Jumapili ya 29 ya Mwaka
C
1. Kut 17: 8-13
|
2. 2 Tim 3: 14-4:2
|
3. Lk 18: 1-8
|
SALI DAIMA NA
KWA MOYO MPAKA USHINDE MAJARIBU
Katika kusali
hatupaswi kusali kama watoto watundu na watukutu ambao hubonyeza kengele
wafunguliwe mlango na baada ya hapo hukimbia kwenda kubonyeza kengele mlango
mwingine. Sali mpaka unasali ni kusali mpaka mlango ufunguliwe. “Tatizo karibu la kila mtu anayesali ni kuwa
anasema ‘Amina’ na kukimbia kabla Mungu hajawa na nafasi ya kujibu.
Kumsikiliza Mungu ni muhimu sana kuliko
kumpa mawazo yetu,” alisema Frank Laubach. George Muller alipoulizwa juu ya
kiasi cha muda anaoutumia kusali alijibu, “Masaa mengi kila siku. Lakini naishi
katika moyo was ala. Nasali ninapotembea na ninapolala na ninapoamka. Na majibu
kila mara yanakuja.” Kabla ya kufanya
shughuli yoyote Sali. Kwa vile shughuli haziishi utasali daima. "Haitoshi kuanza kusali, haitoshi kusali kwa
jinsi inavyopaswa; haitoshi kuendelea kusali kwa muda; lakini lazima tusali kwa
uvumilivu, kwa kuamini, mpaka tupate jibu,” alisema George Müller.
Katika Biblia
kuna kisa cha mjane ambaye hakuacha kumwomba hakimu ampatie haki yake. Aliomba
kwa matumaini ya kusikilizwa. Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu asiyemcha
Mungu wala kumjali mtu. Na katika mji huo kulikuwa na mama mjane, naye
alimwendea tena na tena akisema, ‘Nipatie haki kwa adui yangu.’ Siku nyingi
hakutaka, kisha akajiambia, ‘Ingawa simchi Mungu wala simjali mtu, kwa kuwa
mjane huyu ananisumbua nitahakikisha amepata haki yake, ama sivyo ataendelea
kuja hadi amenichosha.” Bwana akaendelea kusema, “Sikilizeni asemavyo hakimu
mbaya. Na Mungu, je, hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku?
Je, atakawia kuwasaidia?” Nawaambieni atawapa haki upesi (Luka 18: 1-8). Mfano unajaribu kumlinganisha Mungu na hakimu
mbaya. Kama hakimu mbaya anaweza baadaye kusikiliza kwa vile mjane alivumilia
itakuwaje Mungu mwenye huruma. “Bwana wetu baada ya kuongea juu ya majaribu na
hatari ambazo zilikuwa zinakuja anaogeza kwa haraka baadaye kidogo tiba yake
ambayo ni sala ya daima na itolewayo kwa moyo,” alisema Baba wa Kanisa Theophyl.
SALI MPAKA IMANI ISHINDE
Juu ya maneno
“Mwana wa mtu atakapokuja ataikuta imani duniani” Mtakatifu Augustini alikuwa
na haya ya kusema: “Bwana wetu aliongeza maneno haya kuonesha kuwa imani inaposhindwa, sala inakufa. Hivyo ili tusali
lazima tuwe na imani na ili imani yetu isishindwe lazima tusali. Imani inamwaga
sala na kule kumwaga moyo katika sala kunazaa uthabiti wa imani.” Kuna baba ambaye alielezea kisa hiki kuwa
wakati wa wanafamilia kusali kila mwanafamilia ilibidi kumwombea mtu mmoja.
Mtoto wake wa kiume alimwomba Mungu amsaidie rafiki yake kuwa mtu mwema shuleni
alikuwa mbaya. Juma lililofuata walipokutana kwa ajili ya sala za familia baba
huyo alimuuliza mtoto wake kama atamwombea rafiki yake Eddie tena. “Hapana,
nilimuombea Eddie juma lililopita nab
ado ni mbaya.” Kijana huyu alikosa uvumilivu wa mwanamke mjane. Katika somo la
kwanza tunaambiwa hivi: “Ikawa, Musa alipoinua mikono yake, Israeli ilishinda.
Alipoiacha mikono kushuka, Amaleki ilishinda kwa kuwa mikono ya Musa ilichoka,
walitwaa jiwe, wakaliweka chini yake. Akaketi juu yake, Haruni na Huri
wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu, na mwingine upande huo. Na hivi
mikono ya Musa haikulegea tena mpaka jua lilipokuchwa. Yoshua akamshinda
Amaleki na watu wake kwa makali ya upanga” (Kutoka 17: 11-13).Hapa tunaiona
nguvu ya Mungu inayoleta ushindi.
SALI
PAPO HAPO SALI SASA
Kusali mpaka
unasali ni kusali papo hapo, hakuna kungoja kidogo, hakuna goja kwanza, sio
kungoja siku ya pili“Yeye aliyekuokoa amekuonesha ambalo angetaka wewe ufanye.
Angetaka uwe mtu wa papo hapo katika sala,” alisema Mtakatifu Yohane
Chyrisostom. Ishara ya radi kupiga ikijionesha Sali papo hapo. Ukipata taarifa
za msiba muombee marehemu papo hapo. Ukimwambia mtu nitakuombea muombee papo
hapo usije ukasahau. Ukiwa na wazo linalokuondoa kwenye sala lifanye liwe sala
papo hapo. Mtakatifu Bernard alikuwa amepanda farasi siku moja na huku anasali.
Alikutana na maskini omba omba akaanza kuzungumza naye. Maskini alimuuliza
Bernard alichokuwa anafanya juu ya farasi wakati anasafiri, na Bernard alisema
kuwa alikuwa anasali. “Lakini mara nyingi huwa na mambo yanayonitoa kwenye
sala,” alisema Bernard. “Ee, sawa, huwa sina mambo yanayonitoa kwenye sala,”
maskini alisema. “Hilo jambo zuri, nitakupa farasi huyu kama unaweza kusema
sala ya ‘Baba Yetu’ bila hata mara moja kuwa na mawazo mengine.” “ Ee hilo ni
jambo rahisi,” alisema maskini na kuanza kusali, “Baba Yetu uliye mbinguni;
jina lako litukuzwe…” Maskini alinyamaza. “Niambie, kiti cha kukalia kitakuwa
pamoja na farasi?”
SALI KWA KUTAFAKARI BARAKA UNAZOZIOMBA
Yeye aliyekuokoa
amekuonesha ambalo angetaka wewe ufanye. Angetaka uwe mtu wa papo hapo katika
sala, angetaka utafakari moyoni baraka unazoziomba, Angetaka uombe na kupokea
kile ambacho wema Wake unataka kutoa. Hakatai kutoa baraka zake kwa wale
wanaosali,” alisema Mtakatifu Yohane Chyrisostom.
SALI KWA KUSHIRIKIANA NA NEEMA YA MUNGU
Katika jarida la
Your Life (Maisha Yako) kuna hadithi
juu ya wasichana wawili ambao walikuwa katika hatari ya kuchelewa shuleni.
Mmoja alisema, “Tusimame na tusali ili Mungu atusaidie tuweze kufika huko
mapema.” Mwingine alisema: “Hapana, tukimbie kwa nguvu zetu zote, na tusali
wakati tukikimbia.” Kwa kusali wakati unakimbia unashirikiana na neema ya
Mungu.
SALI KAMA KWAMBA KILA KITU KINAMTEGEMEA MUNGU
Baadhi ya watu
husema sala na watu wengine husali. Kusali mpaka unasali sio kusema sala.
Kusali mpaka unasali ni kuwa na moyo wako kuwa katika sala. “Katika sala ni
vizuri zaidi kuwa na moyo bila maneno kuliko kuwa na maneno bila moyo,” alisema
John Bunyan. Kusali mpaka unasali ni kumsifu Mungu yeye havimbi kichwa kwa
masifu yetu. “Usiogope kumsifu Mungu sana; tofauti na binadamu yeye havimbi
kichwa kamwe,” alisema Paul Dibble. Kusali mpaka unasali ni kumshukuru Mungu.
George Herbert alisali, “Wewe ambaye umenipa mambo mengi sana, nipe jambo moja
zaidi – moyo wenye shukrani.” Sala siyo kumtumia Mungu. Ukifanya hivyo hujasali
mpaka umesali. Usipoamini unachokiomba kwamba utakipata hujasali mpaka umesali.
“Sala zetu zitajibiwa tutakapoamini katika tunachokiomba,” alisema John
Iverson. Unaposali kwa imani unasali
mpaka unasali. “Sala zetu zinasikika mbinguni zikiwiana kwa kiasi kikubwa sana
na imani yetu. Imani ndogo itakupatia huruma kubwa , lakini imani kubwa itakupa
huruma kubwa zaidi,” alisema Mchungaji Charles H. Spurgeon.
Tunasoma hivi
katika Biblia: “Lakini hampati kitu kwa sababu hamwombi. Mnaomba, lakini
hampewi kitu kwa sababu mnaomba vibaya, yaani kwa nia ya kushibisha tamaa zenu”
(Yakobo 4: 2-3). Mungu anajibu ombi ambalo litamtukuza zaidi. Kuna Wakristo
ambao waliishi kama sehemu moja. Wa kwanza alikuwa mkulima na wa pili alikuwa
mvuvi. Hapakuwepo na mvua kwa muda wa wiki kadhaa. Mkulima siku moja alienda
kanisani kuomba. Aliomba Mungu afanye
mvua inyeshe. Lakini hapakuwepo na mvua. Jirani yake naye alienda kuomba mvua
isinyeshe kwa vile alikwa anampeleka rafiki yake kuvua samaki . Mvua
haikunyesha siku hiyo. Mungu alisikiliza maombi yote mawili. Lakini alijibu
lile ambalo aliona linampa sifa zaidi. Kama ombi lako halimpi Mungu sifa
hujasali mpaka umesali.
Mungu anawatumia
watu kujibu sala. Licha ya ukweli
mtegemee Mungu hata kama watu
wanachelewa kukupa kile Mungu alichopitisha kwao. Mtoto mdogo alikuwa anasali
sala zake za usiku pamoja na mama yake: “Bwana, mbariki mama, mbariki baba na
Mungu naomba unipe baisikeli mpya!!!” Mama yake alimwambia, “Mbona unasema kwa
sauti ya juu sana maneno ya mwisho, Mungu sio kiziwi.” Mtoto alisema, “Lakini
babu aliyeko chumba jirani masikio yake hayasikii vizuri.” Mt. Augustini
alisema, “Sali kama kwamba kila kitu kinamtegemea Mungu.” Jiweke mikononi mwa
Mungu asilimia 100.
Omba vitu vikubwa toka kwa Mungu. Kumuomba vitu vidogo ni kama kukutana na Bill Gates wa Marekani
ukamwomba shilingi elfu mbili, wakati umekutana na bilionea, mwenye pesa kama
serikali.
Omba mapenzi ya Mungu yafanyike. “Lengo letu la sala lazima liwe mapenzi ya Mungu, na si mapenzi
yetu,” alisema D. Laurence Scupoli katika kitabu chake, The Spiritual Combat (1843). Kuna aliyesema, “Mungu hakupi
unachotaka, anakupa unachostahili.” Usimwambie Mungu sikiliza kwa kuwa mtumishi
wako anaongea, bali ongea kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza. Hapo unasali
mpaka unasali.
Ujue kuwa vita ni vya Mungu. “Msiogope, wala kufadhaishwa na umati huu mkubwa, maana hivi si
vita vyenu bali vita vya Mungu” (2 Mambo ya Nyakati 20:15). Ukiwa na Mungu wewe
ni umati.
FANYA KAZI KAMA KWAMBA KILA KITU KINAKUTEGEMEA WEWE
Mt. Augustini alisema, “Fanya kazi kama kwamba kila
kitu kinakutegemea wewe.” Hapo unakuwa umesali mpaka umesali. Mungu anahitaji
mchango wako. “Bali sisi tulimwomba dua Mungu wetu…tena tukaweka walinzi mchana
na usiku” (Nehemia 4:9). Waliweka walinzi kama kwamba kila kitu kiliwategemea
wao. Lakini walimwomba dua Mungu kama kwamba kila kitu kinamtegema Mungu. Sali
kwa kushirikiana na neema ya Mungu. Katika jarida
la Your Life (Maisha Yako) kuna
hadithi juu ya wasichana wawili ambao walikuwa katika hatari ya kuchelewa
shuleni. Mmoja alisema, “Tusimame na tusali ili Mungu atusaidie tuweze kufika
huko mapema.” Mwingine alisema: “Hapana, tukimbie kwa nguvu zetu zote, na
tusali wakati tukikimbia.” Kwa kusali wakati unakimbia unashirikiana na neema
ya Mungu.