JUMAPILI
YA MSAMARIA MWEMA
Jumapili ya 23 ya Mwaka A
1. Ezekieli 33: 7-9
|
2. Woroma 13: 8-10
|
3. Mathayo 18:
15-20
|
“Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana…Mpende jirani
yako kama nafsi yako…” (Woroma 13: 8-10)
Mama anayenyonyesha mtoto akiamua
kunyonya titi lake mwenyewe na kunywa maziwa ya mtoto jambo hilo halikubaliki.
Ni kujipendelea. Mama huyo amejipenda kupita mipaka ya kujipenda. Jambo la msingi
ujipende lakini usijipendelee. Kumsaidia mtu hakumaanishi kutojijali au
kutojitunza. Anayejihukumu husema yeye ni mzuri wa sura. Hizo ni methali za
Afrika ambazo zinasisitiza umuhimu wa kujipenda. Inashangaza kuona kuwa fundi
seremala licha ya kutengeneza viti vya kukalia yeye hana kiti hata kimoja
nyumbani. Huyo hajipendi. Mtengeneza vyungu vya udongo vya kupikia yeye anakula
chakula kutumia kipande cha chungu kilichovunjika. Huyo hajipendi. Itashangaza
kuona kuwa mjenzi wa nyumba nzuri sana yeye ana nyumba ya makuti ambayo inaweza
kuanguka wakati wowote.
Jambo la katikati ni
kujipenda. Jambo baya kulia kabisa ni kujipendelea, uchoyo, ubinafsi na umimi.
Ni kujipendelea kupita kiasi. Jambo baya kushoto kabisa ni kutojipenda,
kutojijali, kutojitunza. Kujipendelea ni kujifikiria wewe mwenyewe tu.
Kutojipenda ni kujipunguzia heshima au hadhi. Kutojipenda ni kujidhalilisha.
Mtu ambaye hajipendi ni mtu ambaye anajidanganya yeye mwenyewe.
Kuna methali isemayo: Watu
wanajilamba vidole (sababu ya kutoshiba) wewe unasema mbwa wangu aitwaye simba
hajala. Ni methali ambayo inaelimisha umuhimu wa kumtanguliza kwanza binadamu
mwenye shida kama mwenye njaa. Njaa ina matokeo mabaya mengi. Mtu mwenye njaa
ni mtu mwenye hasira. Ni methali yaw a Igbo wa Nigeria. Utamu haumalizi njaa.
Ni methali ya Kenya. Kuna mwanaume mmoja alimwambia mke wake: Haupiki chakula
kizuri kama mama yangu.” Naye mwanamke alijibu: “hauna fedha kama baba yangu.”
Anayepika vizuri anapika alivyoletewa. Pengine chanzo cha ugomvi huo ni njaa.
Ni mtu mbaya ambaye ni mzuri tu
kwa ajili yake tu. Ni ujumbe ambao tunaupata kutoka katika methali ya Haiti
isemayo: wewe ni mbaya, kama ni mzuri kwa ajili ya nafsi yako tu. Methali hii
inambainisha mtu anayejipendelea. Hatuna budi kujipenda. Kumsaidia mtu hakumaanishi
kutojijali. Ni methali ya Mamprussi. Wakati kuna watu wanakula na kusaza kuna
ambao wanalala usiku wakiwa na matumbo matupu. “Njaa ni aibu kubwa katika dunia
ya leo,” alisema Baba Mtakatifu Yohani Paulo wa II. Biblia yasema “Msiwiwe na
mtu chochote, isipokuwa kupendana…Mpende jirani yako kama nafsi yako…” (Woroma
13: 8-10). Tuna deni la kuwalisha wenye njaa. Kuwalisha wenye njaa ni
kuwapenda. Baba Mtakatifu Francis, siku ya kuzindua kampeni dhidi ya njaa
duniani tarehe 10/12/2013 alisema hivi: “Naalika taasisi zote ulimwenguni,
makanisa na kila mtu mmoja, kama familia moja, kuzungumza kwa sauti kuwatetea
wale wote wanaoteseka kimya kimy kwa NJAA, ili sauti yetu kubwa iwe kishindo
kinachoweza kuutikisa ulimwengu.” Kadiri ya tafiti zilizofanyika, njaa inaua
mtu mmoja kila sekunde tano duniani.
Ulimwengu una mali za kumtosha
kila mtu, lakini hauna mali za kuwatosha wanaojipendelea. Ni katika mtazamo huo
naweza kusema ulimwengu una chakula cha kumtosha kila mtu lakini hauna chakula
cha kuwatosha wanaojipendelea. Naye Baba Mtakatifu Francis amekuwa na haya ya
kusema: “Ni jambo la kuiabisha na kuleta huzuni kubwa kufahamu kwamba watu
wengi duniani wanateseka kwa njaa wakati ulimwengu unacho chakula cha
kutosheleza kulisha kila mtu. Hali ya watu kutokuwa na nafasi sawa ya kupata
chakula ndiyo kiini cha janga la njaa duniani. Hali hii inazidi kuwa mbaya
wakati mashirika makubwa yanapoficha chakula ili kipande bei, kuhamasisha
ukulima wa mazao ya kuzalisha nguvu za kuendesha mitambo ya machine kama ‘jatorpher,’
utupaji wa chakula kinachofaa kwa matumizi ya binadamu na ugumu wa kufikia
masoko. Haki ya kupata chakula inalinda haki ya msingi ya binadamu ya kutokuwa
na njaa.”
Bwana Yesu alipofanya muujiza wa kuongeza
mikate mitano na samaki wawili na kulisha umati wa watu zaidi ya elfu tano watu
waliposhiba aliwaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee
bure.” Maneno hayo ni changamoto kwetu kukusanya chakula kinachobaki kisipotee
bure maana kuna ambao wanaenda vitandani matumbo matupu.
Nakumbuka sala ya mkristu moja
nilipoalikwa katika sherehe ya kuanza
mwaka mpya. Chakula kilikuwa kingi na cha kila aina, yaani meza ilikuwa
imechafuka. Mwenyeji wetu alisali hivi, “Baba wa Mbinguni nakushukuru kwa mambo
matatu:chakula, hamu ya kula, na watu wakula chakula hiki. Kuna watu wenye hamu
ya kula lakini hawana chakula, kuna ambao wana chakula lakini hawana hamu ya
kula, kuna ambao wana chakula na hamu ya kula lakini hawana watu wa kula
chakula…”Walioathirika na baa la njaa wana hamu ya chakula na watu wa kula
chakula lakini shida ni uhaba wa chakula. Unapowasaidia wenye njaa unajipenda
maana unajiwekea pointi mbinguni. Unaposhindwa kuwasaidia wenye njaa
unajipendelea.
“Si rahisi kuzungumzia amani pale
ambapo watu wanateseka kwa sababu ya njaa,” alisema Papa Benedict XVI wakati
pia akishutumu wingi wa fedha unaotumika katika kununulia silaha. Ujumbe huu
Baba Mtakatifu aliutoa alipozungumza na maafisa wa ubalozi siku ya Jumatatu
tarehe 9 mwezi wa Januari 2006.
TUMEUMBWA KUPENDA NA KUPENDWA
Mtu anaweza kulipa deni la dhahabu, lakini mtu
huyo atakufa akiwa katika deni la upendo milele yote. Ndivyo isemavyo methali
ya Malaya. Ukiwa unadaiwa shilingi elfu kumi unaweza kulipa lakini sio rahisi
kulipa deni la upendo la mke wako, baba yako, mama yako, mme wako, mtoto wako
au mfadhili wako. Licha ya ukweli huo
tumeumbwa kupenda na kupendwa. Katika Biblia tuna amri mbili za upendo. Amri ya
kwanza ya upendo ni: Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa akili zako
zote na kwa roho yako yote. Na amri ya
pili ya upendo ni mpende jirani yako kama unavyojipenda (Mathayo 22: 34 -40).
Usipopenda unakuwa haujatimiza mojawapo la
lengo la kuumbwa kwako. Kama kitabu hakiwezi kusomwa au kosomeka hakijatimiza
lengo la kuandikwa kwake. Kama kengele haitoi sauti inapogongwa imeshindwa
kufukia malengo ya kutengenezwa kwake. Kama chakula hakiwezi kuliwa au hakiliki
hakijafikia lengo la kupikwa kwake. Hivyo hivyo kama binadamu hawezi kupenda na
kupendwa ameshindwa kufikia lengo la kuumbwa kwake.
Hasiyekujua hakuthamini. Hatuwezi
kumpenda Mungu kama hatumjui. Tunamjua Mungu kupitia mambo mengi. Tukisoma
vitabu vitakatifu tunamjua Mungu. Hauwezi kumpenda jirani yako kama haumjui.
Asiyekujua hakuthamini. Kuna mtu aliyeaniambia, “Padre usinitambulishe kwa huyo
jamaa. Maana nataka kuendelea kumchukia. Nikimjua nitampenda.” Nilichukua
nafasi hiyo kuelezea athari na matokeo ya chuki. Chuki humchoma anayeitunza.
Ukimjua Mungu utampenda. Kuna
fundi aliyekuwa juu sana ya jengo alitaka mafundi chini wampandishie matofari.
Alitupa chini shilingi ishirini toka juu. Fundi aliyekuwa chini aliokota pesa
hiyo na kuweka mfukoni hakutazama juu. Alitupa tena “mbao,” fundi mwingine
akaiokota bila kutazama juu. Baadaye alitupa jiwe dogo likamgonga fundi mmoja
chini. Fundi huyo alitazama juu kwa vile alihumizwa kidogo. Mungu anaweza
kutuletea mateso kwa vile anataka kututumia ujumbe Fulani. Mateso hayo yanaweza
kuwa ni alama ya upendo. Mama umunywesha mtoto wake dawa chungu ili apone kwa sababu
anampenda mtoto wake. Tukijua kuwa Mungu wetu ni Mungu wa namna hiyo
tutampenda.
Amri ya pili ya upendo inasema,
“Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Ni lazima kujipenda na sio kujipendelea
ili uweze kuwapenda wengine kama unavyojipenda. Kula chakula ni kujipenda
lakini kula robo tatu ya chakula na kumwachia mwenzako aliye na tumbo kama wewe
na hamu kama wewe robo tu ya chakula ni kujipendelea. Kuwa na ardhi ni
kujipenda, lakini kuwa na ardhi kama jimbo zima la uchaguzi ni kujipendelea.