NAMNA YA KUIISHI EKARISTI
TAKATIFU
SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTU
1.
Mwa 14: 18-20
|
2. 1 Kor 11: 23-26
|
3.
Luka 9: 11-17
|
UTANGULIZI
v
Tangia kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristu aliishi maisha ya
kiekaristi. Alizaliwa na kuwekwa kwenye chombo cha kulishia mifugo ishara ya
kuwa yeye atakuwa ni chakula cha roho zetu, yeye ambaye ni mchungaji wakati huo
huo ni malisho. Picha ya hori inahusianishwa na chombo cha kulishia kondoo
ambao Luka anawaeleza katika Mdo 20: 28-29 kama kanisa la Mungu. Hori
inayafunua maisha ya Yesu, uwepo wa mafundisho yake kama chakula cha uhai kwa
kanisa.
v
Bethlehemu alipozaliwa maana yake ni nyumba ya mkate. Ukweli huu
unaashiria ekaristi. Unabii juu ya Ekaristi unaonekana tendo la Melkisedeki
mfalme wa Salemu kuleta mkate na divai (Mwanzo 14: 18). Utamaduni wa kikristo
unamwona kama mfano wa Kristo kwa sababu alitolea sadaka kwa Mungu wake mkate
na divai kama Kristo alivyojitoa sadaka katika maumbo ya mkate na divai.
v
“Hapa yupo mkubwa zaidi ya
Solomon.” Hapa yupo mkubwa zaidi ya wachezaji wa Manchester United. Hapa yupo
mkubwa zaidi ya Rais. Hapa yupo mkubwa zaidi ya Prime Minister. Hapa yupo mkubwa
zaidi ya Papa. Hapa yupo mkubwa zaidi ya mwana ndondi Tyson. Hapa yupo mkubwa
zaidi ya Mwanandondi Conjestina. Hapa yupo mkubwa zaidi ya Mbunge wako. Hapa
yupo Bwana wetu Yesu Kristo. Tumsifu. Tumtukuze. Tumwabudu. SIKIO HALIZIDI
KICHWA. SIKIO HALIPITI KICHWA. SAKARAMENTI YA EKARISTI NI SAKRAMENTI AMBAPO
YUMO BWANA YESU KRISTU YEYE MZIMA MWILI WAKE, ROHO YAKE, MOYO WAKE, UMUNGU WAKE
NA DAMU YAKE KATIKA MAUMBO YA MKATE NA DIVAI.
NAMNA YA KUIISHI EKARISTI TAKATIFU
- KUABUDU
Kuabudu ni
kufanya ibada, ni kuomba. Kuabudu ni kusali. Ni kutukuza. Ni kustahi kwa namna
ya hali ya juu. Heshima tunayotoa kwa Ekaristi Takatifu ni zaidi ya heshima.
Tunaabudu. Heshima hiyo ya hali ya juu inaitwa “Latria.” Tunamwabudu Yesu
Kristu. Kuna namna nyingi za kuabudu: Unaweza kujilaza kifudifudi yaani tumbo
chini, mgongo juu. Tunaimba katika wimbo wa
“Sakramenti Kubwa Hiyo.” (Tantum Ergo)- “Sakramenti kubwa hiyo
twaheshimu kifudi.” Tunaabudu kwa kupiga goti kama tusomavyo katika barua ya Mt. Paulo kwa Wafilipi, “Ili kwa heshima ya jina la
Yesu, viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu, vipige magoti mbele yake, na
kila mtu akiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
(Wafilipi 2: 10-11). Tunapiga goti mbele ya Tabernakulo kwa maana yuomo Bwana
wetu Yesu Kristo. Kuna Ibada mbali mbali za Kumwabudu Yesu Kristo: Sala za
binafsi mbele ya Sakramenti Takatifu, Kuwa na Maandamano ya Ekaristi, Sherehe
ya Mwili na Damu ya Yesu, Kuwa na Kongamano la Ekaristi, Kuwa na Masaa ya
kuabudu: Saa Takatifu. Tunasoma hivi katika Injili ya Mathayo, “Akawaendea wale
wanafunzi akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Ndiyo kusema hamkuweza kukesha
pamoja nami hata saa moja? Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika
majaribu.” (Mathayo 26: 40-41) Hatuna budi kuonyesha heshima kwa wenzetu maana
wanampokea Yesu.
- KUGAWANYA
“Kisha akatwaa
kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa; wote wakanywa katika kikombe hicho” (Marko
14: 23). Wakatoliki wanashiriki Meza ya Bwana, meza ya kugawanya. Kugawanya ni
changamoto kwa Wakristu kunawakumbushwa kuwa kugawanya huku haukuishii na
sherehe ya kula pamoja bali wagawanye mali maishani. Wakiishi ukweli huu
kutakuwa na fundisho kwa wengine. Watagawanya ardhi walau na wengine wapate.
Watagawanya walichonacho. Kugawanya raslimali na mali ni msingi wa amani. Kugawanya
kusiishie kwenye mlango wa Kanisa na si suala la maandamano tu bali liguse hao
wanao andamana kuonyesha imani yao
lakini ni imani katima matendo. “Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana
imani, lakini haionyeshi kwa vitendo?” (Yakobo 2: 14)
Jirani ya
Abrahamu Lincoln Rais wa zamani wa Amerika alisikia mtu akilia nje ya nyumba
akatoka nje kuangalia kuna nini? Alimuona Lincoln akipita na watoto wake wawili
ambao walikuwa wakilia kwa sauti ya juu. “Kuna tatizo gani Abrahamu Lincoln?”
“Tatizo walilo nalo watoto ni tatizo katika dunia nzima. Nina matunda matatu na
kila kijana anataka kuchukua mawili,” alisema Abrahamu Lincoln. Chanzo cha
kutokuwa na amani ni baadhi ya watu kutaka kula kiasi kikubwa mgawo wa samba.
Sherehe ya leo inawafundisha wakristu kutokula mgawo wa samba bali kugawanya
ili pawepo na amani.
- KUSHUKURU
Kuna methali
isemayo, “Hasiyeshukuru kwa jambo dago apewalo hatashukuru kwa jambo kubwa.” SHUKURU KWA KILA JAMBO. Sherehe ya Leo
ya wakatoliki inahusu utamaduni wa kushukuru. “Walipokuwa wanakula Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa
wanafunzi wake akisema, Twaeni; huu ni mwili wangu” (Marko 14: 22). Waluhya
wana methali isemayo, “Nyama choma
haiwezi kuwa tamu ukamsahau aliyeichoma.” Methali hii inakazia kuwa na utamaduni
wa kushukuru. Leo hii wakatoliki sehemu wanaandamana kusherehekea sherehe
inayojulikana kama “Mwili na Damu ya Kristu.”
Kwa jina lingine sherehe hii inajulikana kama
“Sherehe ya Ekaristi Takatifu.” Neno “Ekaristi” linatokana na neno la Kigiriki
ambalo linamaanisha shukrani. Ni sherehe inayohusu kumshukuru Mungu na
utamaduni wa kushukuru. Kushukuru ni kitovu cha sherehe hii. Kama
umepewa sio siri. Watu wanaona jinsi Mungu alivyokubariki na hivyo kwa mantiki
hii wakatoliki wanaandamana hadharani kuonyesha shukrani yao
Suala la sherehe
ya leo na shukrani lina msingi wake katika Biblia. “Saa ilipotimia, Yesu akakaa
kula chakula pamoja na mitume wake…Kisha akatwaa kikombe akashukuru, akasema,
‘Pokeeni, mgawanyiane…halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa
akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa
kunikumbuka.” (Luka 22: 14-19) Yesu alishukuru alipochukua mkate na divai.
Ekaristi inamaanisha shukrani na mkate na divai hutumika. Wakristu ambao
wanashiriki kumbukumbu ya Karamu ya Mwisho ya Yesu kwa kuandamana leo
wanakumbushwa kuwa na utamaduni wa kushukuru maana ndio kiini cha sherehe ya
leo.
Kushukuru ni
kumsifu Mungu. Mungu kama amekujalia watoto, akili, utajiri, amani moyoni, jina
jema, mke, mme, mshukuru ukimsifu. Zingatia maneno haya, “Mtukuzeni Bwana pamoja nami, na tuliadhimishe jina lake pomoja.”
(Zaburi 34:3) Mkumbuke Mungu. Hakuna haja ya kujidai sana sote ni “CHAKUPEWA.” “Nani amekupendelea
wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia
kana kwamba hukupewa?” (1 Wakorintho 4:7).
Kuna methali isemayo, “Aliyekupa wewe kiti ndiye aliyenipa mimi kumbi.”
Na aliye na kidogo akitumie kupata kikubwa.
Kushukuru ni
kuthamini zawadi uliyopewa. Kama Mungu ametupa zawadi ya amani, kushukuru ni
kuthamini zawadi hiyo. Kama Mungu amekupa zawadi ya mke, kushukuru ni kuthamini
zawadi hiyo. Kama Mungu amekupa zawadi ya mme, kushukuru ni kuthamini
zawadi yaani mme. Kama unamshukuru Mungu
kwa kuwa Mkenya, basi itendee Kenya
mambo mazuri.
Kushukuru ni
kuomba tena. Ukipata shukuru. Kuna Baba
mmoja ambaye alikuwa anatembea kando ya Bahari ya Indi na mtoto wake wa kiume.
Mara wimbi likamchukua mtoto wake wa kiume lakini akaokolewa na mvuvi Msamaria
mwema. Badala ya kushukuru Baba huyo alimuuliza mvuvi, “Mtoto wangu alikuwa na
kofia umeiweka wapi?” Huo ni ukosefu wa shukrani. Sherehe ya Ekaristi ambayo
inamaanisha shukrani ni changamoto kwa wakristu wote kuwa na moyo wa shukrani
na sio na moyo wa punda. Shukrani ya punda ni mateke.
- KUKUMBUKA
Kwa kukumbuka
kukumbuka tunaiishi Ekaristi Takatifu. Yesu alipokula Karamu ya mwisho na
wanafunzi wake alisema, “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” (Luka 22: 19)
Sherehe ya leo ni ya ukumbusho huo lakini inafundisha utamaduni wa kukumbuka. Ili kushukuru ni lazima kukumbuka. Lakini tuwe na
utamaduni wa kukumbuka mazuri na sio mabaya. Kumbuka walimu wako wa zamani.
Kumbuka wazazi wako waliozeeka lakini walikutendea mengi mazuri. Kuna methali
ya kiafrika isemayo, “Aneyeona mama yake ameezeeka husema mahali waliyolipa kwa
sura hii iliharibika.” Lakini mama alikuwa mzuri ni uzee. Tukiona wazazi
wamezeeka hawana nguvu lakini walitusaidia sana lazima tukumbuke na tulipe hisani kwa
wema. Tumesikia katika somo la kwanza, “Msiwe
na kiburi na kumsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya
Misri, mahali mlipokuwa watumwa.” (Kumbukumbu la Sheria 8: 14) Kiburi
kinaweza kutufanya tusahau. Mtakatifu Augustini alisema hivi juu ya Bikira
Maria, “Maria alimchukua Mimba Neno
kwanza katika akili yake kabla ya kumchukukua mamba katika mwili wake.” Nasi baada ya kumpokea Yesu katika mwili
wetu tumpokee katika akili zetu. Tumfirie. Tumkumbuke. Maneno ya Mtunga zaburi
yatusaidie katika hili, “ Niwapo kitandani ninakukumbuka, usiku kucha
ninakufikiria; maana wewe umenisaidia daima kivulini mwa mbawa yako
nitashangilia.” (Zaburi 63: 6) TUFANYE MAMBO MAZURI AMBAYO WATU WANAWEZA
KUKUMBUKA.
Kuna mtoto
aliyekuwa anatembea na mama yake sokoni. Mtoto huyo alipewa chungwa na muuza
machungwa bure. Baada ya kupewa mtoto chungwa mtoto huyo alimrudishia aliyempa
akimwambia, “Limenye,” badala ya kusema, “Asante, nashukuru.” Mtoto huyo
alisahau kushukuru. Hakuwa na msamiati wa shukrani mtoto huyo. Wazazi hawana
budi kuwafundisha watoto wao kushukuru ili tuwe na utamaduni wa shukrani.
- KUWA KIMYA
Tuna
nyakati za kuwa kimya katika adhimisho la Ekaristi: Baada ya masomo ya misa na
kabla ya Sala ya Mwisho. Ukimya unamaliza magomvi. Ukimya unahitaji kutulia,
“TULIA MBELE YA MWENYEZI-MUNGU.” (ZABURI 37: 7)
- KUFURAHI
“Nyumba ambayo
inasherehekea haikosi kucheka.” (Methali ya Kiafrika) Leo tunasherehekea.
Jumapili tunasherehekea hatuombolezi. “Furaha siyo kutokuwepo kwa matatizo bali
ni kuwepo kwa Yesu Kristo,” alisema, William Vander Haven Mazingira ya Ekaristi
Takatifu ni mazingira ya furaha. Mazingira ya Adhimisho la Misa ni Mazingira ya
Furaha. Nyimbo za Utukufu, Mtakatifu ni nyimbo za furaha. Alipo Yesu kuna
furaha.
- KUTOA SADAKA
“Mtaka cha uvunguni sharti ainame.” Ili Yesu atuinue alijitoa sadaka. Ekaristi Takatifu ni sadaka. Ili tuiishi Ekaristi Takatifu hatuna budi kuinama
uvunguni ili tuwainue wengine.
- KUJIANDAA
MTOTO ALIYEOSHA MIKONO VIZURI HULA NA WAFALME. SAMAKI
MKUNJE ANGALI MBICHI. MTOTO UMLEAVYO NDIVYO AKUAVYO. Methali zote zinahusu
maandalizi. Kuna
watu wawili waliokuwa wanaongea. Mmoja akamwambia mwenzake, “Jana nilikuwa na
mawazo mabaya juu ya adui yangu?” Mwenzake akamuuliza, “Je uliyafurahia mawazo
hayo.” Yeye akajibu, “Mawazo yalifurahisha maana yalihusu kushidwa kwake katika
biashara na magari yake kupata ajali.” Mawazo ya
namna hiyo ni dhambi hauwezi kumpokea Bwana Yesu bila kujiandaa. “…Kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe
cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana.
Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe
kikombe hicho; maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana,
anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe.” (1 Wakorintho 11: 27-29)
Unaptunza dhambi moyoni bila kuiungama, unamkaribisha shetani. Ni kama ukiwa na
uchafu chumbani unawakaribisha mende. Wakati
wa vita vya Napoleon kuna mtu aliyekuanapeleleza kwa ajili ya maadui wa
Napoleon. Alipokamatwa aliulizwa na alikataa kutoa habari yoyote. Aliwekwa
kwenye gilotini-bamba la kukata kichwa (kwa wahalifu ufaransa.) Upanga
uliachiwa ukaanza kukata ulikuwa umekata nusu ya shingo, akaanza kusema,
“Nitawaambia, nitawaambia, nitawaambia!” Alikuwa amechelewa. Tusichelewe
kuungama.
- KUSHIRIKI
Leo hii
wakatoliki sehemu nyingi duniani wanasherekea Sherehe ambayo inajulikana kama Sherehe ya Mwili na Damu ya Yesu Kristu. Sherehe hii
inapata nguvu kutoka katika maneno ya Biblia, “ Ndipo Wayahudi wakaanza
kubishana kati yao:
“Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?’ Yesu akaambia, ‘Kweli nawaambieni,
msipokula mwili wa mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani
yenu.” (Yohane 6: 52-53) Jambo hili la kula mwili na kunywa damu ya Yesu
lilizua utata mkubwa katika historia ya Kanisa Katoliki. Mwanzoni wakristu
walishitakiwa kuwa ni watu wala watu. Ni kama Wayahudi waliojiuliza, “anawezaje
huyu kutupa mwili wake?”
Jambo hili
linaeleweka hivi. Kama maji na madini
yangekuwa na uwezo wa kusema yangeiambia mimea usipokunywa maji na kula madini
hamtakuwa na uhai ndani yenu. Kama nyasi na maji vingekuwa na uwezo wa kusema
vingewaambia wanyama kama ng’ombe na mbuzi
msipokula majani na kunywa maji hamna uhai ndani yenu. Katika msingi huu kwa
vile binadamu ana mwili na roho Yesu alisema msipokula mwili wangu na kunywa
damu yangu hamtakuwa na uhai ndani yenu.
Kushiriki katika karamu ya Bwana ni muhimu.
Leo hii tunapewa changamoto ya kushiriki. Katika neno
kushiriki tunapata neno ushirikiano. “Tunapomshukuru Mungu kwa kiokombe kile
cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa
hatushiriki mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni
wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo.” (1 Wakorintho 10:
16-17) Basi kushiriki kwetu kusiishie Kanisani tushiriki katika Jumuiya Ndogo
Ndogo. Tushiriki katika maendeleo ya Taifa.
- KUAMINI
Tunaamini kuwa
Yesu yumo katika Ekaristi. Tunapokomunika tunasema, “Amina.” Tunaamini. Neno
AMINA lina maana ya “Ni kweli.” “Ninaamini.”
Amina ni sala. Amina ni matendo. Kuna methali isemayo, “Sikusikii
matendo yako yananipigia Kelele.” Amina yako haitisikika kama
matendo yanapiga Kelele.
- UPENDO
“Akupendaye anakupenda na uchafu wako wote.” Yesu alitupenda na uchafu wetu wote. Sakramenti ya Ekaristi
Sakramenti ya Upendo. Yesu alitupenda zaidi ya upeo. Upeo maana yake hadi
anayoweza mtu kuona. Alitupenda na uchafu wetu wote. Upendo ni kama tabasamu. Tabasamu halina maana mpaka umelitoa. “Upendo unatibu watu-wote wanautoa na wale
wanaupokea,” alisema Karl Menninger. “Ukipenda boga penda na ua lake.”
- KUWEPO
“Hasiyekuwepo na
lake halipo.” Yesu yupo hapa lake lipo.
Yesu yupo katika Ekaristi Takatifu. Yeye alisema, “Nami nipo pamoja nanyi siku
zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati.” (Mathayo 28: 20). Tujifunze kuwepo kwa ajili ya Mungu, kuwepo
kwa ajili ya wenzetu, kuwepo kwa ajili yetu sisi. Kutukuwepo ni tatizo katika mambo
muhimu. Ukienda katika mikutano ya siasa utasikia mwanasiasa anauliza, “Vijana
mpo?” Vijana wanaitikia, “Tupo.” Wakina “Baba mmpo?” wanaitikia, “Tupo.”
“Wakina mama mmpo?” Wanaitikia, “Tupo.” Je tukiuliza hivyo katika mikutano ya
Jumuiya ndogo ndogo makundi yote yataitikia hivyo.