JUMAPILI YA 15 MWAKA A
1. Isaya 55: 10-11
|
2.Warumi 8: 18-23
|
3. Mathayo 13: 1-23 (Mt 13: 1-9)
|
“Ni moyo unaompelekea mtu mbinguni au motoni.” Ni
methali ya Kiafrika. Mungu hatazami sura
ya nje anatazama yaliyomo moyoni. Mwenyezi Mungu alimkataa Eliabu hasiwe mfalme
wa Israeli kwa vile Mungu hatazami sura ya nje, hatafuti warembo wa sura bali
warembo wa moyo. Tunasoma katika Biblia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo
chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoangalia binadamu wenye
kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni” ( 1
Samueli 16: 7). Katika Injili ya leo tunapewa aina nne za mioyo.
1.
MOYO
WENYE TRAFIKI
Moyo wenye trafiki ni kama wapita
njia ni wengi, magari ni mengi, baisikeli ni nyingi, boda boda ni nyingi. Katika
Injili ya Mathayo tunaambiwa: “Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Katika kupanda,
mbegu nyingine zilianguka kando ya njia. Wakaja ndege wa angani wakazidonoa”
(Mathayo 13: 4). Moyo wetu ni kama njia. Kuna trafiki. Hoja si kuwepo kwa
trafiki hoja ni namna ya kukabili trafiki. Trafiki isikuhumize kichwa. Mfano
kwenye maisha ya ndoa ni kama msongamano wa magari ambapo hauchi nafasi kubwa
ukiacha nafasi kubwa sana mwenye daladala anaingia. Ni bumper to bumper. Katika
trafiki hiyo uenda kuna marafiki. Biblia yasema: “Msidanganyike! Urafiki mbaya
huharibu tabia njema” (1 Wakorintho 15: 33).
Ni katika mtazamo huo inasemwa niambie rafiki yako nitakwambia tabia
yako. Kuna urafiki ambao unaunganishwa
na jambo baya ukitoa jambo hilo baya hakuna urafiki. Wengine wanaunganishwa na
ulevi, ukitoa ulevi hakuna urafiki. Wengine wanaunganishwa na umbeya, ukitoa
umbeya hakuna urafiki. Urafiki wa kweli lazima uunganishwe na jambo zuri au na
tabia nzuri.
Kuna watu wawili waliokuwa
wanamjadili tajiri aliyefilisika. Mmoja akasema, “Tangia afilisike, nusu ya
rafiki wake hawamtembeli tena, hawamjulii hali tena.” Mwingine akauliza habari
juu ya nusu ya rafiki wake wengine. Mwenzake akamjibu: “Hawajui kama
amefilisika.” Biblia yasema: “Kuna rafiki aliye mwenzi wa mezani, wala hatadumu
karibu nawe siku ya taabu yako (Yoshua bin Sira 6:10). Rafiki katika taabu huyo
ni rafiki wa kweli. Tusipokubali trafiki ituathiri mioyo itakuwa udongo mzuri.
Simoni Petro alipotaka Bwana wetu Yesu Kristu aondokane na mpango wa kutukomboa
Bwana Yesu alisema: “Ondoka kwangu” shetani.
2.
MOYO WENYE MIAMBA AU MOYO MWAMBA
“Mbegu imeanguka kwenye mwamba”
(Mathayo 13: 20). Mwamba haupenyeki. Ni moyo sugu. Dhamiiri imekufa. Mtu hayuko
tayari kusamehe. Moyo unaweza kuwa mwamba kutoka na mabaya mtu aliyotendewa bila
kusamehe. Mzee Joe alikuwa kufani kwenye kitanda cha mahuti. Kwa muda wa miaka
mingi alikuwa hapatani na Bill, ambaye zamani alikuwa mmoja wa marafiki zake.
Akitaka kunyosha mambo yake kabla ya kuaga dunia alimtuma Bill waongee na
kumaliza mambo. Bill alipofika, Joe alimwambia kuwa anaogopa kwenda mbinguni
akiwa na kinyongo naye. Kwa kusita na kwa kujikaza Joe aliomba msamaha kwa
mambo aliyoyasema na kuyatenda. Alimwaakikishia Bill kuwa amemsamehe kwa makosa
yote aliyomtendea. Mambo yote yalionekana kwenda vizuri mpaka hapo Bill
alipojiandaa kuondoka. Alipokuwa anatoka chumbani, Joe alimuita, “Lakini
kumbuka, nikipona, haya yote niliyosema hayana maana wala uzito.”
Yesu
alisisitiza sana hitaji la kuwasamehe wengine kama tunavyosoma katika Biblia “Kisha Petro akamwendea
Yesu, akamwuliza, ‘Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara
saba?’ Yesu akamjibu, ‘Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba.’” (Mathayo
18:21” Kusamehe mara sabini na saba kunamaanisha kusamehe kila mtu kila mara.
Usipofanye hivyo moyo wako unakuwa mwamba. Usiposamehe unafanya moyo wako uwe mwamba
usiopenyeka.
“Jicho kwa jicho” mtazamo huo
utawaacha watu wengi wakiwa vipofu. “Jino kwa jino” mtazamo huo
utawaacha watu wengi wakiwa vibogoyo. Kisasi kilicho bora ni kusahau.
Ndivyo isemavyo methali ya Kiswahili. Lakini kisasi kilicho bora zaidi ni
kusamehe. Na pia kisasi kilichobora
zaidi ni kutokuwa kama yule aliyekufanyia jambo baya ili pasiwepo watu wabaya
wawili, yeye aliyekufanyia ubaya na wewe unayeshindwa kujibu ubaya kwa wema.
Nelson Mandela alikuwa na haya ya kusema juu ya kusamehe waliomtendea vibaya: “Nilivyotembea kutoka mlangoni nakuelekea
lango ambalo likuwa natokea na kwenda kwenye uhuru wangu, nilijua kuwa kama
nisingeacha ukali wangu na chuki nyuma yangu, ningeendelea kuwa gerezani.” Kusamehe ni kumfungua mfungwa utagundua
mfungwa ni wewe. Kabla ya kusamehe unakuwa kwenye gereza la chuki na
kulipiza kisasi. Kumbuka chuki umchoma anayeitunza. “Msamaha ni manukato ambayo ua huacha kwenye kisigino
kilicholikanyaga,” alisema Mark Twain. Kutosamehe ni kurudi nyuma.
Nakubaliana na Libba Bray aliyesema: “Hatuwezi kurudi nyuma. Tunaweza tu kwenda
mbele.” MSAMAHA NI BREKI HAKUNA HAJA YA KUGONGA.
Mungu sio
Adui wa Adui Zako
Martin Niemoller alitoka katika
gereza la Hitler akisema, “Ilininchukua muda mrefu kujifunza kuwa Mungu sio
adui wa adui zangu. Na sio adui wa
maadui zake.” Kama unapenda watu wakupende nawe uwapende. Injili ya leo
inatutaka tuwapende adui zetu: “Mmesikia kwamba imenenwa, ‘umpende jirani yako,
na umchukie adui yako.’ Mimi lakini nawaambieni, wapendeni adui zenu, waombeeni
wanaowadhulumu…” (Mathayo 5:43-44). Adui mpende. Ni methali ya Kiswahili.
Usimchukie hasidi au adui yako. Adui zetu yafaa kuwachukulia makosa yao watutendeavyo. Huenda
wakatubu na kuacha uovu wao. Tunaaswa na methali ya Kiswahili, Adui aangukapo mnyanyue. Ni methali
nyingine ya Kiswahili kuhusu kumpenda adui na kumtendea mema. Ni ubinadamu
kumsaidia adui yako akiwa na shida. “Tunapowachukia
maadui wetu tunawapa uwezo juu yetu: uwezo juu ya usingizi wetu, hamu yetu ya
chakula, shinikizo letu la damu, afya yetu na furaha yetu.” (Dale Carnegie)
“Jinsi miti yote inavyojulikana kwa vivuli vyake, ndivyo hivyo watu wazuri
wanajulikana kwa maadui wao.” (Methali ya Kichina).
3.
MOYO
WENYE MIIBA
Bwana Yesu Kristu alitoa tafsiri
ya miiba: “Mbegu imeanguka kati ya miiba kwa mtu anayelisikia neno, lakini
shughuli za dunia na ulaghai wa mali hulisonga neno” (Mathayo 13:22). Miiba ni shughuli nyingi na ulaghai wa mali. Shughuli
nyingi ni miiba katika kutekeleza neno la Mungu. Shetani anaweza kukushawishi
ili uwe na shughuli nyingi ili usishughulikie jambo lilo muhimu. Eva alikuwa
msaidizi wa Adamu na Adamu msaidizi wa Eva katika raha na shida katika magonjwa
na afya. Lakini Eva alipokuwa anajaribiwa na Adamu, Adamu alikuwa na shughuli
nyingi hakuwa pamoja na Eva. Pengine shughuli nyingi zinaweza kuwa namna ya
uvivu. Nina shughuli nyingi sitaenda Kanisani. Hapo kuna uvivu wa kwenda
Kanisani. Miiba hipo nje. Miamba hipo ndani.
4. MOYO
WENYE UDONGO WENYE RUTUBA
“Mbegu imeanguka katika udongo wenye rutuba kwa mtu
anayelisikia neno na kulitunza moyoni. Akazaa na kutoa matunda, huyu mia, na huyu
sitini, na mwingine thalathini” (Mathayo 13: 23). Hapa kuna udongo uliotayari
kulimwa. Utayari ni jambo muhimu. Kuna
hadithi ya Bwana aliyekuwa tajiri sana.
Alipofika mbinguni alikaribisha kwenye nyumba ya nyasi. Alipinga sana. Aliambiwa hiyo
ndiyo nyumba umeandaliwa. Aliuliza, “Hiyo mansion pale ni ya nani?” “Aliambiwa
ni ya mpishi wako.” “Inakuwaje ana
nyumba nzuri sana
kunizidi. Aliambiwa nyumba hapa zinajengwa kutokana na vifaa unavyotuma
mbinguni. Wewe ulituma nyasi na miti. Ukichukua glasi ya kuweka maji ukakuta ni chafu ina mende waliokufa hauwezi
kuweka maji. Ukitaka kunywa supu ukakuta bakuli ni chafu hauwezi kuweka supu
yako. Mungu anataka kukupa neema lakini anajiuliza niweke wapi neema hizi?