JUMAPILI YA 16 YA MWAKA A
1. Hek 12: 13. 16-19
|
2. Rum 8: 26-27
|
3. Mt 13: 24 -43
|
“ACHENI
VIKUE PAMOJA MPAKA WAKATI WA MAVUNO.” (MT 13: 30)
Kuna hadithi juu ya mzee mwenye miaka sabini aliyemtembelea Abrahamu, akiomba hifadhi ya
usiku mmoja. Mtu huyo alikataa kushiriki kwenye sala za kuomuomna Mungu mmoja. Abrahamu
alimuuliza anaabudu Mungu yupi. Mzee huyo alisema anaabudu “moto.” Abrahamu
alimwambia hawezi kumpokea mtu wa namna hiyo nyumbani kwake. Akamfukuza. Usiku
Mungu alimtokea kwenye ndoto na kumwambia: “Abrahamu mtu huyu nimemvumilia kwa
kipindi cha miaka sabini. Wewe huwezi kumvumilia hata usiku mmoja.” Mungu wetu anatupa muda ili tubadilike. “Lakini wewe, mtawala wa
nguvu, unahukumu kwa upole, na kutuongoza kwa huruma nyingi; maana uwezo unao
wa kutenda utakalo wakati wowote” (Hekima ya Sulemani 12: 18). “Yeye huvumilia,
maana hapendi mtu yeyote apotee” (KKK Na 2822; 2 Pet 3:9; Mt 18:14). Nyuma ya pazia ya kubadilika kuna subira. “Watu wote husifia subira, ingawa ni wachache
wako tayari kuiweka katika matendo,” alisema Thomas a Kempis. “Kipande kikubwa cha barabara ya kwenda
mbinguni kinapitiwa kwa spidi ya maili thelathini kwa saa,” alisema Evelyn
Underhill. Taratibu ndio mwendo. “Subira
ni mzizi na mlinzi wa fadhila zote,” alisema Papa Mtakatifu Gregory I.
Chini kwenye kitako cha subira kuna mbingu. Ni methali
ya Kanuri. Kitakachopoa hakikuchomi. Ni methali ya Wahaya wa Tanzania. Roma
haikujengwa siku moja. Tabia nzuri haijengwi siku
moja. Kuna maneno yalikutwa yameandikwa kwenye ukuta wa Mnara wa London na
wafungwa: “Sio taabu zinoua bali kukosa
subira tunapozikabili taabu.” Hayo yalikuwa maneno ya wafungwa. Magereza ni
nyumba za watakatifu watarajiwa iwapo watabadilika. “Subira ni kifyonza mshtuko kikubwa sana kati ya vifyonza mshtuko vyote.
Jambo pekee ambalo unaweza kupata kwa kufanya mambo kwa haraka sana ni matatizo,”
alisema Henri Fournier Alain. Kwa kawaida tunataka ushauri umbadilishe mlevi
baada ya saa moja. Tunataka mahubiri yawabadili watu wakitoka Kanisani.
Tunataka kufumba na kufumbia mtu mbaya ageuke kuwa mzuri baada ya kupewa onyo
au taadhari. Tunataka hotuba ya kisiasa ilete matokeo ya papo kwa papo.
Tunahitaji kuwapa watu muda wa kubadilika. Tunahitaji kujipa muda wa
kubadilika.
“Ufunguo wa kila
kitu ni subira. Unapata kifaranga kwa kuangua yai na si kwa kuvunja yai,”
alisema Arnold H. Glasow. “Tabia nzuri haijengwi ndani ya wiki moja au mwezi
moja. Inajengwa kidogo kidogo, siku kwa siku. Juhudi za muda mrefu zenye subira
zinahitajika kujenga tabia nzuri,” alisema mwanafalsafa Heraclitus. Katika
Hadithi za Aesop kuna hadithi juu ya subira na uvumilivu.
Kunguru akiwa nusu mfu kwa sababu ya kiu, aliliona
gudulia au jagi la maji ambalo wakati fulani lilikuwa limejaa maji; kunguru
alivyotia mdomo wake uliochongoka na mgumu kwenye jagi aligundua palikuwepo na
maji kidogo yaliyobaki na hakuweza kuyafikia. Alijajaribu na kujaribu lakini
haikuwezekana, mwishowe alikata tama. Baadaye alipata wazo. Alichukua
changarawe na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na
kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye
jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe
nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na
kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye
jagi. Alichukua changarawe nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Alichukua changarawe
nyingine na kuidondosha kwenye jagi. Hatimaye aliona maji yanakaribia mdomo wake. Alichukua changarawe
nyingine chache na kuzidondosha kwenye jagi aliweza kunywa maji na kumaliza kiu
yake. Ukweli tunaojifunza katika hadithi ni: uvumilivu una malipo. Ni ukweli
huo huo tunaojifunza katika methali zifuatazo: tone tone ujaza ndoo. Polepole
ndio mwendo. Mwenye subira mwishowe hupata (Igbo); Mwanamke mwenye subira ana
utajiri wote uliopo duniani (Jabo); Atembeaye polepole hufika mbali (Luyia); Ukikuta
mto umefurika subiri (Kiswahili); Subira ikificha kitu, hasira haitatafuta na kupata
(Mamprussi); Usiwe mkosa subira unapouliza mpaka unakuwa na hasira wakati wa
kusikiliza unapowadia (Misri ya zamani)
Katika Biblia
kuna mfano wa magugu katikati ya ngano. “Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu
aliyependa mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui
yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano
yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda
wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi
magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Wataumwa wakamwambia, Badi,
wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa
ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue pamoja hata wakati wa mavuno” (Mathayo
13: 24-30).
Maneno haya ni
muhimu: acheni vikue pamoja hata wakati wa mavuno. Watu wanasukumwa kuwagawanya
binadamu katika makundi mawili wema na waovu, marafiki na maadui. Matokeo
mabaya ya ubaguzi na mgawanyo wa namna hii ni kushindwa kuvumiliana na hamu ya
kutatua kwa haraka na kwa fujo mivutano inayotokana nayo. Kama Mungu alivyo
mtulivu na mvumilivu kwa watu wote, basi sisi nasi tuchukue msimamo wa namna
hiyo hiyo. Mitume ambao wengi walikuwa wavuvi walifikiri wanajua mambo ya
magugu na ngano. Walizoea kuosha nyavu, kuvua samaki na kuuza samaki. Na kama
waliuliza Bwana hauwezi kuangamiza waovu kama tunavyoangamiza samaki waliooza?
Hauwezi kutumia mbinu za wavuvi katika kilimo.
JIPE MUDA WA KUBADILIKA
Msitari kati ya
dhambi na fadhila, wema na ubaya ni mwembamba. Msitari kati ya uongo na ukweli,
magugu na ngano, baraka na laana, ni mwembamba. Mawili mawili yanaingiliana.
Yameshikamana. Mdhambi wa leo anaweza kuwa mtakatifu wa kesho.
Kuna hadithi juu ya Wema na Uovu. Siku moja Wema na Uovu
walikutana ufukweni mwa bahari. Waliambizana. “Tuvue nguo zetu na tuogelee
baharini.” Baada ya kuogelea kwa muda baharini Uovu ulitoka haraka majini na
kuja ufukweni na kuvaa nguo za Wema na kwenda zake. Baadaye Wema ulitoka majini
na kuja ufukweni na kugundua kuwa nguo zake zimechukuliwa na Uovu. Wema ukiona
aibu kwenda uchi ulivaa nguo za Uovu. Hadi leo Wema na Uovu wanatembea na
mavazi ya uigizaji.
Baraka inaweza
kuwa na sura ya balaa. “Baraka zetu
zinazoeonekana mara nyingi zinajitokeza kwetu katika sura ya maumivu, upotezaji
na kukatishwa tamaa; lakini tuwe na subira na muda mfupi tutaziona katika sura
zake sahihi,” alisema Joseph Addison. Kama mambo ni hivyo jipe muda wa
kubadilika. Iliripotiwa kuwa nyumba yake huko Washington imeungua moto, Thomas
Hart Benton aliacha kikao cha baraza na kufika kwenye eneo la tukio la maafa.
Akitazama mabaki alisema, “Inarahisisiha kuaga dunia. Kuna machache ya kuacha.”
Alijipa muda na kukabili maafa kwa utulivu badala ya hasira. Usikate tamaa. “Mwenye haki ya kukata tamaa ni yule tu
ambaye dhambi zake ni kubwa kama huruma ya Mungu,” alisema Mtakatifu
Augustino wa Hippo (354 – 430). Kwa kawaida dhambi zetu ni ndogo
zikilinganishwa na huruma ya Mungu.
MPE MUDA MWENZAKO
Mpe muda
mwenzako. Tembo hakui siku moja
(Methali ya kigio). Urefu haulakishwi
(Methali ya Ndebele). Baba wa Kanisa Jerome alikuwa na haya ya kusema: “Kuna nafasi ya kutubu, tunaonywa kuwa
tusimgoe ndugu yetu kwa haraka, kwa vile leo aliye na mafundisho potofu leo,
kesho anaweza kukua katika hekima na kuanza kutetea ukweli, Bwana aliongeza
maneno haya, msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.” Katika msingi huu, mpe Mungu muda afanye
mabadiliko ndani mwako. Mpe mke wako muda. Wape watoto wako muda wakue katika
hekima na umbo.
MPE MUNGU MUDA
“Hatuna budi kumgonja Mungu, kwa muda mrefu, kwa
upole, katika upepo na unyevunyevu, katika ngurumo na radi, katika baridi na
giza. Subiri, na atakuja. Haji kamwe kwa wale siosubiri,” alisema Frederick W.
Faber. Stanley alipoanza safari za uvumbuzi mwaka 1871
alikutana na Livingstone, kwa muda wa miezi kadhaa alikaa naye, lakini
Livingstone hakumwambia Stanley mambo ya kiroho. Miezi yote hiyo Stanley
alitazama kwa makini tabia ya Livingstone ambayo ilikuwa ya kushangaza
akizingatia pia subira yake. Hakuelewa huruma aliyokuwa nayo Livingstone kwa
waafrika. Kwa ajili ya Kristu na Injili yake mmisionari huyu alikuwa mwenye
subira, asiyechoka, mwenye shauku, akitumika na kutumiwa na Bwana wake. Stanley
aliandika: “Nilipoona subira isiyochoka, ari isiyokatizwa, wana wa Afrika
waliopewa mwanga, niligeuka na kuwa Mkristu upandeni mwake, ingawa hakusema
neno lolote kuhusu ukristo.” Mungu alimgeuza Stanley polepole. Kazi ya
kutakasa na kugeuza ni ya Roho Mtakatifu. “Lakini Roho anasaidia udhaifu wetu.
Hatujui jinsi inavyotubidi kuomba. Roho mwenyewe anatuombea sisi kwa maombi
yasiyosemeka. Lakini Mungu achunguzaye mioyo ajua nia ya Roho anayewaombea
watakatifu kwa Mungu” (Warumi 8: 26-27).
FADHILA INASIMAMA KATIKATI
Subira ni
fadhila ya kusimama katikakati. Kukosa subira ni jambo baya sana. Haraka haraka haina baraka. Na
kuzidisha subira ni jambo baya sana. Mvumilivu hula mbivu akivumilia sana
anakula mbovu. Subira kupita kiasi
hutengeneza njia ya matatizo (Methali ya Kikuyu). Fadhila ya subira
inasimama katikati ya kukosa subira na kusubiri kupitiliza. Methali ya wahaya
inasema yote: Wamemsifu kuwa ni mkimbiaji mzuri akapitiliza kwao.