DOMINIKA
YA 2 YA MWAKA “A “
1. Isa 49: 3, 5-6
|
2. 1 Kor 1: 1-3
|
3. Yn 1: 29-34
|
“Tazama, Mwanakondoo wa Mungu”
(Yohane 1: 29)
Akiwa amestaajabia mwanga wa
mwezi guru mmoja aliwapeleka wanafunzi wake na kunyosha kidole chake kuwaonesha
mwezi (guru ni mtu mwenye maarifa makubwa au mtaalamu wa jambo fulani) .
Wafuasi wake ambao walikuwa hawajaelewa mambo vizuri walifurahishwa na kidole
cha mwalimu wao. Baadaye wanafunzi wake walikuwa na mdahalo juu ya kidole cha
mwalimu wao. Mwanafunzi wake mwenye hekima alibaki kimya akiutazama mwezi. Kama
guru akionesha kidole. Yohane Mbatizaji aliwaambia wanafunzi wake “Tazama,
Mwanakondoo wa Mungu” (Yohane 1: 29). Yeye alikuwa ni kama kidole cha guru.
Wanafunzi hawakupaswa kumtazama Yohane bali Bwana wetu Yesu Kristo. Katika
matatizo usitazame ukubwa wa tatizo bali ukubwa na ukuu wa Yesu Kristo.
Injili
ya leo ina maneno: ona, tazama, kujua, shuhudia. Neno “kuona” limerudiwa mara
nne. Neno “tazama” limerudiwa mara moja. Lakini linajitokeza tena katika
mistari miwili inayofuata.
SIMAMA
UMTAZAME YESU: “Yohane alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi
wake. Akamtazama Yesu akitembea” (Yohane 1: 36). Yohane
Mbatizaji alisimama. Alisimama kumpisha Yesu. Mwenye nguvu mpishe. Yohane
Mbatizaji alisimama akiwakilisha
kusimama kwa Sheria ili Yesu aikamilishe na kuleta neema ya Injili. Sio sauti
tu inamtangaza Yesu Kristo hata macho ya Yohane Mbatizaji. Alimtazama.
Tumtazame Yesu. Tusimamishe shughuli zetu siku ya Jumapili tumtazame Yesu.
Tusimamishe shughuli zetu za asubuhi sana twende kanisani tumtazame Yesu wa
Ekaristi. Tukitoka kanisani tusimame mbele ya ombaomba tumtazame Yesu. Tusimame
mbele ya mwenye njaa, tumtazame Yesu. Tusimame mbele ya mwenye kiu, tumtazame
Yesu. Tusimame mbele ya mgonjwa tumtazame Yesu. Mtume Petro alishindwa kusimama kwenye maji na kumtazama Yesu. Alitazama
mawimbi akaanza kuzama.
UNAPOTUKANWA
MTAZAME YESU: “Jamaa
zake walipopata habari, walitoka wamkamate, maana walisema, “Amerukwa na akili”
(Marko 3:21). Walimtukana Yesu sembuse Yesu.
Unaposema, “Nimetukanwa.” Yesu anasema, “Na mimi.” Jamaa zake walisema,
“Amerukwa na akili.” Ukiwa mkristo si kwamba umekingiwa kutakanwa. Walimtukana
Kristo mwenyewe. Yesu alikutana na watu wenye majungu, uzushi na fitina.
Tukumbuke hawajawahi kujenga mnara katika historia ya dunia ya kuwaenzi wazushi
na waongo. Anayekutukana huenda anajitukana yeye mwenye. Kuna mtu ambaye aliingia kwenye studio ya
sanamu ya mtu. Alianza kusema vibaya juu ya sanamu. “Sanamu hii ya mwanaume
imevalishwa nguo chafu. Ndevu zimechakaa. Viatu havikupakwa rangi. Mikono ni
michafu.” Mke wa mwanaume huyo alimvuta kando na kumwambia. “Unajisema vibaya
maana unachokiona ni sura yako katika kioo.” Huyo mtu alijaribu kumtukana
mtengenezaji sanamu lakini alikuwa anajitukana.
WAKATI UNAPOKUWA NA HASIRA MTAZAME YESU: Sifa ya mwanakondoo ni upole. Tazama upole wa Yesu. Alirudisha
sikio la Malchus, uvumilivu wake kwa Mt. Petro baada ya kumkana, aliwavumilia
na kuwasemehe wauaji. Namna ya Yesu ya kujibu ilikuwa ya upole. Yuda alipomsaliti Yesu kwa busu, Yesu alimwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja
kufanya.” Mlinzi alipompiga kofi aliuliza kwa upole, “Mbona wanipiga?” Yeye amesema:
“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa
moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu”(Mt 11:29). Upole ni muhimu kwetu kwa
sababu mbili. Kwanza sisi ni viumbe wanaofikiri: Hasira mbaya inazuia kufikiri
vizuri. Kufikiri kunatutofautisha na wanyama. Pili, tuna Roho wa upole. Katika
maandiko matakatifu tunaaswa hivi: “Hamjui ni Roho ya namna gani mliyo nayo;
kwa maana Mwana wa Mtu hakuja kuyaangamiza maisha ya watu, bali kuyaokoa.” . Baba mmoja alimfokea mtoto wake aliyeiba
nyama toka mezani bila kupewa na kabla ya saa ya kula. “Rudisha nyama mezani
wewe mhuni. Muone kichwa kama gari la
Hummer.”Mtoto alijibu, “Baba sema kwa sauti ya chini na kwa upole watu walioko
nje wasijue ulivyonilea vibaya.”
UNAPOSEMWA VIBAYA MTAZAME YESU: “Ana
Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo” (Mk 3:22). Yesu
alikumbana na upinzani. Usiogope upinzani, kumbuka tiara huruka angani dhidi ya
upepo na si pamoja na upepo. Mtu akiwa mkarimu, wanasema anajitangaza. Akiwa
mchoyo wanasema ana gundi kwenye vidole, ni myinmi, ni bahili. Mtu akitoa
hotuba fupi sana wanasema hakujiandaa. Akitoa hotuba ndefu sana wanasema
hatunzi muda. Akiwa motto wanasema ni malaika. Akiwa mtu mzima wanasema achana
na Yule shetani. Akiwa mcha Mungu wanasema ni mkatoliki zaidi ya papa.
Asipokuwa mcha Mungu wanasema shetani amemweka mfukoni. Waalimu wa sheria
walisema Yesu ana Beelzebuli. Kwa tafsiri sisisi Beelzebuli maana yake bwana wa
nzi. Beelzebuli ni mkuu wa pepo wabaya. Yesu alitumia mfano kuwajibu. Kadiri ya
Baba wa Kanisa Theophylact mfano huo una maana hii: Shetani ni mtu mwenye
nguvu, mali yake ni watu ambao amewapokea; mtu asipomshinda kwanza Shetani
atamyanganyaje mali yake, ambayo ni watu anaowamiliki, kwanza mmalize shetani
harafu uwashinde wengine, na mimi ni adui zao. Namna gani wanaweza kusema nina Beelzebuli .
WAKATI RAFIKI ANAPOKUSALITI MTAZAME YESU: Bwana Yesu alikuwa rafiki
mwaminifu kwa mitume wake. Aliwaita rafiki. Lakini Yuda Iskarioti hakuwa rafiki
mwaminifu alimsaliti Yesu kwa busu. Tunasoma katika Biblia hivi: “Lakini Yesu
akamwambia, “Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?” (Luka 22: 47).
Mama Tereza wa Calcutta alikuwa na haya ya kusema: “Ona huruma ya Kristu kwa
Yuda. Bwana aliyetunza ukimya mtakatifu hasingemsaliti kwa mitume wenzake. Yesu
angesema hadharani na kuwaambia watu malengo yaliyojifichwa na matendo ya Yuda.
Badala yake alionyesha huruma badala ya kulaani. Alimuita Yuda ‘rafiki.’ Na
kama Yuda angetazama kwenye macho ya Yesu, leo Yuda angekuwa rafiki wa huruma
ya Mungu.” Mbwa ni mfano wa rafiki aliye
mwaminifu. Kuna tajiri mmoja aliyekuwa anasafiri akiwa amempanda farasi. Mbwa
wake alijaribu kumfuata Bwana wake kwa nyuma lakini Bwana huyo alimfukuza.
Lakini mbwa aliendelea kuwafuata kwa nyuma. Katikati ya safari mfuko wa fedha
uliokuwa juu ya farasi ulidondoka bila bwana huyo kujua. Mbwa kuona hivyo
alikimbia na kuwapita na kuanza kubweka mbele yao. Bwana huyo alikasirika na
kumpiga risasi. Baada ya kumpiga risasi mbwa alichechemea na kwenda kujilaza
juu ya mfuko wa bwana wake. Bwana wake alipofika hotelini na kutazama vitu
vyake aligundua mfuko wa fedha hauonekani. Akaanza kurudi nyuma amempanda
farasi wake akitafuta mfuko huo. Alimkuta mbwa amelala juu ya mfuko wa pesa
amekufa. Mbwa alikuwa rafiki mwaminifu.
UNAPOKUTANA NA WENYE MAJIVUNO YA MALI: Mtazame Yesu. Kuna watu ambao
wakiona simu yako wanajivuna, sababu ya kwao ni ya bei kubwa. Mtazame Yesu.“Mwana wa mtu
hana mahali pa kulaza kichwa.”
UNAPOKUTANA
NA WENYE MAJIVUNO YA WALIPOZALIWA NA TABAKA LAO. Mtazame Yesu. Tunasoma
katika Biblia, “Kuna zuri linaloweza kutoka Nazareti? Baraka Obama alitokea
Kisumu Kijiji cha Kogero akaingia Ikulu ya Marekani si kuitembelea bali kukaa
kama Rais.
UNAPOKUTANA
NA WENYE MAJIVUNO YA HESHIMA WALIYO NAYO. Mtazame Yesu. Tunasoma
katika Biblia, “Huyu si mwana wa seremala?” Yesu alikuwa zaidi ya mwana wa
Seremala. Ni Mungu mtu. Wewe ni zaidi ya kazi unayoifanya. Wewe ni mpendwa wa
Mungu.
UNAPOKUTANA
NA WANAOJIVUNIA UMBO LAO. Mtazame Yesu. Biblia inatwaambia juu ya Yesu wa Ijumaa
Kuu: Hana umbo wala uzuri.
UNAPOKUTANA
NA WENYE MAJIVUNO YA KISOMO: Mtazame Yesu. Tunasoma hivi katika Biblia, watu
walimshangaa Yesu, wakisema, huyu ameyapata wapi haya? na, “Ni hekima gani hii
aliyopewa huyu?”
UNAPOKUTANA NA WENYE
MAJIVUNO YA KUWA BOSI. Mtazame Yesu. Yesu alisema, “Basi, ikiwa mimi, niliye
Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi
kwa ninyi.”
UNAPOKUTANA NA WENYE
MAJIVUNO YA MAFANIKIO. Mtazame Yesu.
Tunasoma hivi katika Biblia, “alikuja kwa walio wake, walio wake
hawakumpokea. Hata jamaa zake hawakumwamini. Ni mtu aliyekataliwa na
kudharauliwa. Lakini tusisahau kwake kila goti linapigwa.
UNAPOKUTANA NA WENYE
MAJIVUNO YA KUSEMWA VIZURI. Mtazame Yesu. Baadhi ya watu walimsema Yesu vibaya:
“ rafiki wa watoza ushuru na wa dhambi.”
UNAPOKUTANA NA WENYE
MAJIVUNO YA AKILI. Mtazame Yesu. Tunasoma hivi katika Biblia: Nazungumzia mambo
haya kama Baba alivyonifundisha.