Jumapili
ya 5 ya Paska
1.
Mdo
14: 21-27
|
2.
Ufu
21: 1-5a
|
3.
Yn
13: 31-33a.34-35
|
“Waliwaimarisha wafuasi roho na kuwatia moyo “ (Mdo 14: 22)
“Hivyo watu wote watawatambua kuwa wafuasi wangu, mkipendana”
(Yohane 13:34-35).
MUHTASARI
·
Upendo
unaonekana katika ukaribu wa mioyo
·
Upendo
unaonekana katika matendo na vipaumbele
·
Upendo
unaonekana katika maneno ya kutia moyo
·
Upendo
unaonekana katika kumbukumbu
·
Upendo
unaonekana katika mahusiano
·
Upendo
unaonekana katika zawadi au kutoa
·
Upendo
unaonekana katika kusikiliza
Upendo unaonekana katika ukaribu wa mioyo. Palipo na upendo mioyo
imekaribiana. Mioyo imeshibana. Wanaopendana ni wataalamu wa moyo. “Mtu yeyote
anaweza kuwa mtaalamu wa moyo. Sharti pekee ni kumpenda mtu fulani,” alisema
Angie Papadakis. Moyo wa Mtume Paulo na moyo wa Barnaba ilikuwa imekaribiana.
Walipendana. Walishibana. Walikuwa wataalamu wa moyo. Jambo hilo linaonekana. Kuna
methali ya Tanzania isemayo, nyumba hupakana lakini mioyo haipakani. Upendo
unaonekana jinsi tunavyozungumza. Kwamba mioyo inapakana ni jambo linaloonekana
kwa namna tunavyozungumza. Profesa alikuwa anatoa mafundisho juu ya haya hii: “Jibu
pole hutuliza ghadhabu, bali neno kuhumiza huchochea hasira” (Mithali 15: 1). Profesa
aliwauliza wanafunzi kwa nini tukiwa na hasira huwa tunapiga kelele au tunapaza
sauti? Kwa nini watu wanapigiana kelele wanapokuwa na mfadhaiko? Mwanafunzi
mmoja alijibu, ni kwa sababu tunapoteza utulivu wetu. “Lakini kwa nini upige
kelele wakati mtu unayemwambia yupo karibu nawe?” aliuliza profesa. Wanafunzi
walitoa majibu mbali mbali lakini hakuna jibu lililomridhisha profesa. Hatimaye
alieleza hivi, “Watu wanapokasirikiana kuna umbali mrefu kati ya mioyo yao
kisaikolojia. Ili kupunguza umbali wanapigiana kelele ili waweze kusikia. Jambo
gani linatokea kama watu wanapendana? Hawapigiani kelele wanaongea kwa upole
wananong’ezana, wanakaribiana palipo na upendo. Hatimaye hawahitaji hata kunong’onezana
wanatazama. Ikitokea siku ukampigia kelele unayempenda jua kuwa unaweka umbali kati yako na wewe.
Jibu pole hutuliza hasira.
“Kuna
mambo mawili tu mtu hawezi kuficha: kwamba amelewa na kwamba anapenda,”
alisema Antiphanes. Lakini yapo mambo mengi ambayo hayafichiki, chuki
haifichiki ikifichika ni kama kuficha moto kwenye karatasi. Kuna methali
isemayo mapenzi ni kikohozi hayafichiki. Upendo unaonekana bila kujali kama mtu
ana ulemavu au la. “Upendo ni lugha
ambao kiziwi anaweza kusikia; Upendo ni wimbo ambao mlemavu anaweza kucheza;
upendo ni mapambazuko ambayo kipofu anaweza kuona,” alisema Ramesh Umadkat.
Palipo na upendo mwenye ulemavu atachangamka hata akiwa na mguu mmoja anaweza
kudansi. “Upendo unaonekaje? Una mikono
ya kuwasaidia wengine. Una miguu ya kuharakisha kuwaendea wahitaji. Una macho
ya kuona shida na hitaji. Una masikio ya kusikia kushusha pumzi kwa majonzi na
mateso ya watu. Hivyo ndivyo upendo unavyofanana,”alisema Mtakatifu
Augustino wa Hippo Afrika ya Kaskazini.
Biblia inathibitisha kuwa upendo
haufichiki, unaonekana. “Amri mpya
nawapeni: mpendane. Kama mimi nilivyowapenda, nanyi pia mpendane. Hivyo watu
wote watawatambua kuwa wafuasi wangu, mkipendana” (Yohane 13:34-35). Watakatifu
wengi walikuwa na haya ya kusema juu ya haya hizo. “Yeyote kati yenu asiwe na hali ya kawaida tu kwa jirani yake isipokuwa
muendelee kupendana ninyi kwa ninyi katika Yesu Kristo” (Mtakatifu Inyasi
wa Antiokioa). Upendo unampambanua mkristo. “Mmoja lazima amwone Mungu katika kila mmoja” (Mtakatifu Katharina
Laboure). “Ninakwambia mambo haya,
kuwaburudisha ninyi, huku nikisali kwamba kwa kuwa wote tumeumbwa kwa dutu ile
ile, ambayo ina mwanzo lakini haina mwisho, tuweze kupendana sisi kwa sisi kwa
upendo mmoja. Kwa wale wote wanaojitambua wenyewe wanajua kuwa ni watu wadutu moja
isiyokufa” (Mtakatifu Antoni wa Misri).
Upendo unaonekana katika matendo na vipaumbele. Vijijini au mijini
wanaposema fulani anampenda fulani ni kwa sababu mapenzi yanaonekana. Asubuhi
anamtembelea. Mchana anamtendembela. Jioni anamtembelea. Usiku anamtembelea.
Watu wanaanza kusema maneno. Hivyo hivyo anayempenda Mungu ataonekana kila mara
anaenda Kanisani kila siku. Atasali sala za asubuhi. Yaani atakutana na Mungu
kabla ya kukutana na shetani. Atakutana na Mungu kabla ya kukutana na mazingira
ya maisha. Atazungumza na Mungu kabla ya kuzungumza na watu wengi. Anaungana na
Mungu kabla ya kuungana na watu wengine. Atasikiliza sauti ya Mungu kabla ya
kusikiliza sauti za watu wengine. Atasikiliza habari kutoka mbinguni kabla ya
kusikiliza habari kutoka BBC. Ataliita jina la Yesu kabla ya kuita majina
mengine madogo. Kwa macho ya imani atamuona Yesu kabla ya kujiona kwenye kioo. Atafagia
moyo wake kabla ya kufagia uwanja wake unaozunguka nyumba. Upendo kwa Mungu
unaonekana. Yesu kwa vile alimpenda Mungu baba alisali asubuhi na mapema. “Asubuhi
na mapema, kabla ya kupambazuka, aliamka, akaondoka, na kwenda mahali pa nyika
alikosali” (Marko 1: 35).
Upendo unaonekana katika maneno ya kutia moyo. Lililo moyoni ulimi
huiba. Moyoni pakiwepo upendo ulimi utaiba utaonekana katika maneno. Upendo wa Barnaba
na mtume Paulo ulionekana katika matendo na maneno. Tunaambiwa. “Waliwaimarisha wafuasi roho na kuwatia
moyo “ (Mdo 14: 22). Jina Barnaba
linamaanisha mwana wa kutia moyo. Unapotia moyo ni upendo unaonekana. Tuna
mifano ya watu mbali mbali ambao wamesema maneno ya kutia moyo. “Hapajakuwepo
kamwe usiku au tatizo ambalo limeweza kushinda mapambazuko au matumaini,”
alisema Bern Williams. Hata pakiwepo usiku wa matatizo ya namna gani kutakucha.
Matatizo hayapigi bao matumaini. Kuna aliyesema, “Mungu huwapeleka watu katika
maji marefu si kwa ajili ya kuwazamisha majini bali kuwatakasa,” alisema John
Aughey. Matatizo yanatakasa mawazo hasi, mawazo taka na mtazamo taka
yanapotafakiriwa katika mtazamo chanya. Mtu fulani alisema, “Watu wasio sahihi
wanapokuacha mambo sahihi yanaanza kutokea.” Maneno hayo yanatia matumaini kwa
yule aliyeachwa na watu ambao wasio sahihi.
Upendo unaonekana katika kumbukumbu. Mchungaji Rick Warren katika
kitabu chake, Maisha Yanayoongozwa na
Malengo alikuwa na haya ya kusema, “Upendo huacha kumbukumbu. Jinsi
unavyowatendea watu wengine, siyo utajiri au mafanikio yako ndicho kitu
kinachodumu unachoweza kuacha duniani.” Kama Mama Theresa alivvyosema, “Sivyo
unavyotenda, lakini kiasi gani cha upendo unaweka katika tendo hilo ndilo jambo
la muhimu sana.”
Upendo unaonekana katika mahusiano. Mahusiano mazuri kati ya mtume
Paulo na Barnaba ni ushahidi wa upendo. Mchungaji Rick Warren katika kitabu
chake, Maisha Yanayoongozwa na Malengo alikuwa
na haya ya kusema, “Nimekuwa kando ya kitanda cha watu wengi wanaokuwa katika
kufa, wanaposimama pembezoni mwa umilele, na sijasikia yeyote akisema, ‘Nileteeni
vyeti vyangu! Nataka kuviona mara moja tena. Nionyeshe zawadi zangu, medali
zangu, ile saa ya dhahabu niliyopewa.’ Maisha yanapokoma duniani, watu
hawajizungushii vitu. Tunachotaka kitunzunguke ni watu – watu tuwapendao na
tulio na uhusiano nao. Katika mahusiano mtu hataki kumhumiza bila sababu
anayempenda. Wakati wa ibada ya ndoa
mchungaji aliuliza kama kuna mtu ana la kusema dhidi ya wanandoa watarajiwa.
Kimya kikuu na mshangao vilitawala pale ambapo mwanamke aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma alienda mbele
karibu na wanandoa amembeba mtoto. Bibi arusi alianguka na kuzirai. Mchungaji
alimuuliza kama ana jambo lolote la kusema, “Hatusikii huko nyuma nimekuja
mbele kusiliza vizuri wakiweka ahadi za ndoa.”
Upendo unaonekana katika zawadi au kutoa. “Upendo unakufa unapouhodhi – unakua unapoutoa,” alisema Elbert
Hubbard. Kuhodhi ni kukusanya mali au bidhaa na kuvirundika kwa matumizi
binafsi. Katika kutoa tunawasaidia wengine. “Lengo letu kuu katika maisha haya ni kuwasaidia wengine. Na kama huwezi
kuwasaidia, walau usiwaumize,” alisema Dalai Lama.
Upendo unaonekana katika kusikiliza. “Weka hili katika kumbukumbu ya moyo wako: Hakuna mtu yeyote ambaye
huwezi kukosa kumpenda kama umesikiliza
hadithi yake,” alisema Mary Lou Kownack. Ukimsikiliza utampenda. Mtume
Paulo na Barnaba waliwatia watu moyo kwa sababu waliwasikiza. Tatizo kubwa siku
hizi ni kutowasikiliza watu. “Barabara
ya kuufikia moyo ni sikio,” alisema Voltaire. Unapomsikiliza mtu unagusa
moyo wake. Kusikiliza ni kutoa huduma. “Kuwasikiliza wengine ni sehemu ya
kwanza ya huduma ya kweli ya kikristo,” alisema Dietrich Bonhoeffer. Kusikiliza
ni changamoto. “Yeye ambaye hamsikilizi tena ndugu yake muda mfupi atakuwa
hamsikilizi Mungu,” alisema Dietrich Bonhoeffer.
Hitimisho
Upendo ni jambo la kujifunza. Kama watu wanajifunza kuchukia
wanaweza kujifunza kupenda.”Hakuna mtu anayezaliwa akiwa anamchukia mtu
mwingine kwa sababu ya rangi yake, historia yake, ama dini yake. Watu ni lazima
wajifunze kuchukia, na kama wanaweza kujifunza kuchukia, wanaweza kufundishwa
kupenda, kwa sababu upendo huja kiasili kwenye moyo wa binadamu kuliko chuki,”
alisema Nelson Mandela (1918 – 2013).