Jumapili ya 3 ya Mwaka
1. Isa 9: 1-4
|
2. 1 Kor 1: 10-13, 17
|
3. Mt 4: 12-23
|
“Kila mtu wa kwenu
husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Petro, na, Mimi
ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika?” (1 Wakorintho 1:12-13). opi
Tukiungana
tutasimama, tukigawanyika tutaanguka. Maelfu ya nati yanashirikia vipande vingi
vya gari pamoja lakini nati moja inaweza kutawanya vipande vya gari. Kupotea
kwa nati moja au kutofanya kazi vizuri kwa nati moja kunaweza kuleta kasoro
katika gari zima. Mgawanyiko waweza kuleta kasoro katika umoja. Umoja wetu
wakristu unatoka katika umoja pomoja na Kristu. Kristu hakugawanyika? Mtume
Paulo aliandika, “Kila mtu wa kwenu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa
Apolo, na, Mimi ni wa Petro, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika?”
(1 Wakorintho 1:13).
Wakristo wa
Korintho ambao Mtume Paulo aliwaandikia barua walikuwa na tatizo la
kubaguana.Kubaguana huku ni kama moto
uliongezewa petroli ya maneno na majungu. Palikuwepo na kauli mbiu nne: Mimi ni
wa Paulo, Mimi ni wa Apolo, Mimi ni wa Petro na Mimi ni wa Kristo.
Waliwashabekia wahubiri mbalimbali lakini wote walikuwa wanamhubiri Kristu.
Hatuna budi kuwa na kauli mbiu moja: Mimi ni wa Kristo. Naweza kusema: Umtafute
Kristu: umpate Kristu:umpende Kristu. Kinachotakiwa ni kuwa na moyo wa umoja.
“Usijali maneno ya watu wakisema kwamba una moyo wa umoja. Wanataka nini? Uwe
Chombo cha kuvunjika vipandevipande mara tu kinaposhikwa?” Alihoji Josemaria
Escriva (1902-1975) wa Hispania.
Mfano wa msumari
unaonesha umuhimu wa umoja. Msumari usipokazwa sana au ulegeapo na kutoka ulipotiwa. Sehemu
kubwa pia ulegea ama magurudumu ya mtambo huathirika au kuvunjika. Kazi
hucheleweshwa. Pengine mtambo mzima huingiwa na ubovu. Josemaria Escriva
alisema, “Usisahu kwamba umoja ndio alama ya uzima: kupotea umoja kuna maana ya
kuoza, ishara dhahiri ya kuwa maiti.”
Jambo lingine la
kuzingatia ni katika kuleta umoja ni kuvumiliana. Kuna hadithi ya wayahudi
inayomhusu mzee wa miaka themanini aliyekutana na Abrahamu. Abrahamu alikuwa
amekaa karibu na mlango wa nyumba yake. Mgeni huyo alimuomba Abrahamu akae
kwake walau siku moja. Abrahamu alimuuliza mzee huyo, je wewe ni mtu
anayeamini? Mzee huyo alijibu, naamini na kuabudu jua. Abrahamu alimfukuza na
kusema kuwa hauwezi kulala hapa na kumuita mbwa mchafu. Usiku alipolala
Abrahamu Mungu alimtokea katika ndoto na kumwambia: Abrahamu haukuweza
kumvumilia mzee huyo walau kwa usiku mmoja. Mimi nimemvumilia miaka themanini.
Katika dunia hii watu wana imani tofauti. Kinachohitajiwa ni kupendana,
kuvumiliana na kueleweshana polepole bila kuleta mfarakano maana sisi ni
wanadamu yaani watoto wa Adamu. Mungu ni Baba yetu sote. Biblia yasema, “Naye
alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wanchi
yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao ” (Matendo 17: 16).
Mwanga wa umoja una
nguvu unaweza kuangaza, taifa zima na dunia nzima na kufukuza giza la kutoelewana na utengano.Tukumbuke
kuwa kidole kimoja hakivunji chawa. Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Kitaifa
umoja ni uhai, utengano ni kifo. “Bwana aliweka wengine sabini na
wawili, aliowatuma wawili wawili wamtangulie katika miji na vijiji vyote
alivyotaka kuvitembelea mwenyewe” (Luka 10:1).
“Peke yetu tutafanya
machache, pamoja tutafanya mengi,” alisema Helen Keller. Nguvu kubwa ya uongozi
wowote ni umoja, na hatari kubwa kwa uongozi wowote ni utengano. Katika
kuungana uongozi unasimama, katika kutengana uongozi unaanguka. Uongozi
unahitaji moyo wa ushirikiano. Yesu kama kiongozi wa kuigwa hakufanya kazi peke
yake. Tunasoma hivi katika Biblia, “Bwana aliweka wengine sabini na wawili,
aliowatuma wawili wawili wamtangulie katika miji na vijiji vyote alivyotaka
kuvitembelea mwenyewe” (Luka 10:1). Kifungu hiki cha Biblia kinabainisha ukweli
kuwa macho mawili huona vizuri kuliko moja. Umoja ni nguvu, utengano ni
udhaifu.
Viongozi wazuri lazima
washirikiane katika kugawana baraka na kugawana lawama, kugawana mema na
kugawana shutuma. Anayefunga gori ni mmoja lakini timu yote husherekea.
Wachezaji wote wanagawana furaha ya ushindi. Hivyo hivyo timu ikishindwa
wachezaji wote wanagawana majonzi ya kushindwa. Ushirikiano katika mambo muhimu
ni jambo muhimu. Yesu aliwataka wafuasi wake wasiwakatishe tamaa wale ambao
walikuwa wanafanya miujiza kwa jina lake
ingawa hawakuwa katika
kundi moja. Kumbuka maneno ya Marko mwinjili katika Biblia, “Mwalimu, tulimuona
mtu akiwafukuza pepo wabaya kwa jina lako, hata baada ya kuwa haandamani nasi,
hivyo tukamkataza. Msimkataze, Yesu akanena, kwani hakuna anayeweza kutenda
miujiza kwa jina langu akarudi kunisema vibaya. Kwa sababu asiye mpinzani wenu
yu upande wenu.”
Yale yanayotuunganisha kama ndugu na binadamu ni ya muhimu kuliko yale
yanayotutenganisha. Kuwa na lengo moja kama
kuboresha maisha ya watu ni jambo ambalo halina budi liunganishe viongozi.
Kwamba viongozi wanamhudumia mtu yule yule ni jambo la kuwaunganisha viongozi.
Yesu alishirikiana na watu wa aina yote. Alishirikiana na matajiri waliomwazima
mwanapunda. Alishirikiana na maskini wengine aliwatibu kama
wakoma kumi. Alishirikiana na wenye dhambi kama Zaccheus na alishirikiana na
watu wasio kuwa na hila kama Nathanaeli.
Uongozi wake ulijumuisha wavuvi kama Simoni Petro na watoza ushuru kama Mathayo.
Vidole siku moja vilikuwa na
ugomvi. Kidole gumba kilisema mimi ni bora sana , bila mimi hauwezi kushika kalamu, pili
ni mnene na mfupi. Kidole cha shahada nacho kilianza kujisifu na kusema, mimi
ni bora sana ,
bila mimi mzazi hawezi kuonya. Bila mimi walimu hawawezi kufundisha na kuonya.
Kidole cha kati kilisema, tujipange mstari nani mrefu zaidi. Mimi ni bora.
Kidole cha pete kilinyamazisha vidole vingine na kusema, mimi ni bora. Bila
mimi maaskofu pete zao hawataziweka wapi? Bila mimi Bwana na Bibi arusi pete
zao wataziweka wapi? Kidole cha mwisho kadogo kikasema, sisi vidole vidogi
viwili ni bora. Mtu akiwa anasali na viganja viko kifuani sisi tunakuwa
tumekaribia altare. Vidole kwa kawaida vinafanikiwa vinapounagana na si pale
vinaposhindwa kushirikiana.