JUMAPILI YA 21 YA MWAKA A
1. Isaya 22: 19 – 23
|
2. Warumi 11: 33 – 36
|
3. Mathayo 16: 13 – 20
|
Aliwauliza
wanafunzi wake, ‘Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?’ “Kristu aliwauliza swali hili wafuasi wake ili katika majibu yao
tujifunze kuwa wakati huo kati ya wayahudi yalikuwepo maoni mbalimbali juu ya
Kristo; na mwishowe tufanye utafiti watu wana maoni gani juu yetu; wakitusema
vibaya tupuzie; wakitusema vizuri tujiongezee fursa hizo,” alisema Origen Baba wa Kanisa.
Uwezi kuwazuia
ndege wa mateso wasiruke juu ya kichwa chako, lakini unaweza kuwazuia wasijenge
viota kwenye nywele zako. Ni methali ya Kichina. Watu watakusema. Si rahisi
kuzuia hilo. Kama unafanya mambo mazuri usiyumbishwe na wanayosema juu yako.
Usikubali ndege wajenge viota kichwani mwako. Nakubaliana na Askofu Mkuu
Desmond Tutu wa Afrika ya Kusini aliyesema: “Mungu amekuita akijua wewe ni
nani. Anakutaka ulivyo wewe na upekee wako. Usikubali wengine wakubadili.” Kuna aliyekuwa kwenye tamasha anasikiliza
wimbo alikuwa na bwana mmoja wanazungumza. Akamwambia bwana huyo: “Mwanamama
anayeimba hana sauti nzuri sijui ni mke wa nani?” Akajibiwa. Ni mke wangu.
Bwana huyo akasema: “Nlitaka kusema aliyetunga wimbo huo alitunga wimbo mbaya
sijui ni nani?” Bwana huyo alijibu: “Ni mimi.” Mfano huu unaonesha huwezi
kuwazuia watu kusema.
Wakikusema
vibaya tumia maneno wanayosema kama mawe ya kuvukia. “Mtu aliyefanikiwa ni yule
ambaye anaweza kujenga msingi imara akitumia matofari waliomrushia,” alisema
David Brinkley (1920 – 2003) mtangazaji wa habari wa Amerika. Yatumie maneno wanayokusema kama mawe ya
kuvukia. Stephen Arnold Douglas (1813 – 1861) mwanasiasa wa Amerika katika
kampeini za kuwania urais wa Amerika mwaka 1858 katika mchuano mkali na Abraham
Lincoln (1809 – 1865) aliwaambia wapiga kura kuwa wasimchague Abraham Lincoln
kwa vile alikuwa na kilabu ya kuuza pombe kali. Naye Abraham Lincoln aliwaambia
wapiga kura kuwa ni kweli na mteja wake mkubwa alikuwa Douglas, yeye aliacha
shughuli ya kuuza pombe kali lakini Douglas hakuacha shughuli ya kuwa mteja.
Abraham Lincoln aliyatumia maneno aliyorushiwa kama matofari ya kujengea msingi
wa kukubalika kwa wapiga kura.
Katika maisha
utasemwa. “Ili kukwepa kusemwa usiseme lolote, usifanye lolote, usiwe yeyote,”
alisema Aristotle. Yesu alijua kuwa watu walimsema. Kuna siku alitaka kujua
maoni ya watu juu yake: “Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza
wanafunzi wake, ‘Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?’ Wakamjibu, “Wengine
wanasema kuwa ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia, wengine Yeremia au mmojawapo
wa manabii.’ Yesu akawauliza, ‘Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?’ Simoni
Petro akajibu, ‘Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.’ (Mathayo 16:13-16).
Yesu hakuuliza mafarisayo na wanasheria wanasema mimi ni nani? Hakuuliza
makuhani na walawi wanasemaje? Alitaka kujua watu wa kawaida wanasemaje.
Mafarisayo na wanasheria walisema ni mlafi kwa vile anakula na kunywa na watoza
ushuru. Mafarisayo na wanasheria walisema anatumtumia Beelzebub mkuu wa pepo
wabaya.
Licha ya kusemwa
hivyo Yesu alizidi kuimarika. “Watu
wanaotusema vibaya wanatuimarisha. Hofu zetu zinatufanya tuwe jasiri.
Wanaotuchukia wanatufanya tuwe na busara. Adui wetu wanatufanya tusibweteke.
Vikwazo vyetu vinatufanya tuwe na shauku. Tulivyovipoteza vinatutajirisha. Maudhi
yetu yanatufanya tupandishwe hadhi. Hazina zetu zisizoonekana zinatupa amani
inayojulikana. Lolote lililopangwa dhidi yetu litafanya kazi kwa ajili yetu,”
alisema Israelmore Ayivor
Watu wanasema
wewe ni mkristu wa aina gani. Kuna aina mbali mbali za wakristu. Kuna wakristu
wanaoitwa: “Nguzo.” Hawa wanakuja Kanisani kila siku, nakutoa sadaka. Kuna
wakristu wanaoitwa “Wachangiaji.” Hawa wanatoa pesa kama wanampenda mchungaji
na mtunza pesa. Kuna wakristu wanaoitwa: “Waegemeaji.” Hawa wanafanya kazi lakini hawatoi chochote.
Kuna wakristu wanaoitwa: “Watu wa Kila mwaka.” Hawa wanakuja Krismasi na
Pasaka. Kuna Wakristu wanaoitwa: “Watu wa pekee.” Hawa wanasaidia na kutoa kila
mara. Kuna wakristu wanaoitwa: “Sponji.” Hawa wanachukua baraka zote na huduma
lakini hawasaidii. Kuna wakristu wanaoitwa: “Watembezi.” Hawa wanatoka Kanisa hili
na kwenda Kanisa lingine na hawasaidii. Kuna wakristu wanaoitwa: “Wambea.” Hawa wanawesengenya watu wote isipokuwa Yesu
Kristu. Kuna wakristu wanaoitwa “Yatima.” Watoto wanatumwa Kanisa kuja kusali
lakini wazazi hawaji kusali. Kuna wakristu wanaoitwa: “Wanafiki.” Hawa ni watu
ambao wanasema hawaendi kanisani kwa sababu kanisani kuna wanafiki. Je, watu
wanasema wewe ni nani?
UTASEMWA TU
Huwezi
kuwakataza ndege wasiruke juu ya kichwa chako. Wataruka tu. Ila wasijenge viota
kichwani. Hauwezi kuwakataza watu wasiseme juu yako. Yesu alitetwa,
alinung’unikiwa, alikataliwa, alinenwa. Kama alivoagua Nabii Simeoni “Tazama,
huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa
ishara itakayonenewa.” Yesu ni
ishara
iliyopingwa na watu”. Mbele ya Kristu hakuna “Kutofungamana na upande wowote”.
Kati ya mawili ni chaguo lako ama uko upande wake au kinyume chake. Yesu
alipingwa, alibishiwa, alikuwa na wapinzani. Ukiwa wake kabisa siyo kusema
umekingiwa kunung’unikiwa, au kutetwa. Yesu aliambiwa maneno ya matusi chungu
nzima.
Mjinga: “Basi,
Wayahudi wakashangaa na kusema, ‘Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma
shuleni?” (Yn 7:15). Yesu hakuwa mjinga. Akiwa na umri wa miaka kumi na miwili
aliketi katikati ya waalimu huko Yelusalemu. “Nao wote waliomsikia
walistaajabia fahamu zake na majibu yake” (Lk 2:47).
MWENDAWAZIMU:
Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?” (Yn 10:20). MLAFI NA
MLEVI: “Akaja mwana wa mtu; yeye anakula na kunywa, mkasema “Mwangalieni huyu
mlafi na mlevi, rafiki ya watoza ushuru na wenye
dhambi!” (Lk 7:34).
MCHAWI: Lakini Wafarisayo wakawa wanasema,
“Anawatoa pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo wabaya” (Mt 9:34).
MWOVU: Pilato aliwaendea nje, akasema, “Mna
mashtaka gani juu ya mtu huyu?” Wakamjibu, “Kama huyu hangalikuwa mwovu
hatungalimleta kwako”. (Yn 18:29-30).
NABII WA UWONGO: Walimfunga kitambaa usoni,
wakawa wanamwuliza, “Ni nani aliyekupiga? Hebu bashiri tuone!” (Lk 22:64).
Yesu alikutana
na watu wenye majungu, uzushi na fitina. Tukumbuke hawajawahi kujenga mnara
katika historia ya dunia ya kuwaenzi wazushi, na waongo. Watu walimsema Kristu
sembuse wewe. Mtu akiwa mkarimu, wanasema anajitangaza. Asipokuwa mkarimu
wanasema ana gundi kwenye vidole, ni mnyimi, ni bahili. Mtu akitoa hotuba fupi
sana wanasema hakujiandaa. Akitoa hotuba ndefu wanasema hatunzi muda. Akiwa
mtoto mchanga wanasema ni malaika. Akiwa mtu mzima wanasema achana na yule
shetani. Akiwa mcha Mungu wanasema ni mkatoliki zaidi ya Papa. Asipokuwa mcha
Mungu wanasema shetani amemweka mfukoni. Akiaga dunia katika uri wa ujana
wanasema angefanya mengi mazuri. Akifariki umri wa uzeeni wanasema miaka yake
aliiharibu tu bila kufanya chochote. Watu watakusema tu. Miaka mitatu ya utume
wa Yesu kwa Bikira Maria ilikuwa ni miaka ya majonzi, miaka ya masikitiko.
Alishuhudia kutanda kwa wingu la wivu dhidi ya mwanawe, mlima wa matusi kwa
mwanawe, mafuriko ya chuki dhidi ya mwanawe. Yote yaliutonesha moyo wake, yote
yaliuchoma moyo wake. Binadamu si pesa ambayo hupendwa na kila mtu. Yesu Kristu
hakupendwa na kila mtu. Naye hakuwa bendera ya kufuata upepo wa maneno ya watu.
Alikuwa na msimamo. Huwezi ukampendeza na kumridhisha kila mtu. Baba mmoja na
mtoto wake wa kiume walimpeleka punda Sokoni. Baba huyo alikaa juu ya mnyama na
mtoto alitembea. Watu waliokutana nao njiani walilalamika, “Ni jambo baya sana:
Pande la mtu, limekaa mgongoni mwa punda wakati mtoto mdogo anatembea”. Kusikia
hivyo baba huyo alitelemka toka mgongo wa punda mtoto alichua nafasi yake.
Watazamaji walitoa maoni yao. “Ni jambo baya sana: mzee anatembea, na mtoto
amekaa”. Kusikia hivyo wote
wakawa
wamempanda punda - wakawasikia wengine wakisema, “Ni ukatili ulioje: watu
wawili wamekaa juu ya punda”. Kusikia hivyo wote walitelemka. Lakini watazamaji
wengine waliotoa maoni, “Ni ujinga ulioje: punda hana kitu chochote mgongoni na
watu wawili wanatembea”. Mwishowe, wote wawili walimbeba punda na hawakufika
sokoni.
Yesu
hakuyumbishwa na maneno ya watu kama mzee huyo na mtoto wake.
Watu hawapigi
teke mbwa aliyekufa bali aliye hai. Watu hawautupii mawe mwembe usio na
matunda. Ukiwa na “matunda” watu watakutupia mawe ya maneno ya kukukatisha
tamaa.
Vumilia.
Mvumilivu hula mbivu. Mama hupenda mtoto wake acheze ashangiliwe badala ya
kuzomewa. Yesu alitukanwa. Matusi hayo ni Upanga uliochoma moyo wa Maria.
Lakini alivumilia. Usiogope upinzani, kumbuka tiara huruka angani dhidi ya
upepo na
si pamoja na
upepo.
MABABA
WAKANISA WASEMAVYO
Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi: “Anaongeza ‘Filipi’ ili kutofautisha na pande nyingine za Kaisarea
kama Strato na anauliza swali hili akiwa Filipi. Hapa palikuwa mbali na
wayahudi ili kuwaondoa wafuasi wake hofu zozote ili waongee kwa uhuru
lilikokuwa kwenye akili zao. Filipi alikuwa ndugu wa Herod…ambaye alilipa jina
mji la Kaiseria kwa heshima ya Kaiseria Tiberias,” alisema Mtakatifu Yohane
Krisostomu. Watu wataongea mengi juu yako wakiwa huru, wakiwa mbali.
aliwauliza
wanafunzi wake, ‘Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?’ “Kristu aliwauliza swali hili wafuasi wake ili katika majibu yao
tujifunze kuwa wakati huo kati ya wayahudi yalikuwepo maoni mbalimbali juu ya
Kristo; na mwishowe tufanye utafiti watu wana maoni gani juu yetu; wakitusema vibaya
tupuzie; wakitusema vizuri tujiongezee fursa hizo,” alisema Origen.
Wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa ni Yohane Mbatizaji,
wengine Elia, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.’ “Ilikuwa rahisi kwa umati kukosea kwa kumfikiri a Yesu kuwa ni Eliya
na Yeremia kama Herod alivyomfikiria kuwa ni Yohane Mbatizaji; nashangaa baadhi
ya wahakiki wangejaribu kutafuta sababu ya makosa haya,” alisema Jerome.
Yesu akawauliza, ‘Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?’ “Wafuasi baada ya kutoa maoni ya watu wa kawaida Yesu anawakaribisha
wafikiria mawazo ya juu zaidi kumhusu yeye na hivyo linafuata swali ‘Na nyinyi
je, mnasema mimi ni nani?’ Nyinyi ambao mmekuwa pamoja name kila mara na mmeona
miujiza mikubwa zaidi ya watu wengi, hampaswi kukubaliana na maoni hayo. Kwa sababu
hiyo hakuwauliza swali hilo alipoanza kuhubiri lakini baada ya kufanya miujiza mingi,”
alisema Mtakatifu Yohane Krisostomu.
Simoni Petro akajibu, ‘Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa
Mungu aliye hai.’ (Mathayo 16:13-16). “Anamuita ‘Mungu
aliye hai,’ ukilinganisha na miungu wale wanaoheshimiwa lakini wamekufa; kama Saturn,
Jupiter, Venus, Hercules na miungu wengine,” alisema Jerome. Yesu ni Mungu aliye
hai.