JUMAPILI YA 18 YA MWAKA A
1. Isaya 55:
1-3
|
2. Warumi 8: 35, 37 -39
|
3. Mathayo 14: 13-21
|
“…alitazama juu mbinguni (Mathayo
14:19)” . “ Alimshukuru Mungu (Yohane 6:11).”
“Toa shukrani kwa jambo dogo na utapata makubwa,” ni methali ya
kabila la Hausa Nigeria. “Asiyeshukuru hupewa mara moja.” Ni
methali ya wahaya. Kusema kweli tukishukuru katika kila jambo Mungu atatufanyia
miujiza. Shukuru kabla ya kula. Shukuru kabla ya kusafiri. Shukuru kabla ya
kufanya mtihani. Shukuru kabla ya kutafuta mchumba. Shukuru kabla ya kutafuta
kazi. Shukuru kabla ya kuanza kazi. Shukuru kabla ya kwenda Hospitalini. Na
baadaye shukuru, yaani baada ya kula, baada ya kutoka Hospitalini kutaja
machache. “shukrani kila mara hutangulia muujiza,” alisema Ann Voskamp.
Kukumbuka kusema “asante” kunaongeza miujiza katika maisha yetu. Maneno mawili
haya “asante sana,” ni maneno ya kimiujiza. “Shukrani ni utajiri. Malalamishi
ni umaskini,” alisema Doris Day. Anton Dvorak, mwanamuziki mashuhuri wa Czeche
alizoea kuandika kwenye ukurasa wa mwisho wa kila mswaada wake maneno haya:
“Namshukuru Mungu! Nimeridhika na kazi hii!
Bwana wetu Yesu Kristu alipofanya
muujiza wa kulisha watu zaidi ya elfu tano alipopewa samaki wawili na mikate
mitano alitazama juu mbinguni (Mathayo 14:19). Alimshukuru Mungu (Yohane 6:11).
Muujiza huu aliufanyia jangwani. Shukrani ilitangulia muujiza. Mtakatifu Yohane
Chyrisostom alikuwa na haya ya kusema: “Wayahudi katika kuelezea muujiza
walikuwa na msemo: ‘Je, aweza kutupa chakula jangwani’ (Zaburi 78: 19). Kwa sababu
hii aliwaongoza kwenda jangwani, ili muujiza usiwe na chembe yoyote ya
kudhaniwa vibaya na mtu asifikiri kuwa chakula kimeletwa toka mji wa karibu.
Lakini hata kama mahali ni jangwa ni yeye anayelisha dunia; ingawa saa ilikuwa
imepita yeye hayuko chini ya masaa. Ingawa Bwana mbele ya mitume aliponya
wagonjwa, mitume hawakuwa wakamilifu kiasi cha kuweza kutambua ambacho angeweza
kufanya kuhusu chakula. Wao walisema, ‘uwaage watu ili waende vijijini
wakajinunulie chakula” (Mathayo 14: 15).
Kuna hadithi ya Wayahudi juu ya nani wa kushukuru. Omba omba wawili
walizoea kuomba misaada kwa mfalme kando kando ya barabara kwenye jiji kubwa.
Walizoea kwenda kwenye ikulu ya mfalme, ambaye alihakikisha wanapewa msaada.
Mojawapo wa omba omba alimshukuru mfalme kwa ukarimu wake, lakini mwingine
alimshukuru Mungu kwa kumpa mfalme nguvu na njia za kusaidia watu wake. Hilo
lilimhuhumiza mfalme alimwambia omba omba huyo: “Kwa nini ninapokuonesha
ukarimu unamshukuru Mungu na sio mimi.” Maskini alimjibu: “Kama Mungu
hasingekuwa mkarimu kwako, usingekuwa na chochote cha kunipa.” Mfalme aliamua
kumpa omba omba huyu fundisho. Alimwamuru mpishi wake kutengeneza mikate miwili
na kuficha kwenye mkate mmoja madini yenye thamani sana na kuhakikisha maskini
aliyekuwa anamshukuru mfalme na sio Mungu anapata mkate huo wenye madini.
Mpishi alifanya hivyo.
Walipotoka kwa mfalme, njiani maskini aliyekuwa anamshukuru mfalme
badala ya Mungu aligundua kuwa mkate wake ni mzito isivyo kawaida; kwake ilimaanisha
uliokwa vibaya. Hivyo alimwomba mwenzake wabadilishane mikate. Walifanya hivyo
na baada ya hapo kila mmoja akashika njia yake. Yule maskini ambaye kila mara
alimshukuru Mungu alipoanza kula mkate alikuta madini yenye thamani sana kwenye
mkate na alimshukuru Mungu kuwa sasa hataenda tena ikulu na kuomba msaada toka
kwa mfalme.
Baada ya muda mfalme aligundua kuwa mmoja wa omba omba haji tena ikulu
kuomba. Alimuuliza mpishi wake kama hakukosea katika kuwapa mikate ile na
kuchanganya. Alikuwa na uhakika kuwa hakuchanganya hiyo mikate. Mfalme
alimuuliza maskini ambaye aliendelea kuja kwake: “Ule mkate wangu usio wa
kawaida uliopewa kipindi fulani uliuweka wapi?” Maskini alikiri kwa kusema
kiukweli: “Mkate wangu ulikuwa mzito, hivyo nilifikiri uliokwa vibaya. Hivyo
nilibadilishana na mwenzangu.” Mfalme alielewa kwa nini ombaomba mwingine
alimshukuru Mungu. Tukumbuke kuwa utajiri wote na mali zote hutoka kwa Mungu.
Mungu pekee anaweza kumfanya mtu maskini awe tajiri na tajiri awe maskini –
bila kujali watu hata wafalme wanafikiria nini.”
Kumshukuru Mungu ni utangulizi wa
muujiza. Muujiza katika hadithi ya wayahudi ni somo tosha juu ya kumshukuru
Mungu. “Unapoamka asubuhi toa shukrani kwa ajili ya mwanga wa asubuhi, kwa
ajili ya uhai wako na nguvu. Toa shukrani kwa ajili ya chakula chako na furaha
ya kuishi. Kama hauoni sababu ya kushukuru, kosa liko kwako,” alisema Tecumseh
(1768-1813). Wamebarikiwa wale ambao wanaweza kutoa bila kukumbuka na wale
ambao wanaweza kupokea bila kusahau. Kutosahau kunamaanisha kuwa na shukrani.
Pale ulipoweka nukta Mungu
anaweka alama ya mkato mambo mazuri yanakuja. Yeye akiamua kuweka nukta usiweke
alama ya kushangaa. Filipo aliweka nukta
kwenye masuala ya kulisha wanaume elfu tano. Filipo mfuasi wa Yesu aliona kuna
tatizo raslimali kidogo zisioweza kutosha kulisha wanaume elfu tano wanaojua
kula chakula. “Filipo akamjibu, “Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, ili
kila mmoja apate kidogo tu.” (Yohane 6: 7). Yesu anatwaa utajiri kutoka kwenye
ufukara wa mtoto mwenye samaki wawili na mikate mitano . Anabadili kidogo kinakuwa kikubwa. “Kuongezwa kwa
mikate kunasimuliwa kikamilifu katika Injili zote nne. Muujiza huo una uhusiano
wa moja kwa moja na Ekaristi.” Mfululizo wa vitenzi: Akaitwaa…akaibariki,
akaimega, akawapa unadokeza Ekaristi. Kidogo unachoweka mikononi mwa Yesu
atakibariki kiwe kingi. Neno kula katika Biblia limetumika mara elfu. Katika
masimulizi ya Injili mara nyingi tunamuona Yesu anaenda kula au anatoka kula. Tunajifunza
kuwa njaa ni tatizo. Ni tatizo la kiuchumi. Ni tatizo la kijamii. Ni tatizo la
kidini pia. Linahitaji pia suluhisho la kidini. Lisilowezekana linawezekana.
MAMBO YA KUKATISHA TAMAA
Mazingira: Nyika Tupu
“Palikuwa na nyasi nyingi
mahali pale” (Yohane 6: 10). Katika Injili ya Marko
tunapata maelezo haya: “Mahali hapa ni pa ukiwa (Nyika tupu)” (Marko 6:35).
Mahali pa ukiwa kuna njaa. Penye nyika tupu kuna njaa. Palipo na njaa ya upendo
ni nyika tupu. Ofisini ukiwa na njaa ya upendo ni nyika tupu. Kwenye familia
ukiwa na njaa ya upendo ni nyika tupu. Lakini katika maisha kuna ambao wanaona
nyika tupu bila kuona raslimali zilizopo. Kuna Kampuni ya kutengeneza viatu
iliyotuma watu wawili kwenda visiwani kuona uwezekano wa kuanzisha biashara ya
kuuza vitua huko. Mmoja alipoona watu hawana viatu wanatembea peku peku,
akatuma ujumbe kuwa ziandaliwe konteina tano huku watu wanahitaji viatu.
Mwingine akatuma ujumbe kwenye makao makuu ya kampuni ya viatu kuwa visiwani
watu wana utamaduni wa kutovaa viatu kwa hiyo wasiandae mzigo wowote wa kutuma
visiwani.
Kupita kwa Wakati
“Mahali hapa ni ukiwa na saa
imepita” (Mathayo 14: 15). Wakati ulikuwa umekwenda. Labda kuna jambo
ulitegemea kupata muda unaona umepita. Ulitegemea kupata mme lakini saa
imepita. Ulitegemea kupata kipato kizuri lakini saa imepita. Ulitegemea kwenda
chuoni lakini saa imepita. Kumbuka
maneno haya: “Mawazo yangu si mawazo yenu” (Isaya 55: 8). Wakati wa Zechariah na Elizabeth kuzaa ulikuwa umepita lakini Mungu
akawafanyia muujiza wakampata mtoto Yohane Mbatizaji. Kupita kwa muda pengine
ni suala la mtazamo. Kijana anapokalia stovu yenye moto dakika moja ni kama saa
moja. Lakini msichana mrembo anapokaa karibu naye saa moja ni kama dakika.
Ukubwa wa Tatizo
“Yesu alipoinua macho na kuona
umati mkubwa wa watu wanamjia, alimwambia Filipo, tununue wapi mikate, ili hawa
wapate kula?” (Yohane 6: 5). Watu walikuwa wengi wanaume wapata elfu tano bila
kuhesabu watoto na wanawake. Watu walikuwa wengi. Tatizo lilikuwa kubwa. Mungu
wetu ni mkubwa kuliko matatizo yetu. Ukiwa na tatizo usimwambie Mungu nina
tatizo kubwa bali liambie tatizo Mungu wangu ni mkubwa. Unapopata tatizo kubwa
kama Goliathi, unajibu vipi? Ni kubwa si rahisi kushambuliwa. Jibu kama Daudi.
Ni mnene sana, siwezi nikalenga nikakosa. “Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na
makucha ya samba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa mfilisti huyu” ( 1
Sam 17:37).
Uchache wa Raslimali
“Andrea, nduguye Simoni Petro,
akamwambia, “Yupo mtoto aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili;
lakini hii ni nini kwa watu wengi kama hawa?” (Yohane 6: 8). Mtu anaweza kusema
hili haliwezekani kwa vile raslimali ni chache. Licha ya uchache wa raslimali
Yesu alifanya muhujiza. Katika somo la kwanza tunaona uchache wa raslimali
mikate ya shayiri ishirini (2 Wafalme 4: 42). Lakini Elisha akasisitiza, “Uwape
watu, ili wale, kwa kuwa Bwana asema hivi: Watakula na kusaza.” (2 Wafalme 4:
42).
VIRUTUBISHO VYA KUTATUA MATATIZO
Kama Kwamba Umepata
Yesu akawaambia, Waketisheni Watu” (Yohane 6: 10). Yesu aliwataka watu wakae mkao wa kula
chakula “kama kwamba” chakula kimeishapatikana. Muujiza wa kuongeza mikate
ulikuwa haujafanyika lakini Yesu alitenda kama kwamba. Kuna wakristu katika
parokia moja hapa Tanzania walimuomba padre Jumapili iliyokuwa inafuatia iwe
siku ya kuomba kupata mvua. Wakristu hao walishangazwa na padre aliposema
hayuko tayari kufanya maombi ya kuomba mvua kwa vile wakristu hawakwenda na
miavuli ya kujikinga na mvua. Suala la kuwa na miavuli linadokeza maana ya
“kama kwamba.” Yesu aliwambia wakoma kumi waende wajioneshe kwa makuhani kama
kwamba wamepona. Bikira Maria aliwaambia watumishi: lolote atakalowambieni
fanyeni “kama kwamba” Yesu amekubali.
Piga picha ya kile unachokitaka.
Bila shaka Bwana Yesu Kristu alipiga picha ya muujiza, picha ya ongezeko la
samali wawili na mikate mitatu. Suala la
kupiga picha ni muhimu ili ufanikiwe. “Akamleta (Abramu) nje akasema:Utazame
mbinguni, uhesabu nyota, kama waweza kuzihesabu.Akamwambia: Ndivyo uzao wako
utakavyokuwa” (Mwanzo 15:5). Mungu alisisitiza umuhimu wa kupiga picha.
Shukuru Usikufuru
“Yesu akaitwaa mikate,
akashukuru” (Yohane 6: 11). Shukrani inabadili “hakitoshi” kuwa “kinatosha.”
Shukrani inabadili kidogo kuwa kikubwa. Kushukuru ni kuomba tena.
Mshirikishe Yesu
Mipango bila kumshirikisha Yesu
haina mafanikio ya kimihujiza. Filipo mwanahesabu hakumweka Yesu katika hesabu
zake. Alisema dinari mia mbili kugawa kwa wanaume elfu tano haitoshi. Angesema
dinari mia mbili kujumlisha na Yesu na
kugawa kwa wanaume elfu tano watoto na wanawake inatosha. Katika mipango yako
mshirikishe Yesu. Katika hesabu zako mshirikishe Yesu.
Kidogo Kivute Kikubwa
Mungu wetu ni Mungu anayehitaji
mchango wako. Mchango wa samaki wawili na mikate mitano ni kidogo kilichovuta
kikubwa. Mungu anahitaji upige hatua ya kwanza. Katika hadithi za Kiyahudi
ambazo hazikuandikwa katika Biblia kuna hadithi isemayo: Musa alipopiga maji
yake na fimbo katika Bahari Nyekundu maji hayakugawanyika wana wa Israeli
wapiti bali mtu wa kwanza ulitangulia na kuingia majini ndipo maji
yakagawanyika. Piga hatua ya kwanza.
Tafakari maneno ya Mtakatifu
Josemaria Escriva: “Omnia possibilia
sunt credenti – yote yawezekana kwake yule anayesadiki. Hayo ni maneno ya
Kristu. Vipi wewe huwezi kumwambia kama walivyosema mitume: adauge nobis fidem
- utuongezee imani.” Nelson Mandela aliyekuwa mstari wa mbele kuleta uhuru
wa walio wengi Afrika Kusini jambo ambalo lilionekana kama ndoto, alisema, “Kwa kawaida jambo linaweza kuonekana
haliwezekani mpaka linapofanyika.” Ndani ya neno kisichowezekana kuna neno
wezekana. Ndani ya neno lisilowezekana kuna neno wezekana.