Jumapili
ya 19 ya Mwaka A
|
|
|
Kumbuka kuwa bahari shwari haitoi
wanamaji stadi. Matatizo kama mawimbi yanaweza kukuimarisha. Hivyo usipoteze
wakati wako kupambana na ukuta ukifikiri utageuka kuwa mlango! Kuwa na mtazamo
hasi dhidi ya matatizo ni kama kupambana na ukuta. “Wavuvi wanajua kuwa bahari
ni hatari na ina dhoruba ya kuogopesha, lakini hawajawahi kuona hatari hizi
kama sababu tosha za kubaki kandokando ya bahari au ufukweni,” alisema Vincent
van Goth. Wavuvi hujitosa kwenye maji marefu. Wavuvi ni mfano wa kuigwa
tunapokumbana na mawimbi ya matatizo katika bahari ya maisha. Kuna mtu
aliyemwambia mvuvi hivi: wewe hauogopi kwenda baharini kuvua samaki. Mjomba
wako, kaka yako, babu yako wote walikufa maji kwa nini hauogopi? Mvuvi alijibu
hivi: watu wengi hufa wakiwa vitandani lakini watu hawaachi kulala vitandani.
“Kuna mambo ambayo unajifunza vizuri sana wakati kuna utulivu na mengine wakati
kuna dhoruba,” alisema Willa Cather
Kwa Yesu kila mara mawingu
hayakuwa bluu. Kuna wakati wingu lilikuwa jeusi likiashiria dhoruba ya
matatizo. Alikataliwa na wasamaria katika kijiji cha Wasamaria. Kwa Ayubu
mawingu hayakuwa kila mara ya bluu. Kuna wakati alifikiria kuwa kama
hasingezaliwa. Katikati ya mawimbi ya matatizo Ayubu alizidi kuimarika. Ni kama
jani la chai linapata nguvu ya kugeuza rangi ya maji likiwa kwenye maji moto. Ukiwa
kwenye mawimbi ya matatizo kumbuka ukweli huu: Kwanza tuko salama kwenye
mawimbi ya matatizo tukiwa na Mungu kuliko tukiwa pasipokuwa na mawimbi ya
matatizo bila Mungu. Mungu anaweza kutuliza mawimbi au akayaacha mawimbi
akamtuliza binadamu. Pili, maisha bila mawimbi ya matatizo na magumu yatafanya
uwezekano wa mazuri kuwa ni ziro. Tatu, joto likizidi kutanuka kunazidi.
Matatizo makubwa yanaweza kukufanya uwe mkubwa. Kuna methali isemayo: anayesema
sijawahi kuliona jambo hili huwa si mkubwa kiumri. Nne ukiomba mvua inyeshe
kuwa tayari kukanyaga matope. Tano jua kuwa mawimbi ya matatizo yanakujia ili
kukuimarisha na wala sio kukudhoofisha.
IMANI HABA
“Ewe mwenye imani haba mbona uliona shaka” (Mathayo 14:31)
Maisha ni
kigeugeu. Mambo yalimgeuka mtume Petro. Petro alikuwa ni mtu aliyefanya maamuzi
ya ghafla na ya haraka. Hakufikiri sana kabla ya kutenda. Jambo hili pengine ni
busara ulikilinganisha na mtu ambaye anafikiri sana mwishowe hatendi lolote.
Katika nafsi ya Petro kuna mchanganyiko wa mambo. Anatamani kuwa na Yesu. Pia
anatamani kuonesha kuwa anaweza kutenda analolitenda Yesu: kutembea juu ya
maji. Kuna upendo na majivuno kama ilivyo kwa kila mmoja wetu. Petro ana
ujasiri na woga. Anaanza vizuri, anaona dhoruba na kuogopa. Anakosa imani.
Sababu kubwa ya kupotea kwa imani ya Petro ni kuwa
macho yake, mawazo yake, moyo wake alivielekeza kwenye dhoruba badala ya
Kristu. Alipomtazama Yesu Kristu imani ilipatikana akalia kwa sauti, “ Bwana,
niokoe !” ( Mt 14; 30). Licha ya Petro kuwa na imani haba Yesu alimuokoa. “
Hapo, Yesu akanyosha mkono wake, akamshika … wakapanda mashuani, na upepo
ukakoma”. ( Mt 14: 31-32). Nasi tunapambana na matatizo. Matatizo ya siku hizi
ni kama: umasikini, makazi yasiyofaa, ukosefu wa kazi, magonjwa yasiyo na tiba,
ukosefu wa riziki, uzinifu, uzazi kwa namna isiyo halali, ukatili na vita,
ukabila- damu inakuwa nzito kuliko maji ya ubatizo. Wakati tunazama kwenye
lindi la maji ya matatizo tumuombe Yesu atuokoe.
Katika
kilele cha dhoruba Yesu alijitokeza. Katika kilele cha hatari, katika upeo wa
wasiwasi Yesu alijitokeza. Anakuja wakati ambapo hategemewi kabisa. Mitume
walifikiri ni mzuka wakauotea mbali. Yesu ni Mkombozi wakubariki. Ni Mkombozi
tunayeweza kumkimbilia. Alifanya kile ambacho binadamu hawezi kufanya.
Alitembea juu ya maji. Vile ambavyo hatuwezi kufanya tumuachie yeye. Wakati
tunapozama kwenye bahari ya matatizo tulie kwa sauti: “Bwana utuokoe !”
Shibisha imani yako na mashaka yako utayakondesha. Imani ikiongezeka
mashaka yanapungua na kinyume chake ni kweli. “Imani si kujaribu kuamini jambo
bila ya kuzingatia ushahidi: imani ni kujaribu kufanya jambo bila kuzingatia
matokeo,” alisema Sherwood Eddy.
“Wanashinda wale wanaoamini
wanaweza,” alisema Virgil. Ni katika mtazamo huo Erasmus alisema, “Amini kuwa
unacho na unakuwa nacho.” Swali kubwa hapa si kuwa una imani au hauna imani.
Jambo la msingi ni imani katika nini na imani katika nani. Ili
kufanikiwa na kushinda unahitaji kuwa na imani katika Mungu na kujiamini hata
ikiwa imani ndogo au haba inatosha kukuondolea vikwazo, vihunzi na vizingiti.
Tunasoma hivi katika biblia, mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. Bwana
akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha
chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao
ungewatii” (Luka 17: 5-6).
Kifungu cha Biblia hicho
kinabainisha ukweli huu, imani kidogo yaweza kufanya mambo makubwa. Ni ukweli
unaoendana na ujumbe wa methali ya Kiswahili, Kidogo kidogo kamba ukatika.
Nguvu ya mbegu haitegemei ukubwa au udogo wake inategemea uhai uliofichwa
katika mbegu hiyo. Kuna nguvu ambayo imefichwa ndani mwako. Kama
ni hivyo unahitaji kujiamini kuwa utaweza kufanikiwa katika maisha. Kwa imani
na kujiamini ndege imevumbuliwa. Kwa imani na kujiamini simu za mkononi
zimegunduliwa. Kwa imani na kujiamini utalaamu wa kutengeneza runinga
umefunuliwa.
Mitume walipoomba kuongezewa
imani, Yesu hakusema nimewaongezea imani. Hakuahidi kuwaongezea imani. Ni kama
aliwaambia anza na mlicho nacho, kidogo huvuta kikubwa, kidogo huzaa kikubwa,
laini huzaa ngumu. Walikuwa kama mfanyabiashara asemaye nina pesa kidogo sana ngoja iwe nyingi
ndipo nianze kufanya biashara. Je, itaongezekaje bila kuzalisha, kuuza na
kununua? Walikuwa kama mkulima asemaye nina mbegu lakini hazitoshi nitalima
nikiwa na mbegu za kutosha. Anza na ulicho nacho. Hawezi kusema sina pesa yote
ya kujenga na kumalizia nyumba. Anza kujenga na pesa uliyo nayo. Ili kuwa na zaidi anza na ulicho nacho. Aliyenacho
ataongezewa ndivyo Bwana Yesu
alivyofundisha.
Imani ni ufunguo wa mafanikio. Na
sifa ya mtu anayefanikiwa ni kuwa ana imani. Imani kamili ndiyo kumtegemea Mungu
na kumtumaini na kumtii. Tukiwa na imani kwa Mungu twaweza kusema, “Bwana ndiye
anisaidiaye, sitaogopa” (Waebrania 13:6). Hatuna budi kuwa na imani na uwezo
Mungu aliotujalia yaani kujiamini. Kuna hadithi juu ya wakristu ambao
walimuomba mchungaji wakati wa ibada wa Jumapili iliyokuwa inafuata waombe
kupata mvua baada ya mvua kutonyesha kwa kipindi cha muda mrefu.
Walishangaa siku hiyo ya maombi ya Jumapili mchungaji aliposema hayuko tayari
kuomba kupata mvua maana watu hawaonyeshi imani kwa vile hawakwenda na miavuli
ya kujikinga mvua. Imani lazima ionekane katika matendo. Ni Mungu nisaidie na
wewe unaweka juhudi na maarifa. Henry Ford alisema, “Kama unaamini unaweza
kufanya jambo fulani au hauamini kama unaweza
kufanya jambo fulani, uko sawa.” Usipoamini kwamba jambo fulani linaweza
kufanyika halitafanyika. Ukiamini litafanyika. Imani inafukuza mashaka kama
mwanga hufukuzavyo giza.
Mashaka yakibisha hodi mlangoni mwako itume imani ijibu mashaka. Sala yetu iwe kama ya kijana mmoja kwenye Biblia, “Naamini, nisaidie
kutokuamini kwangu” (Marko 9: 24).
Yesu anaweza kunyamazisha mawimbi ya matatizo. Tunasoma hivi katika
Biblia: “Ikatokea dhoruba kubwa na mawimbi yakapiga chombo, hata kikaanza kujaa
maji. Naye Yesu alilala usingizi shetrini juu ya matandiko. Wakamwamsha na
wakamwambia, “Mwalimu, huhangaiki tukiangamia? Akaamka, akaukemea upepo,
akaiamuru bahari, “Nyamaza! Tulia!” Upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa (Marko
4: 37-39). Tuwe pamoja na Yesu alale
kwetu tunaposafiri katika bahari ya maisha. Bahari, kama yalivyo maisha yote si
lazima ituchachafye. Mambo yanaweza kuelea na kwenda kwa raha; ikiwa
yanatugeukia basi Yesu hatakosa kutusaidia kwani tunaye karibu. “Yesu
alinyamazisha bahari si kwa kutumia fimbo kama Musa, si kwa kutumia sala kama
Elisha alipokuwa Jordan, na wala si kwa sanduku la agano kama Joshua, mwana wa
Nun kwa sababu hizi wafuasi wake walifikiri kuwa Yesu ni Mungu kweli, lakini
wakati alikuwa amelala walifikiri yeye ni binadamu tu,” alisema Theophil.
Dunia ni bahari yenye mawimbi
inahitaji wanamaji stadi. Duniani kuna mengi sawasawa na bahari. Kuna papa na
nyangumi tena wale wa hatari. Lakini ukweli unabaki: Bahari shwari haitoi wana
maji stadi. Bahari iliyotulia haiwezi kuwatoa wanamaji hodari. Kuna methali ya
Kiswahili isemayo: Bahari haishi zinge. Zinge ni machafuko ya mara kwa mara (mabadiliko
ya ghafla). Bahari daima imo katika mabadiliko wala haitabiriki. Maisha kama
vile bahari yamejawa na mema na maovu na yanapotujia sharti tuwe tayari
kuyakabili. Huko Mkoa wa Kagera nchini Tanzania kuna mashindano ya kupatia
mwaka mpya jina. Mshindi huwa anapewa zawadi. Kuna mwaka ulioitwa kwa lugha ya
Ruhaya “Galaziwa enzii” maana yake:
“Ataogelea mwanamaji stadi”. Nchi ilikuwa katika matatizo makubwa ya kiuchumi
baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda miaka ya 1978 na 1979. Matatizo hayo
ni kama mawimbi kwenye bahari. Kuvuka mwaka huo kulilinganishwa na kuvuka
bahari na ni mwanamaji stadi alitegemewa kuvuka. Mfano huo unaipa nguvu falsafa
hii: DUNIA NI BAHARI inahitaji wanamaji stadi.
Watoto wasipopata malezi mazuri
familia inakuwa ni mtumbwi unaoyumbishwa na mawimbi. Watoto wanahitaji
kueleweshwa. Mfano kuna mtoto aliyefungua chumba cha wazazi wake bila kubisha
hodi. Baba akupenda jambo hilo. Akamwambia. “Kila unapotaka kufungua mlango
wowote ule, lazima ubishe mlango kwa kusema, hodi hapa!” Siku moja baba huyo
alimtuma mtoto akalete soda toka friji au jokufu . Baada ya kumgonja dakika
kumi mtoto bila kurudi. Baba alienda kutazama kulikoni. Akamkuta mtoto anabisha
kwenye mlango wa friji akisema. “Hodi hapa! Hodi hapa!” Biblia inasema, “NAYE
YESU AKAENDELEA KUKUA KATIKA HEKIMA NA KIMO; AKAZIDI KUPENDWA NA MUNGU NA WATU”
(LUKA 2: 52). Muombee mtoto wako azidi kukua katika hekima, azidi kupendwa na
Mungu na watu.
Tunapozungumzia bahari kuwa na
picha ya vurugu, machafuko, ghasia, fujo. Ni picha hiyo tunasoma kitabu cha
Mwanzo: “Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia. Dunia ilikuwa bila umbo na
tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa
ikitanda juu ya maji” (Mwanzo 1:1-2). Tunapozungumzia bahari kuwa na picha ya
maharamia wa kisomalia wanaoteka meli baharini. Kuwa na picha ya meli ya
maharamia. Tunapozungumza mambo ya maji kuwa na picha ya Kisiwa cha Migingo na
vita vya maneno vinazunguka kisiwa hicho. Kuwa na picha ya kuzama kwa meli ya
RMS Titanic. Usiku wa tarehe 14 Aprili 1912 meli hiyo ilikuwa ikitokea
Uingereza na kuelekea jiji la New York ilipogonga mwamba wa barafu ilizama
baadaye baada ya masaa 2 na dakika arobaini na tano usiku wa kuamkia tarehe 15
Aprili 1912. Watu walioaga dunia ni 1, 517. Waliokoka ni watu 706. Jumla ya
watu walikuwa ni 2,223. Huko Tanzania mwaka 1996 meli ya MV BUKOBA ilizama
katika ziwa Victoria watu zaidi ya 700 waliaga dunia.
TUFANYE NINI ILI KUKABILIANA NA MAWIMBI YA
MATATIZO KATIKA BAHARI
Yesu alikuwa na sehemu tatu za
kutafuta usalama, sehemu tatu za kupumzika: kwenye mtumbwi, mlimani na
jangwani. Alipokuwa amezungukwa na watu wengi sana na alipohitaji kupumzika
alienda sehemu mojawapo. Tunahitaji kupumzika na Yesu. Lakini zaidi ya hayo
tunahitaji yafuatayo:
1. KABILI MAWIMBI KWA UTULIVU
BILA HOFU
Tukiona mawimbi tunakuwa na hofu,
pengine hofu kubwa inatuingia ghafla. Hakuna kufikiri sawa sawa. Tunahangaika,
tunakuwa na wasiwasi kama wafuasi wa Yesu kwenye mtumbwi. Watu wana namna
mbalimbali za kujiliwaza. Siku moja baba mmoja kijana alikuwa anamsukuma mtoto
wake ambaye alikuwa akilia kwenye kigari cha watoto. Aliendelea kusema, “Tulia
Donald. Nyamaza sasa, Donald. Mambo yatakuwa shwari, Donald.” Mwanamke
aliyekuwa akipita alimwambia baba huyo, “Unajua namna ya kumbembeleza mtoto
ambaye analia kwa utulivu na pole pole.” Mwanamke huyo aliinama kwenye kigari
na kuanza kusema “Unasumbuliwa na nini Donald.” Baba yake aliingilia kati
haraka, “Hapana, hapana yeye ni Henry! Mimi ni Donald.!” Mama huyo akauliza,
“Mbona ulikuwa ukimbembeleza aache kulia ukimwita Donald!” “ Nilikuwa
ninajibembeleza mimi mwenye moyoni ninalia kama mtoto huyu!”
KABILI MAWIMBI YA MAWAZO MABAYA
KABILI MAWIMBI YA MAHUSIANO MABAYA
KABILI MAWIMBI YA KUSHINDWA
KABILI MAWIMBI YA MATARAJIO KUVUNJIKA
2. YESU NI JIBU: MWAMBIE AKUSHIKE
MKONO
“Yesu alinyamazisha bahari si kwa
kutumia fimbo kama Musa, si kwa kutumia sala kama Elisha alipokuwa Jordan, na
wala si kwa sanduku la agano kama Joshua, mwana wa Nun kwa sababu hizi wafuasi
wake walifikiri kuwa Yesu ni Mungu kweli, lakini wakati alikuwa amelala
walifikiri yeye ni binadamu tu,” alisema Theophil.
3. MATATIZO MAKUBWA YANAHITAJI
IMANI KUBWA
Nyakati za kujaribiwa imani ni
nykati za kuimarisha imani. “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa
kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna
mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko
dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto” (1 Pet 1: 6-7).
4. JUA KUWA YANA MWISHO
Mateso, shida, matatizo yana
mwisho. Mateso hayana kauli ya mwisho. Furaha ina kauli ya mwisho. Katika
kitabu cha Ufunuo tunasoma hivi: “Kisha, nikaona mbingu mpya na dunia mpya.
Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari
pia haikuwako tena” (Ufunuo 21: 1). Bahari haikuwako tena. Mawimbi ya matatizo
hayakuwako tena.
5. JIANDALIE SIKU MBAYA
“Umkumbuke Muumba wako siku za
ujana wako kabla hazijaja siku mbaya wala haijakaribia miaka utakaposema: ‘Sina
furaha katika vitu hivyo” (Mhubiri 12:1). Sasa ndio wakati wa kujenga msingi
katika Mungu. Sasa ndio wakati wa kuanza ukurasa mpya na sura mpya. Sasa ndio
wakati wa kujiwekea bonga pointi mbinguni. “Kwa hiyo, kila mtu anayesikia
maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba
yake juu ya mwamba. Mvua zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka
kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba” (Mathayo 7: 24-25).
6. KWEPA PICHA HASI FIKIRIA PICHA
KUBWA NA PICHA CHANYA
Kwepa picha hasi ya mambo: kwa
nini mimi tu nataabika, Mungu ananiadhibu. “ Maisha yangu yamekwisha kwa
machozi; naam, miaka yangu kwa kulalamika. Nguvu zangu zimeniishia kwa
kutaabika; hata mifupa yangu imekauka” (Zaburi 31: 10).