JUMAPILI
YA HURUMA YA MUNGU (JUMAPILI YA 2 YA PASAKA)
“Tia kidole chako humu, tazama mikono
yangu, lete mkono wako na kuutia katika ubavu wangu na usikose imani” (Yohane 20:
27)
“Bwana anatuonesha kupitia
Injili, vidonda vyake. Ni vidonda vya huruma. Ni kweli; vidonda vya Yesu ni
vidonda vya huruma,” alisema Papa Francis katika mahubiri yake Jumapili ya
Huruma ya Mungu mwaka 2015. Yesu alipofuka vidonda vitano vilikuwa ni
utambulisho wake. Yesu aliwaonesha mitume wake mikono yake na ubavu wake,
walitambua kuwa ni yeye. “Yesu anatualika kutazama vidonda hivi, kuvigusa kama
Thomasi alivyofanya, kuponya kutoamini kwetu. Licha ya hayo yote, anatualika
kuingia kwenye fumbo la vidonda hivi, ambalo ni fumbo la upendo wake wa
huruma,” alisema Papa Francis. Vidonda hivi vilibaki kama makovu si kumbukumbu
ya ukatili kumbukumbu ya ukombozi. Yesu ametukomboa kwa huzuni na mateso.
Utabiri wa nabii Isaya unasema ukweli wote, “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,
alichubuliwa kwa maovu yetu…na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5).
Yesu alibaki na makovu yake kama alama ya ushindi na utukufu. “Nikaona
Mwanakondoo amesimama kati ya kiti cha enzi na wenye uhai wanne waliozungukwa
na wazee. Alionekana kama amechinjwa” (Ufunuo 5:6). Kuonekana kama amechinjwa
kunabainisha makovu yake makubwa matano. Tukiyatazama kwa miwani chanya ni
makovu ya kushinda vita dhidi ya uovu. Tukiyatazama kwa miwani hasi ni makovu
ya ukatili.
Wachimba migodi wana vidonda vya
kubeba mizigo wana “taji la miiba” na
makuli na wabebaji mizigo. Wawindaji wana vidonda miguuni, vidonda vya huruma,
wakitafuta riziki ya familia. Fundi seremala wana vidonda vya kuchomwa na
misumari. Wakati wa kuandikisha watu kwenye daftari la kudumu la wapiga kura
iligundulika kuwa katika jamii za wakulima na wapiga kokoto alama za vidoleni
zilishatoweka sababu ya matendo ya huruma kutafuta riziki kwa ajili ya
wanafamilia. Kuna makovu ya huruma kwenye viganja. Mafundi wa magari vidole vyao vina makovu ya
huruma wakitafuta riziki za wanafamilia. Wakati wa kuandikisha wapiga kura
kwenye daftari ya kudumu, iligundulika tulivyosikia kwenye vyombo vya habari
kuwa watu wengine alama za vidoleni zilikwishafutika sababu ya shughuli za
kilimo. Hayo ni makovu ya huruma kwa nafsi zao na huruma kwa wanafamilia
wakiwatafutia lishe bora. Kuna watawa na mapadre ambao wana makovu kwenye
magoti sababu ya tendo la huruma la kuwaombea wazima na wafu.
Mama aliyejifungua kwa njia ya
operesheni ana makovu ya huruma. Ni huruma kwake na ni huruma kwa mtoto. Siku
moja kuna mtoto wa miaka kumi na miwili aliyekuwa anaogelea mtoni. Mamba
akashika miguu yake kwa meno. Mama yake aliyekuwa karibu akashikilia mikono kwa
nguvu zake zote, hata kucha zikatoboa mikono ya mtoto. Bahati nzuri palikuwepo
na mwindaji karibu. Alimpiga huyo mamba risasi, mamba alimwachia mtoto. Mtoto
alipokuwa anauguza majeraha aliyasifia majeraha aliyokuwa nayo mikononi ni
majeraha aliyopata sababu ya huruma ya mama, aliyemshikilia mpaka kucha za mama
zikatoboa sehemu za mikono yake.
Kuna vidonda ambavyo si vya
huruma: kuchubuka kwa sababu ya ulevi, kuchubuka kwa sababu ya hasira. Siku
moja huko Afrika ya Kusini Gandhiji alikuwa anasafiri kwenye treini daraja la
kwanza kinyume cha sheria. Polisi mzungu alitaka kumwondoa toka daraja la
kwanza Gandhiji. Lakini Gandhiji aliona si haki alikataa. Mambo yalipofikia
hatua hii polisi alikasirika na kumpiga kwa teke. Akijizuia kumtukana Gandhiji
alijibu: “Ndugu, umehumiza mguu wako?” Polisi aliposikia swali hilo aliona
aibu. Kama mguu wa polisi ulihumia kwa kumpiga teke Gandhiji, hicho hakikuwa
kidonda cha huruma.
Bwana wetu Yesu Kristo
alipofufuka alikuwa na makovu ya vidonda vya mwilini bila shaka alikuwa na
makovu ya vidonda vya moyoni. Tunajifunza kwake mtazamo chanya. Alifufuka na
makovu kama ishara ya ushindi na si ishara ya ukatili. Huo ni mtazamo chanya.
Kuwa na mtazamo chanya ni tiba ya vidonda vya moyoni.
MILANGO ILIYOFUNGWA NI BARAKA YA
HURUMA KATIKA SURA YA BALAA
JUMAPILI
YA HURUMA YA MUNGU (JUMAPILI YA 2 YA PASAKA)
“(Yesu), akasimama katikati,
ingawa milango ya chumba walimokaa wafuasi ilikuwa imefungwa kwa kuwaogopa
wayahudi” (Yohane 20: 19).
“Mungu anapokupa mwanzo mpya, unaanza na
mwisho. Mshukuru kwa milango iliyofungwa. Mara nyingi inatuelekeza kwenye milango sahihi!” alisema
mwanamke wa imani. Mlango wa ualimu wa Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere
ulipofungwa ukamwelekeza kwenye mlango wa urais. Naye Joyce Meyer alikuwa na
haya ya kusema, “Usimwombe Mungu tu kufungua milango, lakini pia muombe Mungu
kufunga milango ambayo inahitaji kufungwa.” Mlango wa ualimu kwa Baba wa Taifa
ulihitaji kufungwa. “Leo funga baadhi ya milango. Si kwa sababu ya majivuno,
kutokuwa na uwezo, au ubabe, lakini ni kwa sababu tu haikupeleki popote,”
alisema Paul Coelho.
Kwa mtu anayeomba kazi mlango
uliofungwa ni ishara ya kukataliwa au kucheleweshwa lakini inaweza kuwa baraka
katika sura ya balaa. Kwa milango iliyofungwa kwa sababu ya woga inaweza kuwa
baraka katika sura ya balaa. Yesu alipouawa Ijumaa Kuu wafuasi wake baadaye
waliingia chumbani na kufunga milango ya chumba. Milango iliyofungwa
iliwawezesha mitume kufaidi tendo la huruma la kufundisha wajinga.
Tunasoma katika Injili ya Yohane.
“(Yesu), akasimama katikati, ingawa milango ya chumba walimokaa wafuasi ilikuwa
imefungwa kwa kuwaogopa wayahudi” (Yohane 20: 19). “Yesu alingoja mpaka wote wamekusanyika: na
milango imefungwa, ili kuonesha kuwa namna alivyoingia kwenye chumba ndivyo
alivyoweza kufufuka jiwe likiwa juu ya kaburi,” alisema Baba wa Kanisa
Theophilo. Milango iliyofungwa ilisaidia kama nyenzo za kufundishia somo la
ufufuko. Yesu alifufuka wakati jiwe liko juu. Liliviringishwa na malaika sio
kwa sababu Yesu apite bali mitume na wanawake wafuasi wa Yesu waweze kushuhudia
kuwa amefufuka.
Milango iliyofungwa ilimtenga
Thomasi, hakuwa na mitume. Aliporudi na kuambiwa kuwa Bwana Yesu amewatokea hakuamini.
“Kutoamini kwa Thomasi (Yoh 11:6; 14:5; 20:24.26-29; 21:2) kumeleta faida zaidi
kwenye imani yetu kuliko imani ya wafuasi wengine. Anavyomshika Kristo na
kusadikishwa, kila mashaka yanaondolewa na imani yetu inaimarishwa. Hivyo
mfuasi aliyekuwa akitia mashaka, aligusa madonda ya Yesu na kugeuka kuwa
shahidi wa ukweli wa ufufuko” (Mt Gregori Mkuu). Tukumbuke kuwa kufundisha ni
tendo la huruma, na ni baraka. Ni kweli milango iliyofungwa ni baraka ya huruma
katika sura ya balaa.
Tendo la Yesu kuingia kwenye
chumba wakati milango imefungwa ni somo juu ya ubikira wa Bikira Maria, baada
ya kumzaa Yesu Kristo, alibaki bikira. “Milango iliyofungwa haikuzuia mwili
ambapo umungu ulikaa. Aliweza kuingia bila milango kuwa wazi, ambaye alizaliwa
bila kuharibu ubikira wa mama yake,” alisema Mt. Augustini. Tukumbuke kuwa
kufundisha ni tendo la huruma, na ni baraka. Ni kweli milango iliyofungwa ni
baraka ya huruma katika sura ya balaa.
“Mlango mmoja unapofungwa
mwingine unafunguliwa; lakini mara nyingi tunatazama kwa kujutia mlango
uliofungwa na hatuoni mlango ambao umefunguliwa kwa ajili yetu,” alisema
Alexander Graham Bell. Mwanzoni mtume Thomasi aliutazama sana mlango uliofungwa
wa Yesu wa Ijumaa Kuu na kuchelewa kuuona mlango uliokuwa wazi wa Yesu Kristo
wa Pasaka.
Soichiro Honda wakati alipoomba
kupewa kazi katika Kampuni ya Toyota Motors, baada ya kusailiwa hakupewa kazi.
Mlango ulikuwa umefungwa. Lakini alitazama mlango uliofunguliwa. Tatizo la
kukosa kazi katika kampuni hiyo lilikuwa ni alama ya mkato na si nukta.
Alianzisha kampuni yake mwenyewe na kuanza kutengeneza baisikeli zenye injini
ndogo. Leo hii Honda ni kampuni kubwa ya kutengeneza pikipiki na magari.
Soichiro Honda alisema: “Mafanikio yanawakilisha asilimia moja ya kazi yako
ambayo inatokana na asilimia tisini na tisa zinazoitwa kushindwa.” Kifaranga
kwenye yai kinapopambana na ukuta wa yai uliokizunguka kitoke ukikionea huruma
ukakisaidia kutoka unakinyima nafasi adimu ya kujiimarisha.
Mlango uliofungwa ni baraka ya
huruma katika sura ya balaa. Lakini Yesu
hauzuiliwi na milango iliyofungwa. Kuna methali ya Tanzania isemayo, “Baraka ni
baridi hata uwe umefunga mlango inaingia.” Yesu naye anaingia kwenye milango
iliyofungwa. Mlango wa kupata kazi kama umefungwa Yesu anaweza kukusaidia
kuingia. Mlango wa kupata mchumba kama umefungwa Yesu anaweza kukusaidia
kuingia. “Naamini , ukiendelea kuamini, ukiendelea kutumaini, ukiendelea kuwa
na mtazamo sahihi, na kama una shukrani, utamuona Mungu anafungua milango
mipya,” alisema Mchungaji Joel Osteen.