JUMAPILI YA 17 YA MWAKA
|
|
|
“Ee Bwana…sijui inipasavyo kutoka
wala kuingia…Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima” (1 Wafalme 3: 7-9).
Maisha ni kuingia na kutoka. Ukiingia vizuri
utatoka vizuri. Tunaingia shuleni na kutoka. Tunaingia sehemu za kazi na
kutoka. Tunaingia Kanisani na kutoka. Tunaingia nyumbani na kutoka. Tunaingia
hotelini na kutoka. Tunaingia kiwanjani na kutoka.Tunaingia dukani na kutoka.
Tuingieje? Tutokeje? Kuna kitendawili kisemacho: aliingia kwenye nyama akatoka
bila kula. Jibu ni kisu. Mwanafunzi akiingia shuleni kujifunza na kutoka bila
ushindi ametoka kama kisu kwenye nyama. Timu
ya mpira ikiingia uwanjani na kutoka imefungwa bila kufunga ni kama kisu
kuingia kwenye nyama na kutoka bila kula. Tunahitaji hekima kujua namna ya
kuingia na kutoka. Suleimani au Solomoni alisali: “Ee Bwana…sijui inipasavyo
kutoka wala kuingia…Basi umpe mtumishi wako moyo wa hekima” (1 Wafalme 3: 7-9).
Usiingie mikono mitupu. “Zenani” jina la watu wa kabila la Xhosa wa
Afrika Kusini lina maana ya : “Umeleta nini?” Ni swali ambalo tunaulizwa. Kuna
rafiki yangu alikuwa anafanya sherehe ya kuzaliwa. Aliniimbia nikifika mlangoni
mwake nifungue mlango kwa miguu. Nikamuuliza kwa nini nifungue mlango kwa mguu
akasema: “Ufungue kwa miguu kwa vile mikono itakuwa imebeba zawadi.” Hata
tunapoingia nyumba ya Mungu tuingie tumebeba zawadi. Namna ya kuingia kanisani.
Usiingie mikoni mitupu. Biblia yasema: “wala asitokee mtu mbele yangu mikono
mitupu” (Kutoka 34:20). Hata mamajusi
hawakwenda kumsujudia mtoto Yesu mikono mitupu bali waliingia pangoni na
zawadi.
Ingia kwa mtazamo chanya. Watu wenye mtazamo chanya wanapendwa na
kuheshimiwa kuliko ambao kila mara wanalalamika na kuwa na mtazamo hasi.
“Baadhi ya watu hulalamika kwa vile maua ya waridi yaana miiba: ninashukuru
miiba ina maua ya waridi,” alisema Alphonse Karr, katika kitabu kiitwacho, A
Tour Round My Garden. Huo ni mtazamo chanya. Kuna padre aliyeingia hotelini kwa
mtazamo chanya. Aliagiza kikombe cha kahawa ingawa ulikuwa wakati wa chakula
cha mchana. Ilikuwa ni siku ya kufunga. Kwa mshangao aliona kijana muumini
katika Kanisa lake akiwa na mlima wa nyama choma kwenye sahani yake. Kijana
alisema: “Naamni padre sikakukwaza.” Padre kwa mtazamo wake chanya alisema:
“Nachukulia kuwa umesahau kuwa siku ya leo ni siku ya kufunga.” Kijana alijibu:
“Nakumbuka bila mashaka yoyote kuwa leo ni siku ya kufunga.” Padre kwa mtazamo
chanya akasema: “Utakuwa mgonjwa na daktari bila shaka amekwambia kutofunga.”
Kijana akasema: “Hapana nina afya nzuri sana.” Padre aliinua macho yake
mbinguni na kusema: “ Ee Mungu huyu kijana anatoa mfano mzuri kwa kizazi hiki.
Anakubali makosa yake badala ya kusema uongo.” Padre alikuwa na mtazamo chanya.
Ingia kwa salamu. “Asubuhi njema! Mchana mwema! Usiku mwema! Hizi
sio salamu tu. Hizi ni baraka zenye nguvu, zinazoanzisha mambo mazuri. Kwa hiyo
kama ni asubuhi, mchana au usiku akikisha salamu unaisema vizuri,” alisema Franco Santoro. Bwana Yesu alisema:
“Mnapoingia nyumba isalimuni” (Mathayo 13: 12). Kuna mtu aliingia kwenye nyumba
na kumsalimu mwenye msongo wa mawazo: Habari za leo. Aijibu. Sijui. Akamsalimu
tena . Habari za leo. Yeye alijibu kama za juzi. Alikuwa na msongo wa mawazo.
Kusalimu ni kutakia mtu amani.
Ingia kwa shukrani. “Ingieni malango mwake kwa shukrani” (Zab 100:4).
Toka kwa malengo. Jua unapokwenda. Kutoka kwa malengo kunahitaji
hekima. “Kama haujui unapokwenda, labda utaishia mahali fulani pengine,”
alisema Laurence J. Peter. Kuna mtu ambaye alikuwa kwenye matatu kondakta akamwomba
alipe nauli akasema: “Nauli nitakupa ila najiuliza naenda wapi?” Hakutoka
nyumbani kwa malengo. Thomas Carlyle alisema: “Mtu asiye na lengo ni kama meli
bila usukani – mtu aliyepotea, mtu bure, kabwela.”
Toka kwa furaha. Nyota njema huonekana asubuhi. Anza siku yako kwa
kuvaa vazi la furaha. Njia ya kuwa na furaha ni kuwafanya wengine kuwa na
furaha. “Sambaza upendo kila mahali unapokwenda. Mtu yeyote asije kwako bila
kutoka akiwa na furaha zaidi,” alisema mwenye heri Teresa wa Calcutta. Kama
mfalme Sulemaini au Solomoni tuombe hekima ya kujua namna ya kutoka na namna ya
kuingia.