SIKUKUU YA KUTUKUKA MSALABA
JUMAPILI YA 24 YA MWAKA A
“Hakuna msalaba, hakuna Mkristo,”
alisema Profesa Mchungaji Daniel
Deutschlander wa Ujerumani. Msalaba ni kitambulisho cha mkristo. “Muumini
yeyote ambaye hajaukabili msalaba, bado hajawa mfuasi wa Kristo,” alisema S. E. Entsua-Mensah mchungaji anayeishi
Kumasi Ghana. Msalaba unavyotumika hapa haumaanishi mti bali mateso, matatizo, shida,
udhia, karaha, sononeko, huzuni na maumivu. Binadamu naye anaweza kuwa msalaba
licha ya kuwa neema. Mtoto anaweza kuwa msalaba kwa mzazi. Mke anaweza kuwa
msalaba kwa mumewe. Mume anaweza kuwa msalaba kwa mke wake. Wajibu kwa umma na
kwa Mungu ni msalaba. “Daima imani hubaki kuwa jambo la msalaba,” ameandika
hivyo Papa Francis Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki kwa sasa katika kitabu
chake Furaha ya Injili. Kuna mke wa mtu alipata ujumbe kwenye simu ya
mkono toka kwa mpango wa kando au nyumba yake ndogo uliosema hivi:”Nimekuacha
tangia leo.” Mwanamke huyo akaanza kulia. Mme wako akamuuliza: “Ni ujumbe gani
huo uliosoma halafu unaanza kulia.” Mwanamke akasema: “Ni ujumbe kuhusu namna
ya kupika.” “Sasa kuna jambo la kukufanya ulie?” Mwanamke akasema: “Nimefikia
kwenye sehemu ya kukata vitunguu. Na unajua vitunguu vinafanya mtu atoke
machozi.” Usanii wa namna hiyo ni msalaba. Mwanamke wa namna hiyo ni msalaba.
Wasafiri nao wanaweza kuwa
msalaba. Methali ya Kiswahili inasema yote: Msafiri kafiri. Kuna mtu amenitumia
ujumbe huu kwenye simu ya mkononi: “Jamaa alikuwa kwenye daladala (Matatu)
pembeni kuna dada mrembo kaka. Kamlia timing
kwa muda kisha halafu akamuuliza ‘Samahani dada unaitwa Google?” Dada akamjibu: “Hapana, kwa nini umedhani naitwa hivyo?”
Jamaa: “Una kila kitu ninachokitafuta.” Msafiri mwenzako anaweza kuwa msalaba.
Swali linabaki tubebeje msalaba?
Tusiubebe kwa manung’uniko. Wana wa Israel baada ya Mungu kuwatendea miujiza
walipopata na matatizo walinung’unika: “Njiani watu wakakata tamaa.
Wakawanung’unikia Mungu na Musa. ‘Kwa nini mmetutoa Misri tuje tufe huku
jangwani? Maana huku hakuna mkate wala maji; tumechoka na chakula hiki dhaifu!”
(Hesabu 21: 4-5). Chakula walikuwa nacho lakini walikiita dhaifu. “Maelekeo yetu tukiwa kwenye mateso ni
kumgeukia Mungu. Ni kuwa na hasira na kuwa wakali na kuikunjia mbingu ngumi na
kusema, ‘Mungu, haujui mateso yanavyofanana! Uelewi! Hauna wazo lolote juu ya
yale ninayoyapitia. Uelewi ni kwa kwa kiwango gani inahumiza.’ Msalaba ni njia
ya Mungu ya kuondoa mashitaka yetu, visingizio na hoja zetu kwake. Msalaba ni
Mungu anachukua mwili na damu na kusema, ‘Na mimi pia,” alisema Mchungaji Rob
Bell (Alizaliwa mwaka 1970. Alitajwa mwaka 2011 na gazeti la Time
Magazine la Amerika kuwa ni mmoja kati ya watu 100 duniani wenye ushawishi
mkubwa).
“Mateso yanatualika kuweka
maumivu yetu katika mikono mikubwa. Katika Kristu tunamwona Mungu akitutesekea.
Na kutualika kushiriki katika upendo wa Mungu unaoteseka kwa ajili ya ulimwengu
unaohumiza . Maumivu yetu madogo na yanayotuzidi nguvu ya maisha yetu
yanaunganishwa kwa ukaribu sana na maumivu makubwa ya Kristo. Mateso yetu ya
kila siku yanatia nanga katika mateso makubwa na kwa hiyo kuna matumaini
makubwa,” alisema Padre Henri J.M.
Nouwen
Ubebe kwa uvumilivu na subira
bila kutarajia matokeo ya mara moja. Papa Francis amekuwa na haya ya kusema
katika kitabu chake Furaha ya Injili:
“Shauku inayokithiri iliyopo leo hii kuhusu matokeo ya mara moja inawafanya
wahudumu wa uchungaji waone vigumu kuvumilia jambo lolote linaloonekana kama
vile linakosa makubaliano, lina uwezekano wa kushindwa, kuna maoni ya upinzani,
ni msalaba.” Jani la chai likiwa kwenye maji moto linabadili rangi ya maji. Badili
mambo kwa uvumili wako. Huko ni kubeba vizuri msalaba. Stempu haitoki kwenye
bahasha mpaka bahasha imemfikia mlengwa. Huu ni mfano wa kubeba msalaba kwa
uvumilivu. Yesu hakushuka toka
msalabani.
Ubebe bila kukata tamaa na kwa
upole. Papa Francis ameandika hivi katika kitabu chake, Furaha ya Injili: “Pamoja na
kutambua unyonge wetu kwa uchungu mkubwa, ni lazima tusonge mbele bila kukata
tamaa, tukizingatia kile ambacho Bwana alimwambia Mtakatifu Paulo: “Neema yangu
inakutosha, maana nguvu yangu hufanywa kuwa kamilifu katika udhaifu’ (2 Kor
12:9). Daima ushindi wa Kikristo huwa ni msalaba, lakini ni msalaba ambao
wakati huo huo ni bendera ya ushindi inayobebwa kwa upole wenye guvu dhidi ya
mashumbulizi ya uovu.” Tumebebe msalaba kwa upole na matumaini. Kuubeba vizuri msalaba ni kufikiria juu ya
wengine badala ya kufikiria juu ya mateso yako tu. “Ingawa Yesu alikuwa katika
mateso msalabani, alifikiria juu ya kuwaombea watesaji wake, kutunzwa kwa mama
yake, kuratibisha wokovu wa mwizi,” alisema Thomas Dubay. Akili yako unapoiweka
kwenye mateso ya wengine inasaidia kubeba vyema ya kwako. “Msalaba ni mahali
ambapo mbingu inakutana na dunia na neema inalipuka. Msalaba sio mahali ambapo
Yesu anakabili mateso yetu tu, bali anakuwa mateso yetu ili kubadilisha dunia,”
alisema Mchungaji Matt Farlow wa Kanisa la New Wine, New Wineskins. Tubebe
msalaba kwa hekima tukitafuta suluhisho la matatizo. Tubebemsalaba kwa upole
hasira haisahidii. Tubebe msalaba kwa imani. Tubebe msalaba kwa uvumilivu
tukitafuta suluhisho la matatizo.
NYOKA WA SHABA AL
IYEINULI WA NA MWANA WA MTU AL IYEINULIWA
Kuna kitendawili kisemacho:
“Viwili vyafanana”. Jibu ni Meli na Pasi. Viwili vyafanana ni nyoka wa shaba
aliyeinuliwa, aliyetundikwa na Mwokozi aliyeinuliwa. “Kama vile Musa
alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa mtu atainuliwa juu
vivyo hivyo ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele. (Yohane 3:14) Mwinjili
Yohane hueleza nyoka wa shaba kama mfano wa
Kristo aliyeinuliwa msalabani. Tunasoma
hivi katika kitabu cha hesabu, “Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, “Mbona
mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana
chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu”. Bwana
akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea
Musa, wakasema, “Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe;
utuombee kwa Bwana atuondolee nyoka hawa”. Basi Musa akawaombea watu. Bwana
akamwambia Musa, “Jifanyie nyoka wa shaba ukamuweke juu ya mti, na itakuwa kila
mtu aliyeumwa aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya
mti; hata ikiwa nyoka amemuuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi”
(Hes.21 :4-9).
UFANANO
Nyoka wa shaba hakuwa wa sumu,
ingawa alikuwa na sura ya nyoka. Ingawa Yesu alionekana kama mnyang’anyi, alionekana
kama mdhambi hakuwa na dhambi. “Hapakuwa na hila kinywani mwake” (Isaya 53:9).
Kama nyoka wa shaba alivyoinuliwa Yesu aliinuliwa msalabani. Aliyemtazama nyoka
alipona. Majeraha ya sumu yalitibiwa. Yesu anatibu majeraha ya dhambi. Ingawa
nyoka wa shaba alikuwa ni nyoka lakini ni wa shaba. Yesu alikuwa mtu lakini ni
Mungu,ni Mungu mtu.
TOFAUTI
Zipo tofauti kati ya nyoka wa
shaba aliyeinuliwa na Yesu aliyeinuliwa. Jukwaa la nyoka aliyeinuliwa ni
jangwa. Jukwaa la Yesu aliyeinuliwa ni Kalvari. Watazamaji upande wa nyoka wa
shaba ni wana wa Israeli. Upande wa Yesu aliyeinuliwa ni dunia nzima. Jamii
yote ya binadamu inamtazama Yesu msulubiwa. Wana wa Israeli waliomtazama nyoka
aliyeinuliwa walitibiwa kimwili baadaye, miaka kupita, siku kupita walikumbwa
na kifo cha kawaida. Kifo hakina kalenda na hakuna atakayesahaulika. Yesu
aliyeinuliwa hatibu tu magonjwa ya kimwili na ya kiroho pia. Yeyeanatoa maisha
ya milele.
KUTAZAMA NI KUSADIKI
“Kutazama” katika Injili ya
Yohane kuna maana ya kusadiki. Kumtazama Yesu aliyeinuliwa ni kumsadiki.
“Watamtazama yeye waliyemchoma” (Yohane 19:37). Akida wa kirumi ni mfano wa
wapagani waliomsadiki Yesu kwa kumtazama. “Basi yule akida, na hao waliokuwa
pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo
yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu”
(Mt. 27:54). Kuamini siyo kutaja maneno ya kanuni ya imani bali kuyaishi.
MATATIZO NI MSALABA
“Katika
nchi yangu kwanza unakwenda gerezani halafu unakuwa rais baadaye,” alisema
Hayati Nelson Mandela aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 95. Wajibu wa
Hayati Nelson Mandela kwa umma na uzalendo vilikuwa ni msalaba. Aliuchukua
msalaba huu ukamchukua hadi ikulu. Kuna upande mzuri wa msalaba kama matatizo.
Ni katika msingi huu Yesu alisema: “Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata,
hanistahili” (Mathayo 10: 36). “Huwezi
kukwepa msalaba, popote unapokimbilia; popote unapokwenda, kila mara utaukuta.
Ukiuchukua msalaba kwa kuupenda, utakuchukua na kukupeleka unapopatamani: yaani
kule ambapo patakuwa na mwisho wa mateso, ingawa hapa hakuna mwisho wa mateso.
Ukiuchukua bila kupenda, unaufanya uwe mzigo kwako kuchukulika…ukiuutupa kwa
nguvu msalaba mmoja bila shaka utakutana na mwingine labda mzito zaidi,”
alisema Thomas á Kempis.
Picha ya matatizo kama msalaba
tunaipata katika sala ya Kanisa Katoliki ambayo husaliwa Ijumaa Kuu na kipindi
cha Kwaresima: “Ee Yesu mkarimu, mimi pia ninao msalaba wangu: jirani zangu,
mwenzangu wa ndoa, watoto, wazazi wangu, kazi zangu, joto, baridi, njaa,
kiu,,, vishawishi, magonjwa na matatizo mengine ya maisha, wajibu wangu
kwa Mungu, kwa umma na kwa Kanisa hayo yote ni msalaba. Unipe ukarimu wako ee
Yesu, niyapokee bila kunung’unika na kuyabeba vema.”
Mwenzako wa ndoa anaweza kuwa msalaba.
Kuna mwanaume aliyemsikia mchungaji anahubiri juu ya maneno ya Yesu: anayetaka
kuwa mfuasi wangu abebe msalaba wake na anifuate. Mwanaume alipofika nyumbani
alimbeba mke wake. Akampitisha sebuleni, bafuni, jikoni, barazani. Mwanamke
alishangaa na kusema: ulinibeba siku ya kufunga ndoa. Mchungaji amefundisha
nini Kanisani unanibeba namna hii leo hii. Mwanaume huyo alisema: mchungaji
amefundisha tubebe misalaba yetu.
Usijitengenezee msalaba. Kuna misalaba ya
kujichongea. Kujiingiza kwenye mambo ya watu wengine, sio kwa sababu ya Yesu. Ukisikia
mwanamke anasema sitaolewa tena na mwanamme huyu. Usiijiingize katika ugomvi
wao na kuanza kuchochea. Ni kama kusema shuka kutoka kwenye msalaba wa ndoa.
Ukipata matatizo huko umejiingiza kwenye ndoa ya watu si kujenga bali kubomoa.
Ndugu wakigombana chukua jembe ukalime wakipatana chukua kapu ukavune.
Usichochee ugomvi kati ya ndugu wakipatana watakugeuka na wewe utakuwa
umejichongea msalaba. Wasaidie kupatana. Usichochee mafarakano. Kuwa na kiburi
ni kujitengenezea msalaba. Kutukana watu ni kujitengenezea msalaba.
Kuna kijana wa miaka thelathini
aliyemua baba yake na mama yake. Baada ya kutolewa hukumu aliulizwa kama
anaweza kujitetea. Aliomba kupunguziwa miaka akiota hoja yeye ni mwana yatima hana baba wala mama. Huu ni
msalaba wa kujitakia sio kwa sababu ya Yesu. Kuna aina mbili za misalaba:
msalaba wenye Yesu Kristu na msalaba usio na Yesu Kristo. Msalaba wenye Yesu ni pale ambapo unatazama
matatizo yako kwa kutumia miwani ya Yesu yaani hakuna Jumapili ya Paska bila
Ijumaa Kuu. Ripoti kwa Yesu matatizo yako. Mweke Yesu katika matatizo yako.
Msalaba usio na Yesu ni pale ambapo unashindwa kuripoti matatizo yako kwa Yesu.
Haubebi mtazamo wa Yesu wa Ijumaa Kuu kwanza Jumapili ya Paska baadaye.
Matatizo ni m\salaba. Kuna ishara
ya msalaba. Matatizo yanaweza kuwa ishara ya mafanikio siku za mbeleni. Dalili
ya mvua ni mawingu. Dalili ya mafanikio inaweza kuwa matatizo. Kabla ya kufika
bandarini kuna mawimbi makali na makubwa. Unaweza kuwa mtu mwema lakini ukateseka.
Kwa nini watu wema huteswa na wengine au na jirani. Jirani yako anaweza kuwa
msalaba. Sababu ni kuwa watu wema wanafanya mambo mazuri tofauti na wengine. Watu
kama hawakuelewi watakutesa. Utendaji kazi wa watu wema unawaibisha wavuvi.
Watu katika ofisi wakiamua kubadili
mambo ofisini na wewe haushiriki watakutukana. Watu wema ni kikwazo kwa
mipango ya watenda maovu. Utasikia watu wanasema ficha ficha, fulani amekuja.
Watu wema hawabadili misimamo yao. Mfano wa Danieli. Mfalme alitaka Danieli
abadili msimamo wake. Hakubadili. Alitupwa katika shimo la simba. Lakini kwa
mihujiza Mungu alimtoa. Ukiubeba msalaba vizuri utakubeba. Mwanamke anamkataa
bosi na kumwambia mme wangu ananitosha na kuniridhisha. Ofisini mwanamke huyo
anateswa sababu ya msimamo wao, kwa sababu ya jina la Yesu. Aliapa Kanisani kwa
jina la Yesu. Akibeba vizuri msalaba. Msalaba utambeba.