JUMAPILI YA 3 YA MAJILIO
1. Isa 61:
1-2. 10-11
|
2. 1 Wath 5: 16 -24
|
3. Yoh 1: 6-8. 19-28
|
Mungu wetu ni Mungu anayetaka uwe na
furaha daima. Kufurahi ni wajibu. Una mawazo unayowawazia watu lakini Mungu
anakuwazia mambo mazuri. Furahi kila wakati. Unafikiria watu Mungu
anakufikiria. Furahi kila wakati. Tunapofanya tunaloweza, Mungu atafanya
tusiloweza. Kwa namna hiyo tunaye Mungu anayeleta furaha. Furahi kila wakati. Jumapili
hii katika Kanisa Katoliki inaitwa Jumapili
ya Furaha. Furahi
kwa kilatini “Gaudete.” Hatuna budi kufurahi sababu Yesu Kristo atazaliwa
mioyoni mwetu siku ya Krismasi. Mtume Paulo anatushauri kwa msisitizo. ““Furahini
kila wakati” (1 Wathesalonike 5:16). Pia mtume Paulo anasisitiza mahali
pengine. “ Basi,
furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: furahini!” (Wafilipi
4:4).
Wito ni furahi kila wakati. Katika insha moja
iliandikwa kuwa mtoto anacheka mara 200 kwa siku. Mtu mzima anacheka mara 4 kwa
siku. Kitabu cha mhubiri kinasema kuna wakati wa kucheka na wakati wa kulia.
Kwa nini tofauti hii1. kubwa kati ya mtoto na mtu mzima? Furaha haitegemei
mahali ulipo. Adamu na Eva walikuwa kwenye Bustani ya Eden, lakini baadaye
hawakuwa na furaha baada ya kumkosea Mungu. Lucifer kadiri ya masimulizi ya
maandiko matakatifu aliyekuwa mbinguni alimkosea Mungu na kukosa furaha.
Alitumuliwa huko. Alikuwa mbinguni
hakuwa na furaha. Mtume Paulo anatualika, “Furahini kila wakati” (1
Wathesalonike 5:16). “Wanasema mtu anahitaji mambo matatu kuwa na furaha kweli
katika dunia hii: nafsi ya kupenda, kitu
cha kufanya, na jambo la kutumainia,” alisema Tom Bodet.
Hakuna mtu anayependa Krismasi imkute kifungoni au
jela. Taarifa ambazo huwa tunazipata toka zahanati na hospitalini ni kuwa
wakati wa Krismasi wagonjwa wanapungua wadini. Hakuna ambaye anapenda Krismasi
imkute wadini. Lakini ugonjwa haubishi hodi na hauna kalenda. Kipindi cha
Krismasi ni kipindi cha kufurahi. Mtume Paulo anatukumbusha, “ Basi, furahini
daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: furahini!” (Wafilipi 4:4).
Krismasi inakaribia furahini. Mtume Paulo alipoandika barua kwa wafilipi mnamo
mwaka 55 baada ya Kristo kuzaliwa alikuwa kifungoni. Licha ya kuwa katika
matatizo alivaa vazi la furaha.
Daraja kati ya furaha na mateso sio ndefu. Wakati
mwingine kuna furaha baada ya mateso. Kama tusemavyo, baada ya dhiki faraja.
Kuna watu ambao wana furaha, wengine wana mateso. Baadhi ya watu wanakaa na
kicheko na tabasamu utafikiri wana matangazo ya biashara ya dawa ya meno
wanayotumia. Wengine wanakuwa na ndita za hasira usoni. Kuna ambao wanaambiwa
usicheke uko kanisani. Kuna methali zinazobainisha ukweli huu: furaha ya mwenye
meno, kibogoyo hashiriki, furaha ya kima mbwa hashiriki. Tofauti hizi
zinatufanya tujiulize nini chemchemi ya furaha? Kwa wakatoliki Jumapili hii
kabla ya Krismasi inaitwa Jumapili ya Furahi kwa kilatini “Gaudete.” Hatuna
budi kufurahi sababu Yesu Kristo atazaliwa mioyoni mwetu siku ya Krismasi.
Mtume Paulo anatushauri: “Furahini kila wakati. Salini bila kuchoka. Fanyeni
shukrani katika yote” (1 Wathesalonike 5:16-18). Katika haya hii ya Biblia
tunapata chemchemi ya furaha.
Kuthamini mtu na kushukuru kunaleta furaha. Unaposhukuru
mtu ina maana unathamini zawadi yake naye unamthamini. Katika msingi huu
unaweza kusema furaha yako ni furaha yangu. Furaha ya mwenzako iwe furaha yako.
Katika msingi huu methali ya Kiswahili inasema, “Mzazi yeyote hufurahi amwonapo
mtoto wake akicheka. Methali hii hutufunza kuwa mzazi yeyote humthamini mtoto.
Kila mzazi hufurahi mwanawe anapoishi maisha ya furaha. Usipende pesa
ukawatumia watu bali upende watu utumie pesa. Kwa maneno mengine thamini watu
upate ya watu. Thamini watu upate furaha.
FURAHA IPO KATIKA KUPENDA NA KUPENDWA
Nafsi ya kwanza ya kupenda ni
Mungu. Katika hili Mtakatifu Augustini alisema, “Hatutulii tutatulia katika
Mungu.” Katika Mungu kuna furaha kamili. Kupendwa na Mungu ni furaha. Kumpenda
Mungu ni furaha. Mungu huyu amejificha kati yetu. Yohane anasema, “katikati
yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi” (Yohane 1: 26). Katika Yesu Kristo Mungu
amevaa ubinadamu wetu. Mungu wetu ni “Mungu aliyejificha.” Lakini anatufanyia
makubwa nyuma ya pazia. Ni kama Mwandishi wa maisha ya mtu mwingine. Haonekani
katika kitabu lakini anafanya mambo mengi. Kuna watoto ambao walikuwa wanacheza
mchezo wa kujificha. Mtoto mmoja alipojificha hawakwenda kumfichua. Alipotoka
kwenye maficho akakuta wanaendelea na mchezo mwingine. Mungu amajificha.
Amejificha katika viumbe vyake mpaka watu tunachoka kumtafuta. Tunaambiwa “katikati
yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi” (Yohane 1: 26). Yupo kati ya wagonjwa.
Yupo kati ya maskini. Yupo kati ya wageni.
Kutulia katika Mungu ni chemchemi ya furaha.
Mtakatifu Augustini wa Hippo Afrika ya Kaskazini alisema, “Wewe umetufanya kwa
ajili yako mwenyewe na mioyo yetu haitulii mpaka inapotulia ndani yako.”
Tutakuwa na furaha kamili na ya kweli tutakapotulia katika Mungu, katika
kutimiza mapenzi na amri za Mungu. Andika mipango yako kwa kalamu ya mtI Mungu mwenyewe ana mfutio. Msemo
wetu uwe Bwana akipenda au msemo maarufu wa kiarabu Inshallah. Inatupasa
kusema, “Bwana akipenda tutakuwa wazima bado na kufanya hiki na hiki” (Yakobo
4:15). Chemchemi ya furaha kamili haitokani na matukio yanatokea au mazingira
tuliyomo. Inatoka katika Mungu anayekuwa ndani mwetu. Kutulia katika Mungu
kunahitaji unyenyekevu. Kuna kijiji kimoja kilivamiwa na watu wakatili kuna
mtoto wa miaka kama kumi na mawili ambaye alikuwa mlemavu wa miguu. Hivyo
wazazi walipokimbia hakuwa na uwezo wa kukimbia walimwambia akae kama amekufa
hivi. Hivyo aliachama. Maadui walipofika walishangaa usafi wa meno yake
wakasema huyu amekufa lakini ana meno mazuri na masafi sijui anatumia dawa gani.
Mtoto huyu akasema, “Natumia colgate.” Majivuno yalimuingiza hatarini wakajua
hajafa. Nyenyekea ule vya Mungu na watu. Kukiri hali ya kumtegemea Mungu ni
msingi wa furaha. Mungu ni nguvu yako. Mungu ni ngome yako.
Nafsi ya pili ya kupenda ni mtu
mwingine au watu wengine. Kupendwa na watu ni furaha. Kupenda watu ni furaha. Ya
mwisho ni nafsi yako. Kuwapenda wengine kama ambavyo unajipenda ni furaha.
FURAHA IPO KATIKA MATENDO MEMA
Furaha ipo katika kufanya kitu
fulani hasa kutenda wema. “Furaha sio kitu ambacho kimetengenezwa tayari.
Kinatoka katika matendo yako,” alisema Dalai Lama XIV. Matendo yanayozungumziwa
ni matendo mema. Mtume Paulo anazidi kutuasa, “Kagueni yote: yaliyo mema
yashikilieni. Mabaya ya kila namna yaepukeni” (1 Wathesalonike 5: 22). “Ukifanya
mambo mazuri, watu watakushitaki kuwa una nia ya kujinufaisha iliyofichika,
fanya mazuri vyovyote vile. Kama umefanikiwa,utajipatia marafiki ambao sio wa
kweli na maadui kweli, fanikiwa vyovyote vile. Zuri utakalofanya leo
litasahuliwa kesho, fanya jambo zuri vyovyote vile. Ukweli na uwazi vinaweza
kukufanya udhuriwe. Kuwa mkweli na muwazi
vyovyote vile. Watu wakubwa wa
kike na kiume wenye mawazo makubwa wanaweza wanaweza kushushwa na watu wadogo
wa kiume na kike wenye mawazo madogo. Fikiria makubwa vyovyote vile. Watu huwapenda
watu wanaoonewa lakini huwaiga washindi tu. Pigania wanaoonewa vyovyote vile. Unachotumia
miaka mingi kujenga kinaweza kuharibiwa
usiku mmoja. Jenga kwa vyovyote vile. Watu wanahitaji msaada kweli lakini
wanaweza kukushambulia kama ukiwasaidia. Wasaidie vyovyote vile. Ipe dunia zuri
ulilonalo utakabiliana na upinzani. Ipe dunia zuri kwa vyovyote vile,”
aliandika Kent M. Keith. Katika kuwasaidia wengine kuna furaha. Kuna methali ya
Kichina isemayo, “Ukitaka furaha kwa
saa, lala. Ukitaka furaha kwa mchana wote, nenda kuvua. Ukitaka furaha kwa
mwaka mmoja urithi mali. Ukitaka furaha kwa maisha yako yote, saidia mtu.”
FURAHA IPO KATIKA MATUMAINI
Kuwa na jambo la kutumainia
kunaleta furaha. Mgonjwa akiwa kwenye chumba cha kungojea daktari wakimwambia
kuwa daktari atakeyemtibu ni daktari bingwa, anakuwa na matumaini na matumaini
hayo yanamletea furaha. Sasa hivi wakristu wanatumainia baraka na neema za
Krismasi jambo kubwa zaidi Yesu azaliwe katika mioyo yao. Lakini katika mateso na shida tunaweza kuwa na
furaha. “Ni vigumu kusahau maumivu, lakini ni vigumu zaidi kukumbuka utamu.
Hatuna makovu ya kuonesha furaha. Tunajifunza machache kutoka kwenye amani,”
aliandika Chuck Palahniuk katika Diari yake.
FURAHA IPO KATIKA MAWAZO CHANYA
“Sio kile ulichonacho, au cheo
ulichonacho au mahali ulipo panakufanya uwe na furaha. Ni kile unachofikiria juu
yake,” aliandika Dale Carnegie. Furaha inakutwa katika kusema ndiyo ikawa ndiyo
kweli na hapana ikawa hapana kweli. “Furaha ni pale unachofikiria, unachokisema
na unachokitenda vinapatana kikamilifu,” alisema Mahatma Gandhi. Zaidi ya hayo
furaha ni suala la mtazamo chanya.
GHARAMA YA FURAHA
Tukumbuke kuwa furaha inapatikana
kwa gharama. Wanaoenda kupanda kwa machozi. Watavuna kwa kelele za shangwe. “Tunapotaka
kuifikia furaha ya kweli kwa bei rahisi, tutaikuta imefungwa kama kitu cha bei
rahisi,” aliandika David Roberts katika
kitabu chake, “The Grandeur and Misery of
Man, 1955. Vya bei rahisi huenda visilete furaha. Ni katika msingi huu Yesu
alisema anayetaka kunifuata ajitwike msalaba wake anifuate.
KUSHIRIKISHANA FURAHA
Furaha ni kamili
unapowashirikisha wengine. “Furaha ndilo jambo pekee ambalo linaongezeka mara
mbili unapowashirikisha wengine,” alisema Albert Schweitzer. Maneno hayo
yalikwekwa namna nyingine na Ralph Ingersoll, “Njia ya kuwa na furaha ni
kuwafanya wengine wawe na furaha.” “Furaha ni ya kweli tu wengine
wanapoishiriki,” alisema Jon Krakauer
FURAHA IPO KATIKA FADHILA
Furaha ipo katika kuwa na
fadhila. Unataka kuwa na furaha kuwa mpole. “Kwa kila dakika unayokasirika
unapoteza sekunde sitini za furaha,” alisema Ralph Waldo Emerson. Unataka kuwa
na furaha, kuwa na kiasi. Unataka kuwa na furaha kuwa na shukrani. Kiasi ni
chemchemi ya furaha. Kiasi ni fadhila inayoratibu mvuto wa furaha. Fadhila
inakuwa katikati. Furaha ni kituo cha njiani kati ya mengi sana na
machache sana. Mfano unyenyekevu upo katikati ya majivuno na
kujidhalilisha ambako ni kujinyenyekesha kupita kiasi. Ukarimu upo katikati ya
uchoyo na kutapanya hovyo. Kutapanya hovyo ni ukarimu uliozidi mipaka. “Majonzi
yanaweza yakajishughulikia yenyewe, lakini kupata thamani yote kabisa ya furaha
lazima uwe na mtu wa kugawana naye,” alisema Mark Twain.