JUMAPILI YA 26 YA MWAKA A
1. Ezekieli 18: 25 -28
|
2. Wafilipi 2: 1-11au Wafilipi 2: 1-5
|
3. Mathayo
21: 28 -32
|
UTANGULIZI
Matendo yanapozungumza maneno si kitu. Sisi tunajiendesha kama
watoto. Tunasema ndiyo, lakini hatufanyi
kitu, pengine tunakataa kwanza na baadaye tunajuta na kutimiza tunayoambiwa. Tumuombe
Mungu katika adhimisho la leo atuepushe na mazoea ya kutamka maneno ya ndiyo
ndiyo bila kutimiza kwa matendo.
MAHUBIRI YENYEWE
Mgeni mmoja alitembelea
nchi ya Poland enzi za ukomunisti. Alioneshwa maeneo mengi na mwanachama
wa chama tawala. Mgeni alimuuliza mwanachama huyo, “Je, wewe ni mkatoliki?”
Mwanachama huyo alijibu, “Naamini lakini sitendi.” Mgeni baadaye alimuuliza,
“Je, wewe ni mkomunisti?” Ofisa huyo alitabasamu na kujibu, “Natenda, lakini
siamini.” Dini ya Kikristu inawadai wanachama wake kusema na kutenda yaani
kuhubiri maji na kunywa maji na si kuhubiri maji na kunywa divai. “Jibu
fupi ni kutenda,” alisema Lord Herbert. Ahadi ni mawingu kutumiza ahadi ni mvua.
Haitoshi kuahidi lazima kutenda. “Tendo
ni lugha ya kushawishi,” alisema William Shakespeare.
Neno zuri ni zuri, tendo zuri ni
zuri zaidi. Kwa msingi huo matendo yana kauli kuliko maneno. Maneno matupu
hayajengi ghorofa. Si kwa kusema asali asali utamu unaingia mdomoni. Utukufu
hauji kwa kuuita. Ni methali ya Kenya. Matendo yanapozungumza maneno si kitu. Kuna
methali ya Kiafrika isemayo, “Sikusikii matendo yako yananipigia kelele.” Kwa
matendo yake tunamjua mtu. Watu wote wanaweza kuzungumza lakini si watu wote
wanaweza kutenda. “Neema haitolewi kwa wale ambao huzungumzia juu ya imani yao
lakini kwa wale ambao wanaishi imani yao,” alisema Mt. Gregory.
Injili ya leo inatupa umuhimu wa
matendo. Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, ‘Mwanangu,
leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu,’ Akajibu akasema, ‘Naenda,
Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vilevile. Naye akajibu
akasema, ‘Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je, katika hao wawili ni yupi
aliyefanya mapenzi ya babaye?” Wakamwambia, “Ni yule wa pili.” Basi Yesu
akawaambia, “Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu
kuingia katika ufalme wa Mungu” (Mathayo 21: 28 – 31). “Tunachoweza kujifunza
katika mfano huu Bwana aliwazungumzia wale ambao wanaahidi kidogo au hawaahidi
chochote lakini katika matendo wanafanya makubwa na dhidi ya wale ambao
wanaahidi makubwa lakini hawafanyi lolote kati ya wale ambao wameaahidi,” alisema Origen Baba wa Kanisa.
Baba wa Kanisa Jerome alikuwa na
haya ya kusema, “Mungu anazungumza kwanza kwa watu wa mataifa kupitia kanuni ya
maumbile; ‘Nenda kafanye kazi katika shamba langu la mizabibu;’ ni kusema, ‘Mtendee
mwenzako kama unavyotaka akutendee’ (Tobiti 4:16). Alijibu kwa majivuno , ‘Sitaki.’
Kumbe aliyesema nitaenda baadaye akwenda
ni wayahudi wasio waaminifu. Mzabibu ni taifa teule la Israeli (Isa 5:1).
Mwenye shamba ni Mungu. Watumwa wake ndio manabii. Mwanae ndiye Yesu. Wakulima
wauaji ndiyo wayahudi wasio waaminifu. Watu wengine watakaoaminishwa shamba la
mizabibu ni watu wa mataifa yaani wapagani.
Mfano huu ni mfano juu ya watoto
wabaya wawili. Ni mtoto yupi kati ya hao wawili angekuwa mtoto wa kuigwa au
mfano wa kuigwa? Yule anayesema hapana ya herufi kubwa mbele ya baba yake au
yule anayesema ndiyo. Jibu ni kuwa hayupo hata mmoja wa kuigwa. Mtoto ambaye ni
mfano wa kuigwa ni yule anayesema ndiyo na kuweka katika matendo. Yesu alisema:
“Si kila mtu aniambiaye :Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni,
bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21).
Maneno “umefanya vizuri” ni
mazuri zaidi kuliko maneno “umesema vizuri.” Ni maneno ya Benjamini
Franklin (1709-1790) mmojawapo wa Waasisi wa Amerika, mwandishi na
mwanadiplomasia. Mwanasiasa huyu alitaka kusema matendo yana kauli kuzidi
maneno. Maneno haya yanabainisha maana ya methali au msemo wa Kenya: Kusema na
kutenda. Haitoshi kusema kunahitajika kutenda pia. “Muwe watimizaji wa
neno, si wasikiaji tu; kama sivyo, mnajidanganya wenyewe” (Yakobo 1:22). Dini
ni ya matendo.
Haitoshi kusema tu lazima
tutende. Kunda kijana aliyemtumia mchumba wake ujumbe wa simu wenye maneno
haya: “Nakupenda sana kiasi cha kupanda mlima mrefu kwa ajili yako. Nakupenda
sana kiasi cha kuweza kuogelea kwenye mto TANA kwa ajili yako. Ninaweza kupitia
katikati ya moto kwa ajili yako. Naweza kunyeshewa mvua kwa ajili yako. Naomba
tukutane kesho saa nane kama mvua haitanyesha.” Maneno hayo ni mazuri lakini ni
maneno matupu bila matendo. Kwa nini baadaye kijana anaogopa mvua.
Wanandoa siku ya kufunga ndoa wanaulizwa juu ya
upendo: Padre kwanza anamuuliza Bwana arusi: F. unampokea F. awe mke wako, tena
waahidi kuwa mwaminifu kwake, katika taabu na raha, katika magonjwa na afya,
umpende na kumheshimu siku zote za maisha yako?” Kisha padre anamuuliza bibi
arusi; F. unampokea F. awe mume wako, tena waahidi kuwa mwaminifu kwake, katika
taabu na raha, katika magonjwa na afya, umpende na kumheshimu siku zote za
maisha yako?” Jibu ambalo hutolewa huwa ndiyo. Hiyo ni kusema kunabaki kutenda.
Ukisema mimi ni “memba” au muumini wa Kanisa. Jambo
hilo liweke katika matendo. “Memba” au mwenye hisa ni mmojawapo wa wamiliki wa
kampuni au chama. Wewe kama ni “memba” jua Kanisa ni lako. Jenga chako. Lakini
“Asiyekujua hakuthamini.” Lijue Kanisa. Kanisa lina mafiga matatu: padre, mtawa
na mlei. Mafiga mawili hayaivishi chungu. Kazi yote hawezi kuaachiwa padre na
mtawa. Mafiga mawili hayaivishi chungu. Mlei ujue Kanisa ni lako. Mtawa ujue
Kanisa ni lako. Padre ujue Kanisa ni lako.
Ukiimba wimbo wa “Mkristu miye niko salama…” Wimbo
huo ukauweke katika matendo. Lisaidie Kanisa. Shilingi moja na shilingi mia
moja zilikuwa na mazungumzo. Shilingi moja iliuliza, “Wewe shilingi elfu moja
ya Kenya (17,000/= Tshs) umetembelea sehemu zipi?” Shilingi mia moja ya Kenya
ilijibu, “Nimetembelea mabenki yote. Nimekuwa sehemu za starehe zote, hoteli
kubwa kubwa, nimekukaa sana supermarket, nimelala mara nyingi Dubai, China. Jew
ewe shilingi moja unakaa wapi?” Shinlingi moja ilijibu. “Mimi nitafute kwenye
makanisa ya Kanisa la Peter Claver, Consolata, Yohane Mbatizaji.” Ukristo ni
matendo. LISAIDIE KANISA LIKUSAIDIE. Kama unajiita mkristu lazima kuhudhuria
vikao, adhimisho la ibada ya misa, mikutano ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu.
“Watu wangapi wanahudhuria katika Kanisa lako?” Mchungaji mmoja alimuuliza
mwingine.” Mchungaji alifikiria kidogo halafu alijibu, “60 wapo kila mara, 250
C na E.” “Nini maana ya C na E?” Mchungaji alitaka kujua. “Maana yake ni
Christmasi na ‘Easter” yaaani Paska.
Kupenda ni kitenzi. Upendo ukibaki ni nomino ni
nomino dhahania. Upendo husipotolewa hudumaa na ukitolewa unakua. Tutoe upendo
kwa waliotuzunguka baadaye upendo upae kuwaendea wengine. Kuna mtoto
aliyemuuliza mama yake, “Tupo hapa duniani kwa ajili ya nini?” Mama alimjibu,
“Tupo hapa kwa ajili ya kuwapenda wengine.” Na mtoto akazidi kudadisi, “
Wengine wapo kwa ajili ya nini?” Kuna watu wanafikiri wapo kwa ajili ya
kupendwa na si kupenda. Mungu ametuumba kwa ajili ya kupenda na kupendwa.
Upendo ambao haujawekwa katika vitendo ni kama ujumbe wa simu ulioandikwa
lakini ukasahau kuutuma. Ni kama barua ambayo umeandika ukasahau kuipeleka
posta. Upendo ukibaki ni jina tu au nomino tu ni nomino dhahania lakini lazima
uwe kitenzi-kupenda ni kitenzi.