kwa kutoa machozi ya toba. Toba ni majuto
kwa kutenda maovu.
WASIFU WA MACHOZI
- Machozi ni kiona mbali: “Machozi mara nyingi ni kiona mbali ambacho kwacho watu huona mbali mbinguni,” alisema Henry Beecher.
- Machozi ni Lugha ya huzuni: “Machozi ni maneno ambayo moyo huwezi kueleza,” alisema Loretta Lynn.
- Ni sabuni ya maono: “Labda macho yetu yanahitaji kuoshwa na machozi mara moja moja ili tuyaone maisha kwa muono unaonekana vizuri zaidi,” alisema Alex Tan.
- Ni nyenzo ya makuzi na kusafisha: “Wakati mwingine lazima tuhumie ili tuweze kukua, lazima tushindwe ili kujua, wakati mwingine maono yetu yanaonekana baada tu ya macho yetu kusafishwa na machozi,” alisema Aaron Chan.