1. Mwanzo 1: 26-2:3
|
2. Wakolosai 3: 14-15, 17.23-24
|
3. Mt. 13: 54-58
|
SIKUKUU YA YOZEFU MFANYAKAZI (Mei Mosi 2016 Kwa majimbo Kama Jimbo Kuu la Dar es Salaam na mengine kwa wengine tazama tafakari yangu ya Jumapili ya 6 ya Pasaka)
Mwalimu wa wanafunzi wadogo wa somo la
dini aliwauliza wanafunzi. Kama ungeomba Mungu akupe sehemu ya masalia ya
mtakatifu ungeomba nini? Mwanafunzi wa miaka kumi na miwili akasema, “Mimi
ningeomba tone la jasho la Mt. Yozefu, ni jasho la heshima ya kazi, ni jasho la
unyenyekevu kwa sababu kwa kutoa jasho aliweza kujilisha, kumlisha mtoto Yesu
na kumlisha Bikira Maria.”
Leo ni sikukuu ya Mt.
Yozefu Mfanyakazi. Heshima tunayompa Mt. Yozefu inaitwa, “Proto-dulia.”
Inatangulia heshima kwa watakatifu wote ambayo ni “dulia.” Heshima kwa Bikira
Maria ni “hyper dulia” yaani juu ya heshima kwa watakatifu wote. “Mt. Yozefu alikuwa mtu wa haki, mfanyakazi
asiyechoka, mlinzi mkweli wa wale ambao amekabidhiwa awatunze. Kila mara
alinde, akinge na kuziangazia familia,” alisema Mt. Papa Yohane Paulo II. Sikukuu
ya Mt. Yozefu Mfanyakazi ilianzishwa na Papa Pius XII mwaka 1955 ili dhana ya
kazi kuipa maana ya kikristo na kuwapa wafanyakazi mtu wa kuiga na mwombezi. “Wafanyakazi na wale wote ambao wanafanya kazi
katika hali za umaskini watakuwa na sababu ya kufurahi kuliko kuomboleza, kwa
vile wanajambo linalofanana na Familia Takatifu katika kazi zao na shughuli zao”(Leo
XIII).
Mama mwenye watoto kumi anaweza
kuangaika akiwatafutia chakula wale washibe anawaonea huruma yeye akisha zeeka
watoto kumi wanashindwa kumlisha mama yao. Wanakosa huruma. Kufanya kazi kwenye
taasisi ni kuifikisha huruma ya Mungu maeneo ya kazi. Tuna mifano ya kuigwa ya
mashujaa wa huruma. Kuna hadithi isemayo kuwa huko mbinguni Mtakatifu Petro
aligundua watu wanazidi kuongezeka. Alipochunguza aligundua Mt. Yozefu alikuwa
ametengeneza dirisha anawapitisha watu kuingia mbinguni. Akatishia kumfukuza
mbinguni. Yozefu akasema, “Ukinifukuza naondoka na mke wangu na mtoto Yesu kama
baba yake mlishi.” Mjadala ukaisha. Mt. Yozefu anawaonea huruma wengine kama
alivyowaonea Yesu na Maria duniani.
Kazi ni huruma kwa sababu
inakuwezesha kufanya matendo ya huruma. Inakuwezesha kujitunza na kuitunza
familia. Inakuwezesha kuwa mkarimu. Inakuwezesha kushiriki kazi ya ukombozi.
Inakuweze sha kutoa zawadi.
Kazi ni kujifanyia matendo ya huruma.
Kujihurumia ni kujionyesha moyo wa wema na upole. Ni kujitendea mema.
Kazi inakuwezesha kujitendea matendo ya huruma. Kipato kitokanacho na kazi
kinakuwezesha kujitendea matendo ya huruma na kujiendeleza. Upendo huanzia
nyumbani ingawa unatoka, una sifa ya kimisionari. Unapojivika unajitendea tendo
la huruma. Unapojirisha unajitendea tendo la huruma. Yesu alisema nilikuwa na
njaa ukanilisha. Ukiwa na njaa ukajilisha unajitendea tendo la huruma. “Mungu
anampa kila ndege chakula, lakini hakitupi kwenye kiota,” alisema J.G. Holland.
Mtume Paulo alikuwa na ujumbe mzito kwa wasiofanya kazi: “Asiyefanya kazi
asile” (2 Wathesalonike 3:10). Ukifanya kazi unakula. Kazi inakuwezesha
kujifanyia tendo la huruma la kula. Unapofanya kazi vizuri unajiongezea hadhi
na heshima. KAMA UNAFIKIRI KUFANYA KAZI SI KAZI JARIBU KUACHA KAZI UONE KUPATA
KAZI ILIVYO KAZI. Kumbe Usichezee kazi chezea mshahara.
Kazi ni huruma kwa Mungu. Kazi nzuri na yenye
viwango vya juu na ubora wa hali ya juu inampa Mungu utukufu wake. “LOLOTE MFANYALO, LIFANYE KWA MOYO, KAMA
KWAMBA MNAMFANYIA BWANA.” (Wakolasai 3:23). “ Hakuna jambo linaloonekana
linachosha or linahumiza wakati unamfanyia Bwana kazi ambaye analipa vizuri,
ambaye anakuzawadia hata kikombe cha maji baridi ambacho kinatolewa kwa upendo
Wake,” alisema Mtakatifu Dominiko Savio. “Kazi chini ya viwango inamyima Mungu
utukufu wake. Mhurumie Mungu. Haijalishi mkubwa wako wa kazi ni nani.
Unamfanyia Mungu kazi. Kuwa na huruma usimfanyie kazi ya hovyo. Michelengelo
alikuwa akichora michoro na kupanga rangi kwenye kona ya kikanisa cha Sistine
ambayo ilikuwa haionekani aliulizwa na msaidizi wake kwa nini ameweka nguvu za
ziada kwenye sehemu ya paa ambayo hakuna atakayeiona. Alijibu, “Mungu ataona.”
Kazi ni huruma kwa watu wengine. Waendeshaji wa
teksi Nairobi wanalala kwenye teksi wakitafuta matunzo ya familia. Kazi ni
huruma kwa watu wengine. Mwajiri alikuwa anazungumza na
mwajiriwa mpya: “Kijana, hapa tuna rekodi ya kufanya yasiyowezekana na
yaliyoshindikana.” Kijana: Ndiyo Kiongozi, nitajitahidi kuwa mfayanyakazi
aliyeshindikana siku zote.” Kuwa mfanyakazi aliyeshindakana si kuwahurumia
wengine.
Kufanya kazi ni kuvihurumia vizazi
vijavyo. “Kula uwabakizie” Mzee wa mika 85 alikuwa akipanda miti ya miembe.
Vijana walipita na kumuuliza katika umri huu unapanda miembe na unajua kuwa
utakula amembe yake. Alijibu kwa muda nilioishi nimekuwa nikila maembe
yaliyopandwa na watu wengine, na mimi napanda maembe kwa vizazi vijavyo.`
“Katika kazi yetu ya leo lazima
tufikirie nyakati zijazo,” alisema Padre Adolph Kolping. “Vizazi vijavyo
vituonee huruma vikitazama nyuma kuiona kazi tunayofanya leo. Tulifanya
tulichoweza kwa kile tulichokuwa nacho,”alisema Mira Grant. Mtakatifu
Yozefu Mume wa Bikira Maria na Baba mlishi wa Yesu alifikiria vizazi vijavyo.
Kanisa Katoliki husali, “Ee Mungu Mwenyezi, toka mwanzo ulimkabidhi Mtakatifu
Yozefu kazi ya kuyatunza mafumbo ya wokovu wa binadamu. Tunakuomba kwa maombezi
yake ulijalie Kanisa lako liyatunze siku zote mafumbo yako yote…” Kutunza
mafumbo ni kazi lakini ni huruma kwa vizazi vijavyo. Ni tendo la huruma
kuviachia vizazi vijavyo urithi. Hawa watu hawawezi kukulipa.
Palikuwepo na msichana aliyejichukia
kwa sababu alikuwa kipofu. Alimchukia kila mtu isipokuwa rafiki wake wa kiume.
Alikuwepo kwa ajili yake kila mara. Alimwambia rafiki wake wa kiume. Nikiweza
kuiona dunia nitakubali kuolewa na wewe. Siku moja mtu alijitolea na kumpa
macho mawili. Aliweza kuona kila kitu na hata kumuona rafiki yake wa kiume.
Rafiki yake alimuuliza, “Sasa unaweza kuiona dunia, je uko tayari kuolewa na
mimi?” Yule msichana alimtazama rafiki yake wa kiume na kugundua alikuwa
kipofu. Matundu ya mashimo ya macho yalimshtua. Wazo la kuyatazama maisha yake
yote lilimfanya akate kuolewa na yeye. Rafiki yake wa kiume aliondoka kwa
masikitiko na machozi. Alimwandikia ujumbe, “Tunza macho yako mpendwa wangu
kabla hayajawa yako yalikuwa yangu.” Akili ya binadamu inafanya hivyo pale
ambapo hadhi yetu inabadilika. Leo kabla ya kusema neno baya fikiria yule
ambaye hawezi kuongea. Leo kama umechoka na kulalamika juu ya kazi unayoifanya
mfikirie yule ambaye hana kazi. Kabla ya kulalamikia umbali unaoendesha gari,
mfirikie yule anayetembea umbali huo kwa miguu.