HATUTULII TUTATULIA KATIKA MUNGU
Jumapili ya 18
ya Mwaka C
1. Mhubiri 1:2; 2:21-23
|
Wokolosai 3:1-5,
9-11
|
Luka 12:13-21
|
UTANGULIZI
“Ee Bwana
umetuumba kwa ajili yako hatutulii mpaka tutakapotulia katika wewe,” alisema
Mtakatifu Augustini wa Hippo Afrika ya Kaskazini. Katika mali hatutulii tutatulia katika
Mungu. Katika mapenzi hatutulii tutatulia katika Mungu.Katika mamlaka hatutulii
tutatulia katika Mungu. Kuna anayesema nikipata gari nitakuwa nafuraha. Je ni
kutokuwa na gari kunakuzuia usiwe na furaha.Kuna anayesema nikipanda cheo
nitakuwa na furaha. Je, nikutopanda cheo kunakuzuia kutokuwa na furaha? Ni
katika msingi huo Mhubiri anasema Ubatili. Mali bila Mungu ni ubatili. Mamlaka
bila Mungu ni ubatili. Mapenzi bila Mungu ni ubatili. Furaha kamili tutaipata
katika Mungu.
KATIKA MALI
HATUTULII
Kuna mtoto wa miaka saba alikuwa akitafuta michango ya
kusaidia watoto wenye shida. Alipofika benki moja huko Tanzania. Meneja wa benki
alimwambia kuwa ana sarafu ya shilingi mia mbili na noti ya shilingi mia tano.
Achague kati ya sarafu ya mia mbili na noti ya shilingi mia tano. Mtoto huyo
alimwambia meneja. “Nitachukua sarafu ya mia mbili lakini hili isipotee,
nitaikunja kwenye noti hiyo ya shilingi mia tano.” Mtoto huyo alitaka kuchukua
pesa yote. Hatutulii katika pesa. Katika Injili ya
Luka 12: 16-20 tunapewa mfano wa mtu aliyemiliki mali
lakini mali
ilimmiliki. Alikuwa tajiri. Tumpe jina la Dives jina la kilatini maana
yake tajiri. Dives hakufikiria katika
msingi wa methali isemayo, “Hakuna mifuko katika sanda.” Hakufikiria katika
msingi wa msemo husemao, “sisi ni marehemu watarajiwa.” Mungu alimuita
“mpumbavu.” Mpumbavu ni mtu mjinga, jua na zuzu. Biblia ina picha nyingi za mtu
mpumbavu: “haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa” (Methali 19: 10). Tajiri Dives
aliishi kwa anasa. “Mpumbavu hudharau mafundisho ya baba yake” (Methali 15: 5).
Tajiri Dives alidharau mafundisho ya Mungu Baba yake-Mpende Mungu kwa moyo wako
wote, kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote. Hakumpa Mungu kipaumbele.
“Mtoto mpumbavu ni huzuni kwa baba yake” (Methali 17: 25). Tajiri Dives alikuwa
huzuni kwa Mungu –Baba yake.
Masimulizi hayo
ni kama ifuatavyo, “Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa
mavuno mengi. Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: ‘Nitafanyaje nami sina mahali
pa kuhifadhia mavuno yangu? Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga
kubwa zaidi, nami nitahifadhi humo mavuno yangu yote na mali yangu. Hapo nitaweza kuiambia
roho yangu: sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali,
kula, kunywa na kufurahi.” Lakini Mungu akamwambia: ‘Mpumbavu wewe; leo usiku
roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojirundikia vitakuwa vya nani?”
(Luka 12: 16-20).
Dives alipopata
mavuno mengi alikuwa tayari tajiri kama serikali au mwenye pesa kama njugu. Hakuangalia uwezekano mwingine wa kutumia mali yake kama
kuendeleza kazi ya Mungu, kusaidia maskini, kuacha zawadi ya watunzi, wateteaji
amani. Alifikiria tumbo lake, usingizi wake, anasa zake. Hakumpa Mungu nafasi.
Hakumpa jirani nafasi.
Tajiri Dives
hakutulia katika mali.
Hakumkaribisha Mungu katika maisha yake. Ni katika msingi huo Mhubiri anasema
Ubatili. Mali
bila Mungu ni ubatili. Mamlaka bila Mungu ni ubatili. Tayari alikuwa tajiri
mkubwa sana
alipopata mavuno yakutosha. Ebu tuchambue binadamu hasivyotulia katika mali.
Mtu akijenga nyumba anajenga na ukuta lakini hatulii. Anaweka vipande vya chupa
juu ya ukuta, lakini hatulii. Anaweka nyaya za umeme, lakini hatulii. Anajenga
nyumba ndogo ya mlinzi, lakini hatulii. Anaweka kibao chenye maneno yasemayo,
“Kuna Mbwa Mkali,” lakini hatulii hata kama
mbwa huyo hana meno. Anaweka kibao chenye maneno, “Nyumba hii Inalindwa na
Mitambo Maalum.” Lakini hatulii. Anaweka Kamera za kupiga picha lakini hatulii.
Mtu mwingine ambaye ana imani katika uchawi anaweka mkia wa mjusi kama kusema, “Nyumba hii inalindwa na mkia wa mjusi.” Ni
vizuri kuwa na ulinzi imara bila kuamini katika uchawi, lakini usimsahau Mungu.
Mtunga Zaburi anatwaambia, “Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba,waijengao
wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure”
(Zaburi 127: 1).
Tajiri Dives
angefikiria kukiachia kizazi kijacho urithi. Lakini hakufanya hivyo. Kilikuwa
ni kipindi cha masika yatokanayo na pepo za Monsuni katika Bahari ya Hindi, na
mzee aliyekuwa amekula chumvi alikuwa akilima mashimo katika bustani yake. “
Unafanya nini ?” Jirani yake alimuuliza. “Ninapanda miti ya miembe” lilikuwa
jibu. “ Unategemea utakula maembe toka katika miembe hiyo ?”“Hapana, sitaishi
muda mrefu kwa ajili ya hilo.
Lakini wengine watakula. Lakini maisha yangu yote nimekula maembe ambayo
yamepandwa na watu wengine. Hii ndiyo njia ya kuonesha shukrani”.
Katika pesa hatutulii.
Kuna mtu alienda kwa padre kumwomba padre afanye ibada ya kuzimzika mbwa wake.
Padre akasema huwa tunafanya ibada kuzika binadamu na wala sio mbwa. Yule mtu
akaondoka akiwa amehuzunika. Baada ya kutembea hatua kadhaa mbele aligeuka
nyuma akamwambia huyo padre kama ungefanya
ibada ya kumzika mbwa wangu ningekupa $ 1000. Padre huyo akasema, “Kwa nini
ukuniambia kuwa mbwa wako ni mkatoliki ningemzika haraka.” Pesa ilimpofusha
macho huyo padre hasijue mambo ya kiroho yanayohusu binadamu na wala sio mbwa.
KATIKA MAMLAKA HATUTULII
Napoleoni
aliwahi kusema, “Nimejaribu kuvuta watu kwangu kwa kutumia mabavu lakini Yesu
amewavuta kwake kwa kutumia upendo.” Watu walikuwa wakimshangilia Kaisari na
kusema, “muungu, muungu, muungu.” Upandeni alikaa mtu aliyekuwa akimwambia,
“Kumbuka wewe ni binadamu.” Tunapotafuta mamlaka tukumbuke sisi ni binadamu.
Hatutulii katika mamlaka tutatulia katika Mungu.
Kuna hadithi juu
ya mahali ilipofichwa furaha. Mungu alitaka kuficha furaha. Alijiambia,
nikiificha nchi za kigeni watu watafika huko. Nikiificha kenye mamlaka watu
watafuta mamlaka wayapate, nikiificha kwenye uzuri watu watajipodoa, nikiificha
kwenye biashara watu watafanya biashara waipate, nikiificha kwenye mapenzi watu
watafanya mapenzi waipate. Mungu akaificha ndani mwetu. Nenda katika moyo wako.
Tunasafiri kwenda Ulaya lakini kuna mabao hawataki kusafiri kwenda katika mioyo
kuona kuna nini? Kuna sauti ya Mungu katika moyo wako inayokwaambia kutenda
mazuri na kuacha mabaya isikilize nawe utakuwa na furaha. Furaka kamili ni
katika Mungu.
HATUTULII KATIKA MAISHA SISI NI MAREHEMU WATARAJIWA
“Utufundishe
ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima” (Zaburi 90:12). Tajiri
anayezungumziwa katika Injili ya leo hakufikiria ufupi wa maisha yake.
Vinginevyo angekuwa na hekima akumuacha Mungu aitwe Mungu na kumpa nafasi ya
kwanza katika maisha yake. Hadithi
inapokuwa tamu au nzuri katika gazeti hukatizwa na chini yake maneno
“Itaendelea Toleo Lijalo” huandikwa. “Toleo
Lijalo” kwa marehemu ni mbinguni au toharani au motoni. Tajiri aliyekuwa
anapanga kufurahia mavuno yake aliambiwa ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako
itachukuliwa.” Tajiri huyo hakujua kuwa alikuwa marehemu mtarajiwa. Tunasoma
hivi katika kitabu cha Ayubu, “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za
kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama
vile ua, kisha hukatwa” (Ayubu 14: 1-2). Kuna
kijana aliulizwa, “Baada ya kidato cha nne, nini kitafuata?” Alijibu,
“Nitaendelea na masomo kidato cha tano na sita.” “Halafu?” “Nitajiunga na Chuo
Kikuu.” Alijibu. “Halafu?” “Nitatafuta ajira?” Alijibu. “Halafu?” “Nitaanza
kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.” Alijibu. “Halafu?” “Nitachumbia.” Alijibu.
“Halafu?” “Nitafunga ndoa.” Alijibu. “Halafu?””Nitapata watoto.” Alijibu.
“Halafu?” “Nitawapa elimu nzuri.” Alijibu. “Halafu?” “Nitastaafu.” Alijibu.
“Halafu?” “Nitaanza kula pensheni.” Alijibu. “Halafu?” “Nitazeeka.” Alijibu.
“Halafu?” “Halafu halafu…Mungu ataniita.” Alijibu kwa huzuni na kusitasita.
“Ni mwanaume gani atakayeishi asione mauti?” (Zaburi 89:48). Niliwahi kuona
maneno kwenye kaburi yameandikwa “Jinsi ulivyo ndivyo nilivyokuwa. Jinsi
nilivyo ndivyo utakavyokuwa.” Kama ni hivyo
tujitahidi kutulia katika Bwana.