Jumapili
ya 8 ya Mwaka A
1.
Isa 49: 14-15
|
1 Kor 4:1-5
|
Mt. 6: 24-34
|
“Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake, aweza kumsahau mzao wa tumbo
lake asimhurumie? Hata kama yeye angemsahau lakini mimi sitakusahau wewe hata
kidogo” (Isaya 49: 15-15). Sifa mojawapo
ya Mwenyezi Mungu ni kukumbuka. Tumuige katika hilo. Kumbuka kukumbuka. Kuna
aliyesema, “Kila mara kumbuka kusahau mambo yaliyokuhuzunisha lakini usisahau
kamwe mambo yaliyokufurahisha. Kila mara kumbuka kusahau marafiki waliokusaliti
lakini usisahau marafiki waliobaki nawe. Kila mara kumbuka kusahau matatizo
yaliyopita lakini usisahau kukumbuka baraka zinazokujia kila siku.” Sisi kama
binadamu tuna changamoto ya kusahau.
Visa hivi hapa
vinabainisha ukweli huu. Kuna mtoto mdogo ni kama machoni alikuwa anatuma
ujumbe: Ukimwona mama yangu kwenye “facebook” tafadhali mkumbushe bado niko
kwenye beseni la kuogea. Mama alimsahau mtoto. Kuna baba mmoja ambaye alikuwa
anampeleka shule kwa gari mtoto wake aliyekuwa amesinzia. Akasahau akaenda naye
kazini. Akasahau kuwa yupo kiti cha nyuma akatoka na kufunga gari. Vyoo vyote
vilikuwa vimefungwa. Alipotoka ofisini wazo lake lilikuwa kupitia shuleni
kumchukua mtoto. Alipofungua mlango wa nyuma wa gari kuweka kompyuta yake ndogo
alikuta mtoto ameishaaga dunia. Mwenyezi ni tofauti na wazazi hao. Tumuige
Mungu katika kukumbuka.
Tunasoma katika Biblia,
“Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake, aweza kumsahau mzao wa tumbo lake
asimhurumie? Hata kama yeye angemsahau lakini mimi sitakusahau wewe hata kidogo”
(Isaya 49: 15-15). Kuna majina ya watu yanayosisitiza kuwa Mungu anakumbuka.
Zahari maana yake Mungu amekumbuka. Zakaria maana yake Yehova amekumbuka au
kukumbukwa na Mungu. Sakeri (Jina la Kiebrania) kukumbukwa na Mungu. Alazia
maana yake Bwana amekumbuka.
Kwanza
kukumbuka ni kuhuisha yaliyopita (anamnesis). Bwana Yesu
alisema, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.” Alitaka tuhuishe tendo lake la
kujitoa sadaka. Ni kuweka jana
katika leo. Ni kuitia nguvu leo. Watu hukumbuka siku za kufunga ndoa, kufunga
nadhiri, siku za kuzaliwa, siku ya kupata uhuru, siku ya mashujaa. Wakati wa
kuaga mwili wa marehemu wengine huuisha maisha yao na marehemu au huisha misiba
yao nao hulia sana.
Pili, ni kufukua
kumbukumbu zilizopotea (Zakar kwa kiebrania). Ni kufufua yaliyozikwa zamani. Tuna
methali isemayo bichi huamsha lililokauka. Daudi alifufua ya zamani na kusema, “Mama
yangu alinichukua mimba hatiani” (Zaburi 51: 7). Tatu ni kufikiri au kutafakari
(Zakar). Katika mtazamo huu Ayubu alisema, “Mimi mwenyewe nikifikiri hali
yangu, naona bumbuazi natetemeka mwili wangu wote” (Ayubu 21:6). Nne kukumbuka
ni kutaja (zakar). Tano ni kwendea mtu maalumu (mimnéskó). Kupoteza uwezo wa
kukumbuka kuna matokeo mabaya.
Kwanza, ukipoteza uwezo
wa kukumbuka unapoteza uwezo wa kushukuru. Kushukuru ni kukumbuka. Ukikumbuka
utashukuru. Siku ya Kushukuru ilikuwa imekaribia wanafunzi wa darasa la
awali –Kindergarten au chekechea waliambiwa kuchora picha ya kitu ambacho
katika maisha yao kimewasaidia na hivyo wanamshukuru Mungu kwa kitu hicho.
Baadhi ya wanafunzi walichora nyumba, wengine walichora gari, ndege, chakula,
kinyango. Mtoto mmoja alichora mkono. Wanafunzi walianza kujiuliza ni mkono wa
nani...mkono wa Mungu? Mkono wa Polisi? Mkono wa mkulima? Hakuna aliyeweza.
Wakati wa mapumziko mwalimu alimwendea mwanafunzi huyo na kumuuliza. Mkono huu
ni wa nani? Mwanafunzi wa darasa la awali alijibu, “Ni mkono wako mwalimu.”
Mwalimu alitokwa na machozi alivyokumbuka alivyokuwa anamsaidia mwanafunzi huyo
kuvuka barabara akimshika mkono kwa vile alikuwa ni mlemavu wa mguu. Pia
Alimshika mkono kumsaidia kuandika a, e, i, o, u. Ni kwa namna hiyo Mungu
anatushika mkono tufungue mlango wa kutoka kwenye majaribu.
Pili, ukipoteza uwezo
wa kukumbuka unapoteza uwezo wa kuthamini. Ukikumbuka utathamini. Tatu,
ukipoteza uwezo wa kukumbuka, unapoteza uwezo wa kupenda. Ukikumbuka utapenda.
Tutakase kumbukumbu za
mabaya. “Ni vizuri zaidi kusahau na kutabasamu kuliko kukumbuka na kuhuzunika,”
alisema Christine Rosetti. Namna ya kutakasa kumbukumbu mbaya ni matukio
yaliyopita kuyapa maana. Kosa la Adamu na Eva la kula tunda limeitwa na Kanisa
Katoliki-Kosa lenye heri lililomleta mkombozi.
ROHO
MTAKATIFU NI MKUMBUSHAJI: “Kila dokezo tunalopokea la
kukumbuka ni kwa neema ya Roho Mtakatifu,” alisema Mt. Augustino wa Hippo. “Lakini
huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,
atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yohane 14:26)
Katika masuala ya imani
Roho Mtakatifu anatukumbusha yale ambayo Yesu alisema. Katika masuala ya
majaribu ya kutenda mabaya, tunakumbuka aya fulani kwenye Biblia, amri ya
Mungu, ushauri mzuri wa rafiki, fundisho la Kanisa, methali inayoonya, msemo
unaokataza tendo baya, inakuja picha ya Yesu, picha ya hukumu ya mwisho. Hayo
mambo yanapita akilini mwetu. Ni kazi ya Roho Mtakatifu.