JUMAPILI YA TANO YA PASKA
Mtume wa Yesu Thomasi alimuuliza
Yesu: “Bwana, hata uendako hatujui; basi, twaijuaje njia?” (Yohane 14: 5).
Anayeuliza njia hatakosa njia. Ni
methali ya Kiswahili. Kuuliza ni msingi wa kujua. Kuuliza ni msingi wa hekima. “Ufunguo
wa kwanza wa hekima ni kuuliza kwa uangalifu na mara nyingi …kwa kuwa na
mashaka unauliza na kwa kuuliza unafikia ukweli,” alisema Peter Abelard
mwanafalsafa wa Kifaransa (1079 – 1142). Kuna mtoto aliyemuuliza maswali mengi
baba yake kama: Baba lami inatengenezwa na nini? Baba kwa nini Mungu ameficha
madini mbali sana? Baba kiberiti kinatengenezwaje? Baba mimi nilitoka wapi na
namna gani? Baba yake akamwambia mtoto mimi ningewasumbua wazazi wangu kwa
maswali mengi kama haya ingekuwaje? Mtoto akamjibu: “Ungepata majibu ya
kunijibu.” “Mtoto anaweza kuuliza
maswali elfu moja ambayo mtu mwenye busara sana hawezi kujibu,” alisema Jacob
Abbott. Nakubaliana na Charles Proteus Steinmetz aliyesema: “Hakuna mtu yeyote
anageuka mpumbavu isipokuwa akiacha kuuliza maswali.” Huyu alikuwa mwamerika
mwenye asili ya Kijerumani (1865 – 1923).
Mtume wa Yesu Thomasi alimuuliza
Yesu: “Bwana, hata uendako hatujui; basi, twaijuaje njia?” (Yohane 14: 5). “Kuuliza
si upumbavu ni tamaa ya kusikiliza yote vizuri kabisa.” Ni methali ya Kilozi.
Mtume Thomasi Msimamizi wa Watafiti alikuwa na tamaa ya kusikiliza vizuri. Yesu
alimjibu: Mimi ni Njia Ukweli na Uzima. Wahaya
wa Tanzania wana methali isemayo: Kuulizia njia wakati umekanyaga kwenye njia
hiyo. Thomasi alipoulizia njia alikuwa kwenye njia ya Yesu. Wanafunzi wa Yesu
walijulikana kama Wanafunzi wa Njia. Yesu alisema kuwa yeye ni Njia. Swali la
Mtume Thomasi lilikuwa swali la msingi. Methali ya Kiswahili inasema yote:
Usiende bila kuuliza. Mtume Thomasi alijua kama isemavyo methali ya Uganda:
Kuuliza ni kujua. “Ukitaka jibu lenye hekima, lazima kuuliza swali lenye maana,”
alisema Johann von Goethe. Thomasi aliuliza swali lenye maana na alipata jibu
lenye hekima.
Wayahudi ni watu waliongolea sana
njia. Katika Biblia tunasoma maneno kama haya: Njia za Mungu si njia zetu. “Patakuwepo
na barabara kuu, nayo itaitwa njia takatifu: wasio safi hawataruhusiwa pale”
(Isaya 35:8). Njia inaweza kumaniisha falsafa au mtazamo mfano Njia za Mungu si
njia zetu. Falsafa ya Yesu ni Ijumaa Kuu kwanza Jumapili ya Paska baadaye au
dhiki kwanza faraja baadaye. Yesu yeye ni njia kwa maana hii. Fikiria huko nchi
ya ugenini. Unaulizia njia. Mtu anakwambia. Chukua barabara ndogo upande wa
kulia utakayokutana nayo. Ukifika kwenye makutano ya barabara panda kushoto.
Nenda moja kwa moja. Utaona Kanisa upande wa kulia. Pita hapo. Usitoke barabara
hiyo. Hesabu barabara ndogo nne upande wa kushoto. Barabara ya tano ndipo
penyewe upande wa kulia kwake. Lakini fikiria huyo mtu uliyemuuliza anakwambia
nitakupeleka mimi mwenyewe. Yesu hakutoa ushauri na maelekezo. Anatuongoza yeye
mwenyewe. Hatumwambii tu juu ya njia yeye mwenyewe ni njia.
“Jambo muhimu ni kutoacha
kuuliza,” alisema Albert Einstein. Mitume hawakuacha kumuuliza Yesu. Baada ya
Thomasi kuuliza swali hilo Philipo naye aliuuliza: “Bwana, utuoneshe Baba,
yatutosha.” Philipo alitaka kumuona Mungu kwa macho ya akili yaani kumwelewa.
Mazoea ambayo huleta dharau labda yalimfanya kuuliza swali la namna hiyo. Matendo
ya Yesu yalikuwa ya kimungu kama: kutembea juu ya maji, kufufua wafu, kukemea
upepo na ukamtii, kuponya wagonjwa kwa neno tu, na kusamehe dhambi. Kama
tunataka kumjua Mungu hatuhitaji kuifikiria njia yetu kwa mzunguko au kutumia
muda mwingi katika utafiti wa pekee. Tunachohitaji kufanya ni kumwangalia
Kristo, kuona alichokifanya, kusikiliza kile alichofundisha, kuangalia
alivyotenda, kuangalia jinsi alivyopenda, kuangalia ni nani aliyempendelea,
nani alishirikiana naye na kwa sababu gani, nani na pamoja na nani alikula
chakula chake, ni nani aliyemkaripia au kumtetea, kwa sababu yeye ni sura ya
kibinadamu ya Mungu. Kuna aliyesema hivi: “Mungu atajibu maswali yetu yote kwa
njia moja na njia moja tu – kwa kuitaja, kutuonesha zaidi kuhusu Mwana Wake.”
Mwana wake ni Yesu.
Ni katika kuuliza mambo mengi
yamevumbuliwa. “Katika mambo yote, biashara na shughuli binafsi, ni jambo lenye
tija kwa sasa na baadaye kutundika alama kubwa ya kuuliza kwenye mambo ambayo
umeyachukulia kuwa ni ya kweli,” alisema Bertrand Russell. Kuuliza si ujinga ni
kutaka kujua. “Lugha ilivumbuliwa ili kuuliza maswali. Majibu yanaweza kuwa
minongono au ishara, lakini maswali lazima yaulizwe kwa sauti. Ubinadamu
ulikomaa pale ambapo mtu aliuliza swali la kwanza. Kudumaa kijamii hakutokani
na kukosekana kwa majibu bali kutukuwepo na msukumo wa kuuliza maswali,”
alisema Eric Hoffer.Ukweli unabaki. Kuuliza si ujinga.
MASWALI NI NUSU YA MAJIBU
“Anayeuliza mengi, atajifunza mengi, na kubaki
na mengi,” alisema Francis Bacon (1561 – 1626) mwanafalsafa wa Uingereza.
Methali ya Kiswahili inayapa uzito maneno ya mwanafalsafa huyo: Kuuliza si ujinga.
Kuuliza swali hakumaanishi mwulizaji ni mjinga bali huonyesha kuwa angetaka
kujielimisha au kujifahamisha. Ukiuliza maswali unajua mengi. Baba alimwambia
mtoto wake wa miaka mitano. Wewe ni mtoto wa ajabu katika kuuliza maswali
mengi. Sijui ingekuwaje kama mimi ningeuuliza maswali mengi nikiwa mtoto. Mtoto
akamjibu: ungepata majibu ya kujibu baadhi ya maswali yangu. Maswali yanaweza
kukusaidia kumpima mtu anayeuliza. Ni katika msingi huu Voltaire (1694 – 1778)
mwandishi wa Kifaransa na mwanahistoria alisema: “Wahukumu watu kwa maswali
yao, badala ya majibu yao.” Kadiri ya mwandishi huyu unaweza kugundua mjinga.
“Atakuwa ni mjinga sana kwa vile anajibu kila swali analoulizwa,” alisema
Voltaire.
Yesu akiwa na umri wa miaka kumi
na miwili alikuwa na ufahamu wa kushangaza. Ufahamu huo ulionekana katika
kuwauliza walimu wa sheria maswali. Tunasoma hivi: “Ikawa baada ya siku tatu,
walimkuta hekaluni, ameketi kati ya walimu akiwasikiliza na kuwauliza maswali;
nao wote waliomsikia walistaajabia ufahamu wake na majibu yake” (Luka
2:46). Bila shaka Bwana Yesu aliuliza
maswali sahihi kupata majibu sahihi. Ni kweli “ufundi na sayansi ya kuuliza
maswali ni chanzo cha ujuzi wote,” kama alivyosemaThomas
Berger. Lazima katika maisha hujioji maswali mbalimbali juu ya maendeleo yako
kama: Je una mtazamo chanya au hasi? Je unashindwa kupanga au unapanga
kushindwa? Je umetoka wapi? Uko wapi? Unakwenda wapi? Pilipili usiyokula kwa
nini inakuwasha? Je unatembea barabara kuu ya wito wako au uko kwenye mchepuko
au vichochoroni? Kwa nini uliumbwa? Yaliyopita si ndwele kwa nini unaishi
katika wakati uliopita? Je ya wengine sebuleni ya kwako moyoni?
Zig Ziglar aliyekuwa na ufundi
mkubwa wa kutia watu moyo aliweka katika maandishi maswali kama haya: “Je
unajiandalia ya kesho au unaingoja kesho? Je unajua zaidi kuhusu kazi yako,
familia yako, na kuhusu wewe leo kuliko ilivyokuwa jana? Ni habari gani mpya au
ufundi gani mpya umejifunza? Je unaiacha kesho itokee tu, au unachukua hatua
kesho iwe unavyotaka iwe? Je unaacha jana ikufundishe au ikushinde? Je unajua
kuwa mtu mwingine ana maoni mengine na yanaweza kuwa sahihi?” Alihitimisha kwa
kusema: “Maswali ni majibu kweli, na ukiuliza ya kutosha nay a kweli, utaishia
kwa mtu wa furaha zaidi, mwenye afya zaidi..” Ingawa anayaona maswali ni
majibu, mimi nayaona maswali ni nusu ya majibu. Ni kama barua ilivyo nusu ya
kuonana. Kuelewa swali ni kama nusu ya jibu. Kuuliza swali sahihi unaweza
kupata jibu sahihi. Uwe kama Anne Rice
aliyesema: “Kila mara ninatazama kila mara ninauliza maswali.” Kuuliza swali sahihi ni jambo la msingi.
“Mwanasayansi sio mtu anayetoa majibu sahihi, bali ni yule anauliza maswali
sahihi,” alisema Claude Lévi-Strauss. Alikazia umuhimu wa kuuliza maswali
sahihi.
Sio kila swali linakuwa na
matokeo mazuri. Inategemea ni swali la namna gani. Mwanamke fulani alimwambia mme wake:
haunipendi tena, maana unapoona ninalia hauniulizi kwa nini ninalia. Samahani
sana maswali haya yamenifanya nitoe pesa nyingi katika kuyajibu.