Saturday, September 24, 2016

KUTOFANYA LOLOTE NI KOSA

                                            
                                                 Jumapili ya 26 ya Mwaka C
1.       Amo 6: 1a. 4-7
2. 1 Tim 6: 11-16
3.  Lk 16: 19-31

Kuna hadithi ya mtu ambaye aliaga dunia. Huko mbinguni mtume Petro aliangalia kwenye kitabu kikubwa na kusema, sikuona jina lako. Na kama jina lako halionekani utakwenda motoni. Mtu huyo akamjibu Petro, “Kwa nini niende motoni sikufanya lolote.” Petro akasema kwa vile ukufanya lolote, utaenda motoni. Tuogope kosa la kutofanya lolote kama tunavyoogopa ukoma. Mt. Ambrose alikuwa na haya ya kusema: “Si kila aina zote za umaskini ni takatifu, na si kila aina zote za utajiri ni uhalifu.” Umaskini wa roho ni utakatifu. Lazaro alikuwa maskini wa roho. Alichukuliwa mbinguni kwa vile alimtegemea Mungu. Tajiri Dives alifanya kosa la kutofanya lolote. Hakuwa mkarimu. Alikosa mbingu kwa kukosa kuwa mkarimu. Si kila utajiri ni uhalifu. Tajiri Dives hakuwa fisadi.
MAKOSA YA TAJIRI DIVES
Jicho Lisiloona Maskini
Tajiri anayesimuliwa katika injili ya leo tunaweza kumuita Dives neno la kilatini lenye maana ya tajiri. Dives hakumwona Lazaro ingawa alikuwa mlangoni pake. Labda angemwona angemwondoa kwa nguvu. Lipi kosa la Dives? Hakumfukuza Lazaro. Hakumdhuru Lazaro. Hakumwamuru atoke mlangoni. Hakumzuia kula vipande vilivyoanguka kutoka mezani. Kosa lake ni kuwa hakumwona Lazaro. Lile lililompeleka motoni si lile alilolifanya bali lile alilokosa kufanya alikosa kumsaidia masikini Lazaro.
Mwaka 1950 Albert Schweitzer alitajwa kuwa ni “Mtu wa karne.” Mwaka 1952 alitunukiwa nishani ya Amani ya Nobel. Akiwa na umri wa miaka 30, Schweitzer aliamua kuacha kazi ya kucheza kinanda ili awe daktari. Hatimaye alijenga Hospitali Afrika na kuajiri wafanyakazi. Schweitzer alisema hadithi juu ya Lazaro na tajiri iliathiri uamuzi wake wa kuwa daktari mmisionari. Kimantiki aliona kuwa ndugu yake wa kiafrika alikuwa ni Lazaro na yeye alikuwa ni tajiri. “Ningefurahiaje watu kunishangilia wakati Lazaro anateseka na maumivu,” alibainisha Albert Schweitzer aliyekuwa na macho yanayoona masikini. Huyu ni tajiri aliyekuwa na macho yanayoona masikini.
Kosa la Kutofanya Lolote
Tajiri katika Injili ya Luka (16:19-31) hashitakiwi kwa makosa mengine isipokuwa kosa la kutofanya lolote. Mtakatifu Yohane Chrysostom alikuwa na haya ya kusema juu ya kuteswa kwa tajiri motoni: “Aliteswa si kwa sababu alikuwa tajiri bali kwa sababu hakuwa na huruma.” Tajiri ambaye katika mapokeo ya Kanisa Katoliki anaitwa Dives alijiona yeye peke yake hakumwona Lazaro ingawa alikuwa mlangoni pake. Dives alijifungia katika Dives. Hakutoa. Hakuwa mkarimu. “Heri kutoa kuliko kupokea” (Matendo 20: 35). Tajiri Dives angepata heri kwa kutoa kwa maskini Lazaro. Akitoa maoni juu ya mfano huu Mt. Ambrose alizoea kusema: “Unapotoa chochote kwa maskini humpi yule kitu kilicho chako, bali unamrudishia tu kilicho chake, kwani  mali za ulimwengu huu ni mali ya wote, si ya matajiri tu.”
Kosa la Kuvaa Nguo za Gharama Sana
“Palikuwa na mtu tajiri aliyezoea kuvaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi” (Luka 16: 19).   Rangi ya zambarau ilikuwa ni rangi ya vazi la kifalme. Mtakatifu Gregory akitoa maoni juu ya mfano huu alikuwa na haya ya kusema: “Kama kuvaa nguo za zambarau na kitani safi lisingekuwa kosa, neno la Mungu lisengeelezea kwa uangalifu kamwe jambo hili. Hakuna anayetafuta nguo za gharama sana isipokuwa kwa sababu ya majivuno ili aonekane ni mweheshimiwa kuliko wengine;  hakuna anayetamani kuvaa nguo kama hizo isipokuwa kwa sababu kuonwa na wengine.”  Ukawaida ni fadhila ya kukumbatia maishani. Tajiri Dives hakuwa na fadhila hii ya ukawaida.
Changamoto Maishani
Si lazima ujiulize, “je niko tajiri?” bali jiulize “nani anakaa mlangoni pangu akiomba?” Si lazima yule anayeomba mkate. Kuna anayeomba msamaha. Kuna anayeomba neno la upendo. Kuna anayeomba shukrani, labda amepigwa teke kama methali ya kiswahili isemavyo “shukrani ya punda ni teke.” Kuna anayeomba maneno “pole na kazi.” Kuna anayeomba salamu. Ukweli unabaki tuko matajiri wa kutoa haya.
Kuwa na muda nao ni utajiri, “muda ni mali .” Tuwe na jicho linaloona wenye kuhitaji msaada wowote hata wa kisaikolojia. Ni vizuri kutoa tukiwa hai badala ya kungoja kutoa kwa njia ya  wosia. Hadithi ifuatayo inaeleza lile ambalo nataka kutoa kwa njia ya lugha ya picha. Siku moja nguruwe alilalamika mbele ya ng’ombe kuwa: “Licha ya kuwapa binadamu nyama nzuri, bado jina langu wanalitumia kutukana watu wengine wakisema ‘muone mdomo kama nguruwe’ au ‘wewe mchafu kama nguruwe.” Ngombe alimpa angalisho nguruwe, “ Lakini wewe nguruwe unatoa baada ya kufa. Mimi ninawapa watu maziwa nikiwa badohai.” Tutoe tukiwa bado hai.
Kutoa ni moyo vidole huachia. Hesabu ya kutoa kuwasaidia masikini ina mantiki yake ya kuwa tunazidisha kwa kutoa. Ni kweli kutoa kwaleta heri kama alivyosema mwandishi wa kitabu cha matendo ya mitume. Hata harufu nzuri hubaki kwenye mikono ya mtu anayetoa ua la waridi.
Kuna namna tatu za kutoa kama alivyobainisha Robert Rodenmayer: kutoa kwa kinyongo, kutoa kwa sababu ni wajibu, kutoa kwa kushukuru. Anyetoa kwa kinyongo husema, “Nachukia kutoa.” Mtu wa namna hii utoa kidogo, kwa sababu zawadi bila mtoaji si chochote. Anayetoa kama wajibu husema, “Ninapaswa kutoa.” Mtu wa namna hii anatoa zaidi, lakini hamna wimbo katika zawadi yake. Anayetoa kwa kushukuru husema, “Napenda kutoa.” Mtu huyu anatoa kila kitu na anaionesha dunia sura ya Mungu.”
Masikini kamwe wasifananishwe na kisogo kama kisemavyo kitendawili, “Kipo lakini hukioni.” Jibu la kitendawili hiki ni kisogo. Masikini wapo tuwaone, tuwasaidie. Mtakatifu Basil Mkuu (330-379) alituasa hivi: “Wakataa kutoa fedha kwa sababu eti, fedha zako hazitoshi kwa mahitaji yako mwenyewe; lakini huku ulimi wako ukiomba radhi, mkono wako unakuhukumu, kwa maana ile pete ya kidoleni mwako yadhihirisha uongo wako. Nguo zilizo za ziada zingewatosha maskini wangapi? Nawe wathubutu kumwondoa mtu maskini bila kumpa chochote?”



Neno masikini linaweza kuwa na maana nyingi. Masikini ni mtu yeyote mwenye haja dharura. Masikini ni mtu myonge hasiyekuwa na nguvu. Mtu ambaye yuko waya : ameishiwa na fedha. Mtu hasiyekuwa na mbele wala nyuma. Masiki ni mkata  na umasikini ni ukata. Maneno mengine ambayo yanaweza kutumika badala ya neno masikini ni fakiri, fukara, hohehahe na ombaomba.
Kwa hiyo masikini tunao wengi katika jamii zetu. Wanahitaji kusaidiwa. Marehemu Justin Kalikawe mwanamuziki katika wimbo wake “Bashekera Mbalibyezire” (Watu hucheka kwa sauti ya juu palipo vyakula tele) aliouimba katika lugha ya kabila la wahaya wa Tanzania alibainisha kuwa, “Kwenye msiba wa masikini wapo tu wanaukoo.” Kwenye msiba wa tajiri wanakutwa watu wengi ambao si wana ukoo. Alibainisha mwanamuziki huyo aliyeaga dunia katika asubuhi ya maisha yake.
Upendo kwa jirani unatutaka kuuchangamkia msiba hata wa masikini. Kabla ya kuzinyoshea vidole nchi tajiri na suala la kusaidia masikini lazima kwanza tujinyoshee wenyewe tusije tukagundua kuwa vidole vitatu vinatuelekea sisi wakati kidole gumba kinasema Mungu ni shahidi
Utakatifu wa Maskini
Mt. Ambrose alikuwa na haya ya kusema: “Si kila aina zote za umaskini ni takatifu, na si kila aina zote za utajiri ni uhalifu.” Maskini Lazaro hakupelekwa mbinguni kwa vile alikuwa na umaskini wa vitu alipelekwa mbinguni kwa sababu alikuwa na umaskini wa roho. Alimtegemea Mungu. Ukweli huu unabainishwa kutoka katika jina lake Lazaro maana yake: “Mungu ananisaidia.” Naye papa Yohane Paulo II alikuwa na haya ya kusema kwa wote wanaoteseka kama Lazaro:  “Wakati umefika kwa masikini Lazaro aweze kuketi kando ya yule tajiri ashiriki chakula kile kile badala ya kulazimishwa kula makombo yanayoanguka katoka mezani. Umasikini uliopita kiasi huzaa utumiaji nguvu, chuki na aibu.  Na njia ya kuung’olea mbali ni kufanya kazi ya kuleta haki, na hivyo kujenga amani.”
Lazaro Anafarijiwa
Kuna methali ya Yoruba isemayo, “Mtoto akijiingiza katika kulia mama atajiingiza katika kumfariji.” Tunapokuwa tunalia Mungu anatufariji. Tunapokuwa tunalia Bikira Maria Mfariji wa Wenye Uchungu anatufariji. Huko mbinguni kuna kutulizwa na kufarijiwa. Katika mfano wa Tajiri na Lazaro masikini tunaona Lazaro anatulizwa mbinguni. Kufarijiwa ni sifa ya mbinguni.   Tutafakari sifa hii ya mbinguni ya kufariji na kufarijiwa ambayo lazima ianzie duniani. Abrahamu alimwambia Dives aliyekuwa anateseka motoni, “Kumbuka mwanangu kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateseka.” (Luka 16: 25) Kufarijiwa ni sifa ya maisha ya mbinguni. “Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa.” (Mathayo 5: 4) Ni vizuri kufariji na kufarijiwa kuanzia duniani.
UKARIMU WA MBWA
Mbwa walimwonesha ukarimu Lazaro ambao Tajiri hakumwonesha. Walilamba vidonda vyake. Walimpa huduma ambayo wangejipa wao kama wangekuwa wamehumizwa. Mbwa akihumizwa hulamba vidonda vyake mwenyewe.
YESU KRISTO KAMA LAZARO
Mtakatifu Augustino alikuwa na haya ya kusema juu ya som la injili: “Hadithi hii inaweza kueleweka vinginevyo tukichukua Lazaro kumaanisha Bwana wetu; alilala kwenye mlango wa tajiri kwa  sababu alijishusha na kuwasikiliza wayahudi wenye majivuno katika kujishusha kwake katika ulimwilisho; akitamani kushibishwa na makombo yaliyoanguka kutoka meza ya tajiri hii ina maana alitafuta walau matendo madogo ya haki ambayo kwa majivuno yao wasingetumia katika meza yao (yaani mamlaka yao) matendo ya huruma ambayo yalikuwa madogo na bila nidhamu ya uvumilivu katika maisha ya kutenda mema ambayo wakati mwingine waliyatenda kwa bahati mbaya kama makombo mara nyingi yaangukavyo kutoka mezani. Vidonda ni mteso ya Bwana wetu mbwa waliovilamba ni watu wa mataifa, ambao wayahudi waliwaita najisi na licha ya hayo wakiwa na harufu nzuri ya ibada walilonja mateso ya Bwana wetu katika Sakramenti za Mwili na Damu yake duniani  kote.” 
HITIMISHO
Ushindwe wakati umejaribu. Ni methali ya Tanzania. Usipojaribu hautafanikiwa. Kutojaribu au kutofanya lolote ni zaidi ya kosa, ni dhambi. Kujaribu na kushindwa si uvivu. Ni methali ya Sierra Leone. Kuna ambaye alimuomba Mungu amsaidie kushinda bahati nasibu ya kampuni ya simu ya Safaricom. Kila siku mtu huyo alimuomba Mungu, lakini hakufanikiwa. Akiwa amelala aliota ndoto Mungu anamwambia kuwa yeye anataka ashinde lakini anamuomba anunue vocha (Credit card) aweke pesa kwenye simu. Mtu huyu alikuwa hafanyi lolote.

Si kwamba mambo ni magumu ndio maana hatuthubutu kufanya kitu. Ni kwa sababu hatuthubutu kufanya kitu ndio maana mambo ni magumu,” alisema mwanafalsafa wa Kirumi Seneca. Kutothubutu au kutojaribu ni kosa. Kwa kujaribu mara nyingi, tumbili hujifunza kuruka kutoka mtini. Methali hiyo ni busara ya mababu wetu.  “Binadamu hawezi kuvumbua bahari mpya kama hana ujasiri wa kupoteza kule kuona ufukwe,” alisema Andre Gide (1869-1951)mfaransa mwandishi na  mshindi wa zawadi ya Nobel katika fasihi mwaka 1947. Ili kuvumbua bahari mpya lazima uende mbali lazima ufanye kitu. “Mtu ambaye hajiweki katika hali ya hatari, hafanyi lolote, hana chochote, na si chochote na atakuwa si chochote. Anaweza kukwepa mateso na huzuni, lakini hawezi kujifunza na kuhisi na kubadilika na kukua na kupenda na kuishi,” alisema Leo F. Buscaglia (1924-1998). “guru” wa kiamerika mtetezi wa nguvu ya upendo. Kama kila mtu angejitahidi kufanya lolote zuri dunia ingekuwa mahali pazuri pa kukalika.  

Counter

You are visitor since April'08