Jumapili
ya 3 ya Kwaresima
1. Kut
17: 3-7
|
2. Rum
5: 1-2, 5-8
|
3. Yn
4: 5-42
|
“Huyo mama
akauacha mtungi wake pale, akaenda” (Yohane 4:27).
Masomo ya leo yanahusu wabebaji.
Musa alibeba fimbo. Mwanamke Msamaria alibeba mtungi na Habari Njema baadaye.
Mitume walibeba chakula. Yesu alibeba maji ya uzima. Bwana Yesu alibeba Teolojia aliyozungumza juu
yake na mwanamke Msamaria ambaye hakuwa malaika alikuwa na hadithi yake.
Mwanamke Msamaria alibeba mtungi. “Huyo mama akauacha mtungi wake
pale, akaenda” (Yohane 4:27). “Nakuuliza na kujiuliza: ‘Nini mtungi wako wa
moyoni, ambao unakuelemea, ambao unakuweka mbali na Mungu? Tuuweke kando kidogo
na mioyo yetu tusikilize sauti ya Yesu akitupa maji ya aina nyingine, maji
mengine yanayotuleta karibu na Bwana,” alisema Papa Fransisko. Mwanamke huyu alikuwa kama mtungi wenye nyufa.
Kuna hadithi juu ya mchota maji.
Alikuwa akichota maji na kuyapeleka kwa mfalme. Alitumia mitungi miwili. Mtungi
mmoja ulikuwa na nyufa. Hivyo maji yalimwagika njiani. Mtungi huo ulilalamika
kwa maana ulifikishwa nyumbani bila chochote. Mtungi mwingine ulifikishwa
nyumbani umejaa maji. Mchota maji aliuambia mtungi uliokuwa unalalamika. Tazama
nyuma yako maua yanayopendeza. Nilipanda mbegu za maua njiani baada ya kuona
kuwa una nyufa na umekuwa ukizimwagalia. Mungu anaweza kutumia nyufa zetu kutoa
jambo zuri. Bwana Yesu alitumia nyufa za mwanamke huyu Msamaria kutoa jambo
zuri, mahubiri juu ya Maji ya Uzima.
Mwanamke Msamaria alibeba aibu. Alikuja kuchota maji saa sita ili
kukwepa maneno na macho ya watu. Kisima kilikuwa mahali pa kukutana na mahali
pa ufunuo wa mambo. Ilikuwa ni sehemu ya jumuiya kukutana. Maji yalichotwa
asubuhi sana na jioni. Wanawake na wasichana walikusanyika kisimani. Palikuwepo
muda wa kubadilishana habari: nani alikuwa anachumbiwa, nani alizaa nje ya
ndoa, nani anauza sana sokoni, nani amejifungua mtoto, nani anaiba waume za
watu. Walifua nguo zao karibu na maeneo hayo na kunyesha mifugo. Ni katika
kisima Rebecca na Rachel walipata wachumba wao: Isaka na Yakobo. Palikuwepo na
mkono wa Mungu katika wanandoa hawa (Mwanzao 24: 10-67; 29: 1-14). Kisimani ni sehemu ya ufunuo.
Hagar mwenye mimba alipata ufunuo kisimani (Mwanzo 16: 1-14)
Mwanamke msamaria alibeba maswali. “Injili inamwonesha Yesu
akikutana na Mwanamke Msamaria huko SIkari, karibu na kisima cha zamani ambapo
mwanamke alienda kuchota maji kila siku…Yesu alihitaji kukutana na mwanamke
Msamaria ili kufungua moyo wake: alimuomba maji ili kuleta kwenye mwanga kiu cha
mwanamke. Mwanamke anahamasika kwa kukutana huku. Anamuuliza Yesu maswali kadhaa
ya msingi ambayo sote tunayabeba moyoni, lakini mara nyingi hatuyajali. Sisi
nasi pia tunayo maswali mengi ya kuuliza, lakini hatuna ujasiri wa kumuuliza
Yesu! Kwaresima ndugu zangu ni fursa ya kujitazama ndani na kuelewa mahitaji
yetu ya kweli kabisa ya kiroho, na kuomba msaada wa Bwana katika sala,” alisema
Papa Fransisko (Malaika, Machi 23, 2014). Mwanamke Msamaria alikuwa na ujasiri wa kumuuliza Yesu maswali. Kuuliza
si ujinga: “Je, wewe uliye Myahudi, unaniomba mimi niliye mwanamke Msamaria, maji
ya kunywa?” (Yohane 4:9); “Bwana, huna chombo cha kutekea, na kisima ni kirefu;
utapataje maji ya uzima?” (yohane 4:11); “Je, wewe u mkubwa kuliko baba yetu Yakobo, aliyetupa
kisima hiki, naye mwenyewe, na wanawe, na wanyama wake wakanywa maji yake?” (Yohane
4: 12); “Bwana, nipe maji hayo, nisione tena kiu, wala nisifike tena hapa
kuteka maji” (Yohane 4:15).
Mwanamke Msamaria
alibeba Habari Njema. Alienda mjini na kuwaambia watu: “Njoni mtazame mtu
aliyeniambia yote niliyotenda. Labda huyu ni MAsiya?” (Yohane 4: 29). Watu
walitoka mjini. Mwanamke anakuwa mfuasi na mmisionari. Watu wa mjini wanakuja
kwa Yesu kufuatia neno lake pasipo kuhitaji ishara. Nasi tubebe Habari Njema.
Mwanamke alibeba maneno ya sifa: Alimwita kwanza Yesu Myahudi. Baadaye
alimwita Bwana. Halafu alimwita nabii. Hatimaye alimwita Masiya. Tunapotoa
sadaka ya vitu tumpe Mungu pia sadaka ya maneno.“Mtolee Bwana maneno ya
kitubio” (Hosea 14:3). Mwanamke huyu alitoa sadaka ya maneno.
Mitume walibeba
chakula: “Rabbi kula (Yohane 4:30);” Chakula ni picha nyingine ya uzima wa
milele. Kama mwanamke alivyoshinda kutoelewa kwake kuhusu kuabudu, sasa wafuasi
wanaalikwa waache kutoelewa kwao kuhusu chakula na kanuni za usafi. Kama
chakula kinavyoliwa kwa kushirikiana, vivyo hivyo Mungu anashirikisha zawadi ya
uzima wake wa kimungu kwa binadamu.
Mitume walibeba chuki bila sababu: Katika hadithi ya Mwanamke
Msamaria Injili inasema kuwa wafuasi
walishangaa kuwa Bwana wao alikuwa anaongea na mwanamke huyu. Lakini Bwana ni
mkubwa kuliko chuki yao bila sababu, ndiyo maana hakuogopa kumhutubia mwanamke:
huruma ni kubwa zaidi ya maamuzi mbele (chuki bila sababu). Lazima tujifunze
jambo hili vizuri! Huruma ni kubwa zaidi ya chuki bila sababu, na Yesu ni
mwenye huruma sana! Sana!” alisema Papa Fransisko wakati wa Sala ya Malaika
Machi 23, 2014.
Musa alibeba fimbo.
“Bwana akamjibu Musa, “…ukachukue mkononi ile fimbo uliyopiga nayo mto” (Kutoka
17:5). Kila ulicho nacho Mungu anaweza
kukibariki kikasaidia kuleta muujiza. Mungu alimuuliza Musa kabla ya hapa: Una
nini? Musa alisema nina fimbo. Mungu alisema inatosha. Cheti chochote ulicho
nacho Mungu anaweza kukitumia kukubariki.
Yesu alibeba maji ya
uzima: Yesu Kristo anambeba Roho wa Mungu anayeonjeka katika Ekaristi (Ufunuo
21: 6; 22:17).